Mwenyekiti anayedaiwa kutangazwa kinyemela, Mapesi katika mija ya mikutano yake kama kiongozi wa mtaa wa King'ongo |
Wakizungumza na MICHARAZO wakazi hao wengi wakiwa na hasira, wamedai kuwa wamechukizwa na uhuni waliofanyiwa na wasimamizi wa Uchaguzi wa Mtaa wao kwa kumtangaza kinyemela aliyekuwa Mwenyekiti wa mtaa huo, Demetrius Mapesi wakati mshindi halali waliyemchagua akiwa ni aliyekuwa Mgombea wa UKAWA kupitia chama cha CUF, Aboubakar Nyamuguma.
Wananchi hao walisema wapo katika kujiorodhesha majina kwa ajili ya kuandaa maandamano kwenye ofisi za Manispaa ya Kinondoni kulalamikia waliouita uhuni wa wasimamizi kutumia askari wa jeshi la Polisi kuwatawanya kwa mabomu kisha kutangaza mshindi ambao aliangushwa kwa kura walizopiga.
"Walichelewesha kutangaza majina baada ya kutokea sintofahamu, walipoona tumeamua kuwakomalia wamtangaze mtu tuliyemchagua usiku wa saa 4 wakaita Polisi wakaja kutupiga mabomu kisha wakamtangaza Mapesi kuwa kashinda bila wagombea kusaini fomu wala kubandika mpaka sasa matokeo hayo ubaoni kama inavyotakiwa, huu ni nini kama sio uhuni," alihoji mmoja wa wakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Baba Ramadhani.
Alisema pamoja na hila wanazofanya CCM za kutaka kulazimisha matokeo ili Mapesi aendelee kuwa kiongozi wa eneo lao wameapa hawatakubali na ikiwezekana wataifunga ofisi kwa makufuri mpaka Nyamuguma apewe ushindi wake kwa sababu ndiye waliyemchagua.
Mgombea anayedaiwa kuporwa ushindi, Aboubakar Nyamuguma alisema kuwa mpaka sasa hajui kitu gani kilichotokea baada ya awali kukubaliana na msimamizi kuziondoa kura zilizoonekana zimeongezeka kuliko idadi ya waliojiandikisha na kupiga kura.
"Ilionekana kura 32 zilizidi zaidi ya waliojiandikisha na kupiga kura ambao walikuwa 930, baadaye tukakubaliana zilizozidi ziondolewe kama taratibu zinavyotaka kisha zihesabiwe zinazopaswa na matokeo yalionyesha nimepata kura 461 dhidi ya 431 za mpinzani wangu," alisema.
"Cha ajabu baada ya kuona nimembwaga Mapesi Msimamizi na wasaidizi wake ambao wengi ni walimu wanaofundisha Shule ya King'ongo ambayo mpinzani wangu ni Mwenyekiti wa Kamati ya Shule waligoma kutangaza matokeo na kusababisha wananchi kucharuka kabla ya kuita Polisi na kuwapiga watu mabomu na kuwatawanya na kumtangaza Mapesi kuwa mshindi kwa kumpa kura 32 zilizoondolewa na hivyo kumfanya afikishe kura 463 dhidi ya zangu," alisema Nyamuguma.
Alisema kitu cha ajabu msimamizi alitangaza matokeo bila hata wagombea kusaini fomu kama inavyotakiwa na pia kutobandikwa ubaoni na kutokomea zake.
Aliongeza kuwa kwa kutambua kuwa amepokwa haki yake ameandika barua ya pingamizi dhidi ya kitendo hicho kwa Mratibu wa Uchaguzi Mkuu Kinondoni na nakala kutuma katika ofisi zote zinazohusika ikiwamo kwa viongozi wake wa UKAWA kuhakikisha haki inapatikana.
Alipoulizwa kama ni kweli wapo watu wanaotaka kufanya maandamano alisema, hana taarifa ila kama ni kweli ni uthibitisho kuwa wananchi hata wenyewe wanasbabu ya kufanya hivyo kwani walimchagua ili awaongoze baada ya kutoridhishwa na uongozi wa kiongozi aliyekuwapo awali.
Mapesi mwenyewe hakuweza kupatikana kueleza juu ya mtarafuku huo na anaelezaje wananchi wanavyotaka kufanya maandamano kumpinga kuonyesha hakubaliki katika mtaa huo, ila MICHARAZO inaendelea na juhudi hizo.