Didier Kavumbagu (kushoto) |
Na Adam Fungamwango
WANACHAMA, mashabiki na wapenzi wa Yanga tawi la Mwananyamala, walipata fursa ya kutembelewa na mshambuliaji kipenzi Didier Kavumbagu kwenye tawi la klabu hiyo liitwalo Green Stone maarufu kama 'Uturuki'.
Kwa siku mbili mfululizo, mshambuliaji huyo mwenye magoli tisa Ligi Kuu, alilitembelea tawi hilo la Uturuki na kupata fursa ya kukutana na mashabiki, wanachama na wapenzi wa klabu ya Yanga na kubadilishana nao mawazo.
Mwenyekiti wa tawi hilo, Lumole Matovola maarufu kama 'Big' amesema kuwa wamefurahi kutembelewa na mchezaji huyo na kitendo cha kushikwa mikono na kukumbatiwa na wanachama ni kama tambiko kwa mchezaji ili azidi kuifanyia makubwa Yanga.
"Unajua mchezaji mkubwa kama huyu tena wa kigeni, kuja uswahilini kama huku na kuzungumza na wanachama ni kama tambiko, hivyo tunaamini itampa chachu ya kuona kumbe anapendwa na azidi kutufungia magoli," alisema Big na kuendelea.
"Tumekaa na umebadilishana naye mawazo, kusema kweli amefurahi sana kwa sababu amekuja kwa siku mbili hapa na Jumatano iliyopita akapiga bao lake la tisa, huu ni mfano wa kuigwa kwa nyota wengine, wakipata ruhusa ya kupumzika watembelee wapenzi wako matawini," alisema.
Wakati hayo yakiendelea, Big amesema tawi lao limepokea msaada ya viti sita kutoka kwa mwanachama mwenzao Yusuph Mhandeni na kufanya tawi hilo kuwa na viti nane na kusisitiza wanachama wengine kusaidia tawi hilo kwa hali na mali.
No comments:
Post a Comment