Samuel Ruhuza (kulia) |
ALIYEWAHI kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha NCCR Mageuzi Samuel Ruhuza amesema uelewa mdogo na posho wanaopokea wajumbe wa Bunge la Katiba ndicho chanzo kikubwa kinachosababisha kutohairishwa kwa bunge hilo linaloendelea Mkoani Dodoma.
Ruhuza alisema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam ambaye alitaka kujua nini mtazamo wake juu ya Bunge la Katiba.
Alisema uelewa wa katiba ni changamoto kwa wananchi walio wengi ila inatia shaka pale ambapo wawakilishi wao katika bunge lao wanakuwa na uelewa mdogo zaidi na kinyume chake ni kutoa kauli za kashfa na sio za kujenga hoja ambazo zinaweza kuleta katiba nzuri.
Katibu Mkuu huyo wa zamani alisema kwa asilimia kubwa ya wajumbe wa bunge hilo wanaonekana ni watu ambao wanafikiria maslahi yao jambo ambalo linaweza kupatikana kwa katiba isiyo na tija kwa wananchi na nchi kwa ujumla.
Alisema wapo wajumbe hasa wa chama tawala (CCM) ambao wanaonekana kuwa wameambiwa maneno ya kusema jambo ambalo si haki kutokana na ukweli kuwa kilichopo kwenye rasimu ni maoni ya wananchi na sio chama.
“Mimi nimekuwa nikifuatilia tangu Bunge hilo lilivyo anza tatizo kubwa ni baadhi ya wajumbe hasa kutoka CCM wanaonekana kuwa hawajaenda pale kama wao ila wapo kutokana na msimamo wa chama jambo ambalo sahihi.”, alisema Ruhuza.
Ruhuza alisema pamoja na uelewa mdogo juu ya utengenezaji katika posho pia ni sababu kubwa ambayo inachangia kutohairishwa kwa bunge hilo ambalo limekosa mvuto kwa jamii ya Watanzania.
Alisema iwapo posho isingekuwepo ni dhahiri baadhi ya wajumbe ambao sio wanachama wa CCM wasingeendelea kujadili lakini ni ukweli kuwa 300,000 sio ndogo kwa siku hivyo ni vigumu kuikataa kama huna uzalendo na nchi yako.
Aidha alisema katika kuthibitisha hilo ni katika suala la muda wa wabunge kuwepo katika madaraka kwa kipindi cha miaka kumi na tano ambapo wamekiondoa na kusahau kuwa Rais yeye ana kikomo cha uwepo wa nafasi hiyo.
Ruhuza alisema ni wazi kuwa wabunge wengi waliopo katika bunge hilo wanatetea maslahi yao na sio jambo ambalo linaweza kukosekana au kupatikana katiba ambayo itakuwa na maslahi kwa jamii.
Katibu huyo alisema ni vigumu rasimu ya katiba iliyopendekezwa na tume ya katiba kukubalika kwa wanasiasa kutokana na ukweli kuwa inagusa maslahi ya wanasiasa wengi ambao wapo katika Bunge la Muungano kutokana na mazingira yasiyovutia watu wengi.
Alisema rasimu inataka kuwepo kwa wabunge wawili kila mkoa na kuondolewa kwa viti maalum hivyo ni wazi kuwa wajumbe waliowengi wataendelea kuipinga kwa kila njia kwa dhana kuwa fulani akiingia madarakani atampatia nafasi.
Kuhusiana na sintofahamu iliyopo juu ya idadi ya serikali ambazo zimependekezwa alisema ni vema wananchi na viongozi wote wakatambua kuwa muungano hauwezi ukawa kwa kila kitu hasa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ulizaa Tanzania.
Alisema ni ngumu kuamni kuwa muungano upo wakati ni wazi kuwa Rais wa Zanzibar analindwa na mwanajeshi kama anavyolindwa Rais wa Muungano.
Katibu huyo wa zamani alisema ni vigumu kwa wazanzibar kukubaliana na rasimu iliyopo kwani inawanyanganya madaraka ambayo wamepewa na Katiba ya Zanzibar iliyopo sasa.
Ruhuza alitoa rai kwa Watanzania kutambua kuwa wao ndio wanatakiwa kusimamia maslahi yao wenyewe kwani wanasiasa hawawezi kuwa sahihi kwa kila jambo ambapo alitolea mfano katika suala hilo la katiba wananchi wamekuwa wakiambiwa mambo ambayo hayana tija kwa maslahi yao.