STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 11, 2014

MZEE KINGUNGE ATEMA CHECHE VITA YA DAWA ZA KLEVYA

* Adai bila kunaswa 'vigogo' ni kazi bure
* Asisitiza mfumo wa malezi, tamaa chanzo cha tatizo
Mzee Kingunge akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na blogu hii nyumbani kwake
WAKATI serikali ikitokwa povu la mdomo ikijigamba kuwa, itaongeza ukali dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini, japo tatizo hilo linaloonekana kuzidi kuota mizizi, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru ameibuka na kufichua sababu za biashara hiyo kushindwa kukomeshwa huku taifa likiendelea kushuhudia vijana ambao ni nguvu kazi ikiangamia kwa tamaa za utajiri wa watu wachache.
Mwanasiasa huyo amesema ni vigumu biashara hiyo kukoma nchini kama serikali na vyombo vyake vya dola havitawashughulikia na kuwakamata  'vigogo' wa biashara hiyo pamoja na kutengenezwa sheria kali itakayowafanya wahusika wajutie kujihusisha nayo na kuwatia woga watu wengine wanaoanza au kutamani kuifanya biashara hiyo.
Pia, amesema ni lazima serikali na jamii kwa ujumla ishirikiane katika kuwapa malezi na elimu bora watoto na vijana itakayowafanya wapende kufanya kazi na kujitegemea badala ya kuwa tegemezi, wavivu na wanaopenda anasa na tamaa ya kutamani vitu ambavyo hawana uwezo wa kuvipata.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake wiki iliyopita, Kingunge alisema tatizo la dawa za kulevya ni kubwa na linaloliangamiza taifa, na kwamba licha ya kuwepo kwa juhudi tatizo hilo limeshindwa kupatiwa ufumbuzi kwa sababu wanaonaswa ni watu wadogo tu, huku vigogo na wamiliki wakubwa wa mtandao huo wakiachwa mitaani bila kuguswa.
Kingunge alisema pia hata sheria zilizopo ni nyepesi na zisizowafanya watuhumiwa na biashara hiyo kuziogopa, japo alidai asingependa kupona sheria za kuwapiga risasi au kuwanyonga kama zinazofanywa na mataifa mengine ndizo zitumike nchini, lakini alitaka sheria ziwe kali na zitakazowafanya wanaonaswa wakijishughulisha na biashara hiyo kujuta wao na familia zao ambazo zimekuwa zikifahamu nyendo zao na kunyamaza.
"Juhudi za kudhibiti suala hili zipo,  ila hazizai matunda kwa sababu wanaokamatwa ni watu wadogo, vigogo je kwa nini hawaguswi? Ni vyema nguvu zikaelekezwa kwa vigogo na kuwekwa sheria kali ya kuwatisha wanaojihusisha na biashara hiyo. Dawa za kulevya ni janga na hatari kwa taifa.  Ni tatizo la dunia nzima hivyo tunapaswa kuonyesha ukali katika hili hapo tunaweza kudhibiti, ingawa kukomesha kabisa ni vigumu," alisema.
Alisema pia kuna haja ya kujipanga upya katika kuteua watu wa kushughulikia mapambano ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha wanateuliwa watu waaminifu na wasiojihusisha na mtandao wa biashara hiyo vinginevyo vita dhidi ya dawa za kulevya zitakuwa kazi bure tu.
Kingunge aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ukiwamo uwaziri katika awamu zote nne za uongozi tangu taifa lipate uhuru, alisema pia tatizo la biashara hiyo ya dawa za kulevya limekuwa sugu kutokana na mfumo wa maisha uliopo kwa sasa kuanzia kwenye malezi hadi katika elimu kwa watoto na vijana inayowafanya wakuwe wakiwa wavivu na kuthamini fedha na anasa kuliko kufanya kazi.
"Wazazi, walezi na hata serikali imekuwa ikikumbatia na kuthamini sana watu wenye fedha, pia jamii imekuwa inapenda anasa na njia za mkato za maisha badala ya mfumo wa malezi na elimu unaowafanya watu wapende kufanya kazi kama tulivyokuwa tukihimiza miaka ya nyuma. Hili liunafanya watu watafute kila njia kupata fedha hata kwa njia haramu," alisema.
Kuhusu wimbi la wanawake nao kujiingiza kwenye biashara hiyo na baadhi yao kunaswa katika mataifa ya nje, alisema wanalazimika kwa sababu nao wanatafuta fedha kw akutambua bila ya kuwa na fedha hawathaminiki wala kuonekana ni watu.
"Upo msemo kwamba mtu kitu asiyekuwa na kitu kinyama cha mwitu, tusiwalaumu wanawake na vijana kuingia kwenye biashara hii, wanatafuta fedha kwa sababu wamewaona wazazi na walezi wao na hata serikali ikithamini na kuwapa heshima watu wenye fedha," alisema.
Mwanasiasa huyo alisema hata hivyo kuna tatizo la jamii ya kitanzania kuangalia matokeo ya hali ya mambo badala ya kuangalia chanzo cha suala hilo, akidai biashara ya unga imeanza kitambo kirefu lakini iliwahusisha watu wachache lakini kutokana na mabadiliko ya utandawazi vijana wamekuwa wakijifunza mambo mengi ya upuuzi kupitia runinga na mitandao na kujikuta wakizama kwenye maovu.

