Kamanda Kova (kati) na Kenyela (kulia) wakiwa na IGP Said Mwema katika moja ya shughuli za kitaifa |
JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni, umekanusha taarifa zilizosambazwa kwenye baadhi ya mitaandao ya kijamii na mtaani kwamba Kanisa la KKKT Kunduchi limelipuliwa mabomu kama ilivyotokea kwa Kanisa la Katoliki la Arusha.
Kamanda wa Polisi mkoa huo, Charles Kenyela alisema taarifa zilizoenea kwamba bomu limelipuka katika Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania (KKKT), Kunduchi jijini Dar es Salaam zimeenea ndivyo sivyo ukweli ni kwamba askari walikuwa wanapambana na majambazi karibu na kanisa hilo.
Afande Kenyela alisema kwamba taarifa hizo sio za kweli na kwamba askari wa jeshi la polisi walikuwa wanapambana na majambazi karibu na eneo la kanisa hilo.
Alidai walipata taarifa za kundi la watu hao wanaosadikiwa kuwa majambazi ambao walijificha kwenye jengo ambalo ni la ghorofa na ndipo katika kuwalazimisha watokea askari wao waliamua kuwatupia bomu la machozi ambalo ndilo lililowatisha watu na kusambaza taarifa zisizo za kweli.
"Wakati askari wetu wanapambana na majambazi hayo- waumini wa kanisa hilo wamejitokeza kuwasaidia askari wetu. Naomba unisaidie kukanusha siyo kweli, nitazungumza na vyombo vingine vya habari kuweka sawa," amesema Kamanda Kenyela hivi punde alipokuwa akihojia na kituio cha redio cha Clouds FM.
Ufafanuzi kama huo pia umetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Suleiman Kova, aliyesema hajui uvumi huo umetolewa kwa lengo gani, wakati taifa bado likiwa katika 'vuguvugu' la tukio lililoacha majonzi la Arusha ambapo watu wasiojulikana walilipua bomu lililosababisha vifo vya watu wanne mpaka sasa na wengine kujeruhiwa baadhi vibaya ambapo wanaendelea na matibabu.
Kamanda Kova alisema ni vyema wanaosambaza taarifa hizo wajiridhishe na ushahidi ili kutowatia hofu watu wengine walio, kama alivyosema Kenyela kwamba japo leo haikuwa siku ya ibada lakini katika kanisa hilo la KKKT lililopo salama wa salimu walikuwepo baadhi ya watumishi waliotoa msaada kwao na kufanikiwa kuwanasa watuhumiwa wanne wakiwemo wanafunzi wawili wenye umri kati ya miaka 13 na 16 waliokuwa kundi moja na wahalifu hao waliodaiwa walikuwa wakipanga mipango ya uhalifu.