Zahoro Pazi katika uzi wa JKT Ruvu |
Pazi aliyesajiliwa na Simba akitokea JKT Ruvu aliyokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka Azam, aliwahi kusainishwa mkataba wa miaka minne msimu wa mwaka 2010 ili kujiunga na timu hiyo, lakini akakataa kujiunga nayo baada ya kutishwa na familia.
Anasema watu wa familia yake walimtishia kwamba angejiunga na Simba angeenda kuua kipaji chake kwani 'angepigwa misumari' na hivyo kuamua kubaki Mtibwa Sugar, jambo alililodai lilitokana na akili za kitoto na kutegemea ushauri wa watu wengine.
Pazi, mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyetamba na timu mbalimbali ndani na nje ya nchi, Idd Pazi 'Father' alisema kwa sasa amekuwa na maamuzi binafsi ndiyo maana amesaini kuichezea Simba kwa miaka mitatu.
Alisema kutua kwake Simba kuna changamoto kubwa zinazomfanya apigane ili apate namba na pia kuifanyia makubwa kama alivyofanya baba yake wakati akiidakia timu hiyo.
"Sina miujiza kwa kutua kwangu Simba, lakini naahidi nitajituma na kucheza kwa moyo wangu wote ili kuipa mafanikio timu hiyo na kutouangusha uongozi na benchi zima la timu hiyo walioniamini na kunisajili," alisema Pazi.
Mshambuliaji huyo anayecheza pia kama winga, alisema anaamini Simba ya msimu ujao itakuwa moto wa kuotea mbali chini ya King Abdallah Kibadeni mmoja wa makocha waliochangia kukuza na kuendelea kipaji chake alipokuwa Mtibwa Sugar.
"Chini ya Kibadeni, Simba itarajie makubwa ni bonge la kocha na mtu ambaye siwezi kumsahau kwa jinsi alivyosaidia kukiendeleza kipaji changu nilipotua timu ya vijana Mtibwa," alisema.
Pazi aliyewafanyiwa majaribio ya kucheza soka la kulipwa na klabu ya Bloemfontein Celtic mapema mwaka huu na kufaulu japo alichwa baada ya Mzimbabwe Roderick Mutuma kupewa nafasi yake kwa vile nafasi iliyokuwa ikiwania ni moja, alisema anajisikia fahari kucheza timu aliyoichezea baba yake.