STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, June 18, 2013

Hali ya hewa Arusha yarejea kwenye utulivu

MOTO UNAWAKA BAADA YA KUCHOMWA MATAIRI


HALI ya utulivu imeanza kurejea jijini Arusha baada ya hali kuchafuka kwa Jeshi la Polisi kufyatua mabomu ya machozi dhidi ya wafuasi na viongozi wa CHADEMA baada ya kukusanyika kwenye viwanja vya Soweto ili kujua namna watakavyoshiriki mazishi ya watu waliouwawa kwa Bomu siku ya Jumamosi.
Kwa mujibu wa taarifa toka Arusha zinasema kuwa hali imerejea kuwa tulivu baada ya mshikemshike wa Polisi kuwatimua wananchi hao na kuleta kizaazaa cha kutunishiana misuli na kurejea hali ya taharuki jijini humo baada ya hivi karibuni kukumbwa na matukio yaliyosababisha vifo vya watu wasio na hatia.

Msajili wa vyama alaani mlipuko wa bomu Arusha, avinyooshea kidole vyama vya CCM na CHADEMA

Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, John Tendwa
Na Suleiman Msuya
MSAJILI  wa Vyama vya Siasa nchini John Tendwa amesema ili kuhakikisha kuwa amani inaendelea kudumu ni muhimu kuwepo kwa uvumilivu na kuheshimiana  kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)  na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kauli hiyo ameitoa leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya kutokea kwa mlifuko wa bomu kwenye mkutano wa kampeni ya udiwani uliokuwa unaendeshwa na CHADEMA katika viwanja vya Soweto mjini Arusha.
Tendwa alisema kwa muda sasa kumekuwepo kwa msuguano mkubwa baina ya vyama hivyo viwili jambo ambalo linaonyesha dalili za kuhatarisha amani ya nchi na wananchi kwa ujumla.
Msajili huyo alisema vyama hivyo vinaonyesha kukosa  uvumilivu na kuheshimiana kwani kwa kipindi hiki kifupi cha kampeni za udiwani viomekuwa na fujo ambazo kila mmoja anamshutumu mwenzake jambo ambalo sio nzuri katika nchi.
Alisema kutokana na tukio hilo viongozi wao wameibuka na kushutumiana ambapo  Katibu Uenezi wa CCM Nape Mnauye alisikika akiwashutumu CHADEMA kuhusikana wakati Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe akisema CCM na Jeshi la Polisi wanahusika.
“Inasikitisha sana kuona watu wanakufa alafu watu wanajitokeza na kuanza kushutumiana kuwa huyu ndiye anahusika mimi nomba wapeleke ushahidi Jeshi la Polisi ili kuweza kusaidia upelelezi,” alisema.
Tendwa alisema katika kuhakikisha kuwa vyama hivyo vinaendelea kuheshimiana na kuvumiliana anatarajia kuita kikao ambacho kitashirkisha ofisi yake, jeshi la polisi na vyama hivyo kwani wanapoelekea ni pabaya.
Alisema iwapo uchaguzi wa Udiwani hali inakuwa hivyo je itakuwakuaje katika uchaguzi wa Serikali za Mitaaa na uchaguzi mkuu watu watarajie nini kwani ni ishara mbaya kwa Taifa ambalo linasifika kwa amani.
Aidha Msajili huyo alipotakiwa kuelezea juu ya ofisi yake kuvifuta vyama hivyo viwili vya CCM na CHADEMA alisema ofisi yake ina mamlaka hayo ila hiyo ni hatua ya mwisho kuchukuliwa iwapo itabidi.
Tendwa alisema uamuzi wa kuvifuta vyama hivyo unaweza kuwa na athari kubwa kwani utahitaji gharama kubwa za kufanyika uchaguzi jambo ambalo sio la kukimbilia.
Alisema ofisi yake inahitaji kukutana na vyama hivyo  kwani ndio njia sahihi ya kufikia muafaka kwa maslahi ya vyama hivyo na wananchi kwa ujumla.
“Ni lazima jamii itakatumbua kuwa maamuzi haya yanahusi CCM ambayo ipo madarakani ambapo matokeo yake ni kuvunja Serikali na kwa CHADEMA ni kuwaondoa wabunge wake hivyo uchaguzi kufanyika tena,”  alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini Peter Mziray amevitaka vyama hivyo kutambua kuwa nchi hii iwapo itaingia vitani wao ndio wahusika wakubwa.
Alisema Baraza hilo linatajia kukutana kwa pamoja likishirikisha vyama vyote vya siasa ambapo watatoka na azimio juu ya hali ilivyo hivi sasa kwani inaonyesha dalili za kupotea kwa amani.
Mziray ambaye ni Rais Mtendaji wa Chama cha African Progressive Party Tanzania (APPT Maendeleo alisema hali inayotoke kwa sasa jeshi la Polisi na vyombo vyote vya usalama vinapaswa kushutumiwa kwani vionyesha kutofanya kazi vizuri.
Mwenyekiti huyo alisema hali hiyo inasikitisha sana kutokana na ukweli kuwa watu wasio na hatia kupoteza maisha jambo ambalo halikubaliki.
“Kwa kweli vyama hivi viwili vimekuwa na matukio mbalimbali ambayo kwa muono wangu nadhani vinahitajika kubadilika kwani hali sio shwari ila vyombo vya usalama pia vina mapungufu yao,” alisema

Klabu Thailand yaja kusaka wachezaji wa kulipwa

Nembo ya klabu ya Thai Port FC
Na Boniface Wambura
KLABU ya Thai Port Football ya Thailand inatafuta wachezaji nchini Tanzania kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu nchini humo na katika nchi nyingine barani Ulaya.

Kupitia kwa wakala wake, klabu hiyo imetuma taarifa kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikitaka wachezaji wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 28 kwa ajili ya kuwafanyia majaribio ambapo watakaofuzu watacheza nchini humo na katika klabu nyingine za Ulaya ambazo wana ushirikiano nazo.

Wachezaji wenye nia ya kufanya majaribio wanatakiwa kutuma taarifa za wasifu wao (CV) kwa klabu hiyo kwa njia ya emaili, wawe na pasi ya kusafiria pamoja na pasi ya mchezaji (player passport).

Wakala atapitia vitu hivyo, na kwa wachezaji atakaowahitaji atawatumia tiketi za ndege na viza kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio nchini humo, na watakaofanikiwa kabla ya kusaini nao mikataba watawasiliana na klabu zao nchini (kwa wale wenye klabu).

Polisi wafafanua sababu ya kulipua mabomu ya machozi leo Arusha


JESHI la Polisi limekipiga marufuku chama cha demokrasia na maendelo(CHADEMA)kufanya shughuli zozote za kuaga miili ya marehemu kwenye viwanja vya Soweto kwani zoezi la uchunguzi bado linaendelea kwenye viwanja hivyo .


Akizungumza ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas amesema kutokana na uchunguzi unaoendelea wa tukio la bomu kwenye viwanja hivyo imeonelea kuwa si busara kuweka mkusanyiko wa watu kwani kutaharibu upelelezi.


Kamanda Sabas amedai  kuwa  jeshi la polisi  liliwataka viongozi wa chama hicho kuwaeleza wafuasi wao mahali sahihi watakapoweza kufanyia shughuli hiyo lakini si kwenye viwanja hivyo.

Hali kwenye viwanja hivyo imekuwa ya pilika pilika tangu juzi kwa wafuasi wa chama hicho kujikusanya tokea asubuhi hadi jioni kwa madai ya kuomboleza ..

Hata hivyo viongozi wa chama cha demokrasia na maendeleo walikaidi agizo hilo na  kuanza  kujikusanya uwanjani hapo pamoja na wafuasi wa CHADEMA, hali iliyoleta  mvutano kati ya viongozi  wa jeshi la polisi na  wafuasi hao.
Wakati mabishano hayo yakiendelea, Askari Polisi mmoja  alijichanganya na kuingia katikati ya wafuasi wa Chadema pembeni mwa uwanja huo ambao walikua wanasubiri kujua utaratibu wa kuaga miili ya Marehemu waliolipuliwa na bomu June 15 2013.

Baada ya hapo, wafuasi hao hawakupenda kitendo cha Polisi kujichanganya nao hivyo ikazuka ugomvi huku wakitaka atoke, baada ya dakika kadhaa  mabumu yalianza kusikika.

Baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho waliokuwepo uwanjani haponi mbunge wa jimbo la ubungo John Mnyika,Ezekia Wenje,Tundu lissu, Halima Mdee.

TFF yapongeza mashabiki kuiunga mkono Stars

Stars wakishangilia moja ya mabao yao dhidi ya Ivory Coast

Na Boniface Wambura

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru washabiki kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na Ivory Coast (The Elephants) iliyochezwa juzi (Jumapili) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwitikio wa washabiki katika mechi hiyo ilikuwa ni moja ya chachu ya kiwango kilichoonyeshwa na Taifa Stars, kwani walishangilia mwanzo hadi mwisho licha ya kupoteza kwa mabao 4-2.

Ni matarajio utakuwepo mwitikio kama huo huo katika mechi ijayo ya Taifa Stars ya michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Nyumbani (CHAN) dhidi ya Uganda (The Cranes) itakayochezwa Dar es Salaam kati ya Julai 12-14 mwaka huu. Stars itaingia tena kambini Julai 4 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo.

Mbongo kukipiga Yemen, TFF yatoa ITC yake


Na Boniface Wambura
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Mtanzania Gossage Mtumwa ili aweze kucheza mpira nchini Yemen.

