Jennifer Mgendi |
Nyota huyo wa muziki wa Injili na filamu nchini anasema anaamini watu wengi wamekuwa wakizisikiliza nyimbo na kuangalia filamu zake na kutoka kwenye vifungo mbalimbali vya ukandamizaji vya Mwovu Shetani kama hali ya kukata tamaa, magonjwa na wengi kuacha maisha ya dhambi na kumgeukia YESU.
"Hilo kwangu ni faraja na fanikio kubwa la kujivunia kuliko hata mafanikio ya kiuchumi na kimaisha niliyopata kupitia sanaa. Kuona wanadamu wenzangu wakimgeukia YESU na kuachana na dhambi kwani ni faraja kubwa," anasema.
Jennifer aliyetumbukia kwenye fani ya muziki tangu akiwa mdogo kwa kupenda kusikiliza na kucheza nyimbo za nyota wa zamani duniani kama Yvonne Chakachaka, Abba Group, Jim Revees na nyimbo za kihindi, anasema tangu alipookoka na kujitosa kwenye muziki wa Injili ameshatoa albamu saba.
Tano kati ya hizo ndizo zipo sokoni, moja ikiwa ni mchanganyiko wa nyimbo zake zote kali iliyopewa jina la 'Dhahabu', huku nyingine zikiwa ni 'Yesu Nakupenda', 'Mchimba Mashimo', 'Kiu ya Nafsi' na mpya ya 'Hongera Yesu'.
Kwa upande wa filamu, Jennifer anayependa kula chakula chochote kizuri, japo anauzimia ugali kwa mlenda na kunywa juisi halisi na maji, ameshafyatua kazi nne zilizompatia umaarufu mkubwa ambazo ni 'Joto la Roho', 'Pigo la Faraja', 'Teke la Mama', na 'Chai Moto', akiwa mbioni kutoa kazi mpya ya mwaka 2014.
Anasema ameshaandaa hadithi tatu za filamu, ila hajajua aanze kurekodi ipi kati ya hizo.
"Nina kazi tatu kwa sasa ambazo natarajia kurekodi moja ili kufungua mwaka 2014, ila sijajua ni ipi nitakayoanza nayo ila nitawashirikisha wasanii nyota kama kazi zangu za nyuma," anasema.
Anasema matarajio yake ni kutoa kazi bora zaidi na hasa kuja kufyatua tamthilia ndefu itakayoonyeshwa kwenye runinga kama 'Isidingo', japo anasema jambo hilo litategemea mipango yake ya kifedha kama itakuwa mizuri.
Jennifer katika pozi |
Jennifer, anayezisifia nyimbo zake zote kuwa ni bora, anakiri wimbo wa 'Kiu ya Nafsi', 'Mchimba Mashimo' na kazi yake mpya ya 'Hongera Yesu' ndiyo bomba kwake na kudai fani ya muziki nchini imepiga hatua kubwa kiteknolojia.
Anasema kipindi cha nyuma wasanii walikuwa wakiimba 'live' kwa vile hakukuwa na cd zaidi ya kanda za kaseti, hali kwa sasa kwa wasanii kuimba nyuma ya cd.
Hata hivyo anawataka wenzake kuongeza ubunifu zaidi na kujifunza kupiga ala mbalimbali za muziki badala ya kuacha kila kitu wafanyiwe na mashine studio.
Pia anawahimiza wasanii kujikita zaidi katika kujitangaza nje ya nchi na kutoa kazi zenye ubora zitakazowabamba mashabiki wao.
Huku akiwasihi wanaoimba nyimbo za KIROHO wamuombe MUNGU awafunulie vitu vitakavyokuwa vya faida kwa wanakondoo wake badala ya kuishia kutoa burudani tu kama muziki wa KIDUNIA.
Juu ya masilahi mkali huyo anakiri kwa sasa sanaa inalipa na ina masilahi mazuri kuliko zamani, japo analia na vitendo vya wizi unaoendelea dhidi ya kazi za wasanii.
Anasema, wizi huo hauwaumizi wasanii pekee bali unainyima serikali mapato mengi yanayopotea mikononi mwa maharamia wanaouza kazi kwa wizi na kudai kungekuwa na utaratibu wa kuwabana kama ulioanzishwa sasa wangefanya walipe kodi na kusaidia mambo ya kimaendeleo nchini.
Jennifer anasema serikali kupitia TRA inawabana wasanii kulipa kodi, lakini bado inashindwa kuwadhibiti wezi wanaoendelea kuwaibia wasanii mchana kweupe.
"Kuna watu wanaokamatwa kwa wizi wa kazi za wasanii lakini huishia kuonyesha risiti za malipo walizolipa COSOTA zimeandikwa "Copyright Licence" wakieleza wameruhusuiwa kudurufu. Kwa kweli inaumiza sana hatuelewi tumlilie nani, yaani kama 'kilio cha samaki baharini. Ila binafsi naamini ipo siku mambo yatakuwa sawa baada ya kila upande kujitambua," anasema.
Jennifer Mgendi akiwajibika jukwaani |
Jennifer anayewataka wasanii wenzake kutoridishwa na mafanikio waliyonayo badala yake kuongeza bidii zaidi ili wafike mbali, akiwataka pia kupendana, kushirikiana na kuwa na umoja utakaowasaidia katika mapambano dhidi ya kupigania haki zao.
Mwanamama huyo mke wa Dk Job Chaula, alizaliwa mwaka 1972 jijini Dar es Salaam akiwa ni mmoja wa watoto watatu wa familia yao yenye asili ya mkoa wa Singida, kabila la Kinyiramba.
Elimu yake ya Msingi na Sekondari aliipata katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga kabla ya kufanya kazi ya Ualimu na Ukutubi na baadaye kuacha ili ajiajiri.
Anasema tangu utoto alipenda sana muziki na kuzicheza akijiangalia kwenye kioo wakati wazazi wake wameenda kazini kabla ya kuanza kujifunza kuimba alipokuwa katika kikundi cha ngoma cha Shule ya Msingi, pia akiimba kwaya.
Ndoto ya kuwa muimbaji ilisukumwa zaidi alipokuwa kidato cha sita na alipoajiriwa kama Mwalimu wilayani Handeni alipata bahati ya kupata rafiki za kizungu aliyemfundisha namna ya kupiga gitaa na hapo alianza kutunga nyimbo chache zilizokuja kumtangaza kama 'Barthimayo', 'Nini', 'Ulinipa Sauti' na nyingine zilizopo kwenye albamu yake ya 'Dhahabu'.
Mwaka 1994 alipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipopata mwanga mzuri juu ya kurekodi muziki na kuanza makeke kwa kufyatua albamu yake ya kwanza mwaka 1995 .
Baada ya hapo aliendelea kujipatia umaarufu mkubwa kupitia muziki huo wa Injili kabla ya miaka ya 2000 alipojitumbukiza kwenye utunzi na utayarishaji wa filamu kazi anayoendelea nayo kwa sasa sambamba na hiyo ya muziki wa Injili.
Jennifer anamshukuru Mungu kwa kumjalia kipaji na kufikisha alipo, akiwashukuru pia watu wote wakishiriki kwa namna moja au nyingine kumsaidia kufika mahali alipo sasa akidai hana cha kuwalipa zaidi ya kumwachia Mungu awalipe kwa waliomfanyia kiasi kwamba leo amekuwa mmoja wa wanawake waimbaji wanaoheshimika ndani na nje ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment