STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, November 26, 2014

Spika wa Afrika Mashariki ang'olea

http://www.thelondoneveningpost.com/africa/wp-content/uploads/2014/06/Margaret-Zziwa.jpgHABARI ambazo zimepatikana punde zinasema kuwa aliyekuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Margareth Zziwa ameondolewa kwenye nafasi hiyo.
Nafasi ya Spika huyo aliyekuwa kwenye mzozo na baadhi ya wajumbe wa bunge hiyo, imechukuliwa na Chriss Opoka.

Bayern kumtea Xherdan Shaqiri

http://cdn.forzaitalianfootball.com/wp-content/uploads/2013/10/Xherdan-Shaqiri-Bayern-Munich.jpgRAIS wa heshima wa klabu ya Bayern Munich, Franz Beckenbauer amedokeza kuwa timu hiyo inaweza kumuacha Xherdan Shaqiri katika dirisha dogo la usajili Januari mwakani. 
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ameanza katika mechi tatu pekee za Bundesliga msimu huu huku akitokea benchi katika mechi nne za Ligi ya Mabingwa Ulaya alizocheza. 
Shaqiri, nyota wa kimataifa wa Switzerland ameendelea kukosa muda wa kucheza hatua ambayo imezusha tetesi juu ya mustakabali wake na Beckernbauer anategemea Shaqiri kutafuta klabu mpya pindi dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa. Beckenbauer mwenye umri wa miaka 69 amesema Bayern tayari wameshaonyesha dalili za kutohitaji huduma ya mchezaji huyo hivyo anadhani anaweza kuondoka katika mapumziko ya majira ya baridi.

Make Money at : http://bit.ly/copy_win

Mbrazil mpya wa Yanga atua Dar

jaja 1
Kiungo Mkabaji mpya wa Yanga, Emerson alipowasili mchana wa leo
KIUNGO mkabaji raia wa Brazil Emerson De Oliveira Neves Rouqe anatarajiwa kuwasili siku ya jumanne mchana jijini Dar es salaam kwa ajili ya majaribio katika klabu ya Young Africans na endapo atafuzu moja kwa moja atajiunga na mabingwa mara 24 wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Emerson mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anachezea timu ya Bonsucesso FC iliyopo ligi daraja la pili nchini kwao Brazil, msimu uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Poland katika timu ya Piotrkow Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili nchini humo.
Ujio wa Emerson kuja kufanya majaribio nchini unakuja kufuatia mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil pia Geilson Santos "Jaja" kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda kwao Brazil na kutoa taarifa kwamba hataweza kurejea tena nchini kutokana kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.
Awali ilikua familia ya Jaja ije nchini katika kipindi cha mapumziko, lakini waliomba yeye Jaja ndio aende Brazil na mara baada ya kufika huko matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo yamepelekea kushindwa kurejea nchini kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.
Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Young Africans kubakia na wachezaji wanne tu wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hamis Kizza na Andrey Coutinho hivyo endapo Emerson atafuzu atakua anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kimataifa
Endapo Emerson atafuzu majaribo pamoja na vipimo atajiunga na kikosi cha kocha mbrazil Marcio Maximo katika nafasi ya kiungo mkabaji ikiwa ni sehemu ya kuboresha timu kuelekea kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa.
Aidha kikosi cha Young African baada ya kuwa mapumzikoni kwa takribani wiki mbili, kinatarajiwa kuanza mazoezi siku ya jumatatu katika Uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo wa Nani Mtani Jembe pamoja na mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.

Huu ndiyo mpira utakaotumika AFCON 2015

http://images.supersport.com/2014/11/Marhaba-launched-300.jpg 
KAMPUNI ya Adidas na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) leo Novemba 26, 2014 zimeuwasilisha mpira wa Marhaba, kuwa mpira rasmi wa Fainali za Mataifa Afrika zitakazofanyika Equatorial Guinea mwaka 2015. Marhaba, utaonyeshwa rasmi Jumatano ya Desemba 3 mwaka 2014 wakati wa droo ya michuano hiyo ukumbi wa Sipopo Convention Centre mjini Malabo. Teknolojia iliyotumika kutengeneza mpira huo inashabihiana na ile iliyotumika kwenye Brazuca, uliotumika kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu nchini Brazil na mpira maarufu daima wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mpira huo wa AFCON ya mwakani utaanza kuuzwa Jumatatu ya Desemba 1, mwaka 2014.

MTIKITISKO TENA! RIPOTI YA PAC NOUMA

http://www.bongo5.com/wp-content/uploads/2012/08/Zitto-Kabwe.jpg
MWENYEKITI wa PAC, Mhe. Zitto Kabwe
PRO. MUHONGO
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI JAJI WEREMA
MH.WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA
PROF. ANNA TIBAIJUKA
ZITTO: Kamati imebaini kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa barua yenye Kumb Na. AGCC/E.080/6/70 ya tarehe 18 Novemba, 2013 alimthibitishia Gavana kuwa hakukuwa na kodi ya Serikali katika fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta ESCROW na kwamba fedha hizo zihamishiwe IPTL ili Serikali ijinasue na mashauri yasiyo na tija kwake.


