JAMHURI YA MUUNGANO WATANZANIA
BUNGE LA TANZANIA
__________
TAARIFA MAALUM KUHUSU BUNGE NA KAMATI
Ofisi
ya Bunge imepokea kwa masikitiko taarifa kuhusu tafsiri ya kusitisha
matangazo ya Shughuli za Bunge na Kamati, kinyume na jinsi ilivyoakisiwa
katika mazungumzo ya pamoja kati ya Wanahabari na Katibu wa Bunge. Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa, Bunge la Jamhuri ya Muungano halina
mpango wa kusitisha matangazo ya Bunge wala Kamati zake, ambazo kwa
mahitaji ya sasa nazo zinapaswa kurushwa moja kwa moja kama sehemu ya
mpango kabambe wa kuwapasha Wananchi yanayojiri katika Uendeshaji bora
wa Shughuli za Bunge.Dhamira ya Bunge ni kuhakikisha kuwa mpango kabambe
uliopo ni kumfikia kila Mtanzania alipo na kwa uwezo alionao aweze
kupata na kushiriki katika uendeshaji wa shughuli za Bunge.
Hivyo Mpango
mkakati uliopo utakuwa kuboresha mawasiliano ya kawaida kupitia
Teknolojia ya Mawasiliano TEKNOHAMA, kwa wale watakaokuwa na uwezo wa
kupata huduma za mtandao, na tayari tumeanza kurusha live video striping kupitia
tovuti ya Bunge, na hata wale watakaopenda kujua zaidi, basi wanaweza
kupitia majadiliano ya Bunge kwa nyakati tofauti. Aidha, kwa wale
watakaokuwa na uwezo wa kushika mawimbi ya Radio, basi wataweza
kufuatilia majadiliano ya Bunge katika Radio ya Bunge inayotarajiwa
kuzinduliwa hivi karibuni katika masafa yanayoweza kupatikana nchi
nzima, hii ikiwa ni jitihada za ziada kwa kuwa kuna Radio zinazotoa
huduma hiyo ya moja kwa moja vizuri hadi sasa, kama vile RTD,BBC, STAR
etc. Aidha, kwa wale watakaoweza kuwa na uwezo wa kumudu Luninga, basi
Bunge limejipanga kuwapatia huduma hiyo moja kwamoja kupitia katika
mtandao wake mpya utakaokuwa ukirushwa masaa 24, baada ya mitambo mipya
ya kunakili majadiliano Bungeni na katika Kamati kusimikwa.
Hivyo basi
utaratibu uliopo sasa utaendelea kutumika ambapo vituo vyote vya
Television vitapewa fursa ya kurusha matangazo kwa utashi wao bila
kuwekewa mipaka ya aina yoyote sambamba na matangazo yatakayotolewa na
mitandao ya Bunge. Utaratibu huu unatokana na uamuzi wa pamoja kati ya
Bunge na Tume ya Mawasiliano, ambapo vipindi vyote vya Bunge vitakuwa
vinarushwa bila kudhaminiwa na taasisi yoyote zaidi ya mamlaka tajwa juu
ya mawasiliano TCRA. Hivyo basi kwa maelezo hayo ni dhahiri kuwa Bunge
halina mpango wa kusitisha matangazo ya TV wala yale ya Radio
au Teknohama, bali linatarajia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa
utaratibu ulio rahisi na unaoweza kusimamiwa na pande zote, yaani Bunge
na Wananchi. Aidha, kwa utaratibu uliopo sasa,Bunge halirushi matangazo
ya aina yoyote, bali hutoa nakala ya majadiliano hayo kwa mtu yeyote
atakaye au TV na Radio yoyote kupitia katika mitambo yake. TV zote
zinazorusha matangazo ya Bunge hupata feed toka katika mitambo ya
Bunge, na pale wanapoona yafaa basi huomba kutumia mitambo yao na hivyo
kutumia fursa hiyo kuingiza Camera na Wanahabari ndani ya ukumbi wa Bunge
kwa minajiri hiyo. Kuzingatia mabadiliko tajwa, utaratibu huo umepewa
ukomo, ili sasa hapatakuwa na fursa ya kuingiza Camera ndani ya Kumbi za
Bunge, bali wote watakaotaka kurusha matangazo ya Bunge kwa utashi wao,
watapata clear feed toka katika mitambo ya Bunge na hivyo kurusha live vipindi
vyote vya Bunge bila kuhaririwa kama ilivyonakiliwa katika makala
mbalimbali.
Hata hivyo utaratibu huu wa kutumia Camera katika
Kumbi
utaendelea katika Kamati za Bunge, hadi hapo mitambo mipya ya
mawasiliano itakapofungwa katika Kumbi zote za Kamati. Hivyo basi, ili
kwenda sawia na taratibu hizo, Bunge litaendesha zoezi la kuwatathmini
Waandishi wote wa habari za Bunge na kuwasajili kwa vigezo
vitakavyoafikiwa kati ya Baraza la Habari,Idara ya Habari na Bunge
lenyewe. Aidha ili kulinda heshima na maadili ya utangazaji, Bunge
litatoa utaratibu (Code of Conducts for Media broadcasting) wa
namna ya kunakili na kurusha matangazo ya Bunge bila kujali yanarushwa
kwa utaratibu upi. Hili litasaidia kuweka misingi bora ya mawasilaino na
hivyo kuwapa fursa Wananchi kujua hali halisi ya matukio yote ndani ya
Bunge na katika Kamati, bila kuegemea upande wowote (Non
Partisan). Hivyo
basi, wakati zoezi la maboresho hayo likiendelea, Wananchi watajulishwa
kila hatua na matarajio tajwa na kwamba tunaendelea kusisitiza tena,
Wananchi wasiwe na hofu juu ya taarifa zilizopewa uzito usio stahili za
kusitisha matangazo ya Bunge, ambao hazikuwa sahihi na pia hazikuainisha
zoezi zima la maboresho ya upatikanaji na usambazaji wa habari za
Bunge. Tunasikitika kwa usumbufu uliowasibu wote walioakisiwa na taarifa
hiyo.
Dr. Thomas D.Kashililah
KATIBUWA BUNGE