STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, July 24, 2013

Ofisi ya Msajili wa Vyama yaionya CHADEMA


MSAJILI wa vyama vya Siasa nchini amewaasa wanachama na viongozi wa Chama Cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutumia muda wao kufanya shughuli za siasa ili kuchangia maendeleo ya nchi badala ya kutumia uwezo na muda wao kubuni mambo yanayoleta mtafaruku na kuhatarisha amani ya nchi.

Pia amepinga tamko la chama hicho la kuanzisha mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake nchi nzima.Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa  leo jijini Dar es Salaam na kusainiwa kwa niaba ya Msajili wa vyama vya siasa Sisty Nyahoza alisema  kuwa hajawahi kuruhusu CHADEMA au chama chochote cha siasa kufanya mafunzo ya ukakamavu au mafunzo ya kutumia nguvu  ya aina yoyote kwa wanachama wake au mtu yeyote yule.

Anaongeza kuwa CHADEMA wanaruhusiwa kuanzisha vikundi vya kujilinda lakini hawaruhusiwi kuanzisha mafunzo ya kutumia nguvu kwaajili ya kujilinda kama walivyo tangaza katika mikutano yao ya hadhara kwani ni kinyume na Demokrasia na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano.

Nyahozo ametoa ufafanuzi kuhusu vikundi vya ulinzi na usalama vilivyopo katika Katiba ya Vyama vya Siasa kwamba vikundi hivyo haviruhusiwi kufanya mafunzo ya kutumia nguvu ya aina yoyote katika kutekeleza majukumu yao.
 
Bali wajibu wao ni kutoa taarifa wa vyombo vya Dola pale wanapo sikia au kuona uhalifu ukitokea na wala sio kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru kama tamko la CHADEMA  la tarehe 9 mwezi huu linavyo sema.

“Hakuna maelezo yoyote katika Katiba ya CHADEMA yanayoruhusu kutumia nguvu kufanikisha shughuli za kulinda mali na Viongozi wa Chama.Ni vyema wananchi wote waelewe kuwa Sheria za Nchi zimeweka masharti maalumu kwa Vyama Vya Siasa kutokana na umuhimu wa vyama hivi katika kudumisha aman utulivu na umoja wa Kitaifa”, alisema Nyahoza.

Alisema kuwa kutokana na Ibara ya20(2)C ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997 inasema kuwa “Bila kujali masharti ya ibara ya (1) na (4),haitakuwa halali kwa chama chochote cha siasa kuandikishwa ambapo kutokana na katiba au sera yake:-kinakubali au kunapigani matumizi ya nguvu au mapambano kama njia za kufikia malengo yake ya kisiasa.

Nyahoza alimaliza kwa kuwataka CHADEMA kuacha kutekeleza mpango walio tangaza wa kuanzisha makambi ya kufanya mafunzo ya kujilinda kwa vijana wao nchi nzima,kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi na endapo  watashindwa kutii agizo hilo  hatua za Kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Ukatili! Mwanamke anyongwa kwa wivu wa mapenzi

MWANAMKE mmoja aitwaye Nyamizi Elias Salamba mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa kijiji cha Ilomelo kata ya Ulowa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, ameuawa kwa kunyongwa shingo na mwanamme anayedaiwa kuwa ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kasela wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Taarifa ya jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga imesema tukio hilo limetokea Jumapili ya wiki iliyopita katika kijiji cha Ilomelo wilayani Kahama majira ya saa nne usiku ambapo mwanamke huyo alinyongwa shingo na hawara yake aliyejulikana kwa jina la Kashindye Abeid Sheni mwenye umri wa miaka 45 ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kasela kilichopo mkoani Tabora.

Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga, Evarist Mangalla alikitaja chanzo cha mauaji hayo kuwa ni wivu wa mapenzi baada ya marehemu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamme mwingine ambaye hajafahamika, kitendo ambacho kilimuudhi Mwenyekiti huyo.

