STRIKA
USILIKOSE
Saturday, February 16, 2013
Azam kuvuna nini Afrika leo?
MSHAMBULIAJI John Bocco ataongoza safu ya ushambuliaji ya Azam FC ambayo leo inaikabili timu ya Al Nasri Juba ya Sudan Kusini kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika.
Bocco ambaye alikosa michezo kadhaa ya ligi kuu kutokana na kuwa majeruhi, amepona na leo atakuwepo uwanjani kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa kurejea uwanjani kwa mchezaji huyo ni faraja kwake kwa kuwa ataongeza safu ya ushambuliaji ya timu yake kwenye mchezo wa leo.
"Kwangu ni faraja kuwa na wachezaji wote muhimu kikosini kwa sababu mchezo wa kesho (leo) ni mkubwa na muhimu sana kwetu ukizingatia tunacheza kwenye uwanjawa nyumbani,' alisema Hall.
Aidha, alisema kuwa haifahamu timu hiyo ya Sudan Kusini hivyo watacheza kwa tahadhari huku wakiwa na lengo la kuibuka na uhsindi.
Alisema kuwa anafahamu wapinzani wao matokeo ya sare yatakuwa na faida kubwa kwao hivyo ni lazima wagangamale ili kupata ushindi.
Hall, alisema kuwa katika mchezo wa leo atatumia mfumo wa kushambulia na kulinda goli hili kutowaruhusu wapinzani wao kupata goli la ugenini ambalo litakuwa na faida kubwa kwao (Al Nasri).
Aidha, alisema kuwa kipindi cha kwanza cha mchezo wa leo kitakuwa kigumu zaidi kwa kuwa timu zote hazifahamiani.
"Siijui hii timu lakini kama imefika hapa ina maana ni timu nzuri, tutacheza kwa tahadhari zaidi katika kipindi cha kwanza na pamoja ya kuwa tuna lengo la kushambulia sana pia tutakuwa makini kwenye kulinda goli letu," aliongezea kusema Hall.
Aidha, alisema kuwa pamoja na ugeni wa timu hiyo, amekiandaa vizuri kikosi chake na anategemea kupata ushindi kwenye mchezo huo wa leo ambao ni wa kwanza kwa Azam FC kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa yanayoaandaliwa na Shirikisho la soka barani Afrika, CAF.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment