STRIKA
USILIKOSE
Monday, July 19, 2010
Diego Forlan: Shujaa wa Uruguay WOZA 2010
PENGINE maamuzi yake ya kuachana na mchezo wa tenisi alioupenda utotoni na kuucheza hadi akiwa na miaka 14 na kisha kufuata nyayo za baba na babu yake katika soka, hayakuwa ya kimakosa kutokana na mafanikio anayoyapata kwa sasa katika mchezo huo.
Forlan anayeichezea klabu ya Atletico Madrid ya Hispania na anayetajwa kama mmoja wa washambuliaji wanaotisha zaidi duniani, mbali na mafanikio mengi anayojivunia, kubwa ni kung'ara kwake katika fainali za Kombe la Dunia zilizomalizika wiki iliyopita nchini Afrika Kusini.
Katika fainali hizo za pili kwake, Forlan kwa juhudi binafsi, aliifikisha timu yake katika hatua ya nusu fainali ikiwa ni rekodi baada ya miaka 40 kupita tangu Uruguay, mabingwa wa kwanza wa michuano hiyo iliyoanzishwa mwaka 1930, kucheza nusu fainali kwa mara ya mwisho mwaka 1970.
Kuifikisha Uruguay hatua hiyo, kumemfanya Forlan aweke historia na kumfunika baba yake mzazi, Pablo Justo Forlan Lamarque, aliyekuwa akicheza kama beki aliyewahi kuiwakilisha nchini hiyo katika fainali mbili za Kombe la Dunia mwaka 1966 na 1974.
Amemfunika pia babu yake, Juan Carlos Corazo, aliyewahi kung'ara katika klabu ya Independiente ya Argentina na kuwahi kuinoa timu ya taifa ya Chile mwaka 1962.
Forlan aliibeba kwa kila hali Uruguay katika WOZA 2010, akicheza kwa kujituma na kuifungia mabao muhimu ambayo mwishowe yalimfanya kuwa miongoni mwa wafungaji bora wa michuano hiyo na kunyakua tuzo ya 'Adidas Golden Ball' ya Mchezaji Bora wa Kombe la Dunia 2010.
Nyota huyo alinyakua tuzo hiyo akiwazidi kete nyota wanne, Wesley Sneijder-Uholanzi, David Villa-Hispania, Thomas Muller Ujerumani na Gonzalo Higuain wa Argentina.
Kwa takwimu za waliopiga mashuti mengi langoni katika WOZA, Forlan aliyenyakua tuzo mbili tofauti za Mfungaji Bora Ligi ya Hispania na Ulaya kwa msimu ya 2004-2005 na 2008-2009, amelingana na Villa wakipiga mashuti 32 kila mmoja nyuma ya Asamoah Gyan wa Ghana aliyekuwa kinara.
Mafanikio ya Forlan aliyeanza kuichezea Uruguay tangu mwaka 2002, akifikisha jumla ya mechi 69 na kuifungia mabao 29, yamekuja katika michuano hiyo ya Dunia ikiwa ni miezi michache tangu alipotoka kuisaidia klabu ya Atletico Madrid kutwaa la ubingwa wa Ligi ya Europa, jina jipya la michuano ambayo ni maarufu zaidi nchini kama "UEFA ndogo".
Nyota huyo aliifungia mabao muhimu Atletico katika michuano hiyo mikubwa ya pili nyuma ya Ligi ya Mabingwa barani humo na kuifikisha fainali, ambako yeye mwenyewe "aliinyonga" Fulham ya England na kuipa ubingwa klabu hiyo ya Hispania.
FORLAN NI NANI?
Forlan ambaye majina yake kamili ni Diego Martin Forlan Corazo, alizaliwa Mei 19, 1979 mjini Montevideo, Uruguay na utotoni alipenda mno mchezo wa tenisi, ingawa pia alijihusisha na soka katika klabu za vijana za Penarol na Danubio za nchini mwake.
Inadaiwa alijikita zaidi katika soka baada ya ajali mbaya iliyompata dada yake Alejandra Forlan, iliyomfanya apooze mwili na kumpoteza mchumba wake na ndipo aliponyakuliwa na Independiete ya Argentina, ambapo alianza kwa kuchezea kikosi cha vijana kabla ya kupandishwa kwenye timu ya wakubwa mwaka 1998 hadi Januari 2002 aliposajiliwa na klabu ya Manchester United ya England kwa ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 6.9 (sawa na Sh. Bilioni 15.5).
Manchester ilimnyakua Forlan kwa lengo la kwenda kuziba nafasi ya Andy Cole, lakini ilimchukua miezi nane kufunga goli lake la kwanza katika klabu hiyo katika mechi ya ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Maccabi Haifa ya Israel katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kutokana na kushindwa kufanya vema katika misimu yake miwili ndani ya Old Trafford, aliotwaa nao taji la Ligi Kuu ya England 2002-2003, Kombe la FA 2003-2004 na Ngao ya Hisani 2003, Forlan aliuzwa kwa klabu ya Villarreal ya Hispania Agosti 21, 2004.
Kuondoka kwake Manchester kulitoa fursa kwa nyota wa sasa wa England, Wayne Rooney kutua akitokea klabu aliyolelewa ya Everton.
Katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya Hispania, Forlan alifunga magoli 25 na kuisaidia kuiingiza Villareal kwa mara ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku mwenyewe akinyakua tuzo ya Mfungaji Bora wa la Liga iitwayo 'Pichichi' na ile ya Mfungaji Bora wa Ulaya, akilingana na Thiery Henry (aliyekuwa Arsenal wakati huo).
Aliendelea kuipa mafanikio timu yake hiyo kabla ya mwaka 2007 kutua katika klabu ya Atletico Madrid ambapo aliifungia mabao 32 katika mechi 33 alizoichezea na kunyakua tena tuzo ya Pichichi na ile ya Ulaya kwa mara ya pili msimu wa 2008-2009.
Kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora wa Hispania na Ulaya akiwa na klabu mbili tofauti za La Liga, kulimfanya kuwa mchezaji wa kwanza tangu Ronaldo aliyefanya hivyo katika msimu wa mwaka 1996-97 akiwa na Barcelona, kisha 2003-2004 akiwa na kikosi cha Real Madrid.
Msimu uliopita mkali huyo alishika nafasi ya tano ya ufungaji mabao ya ligi ya Hispania akiwa na mabao mabao 18, akizidiwa mabao 16 na aliyekuwa kinara, Lionel Messi wa Barcelona.
Hata hivyo, ufungaji wake wa magoli muhimu uliibeba Atletico Madrid iliyonyakua ubingwa wa Ligi ya Europa baada ya kuilaza Fulham ya England, ikiwa ni baada ya kusaidia kuingoa Liverpool.
Kuhusu maisha yake binafsi, Forlan anayefahamika kama 'Cachavacha' na aliyemiliki mfuko maalum wa kusaidia wahanga wa ajali kama njia ya kumuenzi dada yake Alejandra Forlan, anaishi na mwanamtindo maarufu wa Argentina, Zaira Nara.
DONDOO MUHIMU
* Alisajili wa Atletico Madrid 2007 kwa ajili ya kuziba pengo la Fernando Torres, aliyehamia Liverpool.
* Alitwaa tuzo yake ya pili ya Kiatu cha Dhahabu kwa kuwa Mfungaji Bora wa Ulaya katika msimu wa 2008/09 kutokana na kuwa na magoli 32 ya ligi kuu, ambapo 12 kati ya hayo aliyafunga katika mechi nane za mwisho za msimu na kumpiku mshmabuliaji wa Barcelona kwa wakati huo, Samuel Eto'o.
* Alikuwa katika kiwango cha juu katika Ligi ya Europo msimu uliopita na kuisaidia Atletico kutwaa ubingwa wao wa kwanza Ulaya katika miaka 48.
* Alifunga magoli yote mawili ya Atletico katika ushindi wa 2-1 wa fainali ya Ligi ya Europa dhidi ya klabu ya Fulham mjini Hamburg.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment