Na Somoe Ng'itu, NairobiSHIRIKISHO la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na la Kenya (FKF) yamechafuka baada ya kushindwa kulipia malazi kwa wakati timu zinazoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji huku pia wakikumbwa na kashfa ya kutoa hundi 'feki'.
Licha ya mbwembwe za Kombe kupelekwa uwanjani kwa helikopta,
Timu ya Taifa ya Sudan ilichelewa kufika uwajani kutokana na uongozi wa Hoteli ya Milele kuwazuia wakitaka kulipwa kwanza fedha zao kutoka FKF.
Waamuzi waliochezesha mechi kati ya Kilimanjaro Stars na Zambia (Chipolopolo), pia uongozi wa Hoteli ya Mvuli House uliwazuia kwa muda kutoka ukidai kulipwa kwanza kwa gharama zao za malazi.
Wachezaji wa timu ya soka ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) jana walizuiwa na uongozi wa Hoteli ya The Strands iliyoko Nairobi West, kuondoka kutokana na deni la Sh.milioni 5.5 za Kenya.
Uongozi wa hoteli hiyo kwa kutumia askari wake iliwazuia wachezaji wa Zanzibar Heroes kuondoka hotelini hapo hadi watakapolipwa fedha wanazoidai FKF.
Wachezaji hao ambao timu yao ilitolewa katika hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Chalenji tangu Desemba 5, mwaka huu walishindwa kurejea kwao kutokana na kukosa tiketi za kurudia pamoja na kuzuiwa na wamiliki wa hoteli mpaka deni lao watakapolipwa na FKF.
Kutokana na vurugu zilizokuwa zinafanywa na wachezaji wa Zanzibar Heroes wakisisitiza kuondoka iliwalazimu wamiliki wa hoteli hiyo kuwaita askari wengine wa Jeshi la Polisi la Kenya kwa ajili ya kuhakikisha amani inakuweao kwenye eneo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa Zanzibar Heroes, Awadh Juma, alisema kwamba walipigiwa simu na Mwenyekiti wa FKF, Sam Nyamweya, jana saa 10:00 alfajiri akiwataka wajiandae ili waondoke na ndege ya saa tatu.
Juma alisema baada ya kujiandaa na kubeba mabegi yao saa 12 asubuhi jana, walikuta askari wamejaa kwenye geti wakiwaeleza hawaruhusiwi kuondoka mpaka FKF watakapolipa deni wanalowadai.
Habari kutoka ndani ya hoteli hiyo zilieleza kuwa FKF ilikuwa inadaiwa zaidi ya Sh. milioni 20 za Kenya ambazo ni gharama za kuihudumia timu hiyo pamoja na kikosi cha Nigeria (Super Eagles) kilichokaa hapo wakati kimekuja nchini hapa kuikabili Harambee Stars mapema mwaka huu.
Hata hivyo, FKF ililipa nusu ya deni hilo na ilidaiwa pia kutoa hundi feki ya Sh. milioni 5.5 za Kenya jambo ambalo liliwaudhi wamiliki wa hoteli hiyo.
Saa 3: 20 asubuhi Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, alifika katika hoteli hiyo ili kuanza mazungumzo na wamiliki wa hoteli hiyo lakini hakufanikiwa mpaka pale alipoamua kumuita Nyamweya.
Saa 4:44 Nyamweya alifika katika eneo la tukio kuendelea na mazungumzo lakini kilichoafikiwa ni uongozi wa hoteli kuhitaji fedha zao ndiyo iwaruhusu wachezaji wa Zanzibar Heroes waondoke.
Hata hivyo, wachezaji wa Zanzibar Heroes waligoma kumruhusu Nyamweya kuondoka kwenye hoteli hiyo na kulazimisha waruhusiwe kuondoka na ikiwezekana wakalale hata uwanja wa ndege na si kubaki hotelini hapo.
Kocha Mkuu wa Zanzibar Heroes, Salum Bausi, alilazimika kufanya maamuzi magumu ya kuwataka wachezaji wake wawe wavumilivu na kumruhusu Nyamweya aondoke na kuongozana na mwakilishi wa hoteli kwenda kulipwa fedha wanazodai.
Saa 6:12 mchana Nyamweya na wenzake pamoja na Musonye waliondoka hotelini hapo na kuelekea benki ili kukamilisha zoezi hilo na kuwaeleza wachezaji kwamba wataondoka leo kurejea Tanzania.
Mbali na Zanzibar Heroes, pia wachezaji wengine wa timu ya Sudan Kusini ambao nao walitolewa kwenye hatua ya makundi walilazimika kujilipia wenyewe tiketi za kurudi nyumbani.
NIPASHE