ANGA WAKATI MWINGINE HUWA NA MVUTO WA KIPEE EBU CHEKI HII ILITOKEA JUZI

Huo unaoonekana pichani siyo moshi wa Roketi au Mwanga wa Radi bali ni shani ya Mungu alivyoyafanya mawingu yalizuie jua na kutoa muonekanao huo katika picha hizi zilizonswa majira ya saa 11 jioni
 



JEZI YA DIDA NOMA YANGA, NDIYO YA MWISHO NA KUBWA JANGWANI

Na Arone Mpanduka,Radio Tumaini
GOLIKIPA wa klabu ya soka ya Yanga Deogratius Munishi ndiye mchezaji pekee katika timu ya Yanga anayevalia jezi yenye nambari kubwa kuliko yeyote kwenye timu hiyo.
 
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti la Tumaini Letu, Munishi maarufu kama Dida anatumia jezi nambari 30 mgongoni pindi anaposimama kwenye milingoti ya timu ya Yanga ambayo ndiyo yak mwisho katika klabu hiyo kwa sasa.
Wachezaji wengine wanaomfuatia Dida kwa kuwa na jezi yenye nambari kubwa mgongoni ni pamoja na mlindamlango namba moja Juma Kaseja ambaye anatumia jezi namba 29.
 
Mbali na Kaseja mchezaji mwingine wa timu hiyo ni Simon Msuva mwenye jezi nambari 27 akifuatiwa na mchezaji Hassan Dilunga mwenye jezi nambari 26 mgongoni.
Mshambuliaji mpya Emmanuel Okwi yeye anavalia jezi nambari 25 huku kiungo mahiri Athuman Iddi Chuji akitumia jezi nambari 24 tangu ajiunge na timu hiyo miaka saba iliyopita.
Beki Nadir Haroub Canavaro naye ni mmoja wa wachezaji wanaovalia jezi yenye nambari kubwa mgongoni akiwa na jezi nambari 23 huku kinda Hamis Nyige akiwa na jezi nambari 22 na mshambuliaji Hussein Javu jezi nambari 21.
NAMBA NA TAFSIRI ZAKE
Wapo baadhi ya wachezaji katika klabu ya hiyo ambao wamechagua namba za jezi kwa sababu maalum akiwemo mshambuliaji Emmanuel Okwi.
Okwi ameamua kuchagua jezi nambari 25 kwasababu alizaliwa Disemba 25 mwaka 1992 huko nchini Uganda hivyo ameona ni bora atumie nambari hiyo ili kuipa heshima tarehe yake ya kuzaliwa.
 
Si Yanga pekee ambako aliweza kufanya hivyo bali hata katika klabu alizopitia ikiwemo Sc Villa, Simba SC na hata timu yake ya taifa amekuwa akitumia jezi nambari 25.
Kwa upande wake Juma Kaseja ambaye sasa ana umri wa miaka 30 mwaka jana wakati alipojiunga na Yanga alipewa rasmi jezi nambari 29 ambayo ilikuwa ikiendana na umri wake.
 
Awali jezi hiyo namba 29 ilikuwa ikivaliwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, raia wa Kenya, Boniface Ambani, kabla ya kustaafu kucheza soka la kulipwa.
JEZI NAMBA 9 NA IMANI POTOFU YANGA
Wachezaji mbalimbali wa Yanga wamekuwa na imani potofu kwamba jezi namba tisa mara nyingi haimpi mchezaji mafanikio anayoyataka ndani ya uwanja.
Imani hiyo imeibuka kufuatia wachezaji kadhaa waliowahi kupita katika timu hiyo kushindwa kufanya vizuri na kupeleka hata wengine kuishia kwenye benchi la wachezaji wa akiba na kushuhudia wenzao wakicheza mechi kadhaa.
 
Awali jezi nambari tisa Yanga ilikuwa ikivaliwa na Mkenya, Boniface Ambani ambaye baadaye aliachana nayo na kuhamia namba 24 na kumfanya awe mfumania nyavu hatari katika timu hiyo.
Baadae jezi namba 9 ikaenda kwa Mcameroon, Jama Mba, ambaye naye alijikuta kama ana mikosi baada ya kuonekana si lolote si chochote na kuishia benchi kabla klabu kumfungashia virago na kurejea kwao.
Baada ya Mbuyu Twite kujiunga na Yanga mwaka 2013, uongozi ukampatia jezi nambari tisa lakini aliikataa na kupewa namba 6 baada ya kusikia tetesi kwamba namba hiyo ina mikosi klabuni hapo.
 
Mchezaji mwingine wa Yanga Omega Seme aliitumia jezi hiyo lakini taratibu makali yake yakapungua na mwishowe Yanga ikamchoka na kumtoa kwa mkopo kwenda klabu ya Tanzania Prisons ya jijini Mbeya.
Kwa sasa jezi hiyo inatumiwa na mshambuliaji Renatus Lusajo Mwakasabule ambaye mara zote amekuwa akiishia kukaa benchi huku akiwaachia nafasi kina Mrisho Ngassa,  Kavumbagu na Tegete wakicheza katika safu ya ushambulizi.
 
Kasumba hiyo mbovu pia imewakumba watani wao wa jadi Simba ambao nao wanaikimbia jezi namba tisa.
Mchezaji Ramadhani Salum ndiye anavaa jezi hiyo huku akiwa hana nafasi katika kikosi cha kwanza.
Katika kipindi cha nyuma namba hiyo alikuwa nayo mchezaji Kago Gervais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambaye alijiunga na klabu hiyo kwa mbwembwe nyingi.
Hata hivyo kiwango chake kilikuwa duni na kuishia katika benchi la wachezaji wa akiba na mwishowe akafungashiwa virago na uongozi wa klabu ya Simba.
Credit:SHAFII DAUDA

KIbao Kata, Baikoko kuwasindikiza Dar Modern

Hassan Kumbi 'Hassani Vocha' (kulia) mmoja wa waimbaji watakaotambulishwa Dar Modern. Msanii huyu alianzia Mkubwa na Wanae na pichani akiwa a Dogo Aslay na Bibi Cheka.
WASANII na makundi ya ngoma asilia ya Kibao Kata na Baikoko wanatarajiwa kunogesha onyesho la utambulisho  wasanii na nyimbo mpya za kundi la muziki wa taarab la Dar Modern 'Wana wa Jiji' waliorejea upya baada ya kimya cha muda mrefu.
Dar Modern lililowahi kulisimamisha jiji kwa nyimbo zake za 'Pembe la Ng'ombe' na 'Kitu Mapenzi', litafanya onyesho hilo Siku ya  Wapendanao, Magomeni Dar es Salaam.
Akizungumza na MICHARAZO, Kaimu Rais wa kundi hilo, Hassan Bakar alisema maandalizi ya onyesho hilo la Ijumaa  yamekamilika na iliyobaki ni kwa mashabiki wa burudani kujitokeza kwa wingi ukumbini kushuhudia Dar Modern mpya.
"Kila kitu kimekaa vyema na inasubiriwa Ijumaa mashabiki kuona nyota wapya wa kundi letu akiwamo msanii Hassani Vocha aliyeibuliwa na kituo cha Mkubwa na Wanae na kutamba na wimbo wa 'Vocha' alioimba na Dogo Aslay," alisema.
Bakar alisema katika kunkuogesha onyesho hilo, Dar Modern itasindikizwa na wasanii wa makundi ya unenguaji ya asilia ya Baikoko la Tanga na Kibao Kata.
"Burudani nyingine za kunogesha uzinduzi huo zitaongezwa wakati tukielekea kwenye onyesho hilo," alisema Bakar.
Dar Modern lililoanzishwa mwaka 2006 na baadhi ya wasanii waliokuwa Babloom Modern Taarab na Zanzibar, lilizimika baada ya baadhi ya nyota wake kujiengua likiwa linatikisa anga la muziki wa miondoko hiyo kupitia albamu zake karibu saba.
Albamu hizo ni pamoja na 'Ni Vijimambo Tu', 'Sote Twasaka Riziki', 'Gharika ya Moyo', 'Kitu Mapenzi','Toto la Kiafrika', 'Nauvua Ushoga' na 'Ndugu wa Mume Mna Hila'.
======================

Inspekta Harun 'Babu' Hujachelewa Bwana!

