Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya mabao yao katika ligi kuu msimu huu, ambapo jana kikosi chao kilitawazwa kuwa mabingwa bila kushuka dimbani baada ya Azam kung'ang'aniwa Mkwakwani. |
NYOTA wa klabu ya Yanga jana wangeweza kuwa katika jumba la starehe wakinywa juice kupooza makoo, lakini wamerefusha rekodi ya kutwaa mara nyingi zaidi ubingwa wa Bara, baada ya sare ya 1-1 kati ya Coastal Union na Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani kuipa taji la 23 la ligi kuu bila jasho.
Kwa matokeo hayo, Azam iliyokuwa na matumaini ya mbali ya kuikatili Yanga katika kuwania ubingwa uliotemwa na Simba msimu huu, sasa itaweza kufikisha pointi 54 kama itashinda michezo yake mwili iliyobaki.
Idadi hiyo ni pointi mbili pungufu ya jumla ya alama za sasa za mabingwa wapya hao ambao pia wana michezo miwili kabla ya kumaliza msimu.
Kocha wa Azam ambayo mwishoni mwa wiki itakuwa Morocco kujaribu kuingia hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika dhidi ya RAF, Stewart Hall alilaumu ubovu wa uwanja wa Mkwakwani kuwa ndiyo sababu ya kushindwa kuweka hai ndoto ya timu yake Bara.
Mwalimu wa Coastal ambayo sasa imefikisha pointi 34 na kujiimarisha katika nafasi za katikati ya msimamo wa ligi kuu, Hemed Morocco alimlaumu muamuzi Andrew Shamba kwa kuwapendelea wageni, kwa upande wake.
Agrey Moris aliipatia Azam bao la kuongoza kwa penalti katika dakika ya 59, baada ya muamuzi kuamuri adhabu hiyo kufuatia Gaudance Mwaikimba kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Yusuf Chuma.
Ilimchukua Dany Lihanga wa Coastal Union dakika moja tu tangu kuingia kutoka benchini kusawazisha bao hilo katika robo ya mwisho ya mchezo, baada ya kumalizia wavuni pasi ya Ibrahim Twaha.
Lihanga aliingia kuchukua nafasi ya Selemani Kassim katika dakika ya 71.
Mbali na mwaka huu, tangu ligi kuu ya Bara (zamani ligi daraja la kwanza) ianze mwaka 1965 Yanga imetwaa ubingwa katika miaka ya 1968-1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991-1993, 1996-1998, 2002, 2005, 2008-2009 na 2011 kwa tofauti ya magoli.
Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo ya Yanga, Clement Sanga alisema pamoja na kufurahai kupata ubingwa mapema wakiwa na mechi mbili mkononi, hawatabweteka na badala yake watahakikisha wanashinda mechi hizo ili kuunogesha ubingwa wao.
Sanga alinukuliwa na kituo kimoja akisema furaha yao na sherehe zao za ubingwa zitanoga kama watawafunga Simba na hasa kurejesha kipigo cha aibu walichopewa msimu uliopita wa kunyukwa mabao 5-0.
Hata hivyo Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are 'Mzee Kinesi' amepuuza ndoto hizo za Yanga na kudai wasitarajie kitu kama hicho kwani Msimbazi wanataka kuivuruga furaha ya wanajangwani.
"Tunataka kuivuruga furaha ya mtani kwa kuwanyuka Mei 18 ili asherehekee kimya kimya ndani wakiwa na maumivu, tunajua hatuna ubingwa lakini tunataka kulinda heshima yetu," alisema Kinesi.
No comments:
Post a Comment