STRIKA
USILIKOSE
Monday, July 19, 2010
Rage aupongeza uongozi mpya wa Yanga, amwagia sifa Nchunga
MWENYEKITI wa klabu ya soka ya Simba, Ismail Aden Rage, ameupongeza uongozi mpya wa watani zao Yanga na kumwagia sifa binafsi mwenyekiti mpya wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, akidai ni mchapakazi na muadilifu.
Akizungumza na Micharazo kwa njia ya simu kutoka Tabora, Rage alisema amefurahishwa mno na umakini wa wanachama wa Yanga wa kumchagua Nchunga na Davis Mosha kuwa viongozi wao kwa madai ni watu makini na watakayoiletea mabadiliko klabu yao.
Rage alisema binafsi anamfahamu Nchunga kutokana na kuwahi kufanya naye kazi na kumtaja kama kiongozi mchapakazi na muadilifu.
"Nawapongeza wana Yanga kwa umakini wao wa kumchagua Lloyd Nchunga kuwa mwenyekiti wao, namfahamu ni muadilifu na mchapakazi na naamini ataendeleza mauhusiano mema baina ya klabu zetu mbili za Simba na Yanga," alisema Rage.
Rage alisema Simba na Yanga ni watani wa jadi na sio maadui na hivyo kuingia madarakani kwa Nchunga na Davis Mosha pamoja wengine waliochagulia watalichukulia jambo hilo hivyo na kujenga umoja na mshikamano kwa lengo la kuendeleza soka la Tanzania.
Nchunga, alichaguliwa kuwa mwenyekiti baada ya kuwabwaga wagombea wenzake watatu, Abeid Abeid, Mbaraka Igangula na Edger Chibula, huku Francis Kifukwe akijiondoa wakati wa kujinadi, wakati Mosha alishinda umakamu mwenyekiti kwa kumshinda Constatine Maligo,.
Uchaguzi huo wa Yanga ulifanyika juzi kwenye uwanja wa PTA, Sabasaba Dar es Salaam, ambapo wagombea wengine nane kati ya 28 akiwemo Ally Mayay walichaguliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.
M
Rage achukua na kurudisha fomu Tabora Mjini
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Tabora, Ismail Aden Rage, mapema leo asubuhi amekuwa mtu wa kwanza kuchukua na kurudisha fomu ya kuwania Ubunge wa Jimbo la Tabora Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi.
Akizungumza kwa simu kutoka Tabora, Rage, alisema alichukua fomu hiyo ya kuwania kiti hicho kinachoshikiliwa na Juma Siraju Kaboyoga majira ya saa 2;55 asubuhi na kuijaza kabla ya kuirudisha saa 5:30.
Rage alisema kuwa alikuwa ni mtu wa kwanza kujitokeza kuchukua fomu hiyo na pia amekuwa wa kwanza kuirudisha na matumaini yake ni kuibuka mshindi katika uteuzi wa CCM ili aweze kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31.
"Nimekuwa mtu wa kwanza kuchukua na kurudisha fomu ya kuwania Ubunge Jimbo la Tabora Mjini, nikichukua muda wa saa tatu kuchukua na kurudisha fomu hiyo na tumaini langu kama ilivyokuwa uchaguzi wa mwaka 2000, naamini nitashinda," alisema Rage.
Katika uchaguzi huo wa mwaka 2000, Rage aliwania uteuzi wa CCM katika jimbo hilo na kuibuka na ushindi wa kishindo, lakini utaratibu wa chama chake uliliengua jina lake na kumpitisha aliyekuwa mshindi wa pili, Henry Mgombelo aliyekuja kuibuka mshindi wa kiti hicho.
Rage alisema ni yake ya kujitosa katika jimbo hilo ni kuipeperusha bendera ya CCM dhidi ya wapinzani na pia kutaka ridhaa ya wananchi ili awatumikie kama ambavyo amekuwa akijitolea kwa hali na mali kwao hata kabla ya kuwa mbunge.
Alisema kwa vile katiba ya nchi na demokrasia ndani ya chama chake inamruhusu yeyote kuwania uongozi naye haoni sababu ya kujiweka nyuma na haswa kusukumwa kwake na nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo.
Rage aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Wazazi-Tabora mwaka 2004 na kukitetea kjiti chake tena mwaka jana, alisema anaamini chama chake kitampa ridhaa ya kuongoza na wananchi wa Tabora Mjini hawatamuangusha Oktoba mwaka huu.
Mtetezi wa kiti hicho cha Ubunge wa Jimbo la Tabora, Juma Kaboyoga, ndiye aliyekuwa mtu wa pili kuchukua fomu majira ya saa 5:40, ingawa haikufahamika kama aliwahi kurejesha au la.
Mwisho
Wawili waiacha bendi ya Kalunde
Wanamuziki wawili wa bendi ya Kalunde ambayo iko chini ya ukurugenzi wa Deo Mwanambilimbi, wameondoka kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kufanya shughuli za muziki
Akizungumza na Micharazo, mkurugeni huyo aliwataja wanamuziki hao kuwa ni mwimbaji Sarafina Mshindo aliyetimikia Marekani na Bonny Kamplobo (solo) ambaye amekwenda Thailand.
Mwanambilimbi alisema wanamuziki hao wameondoka baada ya kupata baraka za uongozi wa bendi na kwamba watakapomaliza mikataba yao huko waliko watarudi kuendelea kazi katika bendi hiyo.
"Sarafina anaweza kukaa Marekani kwa muda mrefu, kutokana na mkataba alioupata, lakini Kamplobo
atarudi baada ya mwezi mmoja ujao kwani atakuwa anamaliza mkataba," alisema Mwanambilimbi.
Aliongeza kuwa Kamplobo amechukuliwa na Kanku Kelly ambaye kwa sasa wanafanya naye kazi ya muziki huko Thailand na kwamba ana uhakika mkataba ukiisha atarudi Kalunde.
Alifafanua kuwa wanamuziki hao wameondoka wakati bendi hiyo ikikamilisha albamu ya kwanza ya
'Hilda' ambayo baadhi ya nyimbo zake ni 'Itumbangwewe', 'Fikiria' na 'Umenigusa Nikakugusa'.
"Hii ndio albamu ya kwanza ya bendi ya Kalunde ingawa watu wengi huwa wanadhani kwamba Uchona ni albamu ya bendi, lakini ukweli ni kwamba bendi ilianzishwa wakati albamu hii ipo tayari mitaani," alisema.
Mwanambilimbi alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo ambazo pia zimesaidia kuiweka juu bendi hiyo kuwa ni 'Siwezi Sema', 'Mwana Mpotevu', 'Chekacheka', 'Masikitiko' na 'Anitha'.
Bendi hiyo imekuwa ikitoa burudani kila Ijumaa katika ukumbi wa New Africa Hotel na kisha humalizia shughuli za burudani Jumapili, katika ukumbi wa Giraffe Ocean View, Mbezi Beach.
Pentagon, Shikito hawarudi Levent
WAIMBAJI wawili nyota wa bendi ya Extra Bongo 'Next Level', Athanas Thomas 'Shikito' na Ramadhan Mhoza 'Pentagon', wamesema kuwa hawana mpango wa kurejea katika bendi yao ya zamani.
Kabla ya kujiunga na Extra Bongo, waimbaji hao walikuwa kwenye bendi ya Levet Musica ya mjini Morogoro ambayo mwenzao Suzuki waliyekuwa naye Extra Bongo ameamua kurejea Levent.
Waimbaji hao wamemwambia mkurugenzi wao Ally Choki kuwa hawawezi kurudi Levent kwa sababu wana imani na uongozi wa Extra Bongo na hamu ya kuona mchango wao unasaidia bendi hiyo kusonga mbele.
Kauli ya waimbaji hao vijana imekuja wakati Extra Bongo leo ikitarajiwa kutua mjiji Morogoro kwa ajili ya onyesho moja linalofanyika katika ukumbi wa Savoy mjini humo.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam, 'Pentagon' na 'Shikito' walisema kuwa sasa hawaoni kama kuna sababu ya wao kurudi tena Levent wakati mambo ndani ya Extra Bongo yakianza kunoga.
"Wakati mwingine kuhama kutoka bendi moja hadi nyingine ni kunamnyima mwanamuziki uzoefu, mimi na mwenzangu tumeamua kubaki Extra Bongo hadi kieleweke," alisema 'Shikito'.
Kwa upande wake 'Pentagon' alisema uongozi wa Extra Bongo hauna sababu ya kuwa na shaka juu yao kwamba huenda wakabaki Morogoro baada ya onyesho lao la leo.
Akizungumzia kauli hiyo, Ally Choki alisema yeye na viongozi wenzake wameipokea kwa moyo mkunjufu akisema kuwa safari ya mafanikio daima haikosi vikwazo wakati mwingine vya kuvunja moyo.
"Kwa kweli ni kauli ya kutia moyo, mimi pia nawaamini na kuwategemea sana wanamuziki wangu, natamani tuwe pamoja daima ili tufanikiwe kuivusha na kuifikisha mbali bendi yetu," alisema.
Kabla ya kujiunga na Extra Bongo, waimbaji hao walikuwa kwenye bendi ya Levet Musica ya mjini Morogoro ambayo mwenzao Suzuki waliyekuwa naye Extra Bongo ameamua kurejea Levent.
Waimbaji hao wamemwambia mkurugenzi wao Ally Choki kuwa hawawezi kurudi Levent kwa sababu wana imani na uongozi wa Extra Bongo na hamu ya kuona mchango wao unasaidia bendi hiyo kusonga mbele.
Kauli ya waimbaji hao vijana imekuja wakati Extra Bongo leo ikitarajiwa kutua mjiji Morogoro kwa ajili ya onyesho moja linalofanyika katika ukumbi wa Savoy mjini humo.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam, 'Pentagon' na 'Shikito' walisema kuwa sasa hawaoni kama kuna sababu ya wao kurudi tena Levent wakati mambo ndani ya Extra Bongo yakianza kunoga.
"Wakati mwingine kuhama kutoka bendi moja hadi nyingine ni kunamnyima mwanamuziki uzoefu, mimi na mwenzangu tumeamua kubaki Extra Bongo hadi kieleweke," alisema 'Shikito'.
Kwa upande wake 'Pentagon' alisema uongozi wa Extra Bongo hauna sababu ya kuwa na shaka juu yao kwamba huenda wakabaki Morogoro baada ya onyesho lao la leo.
Akizungumzia kauli hiyo, Ally Choki alisema yeye na viongozi wenzake wameipokea kwa moyo mkunjufu akisema kuwa safari ya mafanikio daima haikosi vikwazo wakati mwingine vya kuvunja moyo.
"Kwa kweli ni kauli ya kutia moyo, mimi pia nawaamini na kuwategemea sana wanamuziki wangu, natamani tuwe pamoja daima ili tufanikiwe kuivusha na kuifikisha mbali bendi yetu," alisema.
Dady, J-Mupa wote pamoja
WASANII wanaokuja juu kwenye muziki wa kizazi kipya ambao kila mmoja anatamba na kibao chake, Leonard Fidelis 'Dady' na Juma Mussa 'J-Mupa' wanajiandaa kutoa albamu ya pamoja ya nyimbo 16.
Wakizungumza na Micharazo, wasanii hao, walisema albamu hiyo ya pamoja itakuwa na mchanganyiko wa miondoko tofauti ya R&B, Ragga na Hip Hop.
Dady anayetamba na kibao cha 'Ni Gani', alisema ana uhakika hiyo ya pamoja itawaweka kwenye matawi ya juu, kutokana na ukweli kwamba muda mrefu wamekuwa wakijitahidi kutoka bila mafanikio.
Lakini sasa wameangukia mikononi mwa meneja wao mpya waliyemtaja kwa jina la Nassa na kwamba wana imani atasaidia kuhakikisha wanatoka upya na tena kwa kishindo.
"Baada ya kusota kitambo, hatimaye nimeachia kazi mpya iitwayo Ni Gani, huku nikiwa katika maandalizi ya kutoa albamu pamoja na mshirika wangu, J-Mupa, tutakayeshea nyimbo 16," alisema.
Dady alisema baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ya pamoja ni kibao chao cha pamoja walichokitoa mwaka 2006 cha 'Uvumilivu', 'Upungufu', 'Inatosha', 'Rudi', 'Ni Gani', 'Namsaka' na nyinginezo.
Kwa upande wake J Mupa, anayetamba na 'Mzuri Yupi', alisema albamu yao hiyo huenda ikaleta mapinduzi kutokana na jinsi wanavyoumiza kichwa kuiandaa.
"Ni albamu bab' kubwa muhimu ni wapenzi na mashabiki kutupa sapoti ya kutosha ili tufanikiwe kutoka na kuwapa burudani murua," alisema J-Mupa ambaye pia hujihusisha na masuala ya filamu.
Diamond yaja na Power 2010
Diamond Musica yaja na Power 2010
BENDI ya Diamond Musica 'Vijana Classic', imeachana na mipango ya maandalizi ya kuzindua albamu ya pili ya 'Mapenzi Kitu Gani', badala yake sasa imeelekeza nguvu katika kuandaa albamu ya tatu.
Mkurugenzi msaidizi wa bendi hiyo Perfect Kagisa, ameliambia Micharazo Mitupu kuwa kwa vile nyimbo zao albamu ya pili zilishasikika sana redioni, kwenye televisheni na katika kumbi mbalimbali, haina haja kuizindua.
"Tumeamua kuandaa albamu nyingine kwa sababu pia bendi yetu ilifanya mabadiliko kwa kuleta wanamuziki wapya, ndipo tukaona kuwa tuanze pia na vitu vipya," alisema Kagisa.
Kagisa alizitaja baadhi ya nyimbo ambazo bendi hiyo imezikamilisha kwa ajili ya albamu ya tatu kuwa ni 'Power 2010', 'Kovu', 'Supu ya Kongolo' na 'Abdulkarim'.
Alisema wanamuziki wa bendi hiyo wanajiandaa kushuti video ya wimbo wa 'Power 2010' na kwamba kazi hiyo ya kushuti itafanyika wiki ijayo ili uanze kurushwa kwenye vituo mbalimbali vya televisheni.
"Hii intro ya Diamond Musica, ndio maana tumeamua kuanza nayo na kisha nyimbo nyingine zitafuata katika mpangilio wetu wa kurekodi nyimbo za albamu ya tatu," alisema.
Diamond Musica ilitua jijini Dar es Salaam zaidi ya miaka mitatu iliyopita ikitokea Zimbabwe ikiwa na albamu ya kwanza iliyopewa jina la 'Swali' ambayo hata hivyo, haikuitambulisha vyema bendi hiyo.
Baada ya hapo wanamuziki walikuna vichwa na kuibuka na albamu ya pili ya 'Mapenzi Kitu Gani' na kuifanya uanze kukwea matawi ya juu, lakini hadi sasa albamu hiyo haijazinduliwa.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo alisema kuwa licha ya kuandaa albamu nyingine, zile za albamu ya pili zitaendelea kupigwa kwenye kumbi za burudani na kuuzwa madukani kama kawaida.
Ndumbaro bado alia na Boban
WAKALA wa kimataifa wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, Damas Ndumbaro, amezidi kulia na kiungo Harun Moshi 'Boban' akidai mchezaji huyo ana desturi ya kutoheshimu mikataba kama alivyofanya kwa kuitosa klabu ya GIF ya Sweden.
Akihojiwa na kituo kimoja cha redio, Ndumbaro alisema pamoja na Boban kujitetea kuwa kilichomkimbiza Sweden ni kukiukwa kwa mkataba baina yake na klabu hiyo, lakini ukweli ni kwamba inaonekana suala la kutoheshimu ni kawaida ya kiungo huyo mahiri.
Ndumbaro alisema kwa kumbukumbu zake kutaka kuvunja mkataba dhidi ya GIF ni mara ya tatu kwa Boban, kwani alishawahi kufanya hivyo pia alipoenda kucheza soka la kulipwa Arabuni na pia Ethiopia.
"Hili sio jambo la bahati mbaya ni wazi ni Boban ana kawaida ya kutoheshimu mikataba kwani alishawahi kuvunja alipoenda Arabuni na kuiponza klabu yake ya Simba kulipa gharama za huvunjwaji huo wa mkataba huo, pia alifanya hivyo alipokuwa Ethiopia," alisema Ndumbaro.
Wakala huyo alisema dai kwamba labda Boban hakuuelewa mkataba huo wa miaka miwili si sahihi kwa vile alisimamiwa na mwakilishi wa Academy yake anayezungumza kiswahili na ndipo aliposaini na kuanza kuitumia klabu hiyo.
Ndumbaro alisema pengine yale mazoea na kuwakosa 'washkaji' zake wa vijiweni kama anavyokuwa nchini ndio kilichochangia kiungo huyo kurejea nchini ghafla, ingawa Boban alinukuliwa akisema kuwa malipo kiduchu ndicho kilichomrejesha Bongo.
Mwisho
Boban awagawa wadau wa soka nchini
UAMUZI wa kiungo nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Harun Moshi 'Boban' kuamua kurejea nchini kwa kuvunja mkataba na klabu yake ya GIF ya Sweden umewagawa wapenzi na wadau wa soka nchini baadhi wakimuunga mkono wengine wakimshangaa.
Baadhi ya wadau wamedai kitendo cha Boban kurejea ghafla nchini na kuiacha timu yake ya GIF ni kuonyesha jinsi wachezaji wa Kitanzania wavumilivu au kuwa tayari kucheza soka la kulipwa kama wenzao wa mataifa mengine.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya fedha ya klabu ya Simba Onesmo Wazir 'Ticotico'alisema hata kama kulikuwa na matatizo yaliyomkera Boban alipaswa kuzungumza na wakala wake kuona namna ya kutatua ikiwemo kuhamishwa klabu nyingine ya nje kuliko kurejea nchini.
"Unajua nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje huja kwa nadra sana na ilipaswa Boban kutumia nafasi hiyo kuangalia mbele katika kipaji chake badala ya kukimbilia kurejea nchini ili kuendelea kuchedza soka la sifa kwa klabu za Simba na Yanga," Ticotico alisema.
Hata hivyo Kocha Mkuu wa timu ya TMK United, Kennedy Mwaisabula, alisema binafsi haoni sababu ya Boban kulaumiwa, iwapo hakuona faida ya kuendelea kucheza soka la kulipwa katika klabu hiyo ya Sweden kutokana na kuonyesha hakuufahamu vema mkataba wake.
Mwaisabula alisema huenda wakala wake, Damas Ndumbaro hakuwa muwazi kwa kiungo huyo na yeye alipoona mambo yapo ovyo hakuona sababu ya kuendelea kuwepo huko, huku akisema uamuzi wa kurejea nchini kucheza soka sio wa ajabu kwani ni suala lake binafsi.
"Sioni sababu ya kumshutumu na kumdhalilisha Boban, kurudi kwake ni sahihi na hasa baada ya kukaa nae kwa saa zima na kuzungumza nae akieleza kila kitu na sio kweli kama kaikimbia baridi au kuwakumbuka washkaji zake," alisema Mwaisabula.
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Yanga na Bandari Mtwara, alisema huenda Boban ameona soka la Bongo linalipa kuliko huko Sweden kwani kabla hajaenda huko tayari alishakuwa na uwezo wa kiuchumi akimiliki nyumba na gari la kisasa.
Mwaisabula alisema pia Boban hatakuwa mchezaji wa kwanza kucheza soka la nyumbani badala ya nje ya nchi akiwataja, Tresot Mputu wa DR Congo, Mohammed Abutrika wa Misri aliodai pamoja na uwezo wa kisoka hawajahi kuwaza au kwenda kucheza soka la kulipwa licha ya kuwindwa na klabu mbalimbali maarufu za Ulaya.
Mwisho
Njoroge apigiwa ramli Jangwani
HATMA na uwepo wa beki wa kimataifa wa Yanga, Mkenya John Njoroge ndani ya klabu hiyo bado haieleweki, kutokana na uongozi wa klabu hiyo kudai unasubiri maamuzi ya kocha wao, Kostadin Papic
Njoroge aliyetua Yanga akitokea Tusker ya Kenya, kwenye usajili wa dirisha dogo msimu uliopita, amekuwa akitajwa ataachwa ili kutoa nafasi ya kusajiliwa kwa kipa Mserbia, Ivan Knezevic kutekeleza kanuni mpya ya usajili inayosisitizwa na Shirikisho la Soka nchini, TFF.
Kanuni hiyo ya usajili inaelekeza klabu zote za ligi kuu kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi watano, kitu ambacho ndicho kinachomchanganya kocha wa Yanga, kuamua nani abaki na nani aondoke klabuni hapo.
Msemaji wa Yanga, Louis Sendeu aliliambia Micharazo kuwa, pamoja na kwamba usajili wao unaelekea kukamilika vema, lakini hadi sasa haijafahamika nani na nani katika wachezaji wageni watakaokuwa kwenye kikosi hicho hadi kocha wao atakapoamua.
Sendeu alisema kutokana na hilo, ndio maana inakuwa vigumu kwao kuweka bayana kama itamuacha Njoroge au la ambaye ilielezwa awali angeungana na mastaa wengine wa kigeni waliotupiwa virago katika timu hiyo.
"Aisee ni vigumu kuweka bayana juu ya hatma ya Njoroge, tunasubiri suala hilo liamuliwe na kocha na nasisitiza kuwa lolote linaweza kutokea katika usajili huo mpya wa timu yetu ambao utatangazwa wakati wowote kuanzia sasa baada ya kukamilika," alisema Sendeu.
Tayari uongozi wa Yanga umejinasibu kuwasainisha wachezaji wanne kutoka Ghana, kipa Yew Berko, mlinzi, Isaac Bokye, kiungo Ernest Boake na mshambuliaji Kenneth Asamoah, huku ikidaiwa kukaribia kumalizana na kipa Knezevic aliyetua wiki iliyopita kwa majaribio.
Iwapo kipa huyo atasajiliwa ili kuziba nafasi ya Obren Curcovic basi ni lazima kati ya Waghana wanne au Njoroge, mgeni pekee aliyebakishwa kikosi kilichopita mmojawao jina lake likatwe.
Yanga inayoendelea na mazoezi yao katika uwanja wa Uhuru, imedaiwa tayari imewanasa Nsa Job, Yahya Tumbo, George Minja, Chacha Marwa, Stephano Mwasika, Omega Sunday na Salum Telela kwa ajili ya kikosi kipya kuungana na nyota wengine walisalia msimu uliopita.
Mwisho
Diamond kutangaza utalii wa ndani
MSHINDI wa tuzo tatu za muziki nchini na Balozi wa Malaria, Naseeb Abdul 'Diamond' ameingia makubaliano ya mwaka mmoja na waandaaji wa shindano la Miss Utalii Tanzania kwa nia ya kuhamasisha utalii wa ndani sambamba na kuendelezxa vita dhidi ya malaria.
Habari zilizopatikana jijini na kuthibitishwa na Rais wa Miss Utalii, Gideon Chipungahelo, zinasema lengo la kamati hiyo kumshirikisha Diamond ni kuunganisha nguvu za sanaa ya muziki na urembo wa kitalii katika kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza sekta ya utalii na utamaduni pia vita dhidi ya ugonjwa hatari wa malaria nchini na Africa kwa jumla.
Katika makubaliano ya awali kati ya wawili hao ni kwamba Diamond atafanya ziara ndefu maalum ya uhamasishaji itakayofahamika kwa jina la Diamond Tanzania Kamwambie Tour-Malaria Inaua Utalii ni Maisha'.
Pia msanii huyo aliyengara kwenye tuzo za Kilimanjaro Music Awards-2010, atatunga kibao maalum kwa ajili ya Miss Utalii Tanzania 2010 ambao ataimba na kurekodi pamoja na warembo wote wa Miss Utalii Tanzania wanaoshiriki fainali za mwaka 2010.
Kibao hicho ndicho kitakachotumika katika fainali za shindano hilo zitakazofanyika Septemba mwaka huu kwa kushirikisha jumla ya warembo 60 toka kanda na mikoa mbalimbali.
Washindi wa fainali hizo za Taifa watawakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya Dunia na ya kimataifa 2010 na 2011 yakiwemo ya Miss Heritage World 2011,Miss Tourism University World 2011,Miss Globe International 2010,Miss United Nation 2010,Miss Tourism World 2010 na Miss University africa 2011.
Rais wa Miss Utalii alithibitisha kuwepo kwa makubaliano hayo na Diamond, ingawa msanii huyo mwenyewe hakuweza kupatikana kufafanua juu ya suala hilo.
Mwisho
Mabingwa Ngumi EA kusakwa wiki ijayo
TIMU mbili za taifa za mchezo wa ngumi wa ridhaa zinatarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya ngumi ya Mabingwa wa Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati itakayofanyika jijini Arusha kuanzia Julai 26 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Mashanga Makore, alisema, Tanzania kama mwenyeji wa michuano hiyo itawakilishwa na timu mbili zilizopewa majina ya Tanzania A na B zitakazokuwa na wachezaji karibu 39.
Makore alisema timu ya taifa A itakuwa na wachezaji 19 wakati ile ya pili yaani Taifa B itakuwa na mabondia 20.
"Kutokana na uwenyeji wetu wa michuano ya ngumi ya Mabingwa wa Mabingwa wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, tunatarajiwa kuwakilishwa na timu mbili na tayari timu hizo zimeshaanza mazoezi tangu wiki iliyopiuta kujiandaa na michuano hiyo," alisema Makore.
Makore alisema mazoezi ya timu hizo yanaendelea chini ya makocha wazawa, ambao wanawasiliana kila mara na kocha mkuu wa timu hizo, Mcuba Geovanis Hultado ambaye yupo mapumziko nchini kwao.
Katibu huyo alisema imani ya BFT ni kuona Tanzania inafanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, ikizingatiwa kuwa wao ni wenyeji na pia itawakilishwa na timu nyingi tofauti na wapinzani wao.
Kuhusu maandalizi ya michuano hiyo, Makore alisema yanaendelea vema ikiwemo timu zote tano za Afika Mashariki kuthibitisha ambazo ni wenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Mwisho
Nukuu kali za kukumbukwa Kombe la Dunia 2010
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
MAKOCHA na wachezaji wamekuwa wakizungumzwa mara kwa mara, si kwa sababu ya viwango vyao uwanjani pekee, bali pia kwa sababu ya kauli zao za nje ya uwanja. Zifuatazo ni nukuu kali za kukumbukwa zilizowahi kutolewa nao wakati wa michuano ya mwezi mmoja ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.
Milovan Rajevac
* "Nyie watu, hebu tumieni akili. Yeye si shujaa, yeye ni muongo mkubwa. Ni mkono gani wa Mungu? Ule ni mkono wa shetani," kocha wa Ghana, Mserbia Milovan Rajevac, alisema kuhusy mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez, ambaye alizuia kwa mikono mpira uliokuwa ukivuka mstari wa goli katika dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza kwenye mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Dunia.
‘Mkono wa shetani’ wa Suarez uliinyima Ghana nafasi ya kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kufuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Patrice Evra
* "Tunajihisi kama taifa dogo la mchezo wa soka na hili linaumiza. Hakuna cha kuelezea zaidi ya kusema kwamba hili ni balaa," nahodha wa Ufaransa, Patrice Evra, akielezea kwa uwazi hitimisho la kiwango chao kibovu katika fainali zilizomalizika za Kombe la Dunia 2010. Ufaransa, sio tu ilimaliza ikiwa mkiani katika kundi ambalo ilitarajiwa kuwa kinaea, lakini pia ilikumbwa na kashfa ya wachezaji wake kugomea mazoezi kufuatia kutimuliwa kikosini kwa mshambuliaji Nicolas Anelka.
Jean-Louis Valentin
* "Hawataki kufanya mazoezi, ni kashfa. Najiuzulu, naachoa ngazi kwenye shirikisho. Hapa sina zaidi cha kufanya. Narudi zangu Paris," Mkurugenzi wa timu ya Ufaransa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Soka la Ufaransa, Jean-Louis Valentin, alisema baada ya wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa kugomea mazoezi kufuatia kutimuliwa kikosini kwa Anelka.
Diego Maradona
* "Hii ilikuwa ni (kama) ngumi kutoka kwa Muhammad Ali. Sikuwa na nguvu yoyote ile. Siku niliyostaafu soka ingeweza kufanana na hii, lakini hii ya leo ni mbaya zaidi," Maradona alisema baada ya Argentina kupata kipigo kikali cha 4-0 kutoka kwa Ujerumani, kipigo kibaya zaidi kwao katika fainali za Kombe la Dunia tangu waliposhindiliwa kwa magoli 6-1 katika mechi ya michuano hiyo dhidi ya Czechoslovakia mwaka 1958.
Dunga
* "Siku zote tunatakiwa kushinda, lakini hata tunaposhinda, hawatufurahii kwa madai kwamba hatuchezi soka la kuvutia. Tukicheza soka la kuvutia, hawafurahi kwa sababu hatushindi kwa magoli mengi kama sita au saba hivi. Tukishinda kwa magoli sita au saba, wanaibuka tena na kusema wapinzani wetu ni dhaifu," alisema kocha wa Brazil, Dunga, akidai kwamba hata siku moja, vyombo vya habari huwa haviridhiki.
Gennaro Gattuso
* "Miaka minne iliyopita tuliheshimiwa kwa kuwa mabingwa, leo hii tunacheza hovyo kama mabeberu ya mbuzi vile," kiungo wa Italia, Gennaro Gattuso, alisema katika tathmini isiyo ya kawaida ya kujishutumu binafsi kwa kiwango cha hivyo kiichoonyeshwa na timu yao iliyokuwa ikitetea ubingwa wa fainali za Kombe la Dunia na kumaliza ikiwa mkiani katika Kundi lao.
Howard Webb
* "Anashindwa hata kuwaongoza watoto wake mwenyewe. Sijui anamudu vipi jukumu la kuongoza mchezo wa soka uwanjani," mke wa refa aliyechezesha mechi ya fainali ya Kombe la Dunia, Howard Webb, alisema kabla ya mechi hiyo ya fainali iliyozikutanisha timu za mataifa ya Hispania na Uholanzi.
Cristiano Ronaldo
* "Maholi, kama gwiji mmoja wa soka alivyowahi kuniambia, huwa yanafuatana ... wakati mwingine, kadri unavyojaribu kuhaha ili ufunge, hayaji, na wakati yanapokuja, yanakuja mengi kwa wakati mmoja," alisema mchezaji wa bei mbaya zaidi duniani, Cristiano Ronaldo wa Ureno, kuelekea mechi yao ufunguzi ya hatua ya makundi ya Kombe la Dunia. Kiwango cha Ronaldo katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia kilikuwa cha hovyo, huku mshambuliaji huyo akifunga goli moja pekee.
Roger Milla
* "Kwa hakika hakuna anayeweza kucheza kama mimi! Mauno yangu yalikuwa ya kwanza, tena ya ubunifu kabisa. Unahitaji kunengua kiasili, kuchezesha nyonga. Yote ni kuhusiana na uasili wa mguso binafsi, na inatakiwa uwe na mshawasha kutoka moyoni, iwe ni kitu chako mwenyewe. Na hakika, vilevile unapaswa kufunga goli kwanza, usisahau jambo hilo!" alisema Roger Milla kuhusiana na ushangiliaji wake wa goli kwa kukata viuno.
Mauno ya Milla kwenye kibendera cha kona kila mara alipofunga goli yalikuwa maarufu kama magoli yake aliyoifungia Cameroon wakati nchi hiyo ilipotinga robo fainali za Kombe la Dunia mwaka 1990.
England v Ujerumani
* "England walianzisha soka, lakini Ujerumani wanashinda soka", ulisema utani wa zamani uliotumika wakati wa fainali za Kombe la Dunia kuelezea ushindi wa kishindo wa Ujerumani wa 4-1 dhidi ya mahasimu wao wa jadi katika hatua ya 16-Bora ya Kombe la Dunia.
Sepp Blatter
"Itakuwa ni upuuzi kutolifungua tena jalada la mapendekezo ya kutaka kutumiwa kwa teknolojia ya goli," alisema Rais wa FIFA, Sepp Blatter, baada ya makosa ya marefa kuwagharimu England na Mexico.
Felipe Melo
* "Mimi ni mzoefu wa kupenda. Watu wanaweza kufikiri kuwa kuwa nina sura mbaya, lakini ninapenda kutuma kadi na maua kwa mke wangu na ninapenda pia kutumiwa," beki mpambanaji wa Brazil, Felipe Melo, akisema kuwa yeye si mtu mbaya ‘kiivyo’.
Oscar Tabarez
* "Soka ni kama blanketi fupi, ama litatosha kukufunika kichwani au miguuni," kocha wa Uruguay, Oscar Tabarez, alisema kuhusiana na udhaifu wa mabeki wa Korea Kusini kabla ya mechi yao ya hatua ya mtoano ambayo Uruguay walishinda dhidi ya Waasia hao.
Carlos Marchena
* "Sawa, ni pweza," alisema beki wa Hispania, Carlos Marchena, katika muonekano wa kukasirika wakati alipotakiwa kuelezea maoni yake kuhusiana na utabiri wa pweza uliodai kwamba Hispania watashinda katika mechi yao ya fainali dhidi ya Uholanzi. Pweza huyo maarufu alitabiri kwa usahihi matokeo ya mechi zote saba za Ujerumani wakati wa fainali za Kombe la Dunia.
Felipe Melo
* "Najua kwamba wakati mwingine huwa napitiliza. Ni jambo ambalo huwa nalifikiria muda wote na ninajua kwamba hili ni jambo linalohofiwa na Wabrazili wote. Baba yangu siku zote amekuwa akinisisitiza kuhusu jambo hili, haachi kunikumbusha," alisema kiungo wa Brazili, Felipe Melo, kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia, kuhusiana na umuhimu wa yeye kuepuka kadi nyekundu. Hata hivyo, alitolewa uwanjani katika mechi yao ya robo fainali dhidi ya Uholanzi kwa kumkanyaga mpinzani wake.
Dunga
* "Wakati wakionyesha vipande vya picha za video za fainali za mwaka 1970, unachoona ni sehemu nzuri tu. Kuanzia mwaka mwaka 1958, wanaonyesha vipande vya sehemu nzuri tu, na kuanzia mwaka 1962, pia wanaonyesha vipande vya sehemu nzuri tu. Kama tukichukua vilevile vipande vya sehemu nzuri tu za timu ya Brazil ya sasa, mashabiki wataamini kwamba ndio timu bora kabisa. Lakini leo hii, wanaonyesha vipande vingi vya picha za matukio mabaya kama ilivyo kwa matukio mazuri." Dunga akilalamikia kumbukumbu za timu ya Brazil ya mwaka 1970 na kudai kwamba haikuwa timu nmzuri sana kama inavyoonyeshwa kwenye televisheni.
