Waya! Wachezaji wa Arsenal hawaamini kama Robin van Persie kawatungua |
BAO pekee la nyota wa zamani wa Arsenal Robin van Persie limeisaidia Manchester United kuzima ubabe wa vinara wa Ligi Kuu ya England, Arsenal kwa kuwalaza bao 1-0, huku Swansea City ikitoka nyuma na kuwalazimisha wageni wao Stoke City sare ya mabao 3-3 katika mechi nyingine ya ligi hiyo.
Van Persie alifunga bao hilo katika dakika ya 27 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na mshambuliaji nyota wa England, Wayne Rooney na kuifanya Mashetani Wekundu kuendeleza ubabe kwa vijana hao wa London ya Kaskazini kila timu hizo zinapokutana Old Trafford.
Kwa ushindi huo Manchester United imefikisha pointi 20 na kushika nafasi ya tano ikizishusha Everton na Tottenham Hotspur kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika mechi nyingine ambayo ilikuwa ya kusisimua, Stoke City ilichomoa kipigo dakika za nyongeza kwa mkwaju wa penati mbele ya Swansea ambayo ilikuwa ikionekana kuibuka na ushindi wa 3-2 baada ya kutoka nyuma.
Bao la mkwaju huo wa penati ulifungwa na Charlie Adam na kuzima ndoto za vijana wa Michael Laudrup waliochomoa mabao waliyotanguliwa kufungwa katika kipindi cha kwanza.
Stoke walitangulia kupata bao la kwanza katika dakika ya nane kupitia kwa Jonathan Walters na Stephen Ireland dakika ya 26 aliongeza la pili, mabao yote yakitokana na pasi ya Peter Crouch.
Wenyeji walirejesha mabao hayo kupitia kwa Wilfried Bony katika dakika ya 56 na Nathan Dyer dakika ya 74 kabla ya Bony kuelekea kuipa Swansea ushindi kwa kufunga bao la tgatu dk 86 klabla ya Stoke kuchomoa dakika ya 90+6 kwa penati na kuzifanya timu hizo zigawane pointi moja moja.