STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 28, 2015

Mdomo wamponza Jose Mourinho atozwa faini

http://static.guim.co.uk/sys-images/Observer/Columnist/Columnists/2013/6/7/1370621593808/jose-mourinho-010.jpg
Jose Mourinho
KOCHA mwenye maneno mengi anayeinoa Chelsea, Jose Mourinho ametozwa faini ya paundi 25,000 kwa kauli yake aliyodai kuna kampeni za makusudi zinazofanywa na waamuzi kuidhoofisha timu yake.
Mourinho alitoa kauli hiyo baada ya kikosi chake kukataliwa penati katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Southampton Desemba 28 mwaka jana.
Chama cha Soka cha Uingereza-FA kimemtoza faini kwa kauli hiyo ambayo inaweza kuleta mkanganyiko katika soka huku akionywa kutofanya kosa kama hilo katika siku za usoni.
Mbali na hilo Mourinho pia alionywa kwa kauli yake aliyotoa kabla ya mchezo kati ya Chelsea na Stoke City Desemba 22 ambao walikuja kushinda kwa mabao 2-0.
Kikosi cha kocha huyo usiku wa jana kilitinga Fainali ya Kombe la Ligi kwa kuing;oa Liverpool kwa jumla ya mabao 2-1 na Jumamosi inatarajiwa kuvaana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City.

Mbeya City 'yaua' Mnyama Taifa, Chollo akosa penati

mbeyacityfc 1-4 vipers fc_2014_1
Mbeya City
IMG_6078 (2)
Simba
KLABU ya Simba jioni ya leo imewanyima raha mashabiki wake baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mbeya City, huku ikishuhudiwa timu hiyo ikipoteza nafasi ya kuasawazisha bao baada ya beki wake, Masoud Nassoro 'Chollo' kukosa penati sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho.
Simba ambayo ilipata ushindi mfululizo tangu ilipotoka kwenye Kombe la Mapinduzi ambapo walinyakua kwa kuifunga kwa mikwaju ya penati Mtibwa Sugar, walianza kupata bao kupitia kwa Ibrahim Hajibu aliyefunga kwa mkwaju wa adhabu ndogo nje kidogo ya lango la Mbeya City dakika chache kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili katika pambano hilo lililochezwa wenye uwanja wa Taifa, Mbeya walionyesha upinzani mkali zaidi na kufanikiwa kurejesha bao katika dakika ya 77 kupitia Hamad Kibopile kabla ya kupata penati katika muda wa ziada kupitia kwa Yusuph Abdalla baada ya kipa wa Simba Peter Manyika Jr kucheza faulo.
Hata hivyo mfungaji wa bao hilo alifanya kosa la kizembe la kumchezea vibaya Jonas Mkude na kupewa penati ambayo Chollo aliipoteza na pambano hilo kumalizika kwa Simba kulala kwa mabao 2-1.
Kipigo hicho kimewafanya baadhi ya wanachama kjuucharukia uongozi wa juu wa klabu hiyo sambamba na Kamati ya Mashindano wakidai wameshindwa kufanya kazi.
Kwa ushindi huo wa leo Mbeya ambayo ilienda mapumziko Novemba 9 wakiwa mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo, imechupa toka nafasi ya 13 hadi nafasi ya 7 wakiwa na pointi 15 na Simba kusaliwa na pointi  13 na kushuka hadi nafasi yua 11.
Simba itashuka dimbani tena Jumamosi kukabiliana na JKT Ruvu ambao wapo katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 18 sawa na Yanga.

