Kiongera aliyetajwa kuachwa kinyemela |
Dan Sserunkuma |
Uongozi wa Simba juzi ulimsainisha mkataba wa miaka miwili mshambuliaji Mganda Danny Ssrerunkuma huku ukitangaza kusitisha kwa muda mkataba wa Kiongera hadi pale atakapofanyiwa upasuaji na kupona majeraha ya goti yanayomkabili.
Timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) zinapaswa kuwa na idadi isiyozidi wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa Kanuni za Ligi za TFF Toleo la 2014. Ujio wa Sserunkuma umeifanya Simba kuwa na wachezaji sita wa kigeni; Waganda watatu (Emmanuel Okwi, Joseph Owino na Sserunkuma, Warundi wawili (Amissi Tambwe na Pierre Kwizera) na Mkenya mmoja (Kiongera).
Katika mahojiano maalum kwenye ofisi za Makao Makuu ya TFF zilizopo Posta jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema Simba wanapaswa kusajili kwa kufuata Kanuni za Ligi za TFF na taratibu zinazoongoza soka.
"Kwa sasa (jana saa 6:37 mchana) hatujapokea kitu chochote kutoka Simba kuhusu usajili unaoendelea wa dirisha dogo, tunasikia tu wamemsajili Sserunkuma lakini hatujapata taarifa rasmi," Wambura alisema.
"Simba itaruhusiwa kusajili mchezaji mpya/wapya wa kigeni msimu huu endapo tu itavunja mkataba/mikataba na wachezaji wa kigeni ilio nao kwa sasa.
"Kuna mambo matatu yanayothibitisha kuvunjwa kwa mkataba wa mchezaji; mchezaji mwenyewe kuvunja mkataba, mchezaji kufariki au klabu kuamua kuvunja mkataba wa mchezaji husika. Hili la Kiongera na Sserunkuma hawajatueleza maamuzi yao."
Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope imeeleza kuwa imesitisha mkataba wake na Kiongera na kumuondoa kwenye orodha ya wachezaji wake kwa ajili ya msimu huu na atakapopona, mkataba huo utaendelezwa, kauli ambayo inaonekana kama Kiongera bado ni mchezaji wa Simba. Dirisha dogo la usajili lilifunguliwa Novemba 15 na litafungwa Desemba 15.
NIPASHE