Kamanda Mangalla alisema mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Polisi 117 watimuliwa kambini kisa...!


ASKARI Polisi 117 waliokuwa mafunzoni mjini Moshi katika Chuo cha Taaluma na Mafunzo ya Polisi (MPA), wametimuliwa.


Waliotupiwa virago na kufutwa kwenye kozi hiyo ni wale waliopoteza sifa za kuendelea na mafunzo ya kijeshi baada ya kukutwa na makosa ya utovu wa nidhamu, utoro na matatizo ya kiafya.

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Matanga Mbushi, ambaye ni mkuu wa chuo hicho alisema katika mahojiano maalumu kwamba, waliotimuliwa chuoni ni kati ya askari wanafunzi 3,189 waliokuwa wamesajiliwa kuanza mafunzo ya kijeshi katika chuo hicho, Oktoba 25 mwaka jana.
 

Kati yao askari 115 ni wale wa Polisi na askari wawili wanatoka katika Idara ya Uhamiaji iliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kufukuzwa kwa wanafunzi hao , kuna akisi moja kwa moja jinsi menejimenti ya chuo hicho ilivyojipanga upya kupunguza wimbi la baadhi ya askari walioko kazini na ambao wanalipaka matope jeshi hilo kutokana na kupotoka kimaadili kwa kutaka kujinufaisha kimaslahi.

Askari hao walikuwa waungane na wenzao ambao wanatarajiwa kuhitimu mafunzo ya awali ya polisi na uhamiaji, Julai 26 mwaka huu baada ya kupatiwa mafunzo ya medani za kivita. Mgeni wa heshima atakayeshuhudia kuagwa kwa askari 3,092 ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.


Kamishna Mbushi alisema askari hao pamoja na mambo mengine wamepatiwa mafunzo maalumu ya utunzaji wa amani ya nchi iliyopo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Haki za Binadamu, Masuala ya mtambuka (Cross cutting issues), Usimamizi wa majanga na Usimamizi wa kazi za Polisi.

Mafunzo mengine ni pamoja na Polisi Jamii, Sheria ya ushahidi, Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, Upelelezi wa makosa ya jinai, Usalama barabarani na stadi za kazi.

Taarifa za awali kutoka ndani ya chuo hicho, zinaeleza kuwa mahafali hayo ya Polisi yatatanguliwa na medani za kivita yatakayofanyika Julai 25 huko katika Kijiji cha Kilele-Pori, Wilaya ya Siha.

Stars yatua salama kuivaa Uganda The Cranes J'mosi

Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars na benchi la ufundi wakiwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebe nchini Uganda jana tayari kwa mchezo wa marudiano na timu ya Taifa ya Uganda Jumamosi hii.
Timu ya Taifa (Taifa Stars) imewasili Uganda jioni hii Jumatano tayari kuikabili Uganda Cranes kwa mechi ya marudiano kutafuta tiketi ya kucheza katika mashindano ya CHAN.
 
Kikosi hicho chichi nye wachezaji 20, kiliwasili muda mfupi baada ya saa kumi alasiri huku wachezaji na benchi la ufundi wakiwa na matumaini makubwa.
 
Akiongea mara baada ya kuwasili Kocha wa Timu ya Taifa Kim Poulsen alisema wamejiandaa vizuri wakiwa Mwanza na ana imanikikosi hiki kitabadili atokeo ya awali ambapo Stars ilifungwa 1-0 na Cranes Jijini Dar es Salaam.
 
Alisema licha ya kuwakosa wachezaji Shomari kapombe na Mwinyi Kazimoto, ana imani na kikosi chake hiki kuwa kitafanya makubwa Kampala.
 
“Tumekuja kubadilisha mahesabu kwani tumejiandaa vizuri kabisa,” alisema Poulsen.
 
Wadhamini wa Stars, Kilimanjaro Premium Lager wamewaomba watanzania wasikate tama kwani Stars bado ina nafasi kubwa ya kupindua meza.
 
