* Zinakutana katika fainali ya kisasi
|
Ghana Black Stars |
|
Kikosi cha Ivory Coast |
MALABO, Guinea ya Ikweta
AFRIKA inatarajiwa kufahamu Bingwa Mpya wa soka wakati Ivory Coast na Ghana zitakapoumana kwenye mchezo wa fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2015.
Pambano hilo litakalopigwa kwenye uwanja wa Estadio de Bata, linakumbushia fainali za mwaka 1992 wakati Tembo wa Afrika, Ivory Coast na Black Stars ya Ghana zilipokutana nchini Senegal.
Katika fainali hiyo ya aina yake, Ivory Coast waliwazidi kete wapinzani wao hao na kutwaa taji hilo kwa mikwaju ya penati 11-10 baada ya kumaliza dakika 120 milango ya timu zote ikiwa migumu.
Ivory Coast wamefuzu hatua hiyo baada ya kuing'oa timu ya DR Congo kwa kuwachapa mabao 3-1 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa Jumatano, huku kocha wake Herve Renald 'akizuga; kuwa walipenya kibahati kutokana na timu yake kucheza ovyo.
Wenyewe Ghana walifanikiwa kuwatoa wenyeji Guinea ya Ikweta kwa kuwabangua mabao 3-0 katika mechi iliyojaa vurugu za mashabiki waliokuwa wakishinikiza mwamuzi 'kuwabeba' tena kama ilivyokuwa katika mechi ya robo fainali dhidi ya Tunisia iliyomponza refa wa Mauritius kufungiwa.
Wenyeji hao walitarajiwa jana kuvaana na DR Congo kwa ajili ya kuwania nafasi ya mshindi wa tatu na nne wa fainali hizo za 30 ambazo zilianza kutimua vumbi lake tangu Januari 17.
Mchezo huo wa fainali unasubiriwa kwa hamu kutokana na umahiri wa vikosi vya timu hizo za Afrika Magharibi na washiriki wa Fainali zilizopita za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Brazili.
Tembo wa Afrika wanajivunia kikosi kinachoundwa na nahodha wake Yaya Toure ambaye ndiye Mchezaji Bora wa Afrika, sambamba na mwanasoka ghali wa Afrika, Wilfried Bony na wakali wengine.
Wakati wapinzani wao wanatambia nahodha wake, Asamoah Gyan, Andre Ayew na nduguye Jordan Ayew, Kwame Appiah na wengine wanaochezaji soka la kulipwa katika klabu mbalimbali za Ulaya.
Kikosi cha Ghana kinachonolewa na kocha wa zamani wa Chelsea, Avram Grant ambaye atakuwa akitaka kuwapa waajiri wake taji la tano baada ya kulikosa kwa muda mrefu tangu walipotwaa mara ya mwisho mwaka 1982 na kulikosa kwenye fainali za mwaka 2010 mbele ya Misri.
Ivory Coast wenyewe watakuwa wakisaka taji la pili la michuano hiyo baada ya fainali za mwaka 2012 zilizofanyika nchini Guinea ya Ikweta ikishirikiana na Gabon kulikosa kwa kufungwa na Zambia.
Cha kuvutia ni kwamba kocha aliyewapa taji Zambia mwaka huo, Herve Renald ndiye anayeinoa timu hiyo kwa sasa na kama timu yake itashinda leo ataweka rekodi ya aina yake Afrika ya kuw kocha wa kwanza kuchukua taji hilo akiwa na nchi mbili tofauti.
Je ni Tembo wa Afrika au Nyota Weusi watakaoibuka na ushindi katika mchezo huo wa leo? Tusubiri tuone baada ya kumalizika wa fainali hizo zilizohamishiwa Guinea ya Ikweta baada ya waliokuwa wenyeji wa awali Morocco kuchomoa kwa kisingizio cha hofu ya ugonjwa wa Ebola.
Kitendo hicho kimesababisha nchi hiyo ya Morocco kuadhibiwa kwa kufungiwa fainali mbili za Afrika za 2017 na 2019.