Babu akionyesha manjonjo yake jukwaani
MSANII mkongwe wa muziki wa kizazi kipya nchini, Haruna Kahena 'Inspekta Harun' .a.k,a Babu ameachia wimbo mpya uitwao 'Haujachelewa' ikiwa ni utambulisho wa albamu yake mpya atakayoizindua mwezi ujao.

Akizungumza na MICHARAZO, Inspekta Harun alisema wimbo huo ameurekodia kwa mtayarishaji Mbezi na ni kati ya nyimbo zitakazokuwa katika albamu mpya itakayofahamika kwa jina la 'Sharubu za Babu'.

Inspekta alisema tayari wimbo huo umeshaanza kusikika hewani tangu Ijumaa iliyopita na anashukuru umepokelewa vyema na mashabiki wa muziki nchini.

"Nimeachia wimbo wangu mpya uitwao 'Hujachelewa' chini ya prodyuza Mbezi ikiwa ni maandalizi ya albamu yangu iitwayo 'Sharubu za Babu'," alisema Inspekta Harun.

"Albamu hiyo mpya natarajia kuizindua mwezi ujao (Machi) pale Dar Live, taarifa zaidi juu ya wasanii watakaonisindikiza tutafahamisha kadri siku zinavyosonga mbele ila Babu nimerejea kwa kishindo," aliongeza msanii huyo.

Nyota huyo aliyewahi kutamba nchini na vibao murua kama 'Mtoto wa Geti Kali', 'Rapu Katuni', 'Simulizi la Ufasaha', 'Ngangari', 'Asali wa Moyo', 'Nje Ndani' na 'Tunajirusha' na nyingine.
===========================