Marcelo Bielsa
* "Wote tunajifunza kutokana na makosa tunayofanya na kutoka kwenye makosa tuliyoyashuhudia yakifanywa na watu wengine, na kujaribu kuepuka kuyarudia. Huu ni mchakato wa kufanya makosa na kuepuka kuyarudia tena, kuona namna wengine wanavyofanya makosa ili kuyaepuka makosa kama hayo, ni mchakato ambao hausimami, na hauwezi kupimika." kocha asiyetabirika wa Chile, Marcelo Bielsa, akizungumzia umuhimu wa kujifunza kutokana na makosa.
--------------
Diego Forlan: Shujaa wa Uruguay WOZA 2010
PENGINE maamuzi yake ya kuachana na mchezo wa tenisi alioupenda utotoni na kuucheza hadi akiwa na miaka 14 na kisha kufuata nyayo za baba na babu yake katika soka, hayakuwa ya kimakosa kutokana na mafanikio anayoyapata kwa sasa katika mchezo huo.
Forlan anayeichezea klabu ya Atletico Madrid ya Hispania na anayetajwa kama mmoja wa washambuliaji wanaotisha zaidi duniani, mbali na mafanikio mengi anayojivunia, kubwa ni kung'ara kwake katika fainali za Kombe la Dunia zilizomalizika wiki iliyopita nchini Afrika Kusini.
Katika fainali hizo za pili kwake, Forlan kwa juhudi binafsi, aliifikisha timu yake katika hatua ya nusu fainali ikiwa ni rekodi baada ya miaka 40 kupita tangu Uruguay, mabingwa wa kwanza wa michuano hiyo iliyoanzishwa mwaka 1930, kucheza nusu fainali kwa mara ya mwisho mwaka 1970.
Kuifikisha Uruguay hatua hiyo, kumemfanya Forlan aweke historia na kumfunika baba yake mzazi, Pablo Justo Forlan Lamarque, aliyekuwa akicheza kama beki aliyewahi kuiwakilisha nchini hiyo katika fainali mbili za Kombe la Dunia mwaka 1966 na 1974.
Amemfunika pia babu yake, Juan Carlos Corazo, aliyewahi kung'ara katika klabu ya Independiente ya Argentina na kuwahi kuinoa timu ya taifa ya Chile mwaka 1962.
Forlan aliibeba kwa kila hali Uruguay katika WOZA 2010, akicheza kwa kujituma na kuifungia mabao muhimu ambayo mwishowe yalimfanya kuwa miongoni mwa wafungaji bora wa michuano hiyo na kunyakua tuzo ya 'Adidas Golden Ball' ya Mchezaji Bora wa Kombe la Dunia 2010.
Nyota huyo alinyakua tuzo hiyo akiwazidi kete nyota wanne, Wesley Sneijder-Uholanzi, David Villa-Hispania, Thomas Muller Ujerumani na Gonzalo Higuain wa Argentina.
Kwa takwimu za waliopiga mashuti mengi langoni katika WOZA, Forlan aliyenyakua tuzo mbili tofauti za Mfungaji Bora Ligi ya Hispania na Ulaya kwa msimu ya 2004-2005 na 2008-2009, amelingana na Villa wakipiga mashuti 32 kila mmoja nyuma ya Asamoah Gyan wa Ghana aliyekuwa kinara.
Mafanikio ya Forlan aliyeanza kuichezea Uruguay tangu mwaka 2002, akifikisha jumla ya mechi 69 na kuifungia mabao 29, yamekuja katika michuano hiyo ya Dunia ikiwa ni miezi michache tangu alipotoka kuisaidia klabu ya Atletico Madrid kutwaa la ubingwa wa Ligi ya Europa, jina jipya la michuano ambayo ni maarufu zaidi nchini kama "UEFA ndogo".
Nyota huyo aliifungia mabao muhimu Atletico katika michuano hiyo mikubwa ya pili nyuma ya Ligi ya Mabingwa barani humo na kuifikisha fainali, ambako yeye mwenyewe "aliinyonga" Fulham ya England na kuipa ubingwa klabu hiyo ya Hispania.
FORLAN NI NANI?
Forlan ambaye majina yake kamili ni Diego Martin Forlan Corazo, alizaliwa Mei 19, 1979 mjini Montevideo, Uruguay na utotoni alipenda mno mchezo wa tenisi, ingawa pia alijihusisha na soka katika klabu za vijana za Penarol na Danubio za nchini mwake.
Inadaiwa alijikita zaidi katika soka baada ya ajali mbaya iliyompata dada yake Alejandra Forlan, iliyomfanya apooze mwili na kumpoteza mchumba wake na ndipo aliponyakuliwa na Independiete ya Argentina, ambapo alianza kwa kuchezea kikosi cha vijana kabla ya kupandishwa kwenye timu ya wakubwa mwaka 1998 hadi Januari 2002 aliposajiliwa na klabu ya Manchester United ya England kwa ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 6.9 (sawa na Sh. Bilioni 15.5).
Manchester ilimnyakua Forlan kwa lengo la kwenda kuziba nafasi ya Andy Cole, lakini ilimchukua miezi nane kufunga goli lake la kwanza katika klabu hiyo katika mechi ya ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Maccabi Haifa ya Israel katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kutokana na kushindwa kufanya vema katika misimu yake miwili ndani ya Old Trafford, aliotwaa nao taji la Ligi Kuu ya England 2002-2003, Kombe la FA 2003-2004 na Ngao ya Hisani 2003, Forlan aliuzwa kwa klabu ya Villarreal ya Hispania Agosti 21, 2004.
Kuondoka kwake Manchester kulitoa fursa kwa nyota wa sasa wa England, Wayne Rooney kutua akitokea klabu aliyolelewa ya Everton.
Katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya Hispania, Forlan alifunga magoli 25 na kuisaidia kuiingiza Villareal kwa mara ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku mwenyewe akinyakua tuzo ya Mfungaji Bora wa la Liga iitwayo 'Pichichi' na ile ya Mfungaji Bora wa Ulaya, akilingana na Thiery Henry (aliyekuwa Arsenal wakati huo).
