|
Said Mbelwa na Karama Nyilawila wakichuana Jumamosi kabla ya kutibua pambano lao |
WAKATI hatma ya mshindi wa pambano la kimataifa kuwania mkanda wa UBO ikitarajiwa kuamuliwa chini ya jopo la mashirikisho ya ngumi Tanzania na UBO, Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPB)-Limited) imelaani kitendo kilichofanywa na bondia Said Mbelwa kumpiga Karama Nyilawila nje ya ulingo.
Mbelwa alimsukuma na kutupa nje ya ulingo mpinzani wake kabla ya kumrukia miguu miwili wakati wa pambano lao lililochezwa kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese kwa kilichodaiwa kukerwa kupigwa kichwa na mpinzani wake.
Kitendo hicho kilipelekea pambano hilo kuvunjika katika raundi ya 8 kati ya 10 zilizokuwa zichezwe na mpaka sasa wasimamizi wa pambano hilo wameshindwa kumtangaza mshindi.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Anthony Rutta aliiambia MICHARAZO kwa njia ya simu jana kuwa wameshindwa kutangaza mshindi mpaka jopo la wadau wa ngumi wakutane kujadili tukio hilo kwa kina.
"Tunamsubiri Rais wa PST, Emmanuel Mlundwea ambaye ni Mwakilishi wa UBO-Afrika, arejee toka Thailand na kuitisha kikao cha jopo la wadau wa ngumi ikihusisha vyama vya PST, TBBO na TPBC kujadili kilichotokea na kutoa maamuzi kwa sasa nahofia kusema lolote," alisema Rutta.
Alipoulizwa juu ya kanuni na sheria kwa bondia anayeanzisha fujo kwenye ulingoni kwa namna yoyote na kuvuruga pambano adhabu yake huwa ni nini, Rutta alisema huwa si chini ya kifungo cha miezi 6 cha kutocheza ngumi.
"Atalkayebainika anaweza kufungiwa kati ya miezisita na miaka miwili na mpinzani wake kupewa ushindi kulingana na itakavyobainika nani mkosa," alisema.
Hata hivyo, Rais wa TPBO-Limited, Yasin Abdallah 'Ustaadh' waliosimamia pambano ya utangulizi siku ya pambano hilo la Nyilawila na Mbelwa alilaani tukio hilo na kuelekeza lawama zake kwa Mbelwa kuwa hakufanya uungwana.
"TPBO tunalaani kilichofanywa na Mbelwa, kwani siyo uungwana hata kama mwamuzi na mpinzani wake hawakumtendea haki kwenye ulingoni, mambo haya ndiyo yanayovuruga mchezo wetu na kuonekana wa kihuni," alisema.
Ustaadh alisema pia anashangazwa mtandao wa UBO kutoa taarifa mechi hiyo haina mshindi wakati mwakilishi wake, Emmanuel Mlundwa yupo nje ya nchi na hakuwepo kwenye pambano hilo.
"Sidhani kama ni sahihi, Mlundwa hakuwepo ukumbini, ila mtandao wao umetoa ripoti kuwa mchezo hauna mshindi, nani aliyetoa taarifa hizo wakati mwakilishi yupo Thailand," alisema Ustaadh na kuoingeza;
"Kama ingekuwa ni sisi TPBO moja kwa moja trungemtangaza Nyilawila kuwa mshindi kwa sasa kilichofaywa na mpinzani wake kipo nje ya kanuni na sheria ya ngumi na TPBO tunalaani kwai inatuvurugia sana ngumi zetu," alisema.