STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, April 27, 2013

Ruvu Shooting walalamikia gharama, lakini yaionya Simba

Kikosi cha Ruvu Shooting Stars
UONGOZI wa Ruvu Shooting umesikitishwa na gharama ulizobebeshwa na serikali na shirikisho la soka, TFF, kufuatia kuahirishwa kwa pambano la ligi kuu ya Bara dhidi ya Simba juzi.
Lakini uongozi huo umesisitiza kuwa kipigo kwa 'mnyama' kipo palepale timu hizo zitakapokutana katika tarehe mpya - Mei 5.
TFF ilitangaza kuahirisha pambano hilo lililokuwa lichezwe kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa chache kabla ya kufanyika kwake na kupanga lifanyike Mei 5.
Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire aliimbia MICHARAZO jana kuwa wamekerwa na kusikitishwa na kitendo hicho kilichowatia hasara kubwa ya kuweka kambi, kufanya maandalizi na kusafiri kutoka Mlandizi mpaka Dar Es Salaam na kukaa siku kadhaa kisha kuahirishwa mechi.
Bwire alisema licha ya TFF kuwaomba radhi na kujitetea kuwa haihusiki na kuzuiwa kutumiwa kwa Uwanja wa Taifa kutokana na kupisha maandalizi ya sherehe za Muungano, lakini inastahili lawama kwa kitendo hicho kwani walipaswa kulifahamu hilo mapema na kuzipunguzia gharama timu husika.
"Tumeumizwa sana na kilichofanyika, tulifanya maandalizi yenye gharama kwa ajili ya mechi hiyo, hata hivyo hatuna mpango wa kudai fidia yoyote kwani TFF imeshajitetea kwetu na sasa tunafikiria mechi yetu ya Mei Mosi dhidi ya JKT Oljoro," alisema.
Bwire alisema pamoja na kuiwaza mechi hiyo ya Oljoro, lakini Simba wasifikirie tayari wameshaepuka kipigo kutoka kwao, kwani hata Mei 5 wakikutana lazima wakutane nacho kwa maandalizi waliyofanya na kiu yao ya kumaliza kwenye 'Nne Bora'.
"Kipigo kwa Simba kipo pale pale wameahirishiwa tu, tunataka kuonyesha kuwa Ruvu ni timu nzuri na tunataka tumalize katika Tatu au Nne Bora msimu huu, kwani kwa mechi zilizosalia tuna uwezo wa kufikisha pointi 42," alitamba Bwire.
Timu hiyo ipo katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 30 ikiwa na michezo minne kabla ya kumaliza msimu wa 2012-2013.

No comments:

Post a Comment