Mfungaji wa bao la Yanga leo dhidi ya Toto African |
Yanga ikiicheza kwenye uwanja wa Taifa ilishindwa kuonyesha makeke yake licha ya kupata bao katika kipindi cha kwanza lililofungwa na Hamis Kiiza na kukataliwa na mwamuzi akidai mfungaji alimchezea rafu kipa wa Toto kabla ya kutumbukiza mpira wavuni kwa kichwa na kufanya hadi mapumziko matokeo yawe 0-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kosa kosa za hapa na pale baina ya timu zote huku Hamis Kiiza, Simon Msuva na Jerryson Tegete wakiongoza kwa kukosa mabao.
Hata hivyo mabadiliko ya kocha wa Yanga ya kumtoa Tegete na kumuingiza Nizar Khalfan yaliisaidia Yanga kupata bao lililofungwa na Nizar katika dakika ya 78 na kuipa ushindi huo muhimu ambao ulionekana kutowekwa katika pambano la leo.
Toto ilimpoteza mchezaji wake, Eric Mlilo, huku Kiiza akifunga bao katika kipindi hicho cha pili lililokataliwa tena na mwamuzi kwa madai alikuwa ameotea kabla ya kutumbuiza wavuni.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha jumla ya pointi 45 kutokana na mechi 19 ilizocheza na kuiacha Azam waliopo nafasi ya pili kwa pointi nane baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Polisi Morogoro.
Sare hiyo imeifanya Azam kufikisha pointi 37 kwa michezo 19 iliyocheza huku kukisaliwa mechi saba kabla ligi hiyo msimu huu haijamalizika.
Kwenye uwanja wa Chamazi, Azam ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya tano kupitia kwa John Bocco 'Adebayor' bao lililodumu hadi mapumziko.
Bao la kusawazisha na Polisi lilifungwa kwenye kipindi cha pili katika dakika ya 54 na Mokili Rambo na kuifanya timu hiyo iambulie pointi moja na kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi katika duru la pili.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa pambano moja tu litkalokutanisha 'ndugu' wawili, Simba ya jijini Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga pambano litakalochezwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Msimamo kamili wa Ligi Kuu baada ya mechi ya leo:
P W D L GF GA GD Pts
1 Yanga 19 14 3 2 36 12 24 45
2 Azam 19 11 4 4 32 16 16 37
3 Simba SC 18 8 7 3 26 15 11 31
4 Coastal U 19 8 7 4 21 16 5 31
5 Mtibwa 20 8 7 5 22 18 4 31
6 Kagera Sugar 20 8 7 5 21 17 4 31
7 Ruvu Shooting 18 8 5 5 21 17 4 29
8 JKT Oljoro 19 6 6 7 20 22 -2 24
9 Mgambo JKT 20 7 3 10 14 19 -5 24
10 TZ Prisons 20 4 8 8 11 17 -6 20
11 JKT Ruvu 19 5 4 10 16 30 -14 19
12 Polisi Moro 19 3 7 9 10 19 -9 16
13 Toto African 20 2 8 10 15 28 -13 14
14 African Lyon 20 3 4 13 13 32 -19 13