Kutokana na mahojiano kati ya Kamati na Kamishina Mkuu wa TRA ilibainika kwamba Kampuni ya Piper Links haijulikani sio tu British Virgin Islands bali hata nchi nyingine. 



Kamati haielewi ni jinsi gani taasisi kubwa kama Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na nyingine zilizohusika katika suala hili, na ambazo tunaamini zimesheheni Watendaji wenye weledi, zimewezaje.


Wakati mahojiano ya Kamati na Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Kamishna Mkuu wa TRA pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU tarehe 19 Novemba, 2014 waliithibitishia Kamati kuwa kutokana na makubaliano wa Akaunti ya Tegeta ESCROW, sehemu ya fedha au fedha yote katika Akaunti hiyo ilikuwa ni fedha ya umma.


FILIKUNJOMBE: Kamati imethibitisha bila chembe ya mashaka kwamba mchakato mzima wa kutoa fedha katika akaunti ya Tegeta ESCROW uligubikwa na mchezo mchafu na haramu wenye harufu ya kifisadi ulioambatana na udanganyifu wa hali ya juu ambao kwa kufuata sheria tu ungeweza kugundulika na kuzuiwa.


BONYEZA MANENO HAYA KUSOMA RIPOTI YA ESCROW ILIYOWASILISHWA NA ZITTO KABWE BUNGENI

Kama unaona uvivu basi hata ni mapendekezo ya KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC) yaliyotolewa jioni hii Bungeni


