Kiungo Mkabaji mpya wa Yanga, Emerson alipowasili mchana wa leo |
Emerson mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anachezea timu ya Bonsucesso FC iliyopo ligi daraja la pili nchini kwao Brazil, msimu uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Poland katika timu ya Piotrkow Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili nchini humo.
Ujio wa Emerson kuja kufanya majaribio nchini unakuja kufuatia mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil pia Geilson Santos "Jaja" kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda kwao Brazil na kutoa taarifa kwamba hataweza kurejea tena nchini kutokana kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.
Awali ilikua familia ya Jaja ije nchini katika kipindi cha mapumziko, lakini waliomba yeye Jaja ndio aende Brazil na mara baada ya kufika huko matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo yamepelekea kushindwa kurejea nchini kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.
Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Young Africans kubakia na wachezaji wanne tu wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hamis Kizza na Andrey Coutinho hivyo endapo Emerson atafuzu atakua anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kimataifa
Endapo Emerson atafuzu majaribo pamoja na vipimo atajiunga na kikosi cha kocha mbrazil Marcio Maximo katika nafasi ya kiungo mkabaji ikiwa ni sehemu ya kuboresha timu kuelekea kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa.
Aidha kikosi cha Young African baada ya kuwa mapumzikoni kwa takribani wiki mbili, kinatarajiwa kuanza mazoezi siku ya jumatatu katika Uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo wa Nani Mtani Jembe pamoja na mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
No comments:
Post a Comment