STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 28, 2015

Chelsea yatinga fainali Capital One, yainyoa Liverpool darajani

Ivanovic akiruka juu kufunga bao pekee la Chelsea dhidi ya Liverpool katika mechi ya marudiano ya Kombe la Ligi
BAO pekee la dakika za nyongeza lililofungwa na beki Branislav Ivanovic limeiwezesha vinara wa Ligi Kuu ya England, Chelsea kufuzu fainali ya michuano ya Kombe la Ligi (Capital One) baada ya kuing'oa Liverpool kwa jumla ya mabao 2-1.
Chelsea walipata ushindi huo kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Stanford Bridge, katika pambano la marudiano la Nusu Fainali ya michuano hiyo baada ya wiki iliyopita timu hizo kushindwa kutambiana uwanja wa Anfield kwa kutoka sare ya goli 1-1.
Katika pambano hilo lililokuwa na ushindani mkubwa baina ya wachezaji wa timu hizo kiasi cha kushuhudiwa wachezaji tisa, watano wa Liverpool na wanne wa Chelsea wakiwamo manahodha Steven Gerrard na John Terry pamoja na Diego Costa wakionyeshwa kadi za njano dakika 90 zilimalizika kwa timu hizo kushindwa kufungana licha ya kosa kosa za hapa na pale.
Costa alinusurika kupewa kadi nyekundu kwa kuwakanyaga kwa nyakati tofauti mabeki wa Liverpool Emre Can na Martin Skrtel, huku pia Chelsea ikanyimwa penati ya wazi baada ya Skrtel kumuangusha Costa langoni mwake.
Dakika nne baada ya kuanza kwa muda wa nyongeza wa dakika 30, beki Ivanovic aliwainua mashabiki wa Chelsea kwa kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Willian na kuiandikia timu yake bao pekee lililowavusha hadi fainali.
Ushindi huo wa Chelsea umekuwa faraja kubwa kwa kocha Jose Mourinho ambaye mwishoni mwa wiki aliishuhudia timu yake iking'olewa kwenye raundi ya tatu na klabu ya daraja la pili ya Bradford City.
Klabu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu na ambayo mwishoni mwa wiki itakuwa na kibarua kingine kigumu kwa kuumana na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Manchester City sasa itasubiri kujua itacheza na nani kati ya Tottenham Hotspur na Sheffield United ambazo usiku wa leo zitakuwa dimbani zikirudiana katika mechi nyingine ya nusu fainali.
Spurs ikiwa nyumbani kwake White Hart Lane katika pambano la kwanza lililochezwa wiki iliyopita walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 na kama itakuwa imeulinda ushindi huo itaungana na Chelsea kwenye pambano la fainali litakalochezwa mwezi Machi uwanja wa Wembley.

No comments:

Post a Comment