“Sisi kama wadhamini bado tuna imani na Stars na tunajua watatuwakilisha vizuri ni vyema watanzania wawe na imani na kuiombea dua timu iibuke na ushindi mnono katika mechi hii ya marudiano,” alisema Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, george Kavishe.
 
Mechi hii ni gumzo kubwa Jijini Kampala kwani baadhi ya waganda wana hofu kuwa henda wakafungwa nyumbani kwao.
 
Mechi hii itapigwa katika Uwanja wa Nambole Jijini Kampala JUmamosi hii saa kumi jioni.
 
Mashindano ya CHAN yanatarajiwa kufanyika Januari mwakani nchini Afrika Kusini.
 
 

Coastal Union yatafuna 'fupa' lililozishinda Simba, Yanga

Coastal Union
MABINGWA wa zamani wa kandanda nchini, Coastal Union ya Tanga jioni ya leo imekifanya kile kilichowashinda vigogo Simba na Yanga kwa kuidungua URA ya Uganda kwa bao 1-0.
URA iliyoikwanyua Simba kwa mabao 2-1 na kusalia kidogo kuiangusha Yanga baada ya wanajangwani hao kuchomoa jioni na kupata sare ya 2-2, waliduwazwa na wagosi wa kaya kwenye uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Coastal ikiwa na sura mchanganyiko katika kikosi chake inaelezwa iliwakimbiza Waganda hao kabla ya Kenneth Masumbuko kuwalaza mapema kwa bao tamu.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa pambano hilo, Coastal iliwazima kabisa wageni hao waliopo nchini kwa michezo ya klirafiki ya kimataifa kwa pasi murua za Haruna Moshi Boban, Uhuru Seleman, Jerry Santo, Caspian Odula na Daniel Lyanga.
Kikosi hicho ca Coastal ambacho0 ukuta wake ulikuwa chini ya Juma Nyosso, kipo katika maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Agosti 24 ambapo yenyewe itaanzia ugenini dhidi ya maafande wa JKT Oljoro.

Kesho ni Siku ya Mashujaa wa Tanzania waliokufa vitani kukumbukwa

 

KESHO ni siku ya kuwakumbuka Mashujaa wa Tanzania, ambapo kitaifa itafanyika mkoani Kagera, japo kila mkoa nao upo katika maandalizi ya kuadhimisha siku hiyo ya kuwakumbuka wale wote waliojitolea kupotea uhai wao kwa ajili ya taifa lao.
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwaongoza Watanzania katika maadhimisho hayo ya kesho.
Kwa mkoa wa Morogoro shughuli na maandalizi ya siku hiyo ziliendelea leo kama zinavyoonekana pichani ambapo hapo juu Askari wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha maombolezi kikiwa katika mazoezi ya kutoa heshima za mwisho kwa  mashujaa waliofariki dunia katika vita ya Kagera mwaka 1978 na 1979 wakati wa gwalide la pamoja la jeshi la magereza, Polisi na JWTZ katika maandalizi ya mwisho ya kilele cha maadhimisho ya siku kuwakubuka mashujaa hao ambayo yataadhimishwa kimkoa kwenye mnara wa kumbukumbu wa Posta julai 25 mkoani Morogoro. PICHA JUMAMTANDA.BLOG

 Askari wa jeshi la polisi wakiwa katika gwalide
 Askari wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) nao wakiwa katika gwalide la pamoja.
 Hapa ni askari wa jeshi la magereza wakiwajibika kwa ajili ya maandalizi hayo.
Askari wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) Mteule daraja la kwanza, Jonas Philipo kulia akitoa maelekezo eneo la barabara ya Stesheni.
Hapa Aande Philipo kulia akifafanua jambo kwa viongozi wakuu wa mkoa ndani ya jeshi na serikali.
 Moshi ukiwa umezagaa baada ya kulipuliwa kwa mizinga mitatu katika maandalizi hayo.
Hapa vikosi vyote vya JWTZ, Polisi na Magereza vikiingia katika eneo la mzunguko wa posta ambapo ndiko kutaadhimishwa sherehe hizo kimkoa julai 25/ 2013.

Liverpool bado yaidengulia Arsenal juu ya Suarez

Suarez

LONDON, Uingereza
LIVERPOOL imekataa ofa iliyoboreshwa ya Arsenal ya paundi milioni 40 kwa ajili ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez.

Ofa hiyo isiyo ya kawaida, inayofahamika kuwa ni paundi 40,000,001, iliandaliwa maalum kuvuka kidogo bei ya kipengele cha kuvunjia mkataba wa mchezaji huyo, lakini Liverpool wamekataa.

Chini ya vipengele vya mkataba wa Suarez, klabu hiyo inabanwa kutafakari ofa yoyote kwa ajili yake inayozidi paundi milioni 40 na ni lazima imfahamishe mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kuhusu ofa hiyo.

Lakini Liverpool hawataki kumuuza na sasa wamekataa ofa mbili kutoka Arsenal. Ofa ya kwanza ilikuwa ni paundi milioni 30.

Simba kumpeleka Kiggy Makassy India Agosti 18

KLABU ya Simba inapenda kutoa taarifa zifuatazo kwa umma kupitia vyombo vyenu.
KUHUSU MCHEZAJI KIGGI MAKASSY
UONGOZI wa Simba SC umefanikisha miadi (appointment) na madaktari nchini India kwa ajili ya matibabu ya mchezaji wake, Kiggi Makassy.
Mchezaji huyo atakutana na madaktari nchini India Agosti 18 mwaka huu tayari kwa ajili ya kuanza matibabu ya matatizo yake ya goti aliyoyapata wakati akiichezea Simba.
Ikumbukwe kwamba Simba SC ilikuwa klabu ya kwanza ya soka ya Tanzania kupeleka mchezaji nchi za nje kutibiwa takribani miaka minne iliyopita wakati ilipompeleka Uhuru Selemani Mwambungu nchini India.
Kwa taarifa hii, uongozi unapenda kuwahakikishia wapenzi na wanachama wake kwamba dhamira ya klabu ni kuhakikisha wachezaji wanapewa kipaumbele katika afya zao za kimwili na kiakili.
SIMBA DAY
Kama ilivyo ada, mwaka huu Simba itafanya maadhimisho ya Siku ya Simba (SIMBA DAY). Siku hiyo itatanguliwa na WIKI YA SIMBA ambapo wachezaji na viongozi wa klabu watatembelea vyombo vya habari, vituo vya kulelea yatima na hospitali kwa ajili ya kutekeleza wajibu wake kwa jamii (Social Responsibility).
MAANDALIZI YA LIGI KUU
SIMBA imeingia kambini kwa ajili ya mazoezi makali (intensive training) katika eneo la Bamba Beach jijini Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni, ameomba kambi hiyo ili kuwatengeneza wachezaji kimwili, kiakili na kisaikolojia.
Kabla ya mechi ya Simba Day, timu itacheza mechi moja ya kirafiki katika tarehe itayotangazwa baadaye.
Miongoni mwa wachezaji walio kambini ni Ramadhani Chomboh (Redondo).
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

Chelsea bado yamng'ang'ania Rooney

Wayne Rooney
KLABU ya Chelsea inajiandaa kuongeza dau la kumnasa mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney licha ya United kusisitiza kuwa nyota wao huyo HAUZWI.
Kwa mujibu wa duru za kimichezo toka nchini England zinasema kuwa Chelsea wanajiandaa kuweka mezani Pauni Milioni 40 ili kumnasa mchezaji huyo.
Mchezaji huyo amekuwa hana furaha ndani ya United na imedaiwa kuwa anataka auzwe, lakini uongozi unaweka ngumu.
Chelsea chini ya kocha wake Jose Mourinho imekuwa ikimmezea mate mshambuliaji huyo tegemeo wa England na imeendelea  kusisitiza kuwa inahitaji saini yake kwa sasa.
Arsenal pia ilitajwa kuwa katika mbio za kumnasa mkali huyo wa mabao, ikijitapa wana uwezo wa kumlipa mshahara wake wa pauni 250,000 kwa wiki.
Kuna uwezekano mdogo kwa United kulegeza msimamo wake licha kwamba huenda dau hilo litawavutia baada ya timu yao kuandamwa na majeruhi kabla ya kuanza kwa Ligi.
Mfungaji Bora wa EPL, Robin van Persie aliumia wakati United ikilala Asia kwa mabao 3-2 huku Danny Welbeck akitajwa kuwa majeruhi hali inayomtisha kocha David Moyes.

Kocha Liverpool amcharukia Suarez

Kocha Brendan Rodgers

KOCHA wa Liverpool, Brendan Rodgers amesisitiza kwamba Luis Suarez hataweza kulazimisha kuondoka klabuni hapo katika kipindi hiki cha usajili.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ameweka wazi nia yake ya kuhama Anfield akieleza hadharani anavyoipenda Real Madrid na akazungumzia furaha yake baada ya kusikia anatakiwa na Arsenal, huku klabu hiyo ya London kaskazini ikijiandaa kupeleka ofa ya pili ya paundi milioni 40 baada ya ofa ya kwanza kukataliwa na Liverpool.
Lakini Rodgers amesema Liverpool watakuwa na kauli ya mwisho juu ya uwezekano wa kuhama kwa Suarez, huku akisema hakuna mchezaji anayepaswa kutoiheshimu klabu hiyo.
"Hili ni jambo ambalo liko mikononi mwetu," Rodgers aliwaambia waandishi wa habari. "Jambo hili haliko mikononi mwa mchezaji. Niko makini na thamani ya klabu, mahala tulipo na tunavyojiendesha.
"Soka na jamii ni tofauti siku hizi, soko la uhamisho ni tofauti kabisa na wachezaji wanaweza kuzua njia tofauti za kulifungua.
"Lakini daima nimekuwa nikisema kwamba hakuna mchezaji ambaye ni mkubwa kuliko Liverpool na kwamba hilo ni jambo ambalo tuko makini nalo sana.
"Je, namtarajia abaki? Sana kabisa. Mengi yamesemwa mwisho wa msimu, lakini ukweli ni kwamba yeye ni mchezaji muhimu sana. Kila mchezaji ana thamani yake, lakini haimaniishi kwamba tutamuuza."
Suarez alijiunga na wachezaji wenzake nchini Australia Jumapili baada ya kupewa muda wa ziada wa kupumzika kutokana na kushiriki michuano ya Mabingwa wa Mabara mwezi Juni.
Rodgers, ambaye awali alisema mshambuliaji huyo atacheza mechi ya kirafiki ya kujiandaa na msimu leo dhidi ya timu ya Melbourne Victory, anapanga kuzungumza na nyota huyo wa zamani wa Ajax huko huko ziarani.
"Nitafanya kama nilichofanya na wachezaji wengine kwa kukaa naye chini kuzungumza," Rodgers alisema. "Ukweli ni kwamba tuna jambo moja ama mawili ya kukamilisha, lakini hilo litafanyika na tutaendelea na kazi.
"Luis na mimi tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara, lakini tulipokuja hapa Jumapili usiku na kupata mlo, ulikuwa muda umeenda sana. Tuna aina hiyo ya mahusiano, ambayo mawasiliano yako wazi. daima huwa namueleza ninachojisikia.
"Luis yuko hapa kama ilivyotarajiwa, yeye ni sehemu muhimu ya kikosi na tutazungumza wakati fulani. Kubwa zaidi yeye ni mchezaji wa Liverpool. Tuliletewa ofa moja tu kutoka timu inayomtaka na ilikuwa haikaribii thamani yake na hakuna ofa nyingine tangu wakati huo."

