LONDON, England
Mshmbuliaji wa Liverpool Luis Suarez ameomba msamaha baada ya kukubali adhabu ya kutocheza mechi 10 kwa kumng'ata Branislav Ivanovic wa Chelsea katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Uingereza mwishoni mwa wiki iliyopita.
Muuruguay huyo alikuwa na muda mpaka mchana jana kupinga adhabu ya Chama cha Soka ya kuongeza mechi saba katika adhabu ya kawaida ya kukosa michezo mitatu kwa kosa la kufanya ukatili lakini akaamua kutobishia.
"Nataraji kuwa watu niliowaudhi Jumapili iliyopita watanisamehe na narudia tena kumuomba radhi binafsi Branislav," Suarez aliseka katika ukurasa wake wa Twitter.
"Ingawa ni wazi kwamba mechi 10 ni nyngi kuliko vifungo vilivyowahi kutolewa katika kosa kama hili huko nyuma ambapo wachezaji walijeruhiwa, nakubali kuwa kitendo changu kilikuwa hakikubaliki kwenye uwanja wa soka hivyo sitaki kuleta picha mbaya kwa watu kwa kukata rufaa."
Suarez, ambaye alimng'ata Ivanovic mkononi katika sare ya 2-2 kwenye uwanja wa Anfield wiki-endi iliyopita, hatoweza kuichezea Liverpool katika michuano ya ndani mpaka Septemba.
Liverpool, ambayo ilimpiga faini Suarez, ilisisitiza kusikitishwa kwake na uamuzi wa FA wa kumfungia Suarez kwa mechi 10.
"Adhabu dhidi ya Luis ilikuwa yake binafsi kuamua na ni lazima tuheshimu uamuzi wake wa kutokata rufaa kufungiwa mechi 10," mkurugenzi mtendaji Ian Ayre alisema.
Kocha wa Liverpool Brendan Rodgers aikilaumu chama cha soka kwa ukali wa adhabu ya Suarez na palikuwa na kuungwa mkono na makocha wa timu pinzani jana.
"Katika kesi hii, ukubwa wa adhabu na kosa vinaonekana kupishana mno kulingnaisha na makosa ambayo wachezaji wengine wamewahi kuadhibiwa nayo," kocha wa Arsenal Arsene Wenger aliwaambia waandishi wa habari.
"Nadhani kilichommaliza kabisa Suarez ni historia yake, ambayo ina makosa mengi.
"Ndiyo sababu ameadhiwa vikali sana, ndiyo sababu pekee ambayo naweza kuiona."
Kocha wa Manchester City Roberto Mancini alisema katika mkutano wake wa Ijumaa na waandishi wa habari: "Mechi tano au sita zilitosha, huu ndiyo mtazamo wangu lakini sifanyi kazi FA."
Ni mara ya pili kwa Suarez, 26, kufungiwa kwa kumng'ata mchezaji wa timu pinzani baada ya kumng'ata Otman Bakkal wa PSV Eindhoven kwenye shingo wakati akiichezea Ajax 2010, na kufungiwa mechi saba.
Suarez alifungiwa pia mechi nane msimu uliopita baada ya FA kumuona ana kosa la kumbagua kwa rangi ya ngozi Patrice Evra wa Manchester United Oktoba 2011.
Reuters
Suarez