3.2 Kamati inapendekeza kama ifuatavyo: -
3.2.1 Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) mara moja wachukue hatua ya kumkamata Bwana Harbinder Singh Sethi na
kumfikisha mahakamani kwa makosa ya Anti money laundering, ukwepaji kodi na wizi. Kamati pia inaelekeza Serikali kutumia sheria za Nchi, ikiwemo sheria ya ‘Proceeds of Crime Act’ kuhakikisha kuwa Bwana Harbinder Singh Sethi anarejesha fedha
zote alizochota kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Kwa kuwa suala hili ni suala la utakatishaji wa fedha haramu, Mamlaka ziwasiliane na mamlaka za Nchi nyingine kuhakikisha mali za Bwana huyu
zinakamatwa na kufidia fedha hizo.97
3.2.2 Mheshimiwa Spika, Kamati imethibitsha kuwa Bwana James Rugemalira aliuza hisa ambazo Kampuni yake ya VIP inamiliki katika IPTL na kulipwa na Bwana Sethi kutoka katika Fedha za Akaunti ya Tegeta ESCROW. Kamati imethibitisha kuwa fedha
kutoka akaunti za Kampuni ya PAP katika Benki ya Stanbic zilizofunguliwa maalumu kwa ajili ya kupokea fedha kutoka Akaunti ya Tegeta ESCROW iliyokuwa Benki Kuu zilipelekwa katika Akaunti nambari 00151002368801 na Akaunti nambari 00151002368802 za Kampuni ya VIP ziliyopo Mkombozi Commercial Bank.
Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu mbalimbali binafsi. Kamati haina tatizo na watu wawili kuuziana makampuni yao kwa thamani wajuazo wenyewe, au jinsi ya kuzitumia fedha zao, ama kuwachagulia watu wa kuwagawia,
lakini Kamati imejidhihirishia kuwa fedha iliyotumika kulipia manunuzi hayo ni fedha ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa bila huruma wala aibu, kutoka Benki Kuu. Hivyo, Kamati inazitaka mamlaka za uchunguzi kuhakikisha kuwa fedha hizo zinarudi Benki Kuu hata ikibidi kwa kufilisi mali za watu wote 98
waliofaidika na fedha hizo kwa thamani ya fedha walizopewa na Bwana Rugemalira.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya waliofaidika na fedha hizo ni Viongozi wa Umma ambao wanapaswa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Sheria namba 13 ya Mwaka 1995) ambayo inawataka kutoa taarifa ya zawadi wanazopokea au malipo wanayolipwa. Vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi kutambua kama walifuata matakwa ya sheria na hatua mahsusi zichukuliwe, ikiwemo kuvuliwa nyadhifa zao zote za kuchaguliwa na/au kuteuliwa, kufilisiwa mali zao na kushtakiwa mahakamani kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 132 (1) – (6).
3.2.3 Mheshimiwa Spika, Kamati pia imethibitisha kwamba fedha zilizolipwa kwa Watu binafsi zilitokana na Akaunti ya Tegeta ESCROW zilizolipwa kwa PAP ambayo si mmiliki halali wa IPTL.
Kwa maana hiyo fedha hizo zilitolewa kwa watu hao kama rushwa na kuzitakatisha fedha hizo haramu. Aidha, kamati inapendekeza kwamba Akaunti zote zilizohusika na miamala hii haramu ya Akaunti ya Tegeta ESCROW, akaunti zao zifungwe (freeze) na 99
wenye akaunti hizo walazimishwe kurejesha fedha hizo kwa mujibu wa Sheria (Anti Money Laundering) ikiwa ni pamoja na mali zao kufilisiwa. Kwa upande wa viongozi wa Kisiasa wawajibike na Watumishi wa umma wafukuzwe kazi.
3.2.4 Mheshimiwa Spika, Kamati imejiridhisha kwamba, suala la akaunti ya Escrow ni jambo la utakatishaji wa fedha (Money Laundering), kama alivyosema Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU
katika mahojiano yake na Kamati. Kamati inazitaka mamlaka zinazohusika, ikiwemo Benki Kuu kuzitangaza benki za Stanbic na Mkombozi Commercial Bank kama asasi za utakatishaji fedha
(Institutions of Money Laundering Concern).
3.2.5 Mheshimiwa Spika, Aidha, Kamati inalikumbusha Bunge lako tukufu pendekezo muhimu lililotolewa na Kamati Teule ya Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe kuhusu sakata la maarufu la Richmond. Kamati ilipendekeza:
“Mkataba kati ya TANESCO NA Richmond Development Company LLC na sasa Dowans Holdings S.A. kama ilivyo mikataba kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO 100 na Aistom Power Rentals inatoa unafuu usiostahili kwa makampuni hayo ya umeme na kuiumiza TANESCO na hatimaye watumiaji na walipa kodi kimapato, k.m. mikataba hiyo kuwa na vipengele vya kuibana TANESCO kuyalipa makampuni hayo kodi zinazohusika na uendeshaji (operations) matengenezo/marekebisho ya mara kwa mara ya mitambo (maintenance) gharama za bima, ada za mawakili na washauri elekezi (consultants)
gharama za mafuta na gesi ya kuendeshea mitambo,
gharama za ukodishaji mitambo (capacity charges)
ambazo TANESCO hulipa kila mwezi si chini ya wastani wa shilingi bilioni 2 kwa kila kampuni, izalishe au isizalishe umeme. Kamati Teule inatoa rai kwa Serikali kuwa mikataba yote hii ipitiwe upya mapema
iwezekanavyo kama ambavo mikataba ya madini
knavyopitiwa upya sasa na Serikali. Bila kufanya hivyo, mzigo mkubwa wa gharama za umeme utawaelemea wananchi na kushindwa kufikia azma ya Serikali ya maisha bora kwa kila Mtanzania.”101
Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza kwamba, azimio hili litekelezwe kwa kupitia upya mikataba yote ya umeme ambayo inalitafuna Taifa letu.
3.2.6 Mheshimiwa Spika, Kamati imejiridhisha kuwa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Nchini (TANESCO) bila sababu zozote za msingi ilikataa mapendekezo ya Menejimenti ya Shirika ya kutoruhusu uchotwaji wa fedha kutoka Benki Kuu akaunti ya Tegeta ESCROW
na hivyo kusababisha kulikosesha Shirika fedha zake inazohitaji sana kutokana na hali mbaya ya Shirika. Ikumbukwe kuwa Shirika la TANESCO lilipata hasara ya shilingi bilioni 467.7 katika mwaka wa fedha unaoishia Desemba 31, 2013. Hasara hiyo imekuwa
ikiongezeka mwaka hata mwaka toka mwaka 2010 (bilioni 5), 2011 (bilioni 43), 2012 (bilioni 177) na hivyo hadi kufikia Desemba 31, 2013, jumla yote kuu ya hasara (accumulated loss) ilikuwa imefikia shilingi trilioni 1.45.
Kamati pia imethibitisha kuwa Bodi ya TANESCO mpaka sasa haijatekeleza hukumu ya ICSID 2 na kukokotoa upya viwango vya malipo ya ‘capacity charges’ na hivyo kupelekea TANESCO na Serikali kuendelea kuilipa IPTL/PAP kila mwezi shilingi Bilioni 4.5 102 ($2.6m kila mwezi) izalishe au isizalishe umeme. Kamati inaitaka Serikali kuvunja mara moja Bodi ya TANESCO na TAKUKURU iwafungulie mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi wajumbe wote
waliohusika kupitisha maamuzi hayo ya kifisadi, ili iwe fundisho kwa wajumbe wengine wa bodi za Mashirika ya Umma kwamba watahukumiwa kwa maamuzi mabovu wanayoyafanya.
3.2.7 Mheshimiwa Spika, Kamati imethibitisha kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliingia makubaliano ya kutoa fedha katika Akaunti ya Tegeta ESCROW bila kujiridhisha kikailifu kuwa
maamuzi ya hukumu ya ICSID 2 yalikuwa bado kutolewa na hivyo kusababisha fedha kutolewa bila kukokotoa upya gharama za ‘capacity charges’, jambo ambalo limesababisha kupoteza fedha za umma.
Vile vile, Kamati imebaini kuwa, Katibu Mkuu hakufanya uchunguzi wa kina (due diligence) kujiridhisha uhalali wa Kampuni ya Mechmar kuuzwa kwa Piperlink na baadaye kuuzwa kwa PAP, na hivyo kusababisha fedha za akaunti ya Tegeta ESCROW kulipwa kwa asiyestahili na kinyume cha Mkataba wa akaunti ya Escrow.
Kwa maana hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, 103 pengine kwa uzembe wake ama kwa kukusudia kwa sababu
anazozijua yeye mwenyewe zaidi, amesaidia uchotwaji na hatimaye utakatishaji wa fedha haramu.
Mheshimiwa Spika, Kamati pia imethibitisha uzembe wa hali ya juu uliofanywa na Katibu Mkuu huyo, kushindwa kujiridhisha kama masharti ya Sheria ya kodi ya Mapato Sura ya 333, Kifungu cha 90(2) yalitekelezwa. Kifungu hicho kimsingi kinaitaka mamlaka ya ‘approval’’ ya uhamishaji wa Makampuni kutotambua Kampuni mpaka kwanza kodi za uhamishaji ziwe zimelipwa na hati za malipo ya kodi zimetolewa na mamlaka ya kodi.
Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Katibu Mkuu huyu utenguliwe, na TAKUKURU wamfikishe mahakamani mara moja, kwa kuikosesha Serikali Mapato, matumizi mabaya ya ofisi na kusaidia utakatishaji wa fedha haramu.
3.2.8 Mheshimiwa Spika, Kamati imethibitisha kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini alisema uongo Bungeni kwa kutamka kauli ambazo zilizokuwa na lengo la kupotosha umma kuhusu akaunti ya Tegeta ESCROW ikiwemo kutoa kauli ambazo zingeweza 104
kusababisha Nchi kuingia kwenye mgogoro wa kidiplomasia na nchi ya Uingereza.
Kamati inapendekeza kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini) achukuliwe hatua kali za kinidhamu ikiwemo kutenguliwa  uteuzi wake. Kamati pia inapendekeza kuwa Naibu Waziri huyu afikishwe mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili ili aadhibiwe kama Mbunge kwa kusema uwongo Bungeni ili liwe fundisho kwa wabunge wengine kuhusiana na kauli wanazotoa ndani ya Bunge lako tukufu.
3.2.9 Mheshimiwa Spika, Kamati imethibitisha kuwa Waziri wa Nishati na Madini amekuwa, mara kwa mara, akilipotosha Bunge lako tukufu na Taifa kwa ujumla kuhusiana na Fedha za Akaunti ya Tegeta ESCROW kwamba ndani ya fedha hizo hakukuwa na fedha za umma.
Mheshimiwa Spika, hata mtu wa kawaida angeweza kujua kwamba washirika wa ‘Tegeta Escrow Account’ ni akina nani na masharti ya kutoka kwa fedha hizo kwenye akaunti ni yapi kwa mujibu wa Mkataba wa uendeshaji wa akaunti hiyo. 105  Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, aidha kwa makusudi ama kwa sababu anazozijua vizuri zaidi mwenyewe, Waziri wa Nishati ananukuliwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge, Kwa nguvu kubwa na kwa kujiamini, akitetea uchotwaji wa fedha hizo kinyume na masharti ya Mkataba wa Escrow.
Aidha, Kamati imebaini kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye alikuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Bwana Harbinder Singh Sethi na Bwana James Rugemalira, tena katika ofisi ya Umma; na pengine hii ndiyo iliyokuwa sababu ya upotoshaji huu. 

Waziri wa Nishati na Madini alifanya udalali huo akijua dhahiri kuwa Bwana Sethi hana uhalali wa kisheria kufanya biashara kwa jina la IPTL.
Iwapo Waziri wa Nishati na Madini angetimiza wajibu wake ipasavyo, Fedha za Tegeta ESCROW zisingelipwa kwa watu wasiohusika, na Nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama kodi za VAT, Capital Gain Tax na Ushuru wa Stempu ambazo ni
sawa na takribani shilingi bilioni 30. 106 Mheshimiwa Spika, Kamati inapendekeza kuwa Mamlaka yake
ya uteuzi itengue uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana sababu hizo zilizoelezwa.
3.2.10 Mheshimiwa Spika, Kutokana na kukua na hivi sasa kukomaa kwa vitendo haramu vya wizi wa fedha ama mali za umma na kukua ama kukomaa kwa vitendo vya rushwa kubwa na uhujumu uchumi, inapendekezwa kwamba Bunge lako Tukufu
liridhie kuitaka Serikali kuanzisha kitengo maalumu cha kushughulikia rushwa kubwa (grand corruption) kitakachokuwa na nguvu ya kuendesha mashtaka kwa uhuru kamili, na kwamba Bunge lako Tukufu liridhie kuanzishwa kwa Mahakama Maalum ya kushughulikia Rushwa kubwa itakayoshughulikia kesi za rushwa
zitakazokuwa zikipelekwa kwake na kitengo maalum cha kushughulikia rushwa kubwa.
3.2.11 Mheshimiwa Spika, Kamati imethibitisha kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa ushauri ulioipotosha Benki Kuu ya Tanzania kuhusiana na hukumu ya Jaji Utamwa J. Kwa kutumia madaraka yake vibaya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliagiza kodi ya Serikali yenye thamani ya shilingi 21 bilioni isilipwe 

107 na hivyo kuikosesha Serikali mapato adhimu. Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kujua na kwa makusudi alilipotosha Bunge na Taifa kwamba mgogoro uliopelekea kufunguliwa kwa Akaunti ya
ESCROW ulikuwa ni mgogoro wa Wanahisa wa IPTL badala ya mgogoro kati ya TANESCO na IPTL. Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali utenguliwe mara moja na kisha afikishwe mahakamani kwa matumizi mabaya ya Ofisi
yaliyopelekea Serikali kupoteza mabilioni ya fedha.
3.2.12 Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Waziri Mkuu kuhusiana na suala hili, Kamati iliipitia kwa umakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 iliyoainisha Kazi na Mamlaka ya Waziri Mkuu na kubaini kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 52 (1):
“Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti,
usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na
shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.”
Na, Ibara ya 52 (2), inayosema; 