Mtumwa ambaye anatoka katika kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji cha Rollingstone cha Arusha aliombewa hati hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu cha Yemen (YFA) kwa ajili ya kucheza nchini humo.

TFF inamtakia kila la kheri Mtumwa katika safari yake ya Yemen, na ni matarajio yetu kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini humo ili wachezaji wengine wa Tanzania nao wapate fursa ya kucheza mpira wa miguu nchini Yemen.


Kamishna Alferd Rwiza kuhudhuria Semina CAF

Na Boniface Wambura
KAMISHNA Alfred Kishongole Rwiza ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuhudhuria semina ya makamishna itakayofanyika kuanzia Julai 6-7 mwaka huu katika makao makuu ya shirikisho hilo jijini Cairo, Misri.

Semina hiyo inashirikisha baadhi ya makamishna wa CAF walioko kwenye orodha ya makamishna ya shirikisho hilo kwa mwaka 2012-2014.

Rwiza ni mmoja wa makamishna wa CAF kutoka Tanzania, na mechi ya mwisho kusimamia ilikuwa ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa Mei mwaka huu nchini  Msumbiji.

CAF tayari imeshamtumia tiketi Rwiza, na anatarajia kuondoka nchini Julai 4 mwaka huu kwenda Cairo kwa ndege ya EgyptAir.

Mbunge CHADEMA, Mr Sugu atapata ajali akielekea Arusha

Mbuinge wa Mbeya Mjini-CHADEMA, Mhe. Joseph Mbilinyi 'Sugu'
Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi amepata ajali hivi punde katika eneo la kasheki wilayani Hanan'g akielekea Arusha mjini.

Joseph Mbilinyi maarufu Sugu alikuwa akielekea Arusha mjini kuungana na wabunge wengine ktk shughuli ya kuaga marehemu
waliolipukiwa na bomu kwenye mkutano wa Chadema, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika ajali hiyo hakuna mtu yoyote amejeruhiwa, Mbunge huyo yuko salama, gari la Sugu limeharibiwa vibaya baada ya kugongana na basi la abiria.

Kichanga chatafunwa na mbwa baada ya kutupwa kichakani

mbwa kama huyu amemtafuna kitoto kichanga
MTOTO mchanga ameliwa na mbwa na  kubakishwa mguu, baada ya mtu asiyejulikana kukitelekeza kichakani katika eneo la Magole, mtaa wa Kivule, Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.Tukio hilo la kusikitisha limebainika baada ya mbwa huyo kukibeba kiungo hicho kutoka kilipokuwa na kukifikisha nyumbani anakofugwa majira ya sita mchana juzi.
Mwenye mbwa huyo aliyejitambulisha kwa jina la Maria John, aliiambia NIPASHE kuwa, kabla ya kupelekwa mguu huo, jana yake mbwa huyo alikwenda na utumbo ambao hata hivyo hakuna aliyekuwa  na hofu nao, kwani walidhani ni wa kuku.
 
“Niliona ni kitu cha kawaida tu, mbwa hutembelea maeneo mbalimbali labda ameokota mzoga wa kuku, lakini leo (juzi) nilipoona mguu nilistaajabu na kufahamu kuwa ni kiungo cha binadamu nilitoa taarifa kwa majirani na kupata msaada,” alisema.
 
Alisema lengo la kutoa taarifa kwa majirani zake ni ili waweze kujadiliana na  kutamfuta aliyefanya kitendo hicho cha kikatili kisha baadaye kutoa taarifa kwa mjumbe wa mtaa huo.
 
Mmoja wa majirani waliokusanyika kushuhudia tukio hilo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema hajawahi kushuhudia tukio kama hilo.
 
“Ni tukio la kushangaza na kusikitisha sana kwa mtu kukatisha maisha ya kiumbe kisicho na hatia,kwani huwezi kujua mungu alimpangia nini duniani, hivyo kwa kweli kama mama najisikia uchungu sana,” alisema.
 
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa eneo hilo, Grace Martin, alisema alipigiwa simu na mdogo wake kuwa, mbwa ameokota kiungo cha mtoto na  kutakiwa kurudi mtaani hapo haraka.
 
“Nilipofika nilihakikisha kuwa kweli ni mguu wa mtoto, niliamua kumpigia simu Mwenyekiti wa Mtaa kwa ajili ya msaada,”alisema.
 
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule,Joseph Gassaya alisema yeye alipojulishwa alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kituo cha Stakishari Ukonga nao baada ya muda mfupi walifika eneo la tukio.
 
Alisema askari walitoa amri ya kukizika kiungo hicho katika eneo hilo, huku Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wa kumsaka mama aliyefanya ukatili huo ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
 
Chanzo:Nipashe