|
Jerome Lambele |
KIPAJI kikubwa alichonacho katika soka, hasa katika kufumania nyavu kimemwezesha mara kadhaa, mchezaji Jerome Lambele kunyakua tuzo mbalimbali za Mchezaji Bora na Mfungaji Bora.
Akicheza soka kwao Kigoma katika timu ya Kayengeyenge aliwahi kunyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mkoa, na mwaka jana tena alitwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Tuzo hiyo aliipata kwa kufunga jumla ya mabao 16 yaliyoisaidia Ashanti United kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya misimu sita kupita tangu ilipoteremka mwaka 2007.
Mshambuliaji huyo anayeichezea Ruvu Shooting kwa sasa, anasema tuzo hizo na nyingine alizowahi kunyakua kupitia klabu na michuano mbalimbali zimekuwa zikimpa faraja kubwa kama mwanasoka.
"Kwa kweli najisikia faraja kunyakua tuzo mara kadhaa kwa kipaji nilichojaliwa, ila furaha kubwa zaidi kwangu ni kuiwezesha timu ya taifa ya Coca Coca kunyakua taji la dunia nchini Brazili mwaka 2008," anasema.
Lambele, mwenye mabao matatu kwa sasa katika ligi ya msimu huu anasema tukio la Brazili la kunyakua taji bila kupoteza mchezo wowote limebaki kichwani mwake.
"Hili ndilo tukio la furaha lisilofutika kichwani mwangu, kwa sababu hakuna aliyetegemea kama Tanzania tungeweza kunyakua ubingwa huo, lakini tulifanikiwa," anasema.
Lambele anakumbuka katika michuano hiyo ya vijana U17 waliifunga Chile kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali baada ya awali kutoa visago kwa Peru kwa kuilaza 5-0, ikatoka suluhu na Chile kabla ya kuilaza Argentina mabao 2-0 katika mechi za kundi. Hatua ya Robo fainali waliilaza Argentina 2-0 kisha kuifumua Paraguay kwa mabap 3-1 hatua ya Nusu Fainali.
Shabiki huyo wa klabu ya Manchester United anayemzimia nyota wa timu hiyo, Wayne Rooney, anasema kunyakua taji hilo kwa timu yao ilikuwa ni uthibitisho kuwa Tanzania imejaliwa vipaji vingi vya soka.
Anasema vipaji vya soka nchini vipo ila vinashindwa kuendelezwa hasa kutokana na kukosekana kwa mashindano mengi ya vijana.
"Lazima TFF na wadau wa soka wawekeze katika soka la vijana kwa kusaidia kuwe na mashindano mengi kuendeleza vipaji kwa faida ya taifa, pia klabu zitoe kipaumbele kwa timu zao za vijana," anasema.
Lambele anayependa kula ugali kwa samaki na kunywa juisi ya matunda mchanganyiko, anasema bila uwekezaji mkubwa katika soka la vijana ni vigumu taifa kuzifikia nchi nyingine zinazotamba duniani.
|
Lambele akichuana na Niyonzima
|
AJABU
Lambele anayejishughulisha na biashara na anayeshukuru soka kumsaidia kwa mambo mengi ikiwamo kupata elimu yake ya sekondari kwa sababu ya kipaji chake, anasema licha ya kucheza mechi nyingi halisahau pambano la Ligi Kuu msimu 2011-2012.
Anasema anaikumbuka mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Chamazi Novemba 5, 2011 wakati akiichezea Moro United walipoumana na Simba na kutoka nao sare ya 'miujiza' ya mabao 3-3.
Anasema hakuna aliyetarajia mechi hiyo ingeisha kwa sare hiyo kwani Moro Utd waliwatangulia Simba kwa kuwafunga mabao 3-1 hadi mapumziko, bao la Simba likifungwa 'jioni' ya kipindi hicho.
"Kwangu niliona kama miujiza kwa sababu tuliamini tumeshaimaliza Simba baada ya kwenda mapumziko tukiongoza 3-1," anasema.
"Hata hivyo kipindi cha pili mambo yalibadilika na Simba kurejesha mabao hayo na kulazimika tugawane pointi kutokana na sare ya 3-3."
Mkali huyo anasema mbali na mechi hiyo pia anakumbuka mechi ya Moro Utd msimu huo dhidi ya Yanga lililochezwa uwanja wa Jamhuri, Morogoro alipoifungia timu yake bao la kusawazisha.
"Bao hilo ndilo goli tamu na bomba kwangu, kwani nililifunga kiufundi na kuisaidia Moro Utd kupata sare ya 1-1," anasema.
Juu ya huzuni, Lambele ambaye hajaoa wala kuwa na mtoto mwenye kiu ya kutaka kurejea darasani ili ajiendeleze kielimu, anasema ni kipigo walichopewa na Mbeya City katika mechi ya duru la kwanza.
"Kwa kweli kipigo kile cha mabao 2-1 tulichopewa ugenini jijini Mbeya katika duru la kwanza ndiyo huzuni yangu kwani hatukutegemea kwa namna tulivyocheza vyema," anasema.
|
Akiwa mbele ya gari lake
|
KIPAJI
Lambele aliyezaliwa Juni 23, 1993 Ujiji Kigoma na kusoma Shule yua Msingi Buzebazeba kabla ya kufaulu na kuendelea Kichangachui Ujiji na kuja kumalizia elimu yake Shule ya Kanali Idd Kipingu.
Tangu akiwa kinda Lambele alianza kuonyesha kipaji chake cha soka kwa kucheza mtaani kabla ya kutamba shuleni na kupewa Uwaziri wa Michezo akimudu nafasi zote za ushambuliaji.
Baadhi ya timu alizozichezea kabla ya kuja kutamba kwenye ligi ni True Lies, Kayengeyenge, Fire Stone na Kigoma United kabla ya kutua Dar na kutamba kwenye michuano ya Copa Coca Cola-2008.
Michuano hiyo ndiyo iliyomfungulia nyota huyo baraka za kuonwa na timu za Ligi Kuu akidakwa na Moro Utd kabla ya kutua Ashanti Utd ikiwa daraja la kwanza na kuipandisha Ligi Kuu msimu huu.
Lambele aliweka rekodi ya kufunga mabao 6 pekee yake katika mchezo mmoja walipoisulubu Moro Utd kwa mabao 10-1 pia alifunga mabao pekee yake walipoilaza Transit Camp 4-0 na kufunga hat trick nyingine mbili na kuipadisha Ashanti Utd Ligi Kuu.
Hiyo ni rekodi ya aina yake kwa vile katika mechi za ligi ni Edibily Lunyamila na Nsa Job waliokuwa wameweza kufunga idadi kubwa ya mabao katika mechi moja. Kila mmoja alifunga mabao matano.
Pia haikuwahi kushuhudiwa mchezaji mmoja kufunga hat-trick nne mfululizo katika mechi yoyote ya ligi kama alivyofanya mchezaji huyo katika FDL akiwa na Ashanti kabla ya kuihama msimu huu.
Lambele aliihama Ashanti na kutua Ruvu Shooting aliyoisaidia timu hiyo kushika nafasi ya tano kwenye msimamo nyuma ya Simba, Mbeya City, Yanga na Azam.
Matarajio yake ni kufika mbali katika soka na kimaisha na kutoa shukrani zake kwa wazazi wake, Kanali Kipingu kwa kumsomesha na makocha Kim Poulsen aliyemnoa U17 mpaka sasa na Tom Olaba.
Lambele anayedaiu kusumbuliwa dimbani na beki wa timu yake aliyemtaja kwa jina la Chogo, anawataka wachezaji wenzake kuwa na nidhamu, kufanya mazoezi na kusikiliza makocha na kuwa na kiu ya maendeleo hasa ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
"Wachezaji wakizingatia nidhamu, kujituma mazoezini na uwanjani kutasaidia kuinua kiwango cha soka letu, pia wadau na viongozi wathamini mchango wa wachezaji kwani wanavuja jasho," anasema.
===============