WAIMBAJI wawili nyota wa bendi ya Extra Bongo 'Next Level', Athanas Thomas 'Shikito' na Ramadhan Mhoza 'Pentagon', wamesema kuwa hawana mpango wa kurejea katika bendi yao ya zamani.
Kabla ya kujiunga na Extra Bongo, waimbaji hao walikuwa kwenye bendi ya Levet Musica ya mjini Morogoro ambayo mwenzao Suzuki waliyekuwa naye Extra Bongo ameamua kurejea Levent.
Waimbaji hao wamemwambia mkurugenzi wao Ally Choki kuwa hawawezi kurudi Levent kwa sababu wana imani na uongozi wa Extra Bongo na hamu ya kuona mchango wao unasaidia bendi hiyo kusonga mbele.
Kauli ya waimbaji hao vijana imekuja wakati Extra Bongo leo ikitarajiwa kutua mjiji Morogoro kwa ajili ya onyesho moja linalofanyika katika ukumbi wa Savoy mjini humo.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam, 'Pentagon' na 'Shikito' walisema kuwa sasa hawaoni kama kuna sababu ya wao kurudi tena Levent wakati mambo ndani ya Extra Bongo yakianza kunoga.
"Wakati mwingine kuhama kutoka bendi moja hadi nyingine ni kunamnyima mwanamuziki uzoefu, mimi na mwenzangu tumeamua kubaki Extra Bongo hadi kieleweke," alisema 'Shikito'.
Kwa upande wake 'Pentagon' alisema uongozi wa Extra Bongo hauna sababu ya kuwa na shaka juu yao kwamba huenda wakabaki Morogoro baada ya onyesho lao la leo.
Akizungumzia kauli hiyo, Ally Choki alisema yeye na viongozi wenzake wameipokea kwa moyo mkunjufu akisema kuwa safari ya mafanikio daima haikosi vikwazo wakati mwingine vya kuvunja moyo.
"Kwa kweli ni kauli ya kutia moyo, mimi pia nawaamini na kuwategemea sana wanamuziki wangu, natamani tuwe pamoja daima ili tufanikiwe kuivusha na kuifikisha mbali bendi yetu," alisema.
No comments:
Post a Comment