Jennifer Mgendi: Nyota wa Muziki wa Injili anayelia na wizi kazi za wasanii

Jennifer Mgendi
HAKUNA kitu kinachomfariji na  kumpa furaha Jennifer Mgendi katika kuwapo kwake kwenye sanaa ya muziki wa Injili na uigizaji wa filamu kama kuwabadilisha watu kutoka maisha ya vifungo vya shetani  kupitia kazi zake.
Nyota huyo wa muziki wa Injili na filamu nchini anasema anaamini watu wengi wamekuwa wakizisikiliza nyimbo na kuangalia filamu zake na kutoka kwenye vifungo mbalimbali vya ukandamizaji vya Mwovu Shetani kama hali ya kukata tamaa, magonjwa na wengi kuacha maisha ya dhambi na kumgeukia YESU.
"Hilo kwangu ni faraja na fanikio kubwa la kujivunia kuliko hata mafanikio ya kiuchumi na kimaisha niliyopata kupitia sanaa. Kuona wanadamu wenzangu wakimgeukia YESU na kuachana na dhambi kwani ni faraja kubwa," anasema.
Jennifer aliyetumbukia kwenye fani ya muziki tangu akiwa mdogo kwa kupenda kusikiliza na kucheza nyimbo za nyota wa zamani duniani kama Yvonne Chakachaka, Abba Group, Jim Revees na nyimbo za kihindi,  anasema tangu alipookoka na kujitosa kwenye muziki wa Injili ameshatoa albamu saba.
Tano kati ya hizo ndizo zipo sokoni, moja ikiwa ni mchanganyiko wa nyimbo zake zote kali iliyopewa jina la 'Dhahabu', huku nyingine zikiwa ni 'Yesu Nakupenda', 'Mchimba Mashimo', 'Kiu ya Nafsi'  na mpya ya 'Hongera Yesu'.
Kwa upande wa filamu, Jennifer anayependa kula chakula chochote kizuri, japo anauzimia ugali kwa mlenda na kunywa juisi halisi na maji, ameshafyatua kazi  nne zilizompatia umaarufu mkubwa ambazo ni 'Joto la Roho', 'Pigo la Faraja', 'Teke la Mama', na 'Chai Moto', akiwa mbioni kutoa kazi mpya ya mwaka 2014.
Anasema ameshaandaa hadithi tatu za filamu, ila hajajua aanze kurekodi ipi kati ya hizo.
"Nina kazi tatu kwa sasa ambazo natarajia kurekodi moja ili kufungua mwaka  2014, ila sijajua ni ipi nitakayoanza nayo ila nitawashirikisha wasanii nyota kama kazi zangu za nyuma," anasema.
Anasema matarajio yake ni kutoa kazi bora zaidi na hasa kuja kufyatua tamthilia ndefu itakayoonyeshwa kwenye runinga kama 'Isidingo', japo anasema jambo hilo litategemea mipango yake ya kifedha kama itakuwa mizuri.
Jennifer katika pozi
UBUNIFU
Jennifer, anayezisifia nyimbo zake zote kuwa ni bora, anakiri wimbo  wa 'Kiu ya Nafsi',  'Mchimba Mashimo' na kazi yake mpya ya 'Hongera Yesu' ndiyo bomba kwake na kudai fani ya muziki nchini imepiga hatua kubwa kiteknolojia.
Anasema kipindi cha nyuma wasanii walikuwa wakiimba 'live' kwa vile hakukuwa na cd zaidi ya kanda za kaseti, hali kwa sasa kwa wasanii kuimba nyuma ya cd.
Hata hivyo anawataka wenzake kuongeza ubunifu zaidi na kujifunza kupiga ala mbalimbali za muziki badala ya kuacha kila kitu wafanyiwe na mashine studio.
Pia anawahimiza wasanii  kujikita zaidi katika kujitangaza nje ya nchi na kutoa kazi zenye ubora zitakazowabamba mashabiki wao.
Huku akiwasihi wanaoimba nyimbo za KIROHO wamuombe MUNGU awafunulie vitu vitakavyokuwa vya faida kwa wanakondoo wake badala ya kuishia kutoa burudani tu kama muziki wa KIDUNIA.
Juu ya masilahi mkali huyo anakiri kwa sasa sanaa inalipa na ina masilahi mazuri kuliko zamani, japo analia na vitendo vya wizi unaoendelea dhidi ya kazi za wasanii.
Anasema, wizi huo hauwaumizi wasanii pekee bali  unainyima serikali mapato mengi yanayopotea mikononi mwa maharamia wanaouza kazi kwa wizi na kudai kungekuwa na utaratibu wa kuwabana kama ulioanzishwa sasa wangefanya walipe kodi na kusaidia mambo ya kimaendeleo nchini.
Jennifer anasema serikali kupitia TRA inawabana wasanii kulipa kodi, lakini bado inashindwa kuwadhibiti wezi wanaoendelea kuwaibia wasanii mchana kweupe.
"Kuna watu wanaokamatwa kwa wizi wa kazi za wasanii lakini huishia kuonyesha risiti za malipo walizolipa COSOTA zimeandikwa "Copyright Licence" wakieleza wameruhusuiwa kudurufu. Kwa kweli inaumiza sana hatuelewi tumlilie nani, yaani kama 'kilio cha samaki baharini. Ila binafsi naamini ipo siku mambo yatakuwa sawa baada ya kila upande kujitambua," anasema.
Jennifer Mgendi akiwajibika jukwaani
MKALI
Jennifer anayewataka wasanii wenzake kutoridishwa na mafanikio waliyonayo badala yake kuongeza bidii zaidi ili wafike mbali, akiwataka pia kupendana, kushirikiana na kuwa na umoja utakaowasaidia katika mapambano dhidi ya kupigania haki zao.
Mwanamama huyo mke wa Dk Job Chaula, alizaliwa mwaka 1972 jijini Dar es Salaam akiwa ni mmoja wa watoto watatu wa familia yao yenye asili ya mkoa wa Singida, kabila la Kinyiramba.
Elimu yake ya Msingi na Sekondari aliipata katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga kabla ya kufanya kazi ya Ualimu na Ukutubi na baadaye kuacha ili ajiajiri.
Anasema tangu utoto alipenda sana muziki na kuzicheza akijiangalia kwenye kioo wakati wazazi wake wameenda kazini kabla ya kuanza kujifunza kuimba alipokuwa katika kikundi cha ngoma cha Shule ya Msingi, pia  akiimba kwaya.
Ndoto ya kuwa muimbaji ilisukumwa zaidi alipokuwa kidato cha sita na alipoajiriwa kama Mwalimu wilayani Handeni alipata bahati ya kupata rafiki za kizungu aliyemfundisha namna ya kupiga gitaa na hapo alianza kutunga nyimbo chache zilizokuja kumtangaza kama 'Barthimayo', 'Nini', 'Ulinipa Sauti' na nyingine zilizopo kwenye albamu yake ya 'Dhahabu'.
Mwaka 1994 alipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipopata mwanga mzuri juu ya kurekodi muziki na kuanza makeke kwa kufyatua albamu yake ya kwanza mwaka 1995 .
Baada ya hapo aliendelea kujipatia umaarufu mkubwa kupitia muziki huo wa Injili kabla ya miaka ya 2000 alipojitumbukiza kwenye utunzi na utayarishaji wa filamu kazi anayoendelea nayo kwa sasa sambamba na hiyo ya muziki wa Injili.
Jennifer anamshukuru Mungu kwa kumjalia kipaji na kufikisha alipo, akiwashukuru pia watu wote wakishiriki kwa namna moja au nyingine kumsaidia kufika mahali alipo sasa akidai hana cha kuwalipa zaidi ya kumwachia Mungu awalipe  kwa waliomfanyia kiasi kwamba leo amekuwa mmoja wa wanawake waimbaji wanaoheshimika ndani na nje ya Tanzania.

Wachezaji Simba kuwekwa kitimoto Msimbazi

Simba ikiwa na makocha wake, Logarusic (kulia) na Matola (kushoto waliosimama)
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage anayetkutana na wachezaji leo mchana klabuni kwao
MWENYEKITI wa klabu ya Soka ya Simba, Ismail Aden Rage mchana wa leo anatarajia kukutana na kuzungumza na wachezaji ili kujua kinachoendelea baina yao na benchi lao ufundi baada ya kuelezwa kuna 'mgomo' baridi uliosababisha Simba kupata matokeo mabaya katika mechi zao mbili zilizopita.
Hata hivyo uongozi wa Simba umenukuliwa jana ukisema kikao hicho ni cha kawaida na hakina uhusiano wowote na matokeo ya mechi zilizopita ambapo Simba iliambulia pointi moja katia ya sita.
Awali MICHARAZO ilipenyezewa taarifa kuwa, wachezaji wa Simba watakutana na uongozi wa Simba leo saa 6 mchana ili kuwekwa kitimoto kama njia ya kuzima mgomo baridi uliowekwa na wachezaji dhidi ya kocha wao, Zdravko Lugarusic anayedaiwa amekuwa mkali na anatusi wachezaji wakati wa mazoezi.
"Matokeo ya Simba siyo yanatokana na timu kushuka kiwango, bali wachezaji wanamuonyeshea kocha wao ndiyo wanaoweza kumbeba au kumuangusha kwa vitendo vyake vya kuwafanya kama watoto wadogo kwa kuwatusi na kuwakaripia ovyo hata katika makosa yanayopaswa kuelezwa kwa upole," chanzo kilidokeza.
Hata hivyo Msemaji wa Simba, Asha Muhaji alinukuliwa jana na kituo kimoja cha redio akisema kikao hicho ni cha kawaida na kukanusha taarifa za kuwepo kwa mgomo baridi.
Kikao hicho kimeitishwa na Mwenyekiti Ismail Aden Rage na kitawahusisha wachezaji pekee yao kabla ya uongozi huo kukutana tena na benchi la ufundi, lengo likiwa kuweka mambo sawa kabla ya kuifuata Mbeya City watakaoumana nao katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara siku ya Jumamosi jijini Mbeya.
Simba ilianza mechi zake za ugenini kwa kulazimishwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar, wakilazimika kurejesha bao kabla ya kulala Mkwakwani Tanga Jumapili walipoumana na Mgambo JKT iliyokuwa mkiani kwa msimamo kitu ambacho kimeishtua klabu hiyo kwa kuhisi mambo siyo mazuri.
Mabingwa hao wa zamani wa soka, kwa kipigo cha Mgambo wamerejeshwa hadi kwenye nafasi yao ya nne waliyokuwa awali kutokana na Mbeya City kuzinduka toka kwenye kipigo cha Yanga kwa kuilaza Mtibwa Sugar na kufikisha pointi 34 tatu zaidi ya ilizonazo Simba.
Katika mfululizo wa ligi hiyo kesho kwenye uwanja wa Chamazi, maafande ndugu, JKT Ruvu na Ruvu Shooting zinatarajiwa kupepetana kwenye pambano pekee.
Timu hizo zitakutana zikiwa zimetoka kupoteza mechi zao za mwisho,. JKT Ruvu ambao ni wenyeji wa mechi hiyo wakishtukizw ana kipigo cha Ashanti United na Ruvu Shooting kubabuliwa mabao 3-1 na Prisons Mbeya.