STRIKA
USILIKOSE
Saturday, February 16, 2013
TFF yashitakiwa mahakamani Mwanza
Na Faustine Feliciane
ALIYEKUWA mgombea wa nafasi mbili za Rais na mjumbe wa Kamati ya utendaji katika uchaguzi wa Shirikisho la soka (TFF) uliopangwa kufanyika Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam, Richard Rukambula amefungua kesi Mahakama Kuu kanda ya Mwanza kuzuia uchaguzi huo akishinikiza kurejeshwa kwenye mchakato.
Rukambula amefungua kesi hiyo itakayosikilizwa keshokutwa katika Mahakamu Kuu kanda ya Mwanza kupinga mchakato wa kumuengua kwenye uchaguzi huo kwa madai kuwa hakutendewa haki katika kuengeliwa kwake kwenye mchakato huo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana kutokea Mwanza, Rukambula alisema kuwa amefika hatua ya kusimamisha uchaguzi huo wa TFF ili suala lake lijadiliwe na haki itendeke kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Wakati Rukambula akifikia hatua hiyo, Katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema shirikisho halijapata taarifa hizo lakini akasema pindi watakapoitwa mahakamani, vyombo husika ndani ya TFF vitakaa na kufanya maamuzi.
Rukambula amefungua kesi hiyo akisistiza hakutendewa haki katika kumuengua kwenye mchakato wa uchaguzi huo kwa maelezo kuwa aliomba nafasi mbili badala ya moja tu, kama inavyotakiwa.
"Tayari hili jambo limeshafika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza na kesi imeshapangiwa jaji atakayesikiliza suala hili ," alisema Rukambula,
Aidha, alisema jalada la kesi hiyo lipo kwa Jaji Muruma.
"Leo hii (jana) nimemtuma mtu na anakuja huko Dar es Salaam na ndege ya jioni ili kuleta barua kwa TFF ya kuitwa Mahakamani kusikiliza kesi hiyo," alisema Rukambula.
Aidha, alisema ameiomba Mahakamu Kuu kuisikiliza kwa haraka kesi hiyo ili imalizike kabla ya siku ya kufanyika kwa uchaguzi wa TFF; ili ikiwezekana arudishwe kwenye mchakato huo wa uchaguzi.
Aidha, alisisitiza kuwa maombi aliyoyapeleka mahakamani hapo ni ya kusimamisha uchaguzi huo ili mchakato wa kusaili wagombea urudiwe tena.
Rukambula anasema kuwa kamati ya uchaguzi ya TFF ilimuengua kwa madai kuwa aliomba kugombea nafasi mbili tofauti kwenye uchaguzi huo kitu ambacho ni kinyume na kanuni za uchaguzi wa TFF.
"Mimi sikuomba kugombea hizo nafasi kwa kufuata kanuni hizo wanazozisema bali nilifuata tangazo lao la uchaguzi walilolitoa ambalo halikuelezea kikomo cha kuwania nafasi kwenye uchaguzi huo," alisema Rukambula.
Aidha, alisema kuwa kama ni kosa kugombea nafasi mbili ni kwa nini TFF walikubali malipo yake ambapo alilipia fomu ya kuwania Urais na ile ya Ujumbe na kupewa stakabadhi zilizofuatana?
CHANZO:NIPASHE JUMAMOSI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment