Kocha Brendan Rodgers |
KOCHA wa Liverpool, Brendan Rodgers amesisitiza kwamba Luis Suarez hataweza kulazimisha kuondoka klabuni hapo katika kipindi hiki cha usajili.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ameweka wazi nia yake ya kuhama Anfield akieleza hadharani anavyoipenda Real Madrid na akazungumzia furaha yake baada ya kusikia anatakiwa na Arsenal, huku klabu hiyo ya London kaskazini ikijiandaa kupeleka ofa ya pili ya paundi milioni 40 baada ya ofa ya kwanza kukataliwa na Liverpool.
Lakini Rodgers amesema Liverpool watakuwa na kauli ya mwisho juu ya uwezekano wa kuhama kwa Suarez, huku akisema hakuna mchezaji anayepaswa kutoiheshimu klabu hiyo.
"Hili ni jambo ambalo liko mikononi mwetu," Rodgers aliwaambia waandishi wa habari. "Jambo hili haliko mikononi mwa mchezaji. Niko makini na thamani ya klabu, mahala tulipo na tunavyojiendesha.
"Soka na jamii ni tofauti siku hizi, soko la uhamisho ni tofauti kabisa na wachezaji wanaweza kuzua njia tofauti za kulifungua.
"Lakini daima nimekuwa nikisema kwamba hakuna mchezaji ambaye ni mkubwa kuliko Liverpool na kwamba hilo ni jambo ambalo tuko makini nalo sana.
"Je, namtarajia abaki? Sana kabisa. Mengi yamesemwa mwisho wa msimu, lakini ukweli ni kwamba yeye ni mchezaji muhimu sana. Kila mchezaji ana thamani yake, lakini haimaniishi kwamba tutamuuza."
Suarez alijiunga na wachezaji wenzake nchini Australia Jumapili baada ya kupewa muda wa ziada wa kupumzika kutokana na kushiriki michuano ya Mabingwa wa Mabara mwezi Juni.
Rodgers, ambaye awali alisema mshambuliaji huyo atacheza mechi ya kirafiki ya kujiandaa na msimu leo dhidi ya timu ya Melbourne Victory, anapanga kuzungumza na nyota huyo wa zamani wa Ajax huko huko ziarani.
"Nitafanya kama nilichofanya na wachezaji wengine kwa kukaa naye chini kuzungumza," Rodgers alisema. "Ukweli ni kwamba tuna jambo moja ama mawili ya kukamilisha, lakini hilo litafanyika na tutaendelea na kazi.
"Luis na mimi tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara, lakini tulipokuja hapa Jumapili usiku na kupata mlo, ulikuwa muda umeenda sana. Tuna aina hiyo ya mahusiano, ambayo mawasiliano yako wazi. daima huwa namueleza ninachojisikia.
"Luis yuko hapa kama ilivyotarajiwa, yeye ni sehemu muhimu ya kikosi na tutazungumza wakati fulani. Kubwa zaidi yeye ni mchezaji wa Liverpool. Tuliletewa ofa moja tu kutoka timu inayomtaka na ilikuwa haikaribii thamani yake na hakuna ofa nyingine tangu wakati huo."
No comments:
Post a Comment