Ramadhani Singano 'Messi' |
WACHEZAJI wawili wa klabu ya Simba, Shomari Kapombe na Ramadhan Singano 'Messi' watakwenda Uingereza kufanya majaribio kwenye kituo cha vijana cha klabu ya Sunderland inayoshiriki ligi kuu nchini humo mara baada ya kumalizika kwa ligi kuu ya Bara, imedaiwa.
Mwaliko wa wachezaji hao kwenda nchini humo umekuja kufuatia ziara ya mmiliki wa Sunderland Ellis Short na viongozi wa klabu hiyo waliyoifanya Desemba mwaka jana hapa nchini, imedaiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti Simba, Ismail Aden Rage, ambaye uongozi wake umelaumiwa kwa mwenendo mbovu wa timu katika mechi za karibuni alisema wachezaji hao wakiwa nchini humo watafanya majaribio kwenye kituo hicho.
Aidha, alisema kuwa wakati wachezaji hao wakitarajiwa kwenda nchini humo baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi, makocha wa Simba watakwenda nchini humo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali huku pia makocha wa klabu hiyo ya ligi kuu ya Uingereza watakuwa wakija nchini kutoa mafunzo mbalimbali kwa wachezaji.
Aidha, alisema kuwa kwa kuanzia kwenye mchezo wa kesho wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Reacreativo Libolo ya Angola, Simba itavaa jezi walizopewa na klabu hiyo ya Sunderland.
"Lakini pia tumekubaliana kuanzia msimu ujao tutakuwa tukipokea vifaa kamili kutoka kwa wenzetu wa Sunderland na tutakuwa tukivitumia kwenye michezo mbalimbali," alisema Rage.
Alisema kuwa jezi hizo walizopewa na Sunderland pia zitakuwa na nembo ya wadhamini wao wa nyumbani na kampuni inayoidhamini timu hiyo ya Ulaya ya Invest in Africa.
No comments:
Post a Comment