Na Arone Mpanduka,Radio Tumaini
GOLIKIPA wa klabu ya soka ya Yanga Deogratius
Munishi ndiye mchezaji pekee katika timu ya Yanga anayevalia jezi yenye nambari
kubwa kuliko yeyote kwenye timu hiyo.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti la
Tumaini Letu, Munishi maarufu kama Dida anatumia jezi nambari 30 mgongoni pindi
anaposimama kwenye milingoti ya timu ya Yanga ambayo ndiyo yak mwisho katika
klabu hiyo kwa sasa.
Wachezaji wengine wanaomfuatia Dida kwa kuwa na jezi
yenye nambari kubwa mgongoni ni pamoja na mlindamlango namba moja Juma Kaseja
ambaye anatumia jezi namba 29.
Mbali na Kaseja mchezaji mwingine wa timu hiyo ni
Simon Msuva mwenye jezi nambari 27 akifuatiwa na mchezaji Hassan Dilunga mwenye
jezi nambari 26 mgongoni.
Mshambuliaji mpya Emmanuel Okwi yeye anavalia jezi
nambari 25 huku kiungo mahiri Athuman Iddi Chuji akitumia jezi nambari 24 tangu
ajiunge na timu hiyo miaka saba iliyopita.
Beki Nadir Haroub Canavaro naye ni mmoja wa
wachezaji wanaovalia jezi yenye nambari kubwa mgongoni akiwa na jezi nambari 23
huku kinda Hamis Nyige akiwa na jezi nambari 22 na mshambuliaji Hussein Javu
jezi nambari 21.
NAMBA
NA TAFSIRI ZAKE
Wapo baadhi ya wachezaji katika klabu ya hiyo ambao
wamechagua namba za jezi kwa sababu maalum akiwemo mshambuliaji Emmanuel Okwi.
Okwi ameamua kuchagua jezi nambari 25 kwasababu
alizaliwa Disemba 25 mwaka 1992 huko nchini Uganda hivyo ameona ni bora atumie
nambari hiyo ili kuipa heshima tarehe yake ya kuzaliwa.
Si Yanga pekee ambako aliweza kufanya hivyo bali
hata katika klabu alizopitia ikiwemo Sc Villa, Simba SC na hata timu yake ya
taifa amekuwa akitumia jezi nambari 25.
Kwa upande wake Juma Kaseja ambaye sasa ana umri wa
miaka 30 mwaka jana wakati alipojiunga na Yanga alipewa rasmi jezi nambari 29
ambayo ilikuwa ikiendana na umri wake.
Awali jezi hiyo namba 29 ilikuwa ikivaliwa na
mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, raia wa Kenya, Boniface Ambani, kabla ya
kustaafu kucheza soka la kulipwa.
JEZI
NAMBA 9 NA IMANI POTOFU YANGA
Wachezaji mbalimbali wa Yanga wamekuwa na imani
potofu kwamba jezi namba tisa mara nyingi haimpi mchezaji mafanikio anayoyataka
ndani ya uwanja.
Imani hiyo imeibuka kufuatia wachezaji kadhaa
waliowahi kupita katika timu hiyo kushindwa kufanya vizuri na kupeleka hata
wengine kuishia kwenye benchi la wachezaji wa akiba na kushuhudia wenzao
wakicheza mechi kadhaa.
Awali jezi nambari tisa Yanga ilikuwa ikivaliwa na
Mkenya, Boniface Ambani ambaye baadaye aliachana nayo na kuhamia namba 24 na
kumfanya awe mfumania nyavu hatari katika timu hiyo.
Baadae jezi namba 9 ikaenda kwa Mcameroon, Jama Mba,
ambaye naye alijikuta kama ana mikosi baada ya kuonekana si lolote si chochote
na kuishia benchi kabla klabu kumfungashia virago na kurejea kwao.
Baada ya Mbuyu Twite kujiunga na Yanga mwaka 2013,
uongozi ukampatia jezi nambari tisa lakini aliikataa na kupewa namba 6 baada ya
kusikia tetesi kwamba namba hiyo ina mikosi klabuni hapo.
Mchezaji mwingine wa Yanga Omega Seme aliitumia jezi
hiyo lakini taratibu makali yake yakapungua na mwishowe Yanga ikamchoka na
kumtoa kwa mkopo kwenda klabu ya Tanzania Prisons ya jijini Mbeya.
Kwa sasa jezi hiyo inatumiwa na mshambuliaji Renatus
Lusajo Mwakasabule ambaye mara zote amekuwa akiishia kukaa benchi huku
akiwaachia nafasi kina Mrisho Ngassa,
Kavumbagu na Tegete wakicheza katika safu ya ushambulizi.
Kasumba hiyo mbovu pia imewakumba watani wao wa jadi
Simba ambao nao wanaikimbia jezi namba tisa.
Mchezaji Ramadhani Salum ndiye anavaa jezi hiyo huku
akiwa hana nafasi katika kikosi cha kwanza.
Katika kipindi cha nyuma namba hiyo alikuwa nayo mchezaji
Kago Gervais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambaye alijiunga na klabu hiyo kwa
mbwembwe nyingi.
Hata hivyo kiwango chake kilikuwa duni na kuishia
katika benchi la wachezaji wa akiba na mwishowe akafungashiwa virago na uongozi
wa klabu ya Simba.
Credit:SHAFII DAUDA
No comments:
Post a Comment