Kikosi cha KMKM kitakachotua leo Dar kuumana na Simba na Yanga mwishoni mwa wiki |
Kwa mujibu wa mratibu wa mechi hiyo George Wakuganda alisema, timu hiyo itawasili jioni kwa Boti ya kwenda Kasi ikiwa na kikosi kamili na mechi ya kwanza ni kati ya Yanga na KMKM Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam, huku Simba wakicheza keshokutwa katika uwanja huo huo.
Alisema vingilio kwa VIP A ni sh.20,000, VIP B sh.15,000, VIP C sh.10,000, orange sh.7,000 , bluu na kijani viingilio ni sh.5,000.
"Tunaamini kwa kipindi hiki kirefu ambacho timu zilikuwa mapumzikoni, wachezaji watarudi na kitu kipya uwanjani ikiwa na makocha kuwatambulisha wachezaji wao wapya," alisema Wakuganda
Kwa upande wa kocha wa Yanga Ernest Brandts alisema anaimani kabisa mechi hiyo itampa mwanga kuelekea mechi hiyo na wapinzani wao Simba, hivyo anazidi kuwanoa wachezaji wake ili wawe fiti zaidi.
"Naamini KMKM sio timu mbaya hasa kipindi hiki ambacho timu yangu inajiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo kwa kiasi kikubwa itanisaidia kujenga kikosi changu," alisema kocha huyo.
Alisema pia mechi hiyo atawatumia wachezaji wake wapya kipa Juma Kaseja na kiungo Hassan Dilunga ambao wamesajiliwa kipindi hiki cha dirisha dogo kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kikosi chake.
Kocha huyo alisema wachezaji wake wote wapo fiti ukiondoa wale ambao wapo kwenye timu zao za Taifa, waliomo kwenye michuano ya Kombe la Challenji ambayo inamalizika leo nchini Kenya.
Alisema mechi hiyo imekuja kipindi kizuri kwa kuwa wachezaji wake walikuwa mapumziko, hivyo hata wakivaana na Simba atakuwa amejua wapi kuna mapungufu katika kikosi chake kabla ya mechi hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.
Hata hivyo kocha huyo alisema wachezaji waliomo kwenye timu za Taifa, hana uhakika kama watacheza mechi hiyo kwa kuwa siku ya mechi ndio wanatua nchini wakitokea Nairobi, Kenya.
No comments:
Post a Comment