Luis Figo naye ajitosa Urais FIFA

http://static1.purepeople.com/articles/5/66/45/@/23351-luis-figo-au-gala-iwc-637x0-1.jpg
Luis Figo
GWIJI wa zamani wa soka wa Ureno, Luis Figo ametangaza uamuzi wake wa kugombea nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Mei mwaka huu. 
Figo amechukua uamuzi huo wa kugombea nafasi ya hiyo siku muda kabla ya muda wa mwisho wa kutuma maombi baada ya kukusanya vielelezo vyake vikiwemo vyama vitano vya soka vinayomuunga mkono. Akihojiwa na CNN, Figo amesema anajali mpira hivyo anachikiona sasa katika taswira ya FIFA hakubaliani nacho ndio maana ameamua kugombea nafasi hiyo ili kumng’oa rais wa sasa Sepp Blatter ambaye amepanga kugombea kwa kipindi cha tano.
Gwiji huyo aliendelea kudai kuwa kama utaitafuta FIFA katika mtandao jambo la kwanza litakalokuja ni kashfa mbalimbali zinazoiandama katika miaka ya karibuni jambo ambalo sio zuri kwa ukuaji wa soka. 
Figo amesema amezungumza na watu wengi muhimu katika soka, wachezaji, mameneja, marais wa mashirikisho na wote wanadhani kunatakiwa kufanyika mabadiliko. 
Mshambuliaji huyo wa zamani wa vilabu vya Barcelona, Real Madrid na Inter Milan ameungana na Jerome Champagne, Prince Ali Bin Hussein, David Ginola na Michael van Praag ambao tayari wametangaza nia hiyo ya kupambana na Blatter.

Baby Madaha atambia Saint and Ghost

MUIGIZAJI nyota wa filamu na muimbaji wa muziki wa Bongofleva, Baby Madaha, ametamba kuwa filamu yake mpya anayoianda kwa sasa iitwayo 'Saint and Ghost' ni kati ya kazi zitakazoleta mapinduzi makubwa nchini katika ulimwengu wa filamu.
Madaha, alisema filamu hiyo ambayo inawashirikisha nyota mbalimbali nchini akiwamo yeye mwenyewe (Madaha) ni kati ya filamu za kusisimua ambazo hazijawahi kutengenezwa nchini kutokana na msuko wa simulizi lake.
"Hata aina ya wasanii walioshiriki ni vichwa kwelikweli kitu kinachoifanya filamu hiyo kuwa ya kipekee, alisema Madaha.
Madaha aliwataja wasanii walioshiriki kazi hiyo iliyozalishwa chini ya kampuni yake ya DarkAngel Film Production & Entertainment ni pamoja na Kulwa Kikumba 'Dude', Hidaya Njaidi,  Grace Mapunda 'Mama Kawele', Ramadhani Ally 'Tafu', Ahmed Olotu 'Mzee Chillo' na wengine.
Kabla ya filamu hiyo Madaha, alicheza filamu kama 'Nani', 'Misukosuko3', 'Mpishi', House Na.44' na 'Ray of Hope' iliyompa tuzo kadhaa ikiwamo ya ZIFF na African Movie.

C.P.U kutinga Uganda kufuatilia mkasa wa mtoto aliyeteswa

WARATIBU wa Filamu ya kutetea watoto ya  C.P.U iliyoshirikisha nyota mbalimbali nchini na ambayo itakuwa ikitolewa kwa mtindo wa matoleo (episode) wanatarajiwa kutinga nchini Uganda kwa ajili ya kufuatilia mkasa wa 'hausi gel' aliyefungwa nchini humo kwa sababu ya kumfanyia kitendo cha ukatili mtoto wa bozi wake.
Filamu hiyo iliyotungwa na Stanford Kihore na kuandikwa na Novatus Mgulusi 'ras' imetengenezwa  kwa ushirikiano wa kampuni mbili za kitanzania za Haak Neel Productions na Wegos Works Ltd ilizinduliwa mwaka juzi na kuanza kuonyeshwa kwenye majumba ya sinema kabla ya sasa kuandaliwa katika mtindo wa DVD ili kuonwa na watu mbalimbali ndani na nje ya nchi,.
Wakizungumza na MICHARAZO waratibu wa filamu hiyo walisema kuwa kwa sasa filamu hiyo ina kuendelezo wa sehemu ya kwanza na itakuwa na matoleo 16 yanayohusu namna ya kukabiliana na unyanyasaji na ukatili kwa watoto.
Waratibu hao walisema kuwa, mwandishi wa C.P.U, Ras Mgulusi anatarajiwa kwenda nchini Uganda kuongea na familia ya mtoto aliyefanyiwa tukio baya na msichana wa kazi kupigwa na kutupwa chini kisha kupigwa mateke sambamba na kufanya mahojiano msichana huyo ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka minne kwa kosa hilo ili kutambua kilichomfanya afanye unyama ule.
"Lengo kubwa ni katika kuboresha na kuliweka tukio hilo ndani ya filamu hiyo ya CPU, ambayo ni kitendo maalum cha kutetea watoto ikiwa imeshirikisha nyota mbalimbali nchini," taarifa ya waratibu wa filamu hiyo inasomeka.
“Nilikuwa nafuatilia ripoti ya Unisef kuhusu taarifa za unyanyasaji wa Watoto kitu kilichonigusa na kuamua kuandika filamu ambayo inaweza kuwa ni dira na mwongozo wa jamii kukwepa au kuwasaidia watoto wanaonyanyaswa katika familia zao,”alisema Ras Mgulusi.
Filamu hiyo imeshirikisha zaidi ya wasanii 100 baadhi yao ni; Kulwa Kikumba ‘Dude’ Illuminata Posh 'Dotnata', Richard Mshanga ‘Mzee Masinde’, Hashim Kambi ‘Ramsey’, Sauda Simba, Subira Wahure, Steve Sandhu 'Pride', Nkwabi Juma, Mohamed Fungafunga ‘Mzee Jengua’ Mobby Mpambala ambao ndiyo vinara wake.
Kwa mujibu wa warartibu hao filamu hiyo inatarajiwa kuwa sokoni kuanzia mwezi ujao.

Hammer Q mkewe wajipanga kutoa mpya

MKALI wa miondoko ya mduara, Hussein Mohammed 'Hammer Q' pamoja na mkewe Salha Abdallah 'Salha wa Hammer' wanatarajia kuachia wimbo wao mpya wa 'Safiri Salama' ikiwa ni muendelezo wa maandalizi ya kutoa albamu yao kamili.
Akizungumza na MICHARAZO, Hammer Q alisema kazi hiyo mpya ambayo imesharekodiwa kitambo itaachiwa mara baada ya kumalizika kwa maonyesho ya sherehe za miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT).
Hammer Q, alisema mpaka sasa wamefanikiwa kutoa wimbo mmoja wa 'Wapendanao' ambao umekuwa ukifanya vema kwenye vituo vya redio na kwamba utakaofuata ni 'Safiri Salama' kabla ya kumalizia kurekodi nyimbo nyingine za albamu hiyo inayaokuwa na nyimbo tano.
"Kwa sasa tupo bize na sherehe za miaka 10 ya THT, baada ya hapo tutaachia wimbo wetu wa pili kabla ya kumalizia albamu ambayo tumepanga kuitoa kabla ya Juni mwaka huu," alisema Hammer Q.
Msanii huyo aliwahi kutamba kwenye Bongofleva kupitia wimbo wa 'Lady' kabla ya kuhamia kwenye miondoko ya taarab akipitia makundi kadhaa likiwamo la Dar Modern, Five Star, na TOT taarab.

Ommy Dimpoz akiri kutengeneza video na Avril si mchezo!

Dimpoz akiwa na Avril
Avril
Dimpoz na Avril
MSANII nyota nchini, Omar Nyembo 'Ommy Dimpoz' amesema haikuwa kazi rahisi kwake kutengeneza video na mwanadada Judith Mwangi 'Avril' aliyeimba naye wimbo uitwao 'Hello Baby'.
Dimpoz aliyeshirikishwa katika wimbo huo ambao 'audio' na video yake zinafanya vema hewani Afrika Mashariki kati zilipoachiwa, alinukuliwa na mtandao wa Bongo5 kwamba utengenezaji wa video ya wimbo huo ulikuwa mtihani mgumu kwake.
Msanii huyo alisema Avril ni mrembo ambaye jicho la mwanamme yeyote rijali ni vigumu kuvumilia anapobadilisha nguo mbele yake ili kuinogesha video, lakini yeye alijikaza kiume.
'Ilikuwa mtihani kidogo unajua kufanya kazi na msichana mrembo ushawishi unakuwa mwingi. Kwa hiyo nilikuwa najizuiazuia," alisema kabla ya kuongeza;
"Kwa sababu kwenye video kuna mambo mengi, mtu anaweza akatokea akabadilisha nguo mbele yako, kwa hiyo yote niliyavumilia, ni lazima uvumilie majaribu ili kazi iende," alinukuliwa mkali huyo.
Dimpoz alidokeza pia namna picha zake na Arvil katika utengenezaji video alizotupia kwenye mtandao wa Instagram zilivyotaka kuibua kasheshe kwa mchumba wa mwanadada huyo mrembo

Hofu yatanda AFCON baada ya wenyeji kufuzu robo fainali

Mashabiki wa Guinea ya Ikweta
Mashabiki wa Guinea ya Ikweta wakijiandaa kuingia uwanjani siku ya ufunguzi wa AFCON 2015
MALABO, Guinea ya Ikweta
KUFUZU kwa wenyeji Guinea ya Ikweta katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika kumetengeneza wasiwasi juu ya usalama kwa waandaaji wa michuano hiyo.
Wenyeji waliwashangaza majirani zao Gabon kwa kuwachapa mabao 2-0 Jumapili iliyopita na kumaliza katika nafasi ya pili katika kundi A. Guinea ya Ikweta sasa itachuana na Tunisia katika hatua ya robo fainali Jumamosi hii huko Ebibeyin. Lakini kuna wasiwasi kuwa uwanja huo mpya wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 5,000 pekee utakuwa mdogo kwa ajili ya mashabiki wengi wanaotegemewa katika mchezo huo. Michuano hiyo tayari imeshashuhudia mashabiki wakibomoa na kupita katika uzio katika mchezo wa ufunguzi uliofanyika Bata Januari 17 ambapo uwanja wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 35,000 ulifurika.
Katika viwanja vingine mara kadhaa maeneo ya maalumu na sehemu za wanahabari zimekuwa zikivamiwa mara kadhaa na mashabiki huku polisi wakipambana kurejesha hali ya utulivu.
Waandaaji sasa inabidi waangalie uwezekano wa kuupeleka mchezo huo katika Uwanja wa Bata ambao ndiyo mkubwa katika nchi hiyo ambapo tayari Guinea ya Ikweta wameshacheza mechi zao tatu huku mashabiki wakiwa wamejaa.
Uwanja huo pia ndiyo utakaotumiwa kwa ajili ya mchezo wa fainali Februari 8.

'Bosi' Bayern adai Guardiola ni zaidi ya Wajerumani

Pep Guardiola
MWENYEKITI wa klabu ya Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Pep Guardiola na kutania kuwa kocha huyo wa zamani wa Barcelona anafanana na Wajerumani kuliko Wajerumani wenyewe.
Rummenigge amesema kutokana na bidii ya kazi aliyokuwa nayo Guardiola anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa watu wote.
Mwenyekiti huyo aliendelea kudai kuwa wakati wachezaji wote wamerejea nyumbani na kupumzika katika masofa yao, Guardiola yeye huendelea na kazi akipanga mikakati kwa ajili ya mchezo ujao.
Juu ya tetesi za kuwapo kwa mpango wa Guardiola kuondoka na kurejea Barcelona, Rummenigge alipuuza taarifa hizo na kudai kuwa kocha huyo ataendelea kuinoa Bayern hata katika msimu ujao wa Bundesliga
Tangu kocha huyo aliyeipa mataji lukuki Barcelona kutua Bayern ameifanya ibadilishe soka lake lililozoeleka kiasi cha awali kuzua hofu kabla ya mashabiki kutulia kufuatia kufanya vema kwa timu hiyo inayoongoza Bundesliga bila kupoteza mchezo wowote hadi sasa.

Bale asisitiza hana 'bifu' na Ronaldo, achekeea maisha Bernabeu

Ronaldo akiwa na Bale
MCHEZAJI ghali wa Real Madrid, Gareth Bale amesema hana mpango wa kuihama klabu hiyo akisisitiza kuwa ana uhusiano nzuri na nyota wa klabu hiyo, Cristiano Ronaldo na pia anapendwa na mashabiki.
Mshambuliaji huyo kutoka Wales, akihojiwa na kituo kimoja cha redio nchini Hispania, alisema uhusiano wake na Ronaldo ni nzuri na wenye nguvu na kudai hajawahi kuambiwa lolote na Ronaldo juu ya taarifa kwamba alimnyima pasi wakati wakiumana na Espanyol.
Bale alisema uhusiano wake na Ronaldo haujabadilika tofauti na inavyoelezwa, huku akisema anakumbuka kila kitu katika pambano hilo na kukiri kwamba hakumuona Ronaldo kiasi cha kumnyima pasi.
"Nakumbuka kila  kitu wakati nilipochukua mpira na nilikuwa katika kuhakikisha najaribu kufunga bao. Sikumuona, nafikiri ingeweza kuwa pasi ngumu kwake. Sijawahi kuzungumza na Ronaldo kuhusu habari hizo za  kumnyima pasi," alisema Bale.
Bale alisema kwa vyovyote anavyojua yanayotokea uwanjani huishia uwanjani ndiyo maana hawakuweza kujadili suala hilo, licha ya kwamba alijikuta akizomewa na mashabiki wa Santiago Bernabeu.
Nyota huyo mwenye miaka 25, alisema anajisikia furaha kucheza Bernabeu kutokana na sapoti ya mashabiki wa klabu hiyo na kudai hufanya kila linalowezekana ili kuonyesha uwezo wake na kuwapa furaha mashabiki hao.
Bale ameifungia Madrid jumla ya mabao 36 katika mechi 72 alizoichezea tangu ilipomsajili kwa kitita kilichoweka rekodi duniani akitokea Tottenham Hotspur, miongoni mwa mabao hayo 25 ameyafunga katika mechi 43 za La Liga.
Hata hivyo mchezaji huyo amekuwa akihusishwa na mipango ya kutaka kuihama klabu hiyo ili kujiunga na Mashetani Wekundu kwa kile kilichoelezwa kutokuwa na furaha klabuni hapo, japo mwenyewe amesisitiza anafurahia maisha Madrid pamoja na familia yake.

Chelsea yatinga fainali Capital One, yainyoa Liverpool darajani

Ivanovic akiruka juu kufunga bao pekee la Chelsea dhidi ya Liverpool katika mechi ya marudiano ya Kombe la Ligi
BAO pekee la dakika za nyongeza lililofungwa na beki Branislav Ivanovic limeiwezesha vinara wa Ligi Kuu ya England, Chelsea kufuzu fainali ya michuano ya Kombe la Ligi (Capital One) baada ya kuing'oa Liverpool kwa jumla ya mabao 2-1.
Chelsea walipata ushindi huo kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Stanford Bridge, katika pambano la marudiano la Nusu Fainali ya michuano hiyo baada ya wiki iliyopita timu hizo kushindwa kutambiana uwanja wa Anfield kwa kutoka sare ya goli 1-1.
Katika pambano hilo lililokuwa na ushindani mkubwa baina ya wachezaji wa timu hizo kiasi cha kushuhudiwa wachezaji tisa, watano wa Liverpool na wanne wa Chelsea wakiwamo manahodha Steven Gerrard na John Terry pamoja na Diego Costa wakionyeshwa kadi za njano dakika 90 zilimalizika kwa timu hizo kushindwa kufungana licha ya kosa kosa za hapa na pale.
Costa alinusurika kupewa kadi nyekundu kwa kuwakanyaga kwa nyakati tofauti mabeki wa Liverpool Emre Can na Martin Skrtel, huku pia Chelsea ikanyimwa penati ya wazi baada ya Skrtel kumuangusha Costa langoni mwake.
Dakika nne baada ya kuanza kwa muda wa nyongeza wa dakika 30, beki Ivanovic aliwainua mashabiki wa Chelsea kwa kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Willian na kuiandikia timu yake bao pekee lililowavusha hadi fainali.
Ushindi huo wa Chelsea umekuwa faraja kubwa kwa kocha Jose Mourinho ambaye mwishoni mwa wiki aliishuhudia timu yake iking'olewa kwenye raundi ya tatu na klabu ya daraja la pili ya Bradford City.
Klabu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu na ambayo mwishoni mwa wiki itakuwa na kibarua kingine kigumu kwa kuumana na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Manchester City sasa itasubiri kujua itacheza na nani kati ya Tottenham Hotspur na Sheffield United ambazo usiku wa leo zitakuwa dimbani zikirudiana katika mechi nyingine ya nusu fainali.
Spurs ikiwa nyumbani kwake White Hart Lane katika pambano la kwanza lililochezwa wiki iliyopita walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 na kama itakuwa imeulinda ushindi huo itaungana na Chelsea kwenye pambano la fainali litakalochezwa mwezi Machi uwanja wa Wembley.

Ndanda yaipiga mkwara Yanga pambano lao la Jumapili

Ndanda Fc
KLABU ya Ndanda imetamba kuwatoa nishai Yanga watakaoumana nao siku ya Jumapili kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ndanda ambayo tayari wameshatua jijini Dar es Salaam wakitokea Mwanza walipoisambaratisha Kagera Sugar kwa kuilaza mabao 2-1, imesema kuwa lengo lao ni kuvuna pointi tatu ili kujiweka pazuri katika msimamo wa ligi hiyo.
Katika Mkuu wa Ndanda, Edmund Njowoka amesema kuwa kikosi chao kinatambua ugumu wa pambano hilo dhidi ya Yanga, lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi uwanja wa ugenini.
Kikosi cha Ndanda kinachocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, kipo nafasi ya 11 kikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi 12 ikishinda michezo minne na kupoteza saba kitavaana na Yanga wanaokamata nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 18 baada ya mechi 10.
Njowoka alisema kikosi chao kipo tayari kwa vita na amehakikishiwa na benchi lao la ufundi chini ya Kocha Meja Mstaafu Abdul Mingange kwamba vijana wao watapambana kufa na kupona kuhakikisha wanavuna pointi nyingine tatu.
"Tumekuja kwa ajili ya kuvuna pointi, kama tulivyofanya kwa Kagera ndivyo tunavyotaka kufanya kwa Yanga, licha ya kutambua ugumu wa pambano hilo la Jumapili," alisema Njowoka.
Yanga iliyolazimishwa sare mbili mfululizo na Azam na Ruvu Shooting, ilirekebisha makosa yake mwishoni mwa wiki kwa kuinyuka Polisi Moro kwa bao 1-0 na kuwajongelea watetezi wa ligi hiyo, Azam wanaoongoza wakiwa na pointi 21.
Azam kwa sasa ipo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kushiriki michuano maalum kujiandaa na pambano lake la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Marreikh. Michuano hiyo inashirikisha jumla ya timu nne zikiwamo TP Mazembe, Don Bosco na Zesco ya Zambia.
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm alinukuliwa juzi kwamba kikosi chake kimejiandaa kupata ushindi dhidi ya Ndanda, akiwasisitiza vijana wake kuwa makini uwanjani ili kutopoteza nafasi za wazi kama walivyofanya katika mechi zao zilizopita.

Kumekucha Bungeni, kikao chaahirishwa kisha Prof Lipumba

Prof Lipumba akiwa ndani ya gari la Polisi baada ya kutiwa mbaroni jana
SPIKA wa Bunge la Jamhuri wa Tanzania, Anna Makinda amelazimika kuahirisha kikao cha Bunge kilichoanza jana, baada ya vuta nikuvute iliyotokea  baada ya kutolewa kwa hoja binafsi kutoka kwa Mbunge na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia kuhusu jeshi la polisi kumshambulia Profesa Ibrahim Lipumba jana akiwa kwenye maandamano .
Akizungumza katika bunge hilo Mbatia amesema kuwa kitendo cha polisi cha kuwapiga raia wasiokuwa na hatia, kuwadhalilisha waandishi wa habari na kupiga mabomu ya machozi kiasi cha kuwafanya watoto wadogo kuhangaika hakikubaliki.
Amesema polisi wakiendelea kuachwa kufanya vitu vya uvunjifu wa Amani Serikali haitatawalika hivyo ili kurejesha amani na imani ya wananchi kwa Serikali yao ni vema shughuli zote za Bunge zikaahirishwa kupisha mjadala wa hoja hiyo binafsi kwa lengo la kuinusuru nchi.
“Mheshimiwa Spika naliomba bunge lako liahirishe shughuli zake ili leo tuweze kujadili suala hili la uvunjifu wa amani uliofanywa na  jeshi letu la polisi jijini Dar es Salam jana, wao wanasema kuwa wamepewa amri kutoka ngazi za juu tunataka serikali ituambie ni nani anayetoa amri hizi za kupiga watu wasiokuwa na hatia yeyote, amesema Mbatia.
Baada ya kuwasilisha hoja hiyo asilimia kubwa ya wabunge walisimama juu ishara ya kuunga mkono hoja hiyo, lakini Spika Makinda akawaomba wakae ili aweze kutoa ufafanuzi kwa mujibu wa kanuni.
Spika Makinda aliwaeleza wabunge hao kuwa suala hilo ni nyeti kwa sababu ni la kiusalama, ili kupata ufafanuzi zaidi anaiagiza Serikali kufikisha bungeni hapo majibu ya hoja hiyo kesho ili wabunge waweze kujadili.
Baada ya maamuzi hayo ya Spika Makinda kelele zikasikika bungeni huku wabunge wakitaka kufanyika kwa mjadala huo leo leo, ndipo Spika alipoamua kuahirisha bunge hadi saa kumi jioni.

