Wachezaji wa Kiafrika wazidi kupata soko Barani Ulaya hivyo Watanzania wasichezee fursa ya soka la kimataifa.
* Zaidi ya Mawakala 15 wawasiliana na Tanzania Mwandi kuwahitaji wachezajiZaidi ya mawakala 15 tayari wamewasiliana na Kampuni ya Tanzania Mwandi kuwahitaji wachezaji mbalimbali kwaajili ya kuwapeleka kwenye klabu za barani Ulaya, Asia na Afrika ili kucheza soka la kulipwa.
Mwitikio huo umeongezeka kutokana na vijana wa kiafrika kuwa na soko kubwa katika ulimwengu wa sasa wa mpira wa miguu kwa nchi mbalimbali kama Sweden, Uholanzi, Denmark, Ureno na nchi nyinginezo.
Arne Anderson kutoka AA Football Service ya Sweden amesema kuwa binafsi yuko tayari kuchukua wachezaji wawili kwaajili ya kuwatafutia clubs nchini humo kwani tayari mafanikio ya wachezaji watano wa kiafrika aliowapeleka yamempa maombi ya timu nyingi za Sweden.
“Niko tayari kuchukua wachezaji wawili endapo tutakubaliana kuhusu maslahi yangu pindi wachezaji hao wakianza kucheza hapa”, Arne amesema.
Kutokana na mafanikio hayo na maombi ya mawakala lukuki Kampuni ya Tanzania Mwandi inazidi kuwasisitizia wachezaji wa Kitanzania kujaza fomu zinazopatikana kupitia blog.tanzaniamwandi.co.tz ili kufanya majaribio ya kucheza soka nchini Sweden, Norway, Denmark, Uholanzi, Ureno, Uswiss, Ufaransa na Ubelgiji, barani Asia (Kuwait, China, Qatar nk) na klabu nyingine barani Afrika.
Mpaka sasa jumla ya wachezaji wa kitanzania 15 wamekwishajaza fomu za haraka kwenye tovuti ya Tanzania Mwandi huku kampuni ikiwa imepokea pia maombi ya wachezaji 25 kutoka nje ya nchi.
“Maombi yanazidi kuja ingawa tunawahimiza Watanzania wasikimbie kiingilio cha shilingi 300, 000 wakumbuke kuwa wanafanya majaribio wakiwa nyumbani na watakapopata timu Kampuni ya Tanzania Mwandi haitachukua chochote kwenye mikataba yao, ni wao na mawakala ndio watakokubaliana juu ya watakachokipata kutoka kwa klabu husika”, alisema Teonas Aswile, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Mwandi, waandaaji wa African Youth Football Tournament.
Aswile amezialika klabu mbalimbali za ligi kuu ya soka Tanzania Bara na Visiwani kutazama wachezaji watakaofika katika michuano hiyo kwani wapo baadhi ya wachezaji kutoka nje ya nchi ambao watafika na wangependa kucheza soka la Tanzania.
“Kati ya wachezaji 25 wa nje ya nchi wengine wameomba tuwatafutie timu hapa nchini hivyo klabu zikija zinaweza kuwapata wachezaji hao wakiwa huru kwasababu watakuja kwa gharama zao kufanya majaribio nchini. Pia klabu hizo zitumie fursa hii kuuza wachezaji wake.”
Michuano ya African Youth Football Tournament inatarajia kufanyika Juni 10 hadi 14 mwaka huu katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam na kushirikisha vijana kati ya miaka 18 hadi 21 kutoka Tanzania na bara zima la Afrika. Taarifa zaidi kuhusu michuano hiyo zinapatikana kupitia; blog.tanzaniamwandi.co.tz
Imetolewa na Idara ya Habari
Kampuni ya Tanzania Mwandi,
TANCOT House, Ground Floor,
S. L. P 79944,
Dar es Salaam.