108
“Waziri Mkuu atakuwa kiongozi wa shughuli za Serikali
Bungeni.”
Kisha Kamati ikajiuliza maswali kadhaa. Kwa mfano katika kutaka kubaini ukweli na kujiridhisha Kamati ilijiuliza maswali yafuatayo kuhusu Waziri Mkuu:
(a) Je, Waziri Mkuu alikuwa anajua sakata la utoaji wa
fedha katika Akaunti ya Tegeta ESCROW?
(b) Je, Waziri Mkuu alitimiza wajibu wake kwa mujibu wa Ibara ya 52(1)?
(c) Je, Waziri Mkuu wakati akitoa matamshi yake Bungeni alikuwa akitimiza wajibu wake kwa mujibu wa Ibara ya 52 (2)?
(d) Je, nini maana, uzito na ukweli wa matamshi ya mara kwa mara ya Waziri Mkuu ndani na nje ya Bunge
kuhusiana na suala hili?
(e) Je, Waziri Mkuu alitoa maamuzi au maelekezo yoyote ya kuzuia jambo hili lisifanyike?

109
Mheshimiwa Spika, Baada ya kupitia vielelezo vilivyomo kwenye ripoti ya CAG, Kamati imejiridhisha pasipo mashaka kuwa, Waziri Mkuu, alikuwa ana taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa
kuchotwa fedha kutoka katika akaunti ya ESCROW.
Ushahidi ulioletwa na ofisi ya CAG kwenye Kamati unaonyesha kuwa Waziri Mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hili. Na Kamati imesikitishwa kuona kuwa Waziri Mkuu hakuchukua hatua zozote kuzuia muamala huu usifanyike.
Mheshimiwa Spika, Kamati, kwa kuzingatia kielelezo namba 22, inathibitisha bila shaka kwamba, Waziri Mkuu alikuwa analijua jambo hili vizuri na kwamba aliridhia muamala huu ufanyike. Ndiyo maana katika maelezo yake ya Bungeni mara kadhaa Waziri Mkuu
alithibitisha kuwa fedha za Escrow hazikuwa fedha za Umma. 

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania aliandika:
“…kubadili Waziri Mkuu sio jambo la ajabu. Ndugu
Rashid Mfaume Kawawa alikuwa Waziri Mkuu wangu 110 kwa muda mrefu. Hakuwa amefanya kosa lolote; lakini nilitaka kumbadili na kuteua Waziri Mkuu mwingine.
Nilimwita, nikamwambia hivyo. Tukakaa pamoja mimi
na yeye, tukashauriana na kukubaliana nani anafaa
kushika nafasi yake. Nikamteua Hayati Edward Moringe Sokoine. Najua kuwa watu wa aina ya Rashidi Kawawa ni adimu sana Duniani, hawazaliwi kila siku; hata hivyo ni jambo la kushangaza kidogo kwamba viongozi wetu wa Mageuzi, hata bado hatujafa, wanaona kuwa ni kosa kuwakumbusha kuwa vyeo walivyonavyo ni dhamana. Wanadhani kuwa Uwaziri ni Usultani; ukishakuwa Sultani utakufa sultani! Nadhani
kumbadili Waziri Mkuu sio jambo la ajabu. Anaweza
kujiuzulu, anaweza kufukuzwa Nchi isitikisike. Lakini
huwezi kumtimua Rais wa Nchi bila kuitikisa Nchi
yenyewe. Ni vizuri jambo hili likatamkwa waziwazi na
likaeleweka sawasawa. Maana watu wengine
wananong’ona nong’ona kuwajibika kwa Rais kana 111
kwamba ni jambo la mchezo mchezo tu. Kulazimika
kumchukulia hatua Rais wa nchi ni mkasa na balaa kwa Nchi yeyote ile.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba viongozi wenye mamlaka makubwa wanapaswa kila wakati kukumbuka kauli ya muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Muasisi wa Muungano, Sheikh Thabit Kombo, ambaye alikuwa akipenda kusema ‘weka akiba ya maneno’.
Ni wazi kwamba maneno ya Waziri Mkuu hapa Bungeni yaliuaminisha umma kuwa fedha zile siyo fedha za umma kiasi kwamba gazeti la Serikali la Daily News la tarehe 1 mwezi Mei, 2014, likachapisha habari yenye kichwa kikubwa cha habari ‘IPTL clean Deal – Pinda’. Na ofisi ya Waziri Mkuu haikukanusha.
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kushangaza kuona kwamba, jambo kubwa na zito kama hili lingeweza kufanyika bila ya mamlaka za juu, hususan Mhe. Waziri Mkuu kufahamu. 

112
Mheshimiwa Spika, kwa uzito na unyeti wa jambo hili, kwa vyovyote vile, Waziri Mkuu anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa kutokutekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ili kurejesha imani ya wananchi kwa serikali yao na viongozi wao wa kisiasa.
3.0 HITIMISHO
Mhesimiwa Spika, napenda kukushukuru sana kwa kuiamini Kamati yetu kwa kuikabidhi jukumu hili nyeti. Nakuhakikishia kwamba kazi hii imetekelezwa kwa haki iliyojengwa katika msingi wa Taarifa ya Ukaguzi Maalum wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, na vyanzo vingine muhimu vikijumuisha maelezo ya Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Mheshimiwa Spika, Kamati inatoa shukrani za dhati kwa vyombo vya habari kwa kuwapasha habari Watanzania kuhusiana na suala hili. Kwa namna ya pekee kabisa Kamati inalipongeza gazeti la
The Citizen kwa msimamo wake thabiti bila kujali vitisho.

113 Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inayo imani na Bunge Lako Tukufu kwamba litaitumia Taarifa hii ipasavyo katika kutekeleza Wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri Serikali itekeleze wajibu
wake katika misingi ya haki, uadilifu, uzalendo, usawa, uwazi na uwajibikaji. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwani katika kipindi chote cha kuandika Taarifa hii mlitutia moyo
kwa kuonesha dhahiri kwamba mnaihitaji Taarifa yetu ijadiliwe Bungeni.
Mheshimiwa Spika, naomba pia kuishukuru Ofisi ya Spika kwa maelekezo thabiti ya namna ya kutekeleza jukumu hili.
Naomba pia kumshukuru Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas D. Kashillilah na Wajumbe wa Sekretarieti yake kwa ushauri makini katika kipindi chote ambacho Kamati ilikuwa ikitekeleza jukumu hili. Kipekee nawashukuru pia Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ndg. Francis Mwakapalila, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Dkt. Edward Hoseah na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini, Bw. Rished Bade kwa ushirikiano walioipatia Kamati.

114
Mwisho, nawashukuru Watumishi wote wa Bunge na vyombo vingine vya kiusalama vilivyohusika katika kuisaidia Kamati kutekeleza jukumu lake.
Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako tukufu lipokee Taarifa hii, lijadili na kupitisha mapendekezo yote tuliyoyatoa kuwasilisha.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Zitto Zuberi Kabwe, Mb.
MWENYEKITI
KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC)
26 NOVEMBA, 2014

Mizengo Pinda kuzindua albamu ya Family Singers Dec 7

Mkurugenzi wa kikundi cha uimbaji wa muziki wa Injili cha Family Singers, Daniel Masheto Jr akizungumza na wanahabari leo juu ya uzinduzi wa albamu yao utakaofanyika Desemba 7
Mwenyekiti wa Family Singers, Jonas Danny akifafanua jambo kwa wanahabari (hawapo pichani) wakati akitangaza uzinduzi wa albamu yao uya pili ya 'Usilie' utakaofanyika Des 7 katika ukumbi wa PTA.
Bango lenyewe na uzinduzi huo
Kikundi chetu hatuimbi tu muziki wa Injili pia tunajitolea kuihudumia jamii. Mkurugenzi Masheto Jr akitoa ufafanuzi
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albamu ya 'Usilie' ya kundi la waimbaji wa muziki wa injili la Family Singers.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Desemba 7, mwaka huu kwenye Ukumbi wa PTA maarufu kama Sabasaba, Temeke jijini Dar es Salaam na kusindikizwa na waimbaji wa muziki wa Injili na kwaya mbalimbali na wasanii wa Bongo Movie.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kundi hilo, Daniel Misheto Jr, alisema hiyo ni albamu yao ya pili baada ya awali kutamba na ile ya 'Machozi Yatafutwa' na kwamba waziri mkuu ndiye atakayekuwa mgeni rasmi baada ya kuwasiliana naye na kuwathibitishia atakuwapo siku ya uzinduzi huo.
Misheto alisema kundi lao mbali na kushughulika na masuala ya uimbaji wa muziki wa Injili, pia limekuwa likijitolea kwa jamii kwa kutoa huduma mbalimbali ikiwamo ya afya na kwamba hata siku ya uzinduzi huo kutakuwa na huduma ya afya bure kwa wananchi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana kabla ya kupisha huduma ya uimbaji itakayoongozwa na wasanii mbalimbali.
"Tunatarajia kuzindua albamu yetu ya pili iitwayo 'Usilie' na shughuli hiyo itafanyika Desemba 7 katika Ukumbi wa PTA na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndiye atakayekuwa mgeni rasmi na viongozi mbalimbali wamealikwa na tutasindikizwa na wasanii kadhaa akiwamo Leah Mudy, AIC (T) Vijana Chang'ombe, Martha Mwaipaja na wengine kutoka nje ya nchi," alisema.
Naye Mwenyekiti wa Family Singer Jonas Danny, aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwa ajili ya kupata huduma ya afya itakayoendeshwa na madaktari 20 kutoka hospitali za Muhimbili,  Dk Kairuki na IMTU.