Ghana, Algeria watinga robo fainali, vumbi jingine leo

Andre Ayew akichuana na mchezaji wa Bafana Bafana
Wachezaji wa Algeria wakishangilia ushindi wao dhidi ya Senegal
VINARA wa soka Afrika, Algeria na Ghana zimefuzu hatua ya Robo Fainali ya michuani ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON), kwa kishindo baada ya kuziondosha patupu timu za Senegal na Afrika Kusini katika mechi zao za mwisho za Kundi C zilizochezwa katika miji ya Malabo na  Mongomo.
Algeria walikuwa wametoka kuduwazwa na Ghana kwa kufungwa bao 1-0 katika mechi yao iliyopita, walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya waliokuwa vinara wa kundi hilo la kifo, Senegal katika pambano tamu lililochezwa kwenye uwanja wa Malabo.
Ikiwa bila nyota wake Islam Slimani, Algeria wanaoongoza orodha ya viwango vya soka barani Afrika waliwashtukiza wapinzani wao kwa bao la mapema la dakika ya 11 lililowekwa kimiani na Riyad  Mahrez lililodumu hadi wakati wa mapumziko.
Senegal walicharuka kusaka kurudisha bao hilo ili angalau waambulie sare na kuwavusha hatua hiyo ya mtoano, lakini walijikuta wakikatishwa tamaa baada ya Algeria kuandika bao la pili dakika nane kabla ya kumalizika kwa pambano hilo baada ya Nabil Bentaleb kumalizia kazi nzuri ya
Sofiane Feghouli.
Kwa kipigo hicho Senegal wameyaaga mashindano hayo sambamba na Afrika Kusini ambayo ilikumbana na kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Ghana waliokuwa nyuma hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Bafana Bafana iliyofuzu fainali hizo kwa kishindo bila ya kupoteza mchezo katika kundi lake lililokuwa na waliokuwa mabingwa Nigeria, ilianza kupata bao katika dakika ya 17 kupitia kwa Mandla Masango, lakini katika kipindi cha pili waliruhusu wapinzani wao kurejesha bao hilo na kuongeza jingine lililowapeleka robo fainali bila kutarajiwa baada ya kuianza michuano hiyo kwa kichapo cha mabao 2-1 toka kwa Segenal.
Bao la kusawazisha la Ghana liliwekwa kimiani na John Boye katika dakika ya 73 baada ya kuunganisha mpira wa krosi ya Andre Ayew 'Pele' kabla ya mtoto huyo wa nyota wa zamani wa Afrika, Abeid Pele kufunga bao la ushindi kwa kichwa katika dakika ya dakika ya 83 na kuwavusha mabingwa hao manne wa michuano hiyo katika hatua hiyo ya robo fainali.
Ghana imemaliza kileleni mwa kundi hilo wakilingana pointi sita na Algeria waliokamata nafasi ya pili, huku Senegal wameshika nafasi ya tatu wakiwa na pointi nne na Bafana Bafana wameburuza mkia wakivuna pointi moja tu.
Hatua ya robo fainali inatarajiwa kuanza kuchezwa siku ya Jumamosi kwa pambano la kukata na shoka baina ya majirani Congo-Brazzaville dhidi ya DR Congo kabla ya Tunisia kuvaana na wenyeji Guinea ya Ikweta katika pambano jingine la pili.
Ghana na Algeria zenyewe zinatarajiwa kushuka dimbani siku ya Jumapili kumenyana na washindi wa kundi D ambalo usiku wa leo zibnatarajiwa kuumana kuwania nafasi mbili zilizobaki za kutinga hatua hiyo ya robo fainali.
Wakati Ivory Coast na Cameroon zitaumana kwenye uwanja wa Malabo, wenzao Mali na Guinea watapepetana kwenye uwanja wa Mongomo, huku timu zote zikiwa na nafasi sawa kutokana na kulingana kila kitu wakiwa na pointi mbili baada ya kila moja kucheza mechi mbili.