Miaka 13 ya Jide kuhamia Arusha wakati wa Idd el Fitri

Lady Jaydee

MWANADADA mkali wa muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura Mbibo 'Lady Jaydee' a.k.a Anaconda, anatarajia kuendeleza shamrashamra za maadhimisho ya miaka 13 ya uwepo wake kwenye fani hiyo katika mkoa wa Arusha wakati wa sikukuu ya Idd el Fitri.

Kwa mujibu wa Meneja wa msanii huyo, Gadna G. Habash maonyesho hayo yafanyika kwa siku mbili mfululizo kuanzia Idd Mosi na Idd Pili na atashirikiana na wasanii kadhaa wakongwe akiwamo Joseph Haule 'Profesa Jay wa Mitulinga a.k.a Big Daddy ambaye ni mkongwe mwenzake katika tasnia hiyo nchini.

Onyesho la kwanza la Binti Machozi litafanyika kwenye ukumbi wa  'Triple A' siku ya Idd Mosi na siku inayofuata atawapa shangwe wakazi wa jiji hilo katika ukumbi wa Botaniko Garden ambapo shughuli nzima ya burudani itaanza majira ya mchana kwa kushirikisha watoto kuonyesha vipaji vyao.

Watoto haao watashindana kucheza, kuimba na vipaji vingine mradi nao kujumuika na Anaconda kabla ya kuwapisha wazee wao kuadhimisha miaka hiyo 13 na mkali huyo asiye na mpinzani nchini miongoni mwa wasanii wa kike.

Hayo yatakuwa maadhimisho ya pili kwa Jide baada ya awali kufanya kama hivyo jijini Dar es Salaam Juni 14 ambapo alifunika mbaya kiasi kwamba ukumbi haukutosha kwa jinsi ulivyofurika watu waliojitokeza Nyumbani Lounge.

Mara baada ya maadhimisho hayo ya Arusha, Jide anatarajiwa kufanya ziara mikoa mbalimbali ili kuwapelekea burudani mashabiki wake katika kuadhimisha miaka hiyo 13 ambapo mwanamuziki huyo amekuwa akizifanya shughuli za muziki bila kutetereka akitajwa kama mmoja wa wanamuziki matarajiri Afrika Mashariki, lakini asiye na makeke.

Katika mipindi chote cha miaka 13 katika ulimwengu wa muziki, Jide ameshatoa albamu sita ambazo ni Machozi (2000), Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007), The Best of Lady Jay dee(2012) na ya sasa ya Nothing but the Truth akiwa pia anamiliki bendi ya Machozi, Hoteli na miradi mingine ya kiuchumi.

Taifa Stars kuifuata Uganda the Cranes leo

Vijana wa taifa Stars
TIMU ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajiwa kuondoka mchana wa leo ikitokea Mwanza kwenda Kampala, Uganda kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la CHAN itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mandela kuanzia saa 10 kamili jioni.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilikuwa kambini jijini Mwanza chini ya Kocha Kim Poulsen tangu Julai 14 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakayocheza fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Stars itaondoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir, na inatarajiwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 10.15 jioni.
Stars inahitaji ushindi wa mabao yasiyopungua mawili ili kusonga mbele kwenye fainali hizo baada ya kupoteza ya kwanza iliyochezwa nyumbani wiki mbili zilizopita kwa kufungwa bao 1-0.
Kocha wa timu hiyo jana alizungumza na wanahabari jijini humo na kutamba kwamba vijana wake wapo tayari kwa pambano hilo la Jumamosi na kuahidi watafia uwanjani, mradi kuipa nafasi Stars kurejea ilichokifanya mwaka 2009 iliposhiriki fainali hizo za CHAN zilipofanyika Ivory Coast.