Aliendelea kuipa mafanikio timu yake hiyo kabla ya mwaka 2007 kutua katika klabu ya Atletico Madrid ambapo aliifungia mabao 32 katika mechi 33 alizoichezea na kunyakua tena tuzo ya Pichichi na ile ya Ulaya kwa mara ya pili msimu wa 2008-2009.
Kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora wa Hispania na Ulaya akiwa na klabu mbili tofauti za La Liga, kulimfanya kuwa mchezaji wa kwanza tangu Ronaldo aliyefanya hivyo katika msimu wa mwaka 1996-97 akiwa na Barcelona, kisha 2003-2004 akiwa na kikosi cha Real Madrid.
Msimu uliopita mkali huyo alishika nafasi ya tano ya ufungaji mabao ya ligi ya Hispania akiwa na mabao mabao 18, akizidiwa mabao 16 na aliyekuwa kinara, Lionel Messi wa Barcelona.
Hata hivyo, ufungaji wake wa magoli muhimu uliibeba Atletico Madrid iliyonyakua ubingwa wa Ligi ya Europa baada ya kuilaza Fulham ya England, ikiwa ni baada ya kusaidia kuingoa Liverpool.
Kuhusu maisha yake binafsi, Forlan anayefahamika kama 'Cachavacha' na aliyemiliki mfuko maalum wa kusaidia wahanga wa ajali kama njia ya kumuenzi dada yake Alejandra Forlan, anaishi na mwanamtindo maarufu wa Argentina, Zaira Nara.
DONDOO MUHIMU
* Alisajili wa Atletico Madrid 2007 kwa ajili ya kuziba pengo la Fernando Torres, aliyehamia Liverpool.
* Alitwaa tuzo yake ya pili ya Kiatu cha Dhahabu kwa kuwa Mfungaji Bora wa Ulaya katika msimu wa 2008/09 kutokana na kuwa na magoli 32 ya ligi kuu, ambapo 12 kati ya hayo aliyafunga katika mechi nane za mwisho za msimu na kumpiku mshmabuliaji wa Barcelona kwa wakati huo, Samuel Eto'o.
* Alikuwa katika kiwango cha juu katika Ligi ya Europo msimu uliopita na kuisaidia Atletico kutwaa ubingwa wao wa kwanza Ulaya katika miaka 48.
* Alifunga magoli yote mawili ya Atletico katika ushindi wa 2-1 wa fainali ya Ligi ya Europa dhidi ya klabu ya Fulham mjini Hamburg.
Matumla adundwa na Maugo, astaafu ngumi
BINGWA wa zamani wa Dunia wa ngumi za kulipwa, Rashid Matumla 'Snake Boy' jana alipigwa kwa pointi na Mada Maugo na kutangaza kustaafu kuendelea kupigana na ulingoni na badala yake kugeukia kazi ya ukocha.
Pambano hilo lililoandaliwa na Oganizesheni ya Ngumi za Kulipwa nchini, TPBO, lilifanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba Dar es Salaam kwa nia ya kumaliza ubishi baina ya wawili hao waliokuwa wakitambiana kwa muda mrefu.
Matumla ambaye alishawahi kutangaza kuacha ngumi baada ya kupigwa kwa mara nyingine na Francis Cheka 'SMG', alishindwa kuhimili vishindo vya Maugo, ingawa alimudu hadi mwisho wa mchezo huo uliokuwa wa raundi 10 uzito wa kilo 72.
Mara baada ya kumalizika kwa pambano hilo lililotanguliwa na michezo kadshaa ya utangulizi, Snake Boy, alitangaza kuwa huo ndio mchezo wake wa mwisho kupanda ulingoni na kwamba anaamini 'ameshazeeka' na kusema atageukia ukocha ili kuwarithisha vijana ujuzi wake wa mchezo huo uliompa sifa kubwa ndani na nje ya nchi.
Kutokana na ushindi huo wa pointi, Mada Maugo sasa anaweza kupigana na Cheka, ambaye alishatangaza kama bondia huyo atashinda basi atakuwa radhi kupigana nae au la yeye (Cheka) atamtafuta Karama Nyalawila ili kumaliza ubishi baada ya wawili hao yaani Maugo na Nyalawila kutamba kuwa ndio pekee wanaoweza kumsimamisha Cheka.
Nchunga amrithi Madega Yanga, Mosha aula...!
MWANASHERIA, Lloyd Nchunga amefanikiwa kuibuka kidedea na kumrithi aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega katika kiti hicho baada ya kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu wa Yanga uliokesha ukifanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba, jijini Dar.
Nchunga, anayeendesha kampuni ya uwakili, aliibuka kidedea kwa kuwabwaga wagombea watatu aliokuwa anachuana nao baada ya Francis Kifukwe 'kuchomoa' mapema kwa kile alichodai kuwa kulikuwa na mizengwe ambayo anaamini ingemuangusha katika uchaguzi huo.
Mshindi huyo aliyekuwa akipewa nafasi kubwa katika uchaguzi huo na kuwa tishio la Kifukwe, aliwashinda Abeid Abeid 'Falcon', Edger Chibura na Mbaraka Igangula, ambaye huenda asiamini kama pamoja na kujitangaza kwa mabango barabarani bado kapigwa chini.
Kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti, nafasi iliyokuwa wazi kwa muda mrefu tangu kufariki kwa aliyekuwa akiishikilia, Marehemu Rashid Ngozoma Matunda, ilienda kwa mfanyabiashara maarufu wa mafuta, Davis Mosha aliyemuangusha Constatine Maligo.
Kura za nafasi nane za Wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo zilikuwa bado zikiendelea kuhesabiwa hadi muda huu, ingawa kuna baadhi ya waliokuwa wakipewa nafasio ya kuibuka kidedea kama Ally mayai Tembele, Mohammed Bhinda na wengine.
Subscribe to:
Posts (Atom)