Wanajeshi wakipokea mwili ya askari mwenzao. Picha hii haihusiani na habari hapo chini |
WANAJESHI wanne wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakielekea Mtwara kusaidia kutuliza ghasia zinazoendelea mjini humo wamefariki dunia, huku wengine 20 wakijeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali wilayani Nachingwea mkoani Lindi.
Habari zilizopatikana hivi punde na kuthibitishwa na baadhi ya mashuhuda zinasema kuwa ajali hiyo ilihusisha lori la wanajeshi hao na gari nyingine imetokea eneo la Kilimani Hewa, kilomita mbili toka kambi ya Jeshi hilo ya 41KJ wilayani humo.
Taarifa hizo zinasema kuwa jumla ya wanajeshi 31 walikuwa kwenye msafara huo na kwamba 20 wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya wilaya hiyo, huku wengine saba wakitoka salama bila ya kuwa na majeruhi yoyote.
Inaelezwa kuwa mwendo kasi na kona kali iliyopo eneo la tukio ndiyo chanzo cha ajali hiyo, ingawa Polisi bado haijathibitisha taarifa hizo kuhusiana na vifo vya wanajeshi hao wanne walioelezwa wamefariki katika ajali hiyo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Viginia Ole Swai, amenukuliwa na kituo cha Radio One Stereo akisema huenda vumbi nalo lilichangia kutokea kwa ajali hiyo baada ya gari hizo kugongana katika ajali hiyo ambayo imepoteza uhai wa wapiganaji hao wa JWTZ wanne na wengine kujeruhiwa ambapo wapo hospitali wakitibiwa.