Mcheza Kriketi mahututi baada ya kupigwa na gongo uwanjani

MCHEZA Kriketi nyota wa nchini Australia, Phil Hughes yupo mahututi akiipania roho yake hospitalini mjini Sydney baada ya kugongwa kichwani na gongo la kuchezea mchezo huo wakati wa mechi ya Sheffield Shield.
Nyota huyo aliyeichezea mechi yake mechi 26 Australia ikiwemo michuano mitatu ya Ashes, amefanyiwa upasuaji na yupo kwenye kitengo cha wagonjwa walio katika uangalizi maalum.
Hughes, 25, aliyeichezea Australia Kusini dhidi ya Wales Kusini mpya katika michuano ya Sydney Cricket Ground (SCG), alipigwa na gongo hilo akiwa na helmet kichwani na Sean Abbott kabla ya kupoteza fahamu na kukimbizwa hospitali.
Mara baada ya tukio hilo mchezaji huyo alizimia uwanjani na kuwafanya madaktari kuharaakisha kumwahisha hospitalini alipofanyiwa upasuaji huyo, lakini inaelezwa hali yake bado tete na mamia wa mashabiki wake wakiendelea kumuombea apate nafuu haraka.

Sepp Blatter azidi kuandamwa FIFA

http://i.telegraph.co.uk/multimedia/archive/01781/balt_1781366b.jpgRAIS wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, Sepp Blatter ameendelea kuandamwa baada ya Rais wa  Ligi ya Soka ya Ujerumani-DFL, Reinhard Rauball kumtaka rais huyo kujiuzulu nafasi yake.
Rauball alikaririwa na gazeti la Kicker akidai kuwa anadhani wakati wa Blatter kuachia nafasi hiyo umefika kutokana na kashfa mbalimbali ambazo zimeendelea kuliandama shirikisho hilo.
Kashfa ambayo inaiandama shirikisho hilo kwa sasa ni kuhusu ripoti ya uchunguzi ya Michael Garcia yenye kurasa 430 ambayo FIFA imegoma kuichapisha kwa kuogopa kukiuka sheria.
Rauball amesistiza kuwa kashfa hiyo inayohusu mchakato wa kutafuta wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 inapaswa kumpelekea Blatter kujiuzulu ili kulinda heshima ya michuano hiyo. Michuano hiyo imepangwa kufanyika Russia na Qatar.
Rauball alifafanua kuwa jambo hilo kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari alimpigia simu Blatter na kumueleza mawazo yake kuhusiana na hilo

Messi ndiye baba lao Ulaya, apiga hat trick ya 31

MSHAMBULIAJI nyota wa Argentina, Leonel Messi amevunja rekodi ya mabao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuiongoza Barcelona kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 ugenini mjini Nicosia, Cyprus katika mfululizo wa michuano hiyo.
Messi ambaye amekuwa gwiji wa kuvunja rekodi zilizowekwa na wanasoka wenzake, alifunga 'hat trick' iliyomfanya kufikisha mabao 74 katika michuano hiyo na kumpita aliyekuwa akishikilia rekodi ya mabao mengi katika michuano hiyo Raul aliyekuwa na mabao 71.
Nyota huyo wa Barcelona alikuwa akilingana na Raul baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Ajax mapema Novemba, lakini 'hat trick' hiyo ya 30 katika maisha yake ya soka yalimfanya awapiku wachezaji wote.
Messi alifunga mabao hayo katika dakika ya 38 akimalizia kazi nzuri ya Rafinha, ambalo lilikuwa bao la pili la timu yake baada ya mapema kwenye dakika ya 27 Luis Suarez kufungua akaunti yake ya mabao katika klabu hiyo aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Liverpool, alipofunga bao la kuongoza akimalizia kazi nzuri ya Jordi Alba.
Nyota huyo anayeshikilia rekodi kibao katika ulimwengu wa soka ikiwamo wa kuwa Mfungaji Bora wa La Liga akiwa na mabao 253, alifunga mabao mengine mawili katika dakika za 58' na 87 kwa kumalizia pasi za wachezaji wenzake, Dani Alves na Pedro.
Ushindi huo umeifanya Barcelona kushika nafasi ya pili katika kundi lake la F wakiwa na pointi 12, moja pungufu na vinara wa kundi hilo PSG ambayo ilipata ushindi mnono nyumbani dhidi ya Ajax katika mfululizo wa michuano hiyo ya Ulaya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mechi Messi amesema: "Nina furaha sana kuvunja rekodi hususan katika mashindano muhimu kama haya, lakini huu ulikuwa mchezo mkubwa kwetu mbali na rekodi zote," amesema.
Mshindi huyo mara nne wa tuzo ya Mwanasoka Bora Duniani, mwenye umri wa miaka 27, kwa mabao yake dhidi ya APOEL yamemfanya afikishe jumla ya mabao 371 akiwa na kikosi cha Barcelona, mbali na mabao 45 aliyonayo akiifungia timu yake ya taifa ya Argentina.
Naye Suarez aliyefunga bao lake la kwanza kwa Barcelona tangu aliposajiliwa kwa kitita cha pauni Mil. 75 alinukuliwa baada ya pambano hilo akisema kuwa anajisikia vizuri kufunga bao hilo.
"Kawaida ni muhimu kwa mshambuliaji kufunga mabao pamoja na kwamba kipaumbele ni kucheza vizuri kwa ajili ya timu. Lakini unajisikia vizuri kupiga bao,"amesema nyota huyo wa Uruguay.
Katika michezo mingine iliyochezwa juzi, Chelsea walipata ushindi mnono ugenini baada ya kuifumua Schalke 04 ya Ujerumani kwa mabao 5-0, huku mkongwe Didier Drogba alifunga bao moja kuthibitisha kuwa bado wamo.
Mabao mengine ya vinara hao wa Uingereza, ambayo imeendeleza rekodi yao ya kucheza mechi mfululuizo bila kupoteza msimu huu yaliwekwa kimiani na nahodha John Terry, Willian, Jan Kirchhoff aliyejifunga, na Ramires.
Ushindi huo wa Chelsea inayofundishwa na Mreno Jose Mourinho, umeihakikishia timu hiyo kwenda hatua ya mtoano kutoka kundi G baada ya kufikka pointi 11, ikifuatiwa na Spoting Lisbon ya Ureno ikijiweka pazuri katika nafasi ya pili baada ya kuinyuka Maribor 3-1.
Matokeo Kamili:
CSKA Moscow     1-1 Roma
BATE  0-3     Porto
Manchester City     3-2 Bayern Munich
APOEL  0-4 Barcelona
PSG     3-1 Ajax
Schalke 04 0-5 Chelsea
Sporting 3-1 Maribor
Shakhtar Donetsk 0-1 Athletic Bilbao
=======

Coastal Union yaita nyota wake Tanga

UONGOZI wa mabingwa wa zamani wa soka nchini, Coastal Union walioanza mazoezi jijini Tanga kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara, imewachimba mkwara nyota wake kwa kuwapa muda wa wiki moja wawe wameripoti kambini kabla ya kuchukuliwa hatua.
Aidha klabu hiyo imesema haina mpango ya kufanya usajili wowote kwenye dirisha dogo la usajili linaloendelea kwa sababu kikosi chao kimekamilika kila idara.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Kassim El Siagi, aliliambia MICHARAZO kuwa, mapumziko ya wiki mbili waliyowapa wachezaji wao walishaisha na timu kuanza mazoezi chini ya makocha wao Wakenya Yusuf Chipo na Ben Mwalala, lakini ni idadi ndogo tu ya wachezaji walioripoti kwenye kambi ya mazoezi na kuufanya uongozi wao kutoa muda wa wiki moja kwa wachezaji hao kuripoti haraka.
"Tumeshanza mazoezi na tumetoa hadi wiki moja kwa nyota wote wawe wamesharipoti, kwa sababu timu inatarajiwa kucheza mechi kadhaa za kirafiki za kujipima nguvu kabla ya kuikabili ligi kuu," alisema.
El Siagi alisema kwa mujibu wa kocha wao, klabu hiyo haihitaji kufanya usajili wowote kwenye dirisha dogo kwa sababu wachezaji waliopo wanakidhi kila idara.
"Hatutaongeza mchezaji yeyote kwenye dirisha dogo, kwa sababu idara zote za wachezaji katika kikosi chetu zimekamilika," alisema.
Coastal waliotwaa ubingwa wa Tanzania mwaka 1988 inakamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiwa nyuma ya timu za Mtibwa Sugar, Yanga na Azam baada ya kukusanya pointi 11 kutokana na mechi saba ilizocheza.

Kipusa cha Kaole Kwanza kuanza kurushwa Jan 4

Mwenyekiti wa kundi la Kaole Kwanza, Thea
KUNDI la Kaole Kwanza linaloundwa na wasanii wa zamani wa Kaole Sanaa linatarajiwa kuanza kurusha tamthilia yao mpya iitwayo 'Kipusa' Januari 4, mwakani.
Mwenyekiti wa kundi hilo, Misayo Ndimbagwe 'Thea' aliliambia MICHARAZO mapema leo kuwa, tayari wameshakamilisha kila kitu juu ya kuanza kurushwa kwa igizo hilo ambalo limewashirikisha wasanii mbalimbali nyota nchini akiwamo Bi Hindu, Muhogo Mchungu, Davina, Kipemba, Nyamayao, Bi Staa, Bi Terry, Swebe na wengine.
Thea alisema kituo kimojawapo nchini ndicho kilichopewa jukumu la kuanza kurushwa kwa igizo hilo ambalo lilizinduliwa mapema mwaka huu mbele ya wadau ambao walitoa maoni yao kwa ajili ya kuboreshwa.
"Tumekamilisha kila kitu na tamthilia yetu itaanza kurushwa mapema mwakani na kituo kimoja cha hapa nchini, hivyo mashabiki wajiandae kupata uhondo walioukosa kwa muda mrefu," alisema Thea.
Aidha, Thea alidokeza kuwa baada ya igizo hilo kuanza kurushwa hewani wataanza mchakato wa kuzalisha filamu zao ambazo zitaanza kuingia sokoni kuanzia Februari.
"Tumepania kuwapa uhondo mashabiki wa fani ya uigizaji, baada ya igizo kuanza kurushwa tutaanza kazi ya kurekodi filamu zetu ambazo zitakuwa sokoni kuanzia Februari," alisema Thea, mmoja wa nyota wa filamu aliyepata jina kubwa kupitia Kundi la Kaole Sanaa