* Ashanti Utd kujiuliza kwa Rhino Rangers
* Tambwe kuendelea kucheka na nyavu
Mshambuliaji nyota wa Simba na kinara wa mabao katika ligi kuu, Amissi Tambwe atawanyamazisha Ruvu Shooting leo |
Pambano hilo litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ni kati ya mechi nne za ligi hiyo iliyopo raundi ya ya 20 zitakazochezwa leo katika viwanja tofauti na mashabiki wana hamu kubwa ya kutaka kuona Simba itavuna nini kwa maafande hao waliobugizwa mabao 7-0 na Yanga.
Simba inayokamata nafasi ya nne ikiwa na pointi 32 inahitaji ushindi ili kutuliza hasira za mashabiki wao ambao wamekosa amani baada ya timu yao kupata matokeo yasiyoridhisha katika mechi zao nne zilizopita walizoambulia pointi mbili tu huku ikipoteza michezo miwili na kuambulia sare mbili.
Wanachama na mashabiki wa Simba wanaoushutumu uongozi wa Ismail Aden Rage kwa madai ya kuitelekeza timu, huku baadhi wakihisi kuna hujuma zinazofanywa ili timu ifanye vibaya, kitu ambacho kinaweza kutulizwa iwapo Simba itashinda tu leo vinginevyo moto utawaka Msimbazi.
Kocha Zdrakov Logarusic anayeshutumiwa kwa kuchangia kufanya vibaya kwa timu hiyo kitendo chake cha kuwafokea na kuwatulea maneno machafu wachezaji anaweza kukiweka kibarua chake rehani, iwapo Simba itapoteza mechi yao leo kwa Ruvu Shooting inayonolewa na Tom Olaba.
Logarusic amedaiwa amekuwa mkali kupita kiasi hali inayowafanya wachezaji wasijiamini uwanjani na kufanya timu ipate matokeo mabaya, hali inayoweza kuwa mbaya zaidi kama Ruvu itafuata nyayo za 'kaka' zao wa JKT Ruvu kwa kuisulubu vijana wa Msimbazi.
Wachezaji wa Simba chini ya manahodha wao, Nassor Masoud 'Chollo' na Amri Kiemba wameapa kupigana kiume ili kurekebisha makosa, huku wakijaribu kuficha 'siri' juu ya tatizo ambalo linawakabilia wachezaji kwa kudai hawadai wala kucheza chini ya kiwango kwa kudai posho zao.
"Hali hii inatuhuzunisha hata sisi, lakini ni ugumu wa ligi na tutapigana kiume kuona tunashinda mechi zetu zilizosalia za ligi kuu," alisema Chollo alipozungumza na wanahabari wiki hii.
Hata hivyo Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire ametamba kuwa, baada ya kuotewa na Yanga jumamosi iliyopita na kubugizwa mabao 7-0 wasingekubali kuona wakifungwa pia na Simba leo.
Bwire alisema kochao kutoka Kenya, Tom Olaba na wachezaji wameuhakikishia uongozi kuwa leo watakufa na Simba ili kunyakua pointi tatu na kujiweka pazuri kwenye msimamo baada ya wiki iliyopita kuteleza kwa mabingwa watetezi na kudai Simba leo hawaponi Taifa.
"Hawaponi. Hatukubali kufungwa kwa mara nyingine tena. Yanga wametudhalilisha vya kutosha na sasa ni zamu ya kurekebisha makosa kwa kuichabanga Simba kwenye uwanja wa Taifa," alisema.
Ukiondoa mechi hiyo ya Simba na Ruvu, leo pia kutakuwa na mechi nyingine nne zitazikutanisha timu nane ambapo Kagera Sugar itakuwa nyumbani kuikaribisha JKT Ruvu uwanja wa Kaitaba, Kagera huku Rhino Rangers itakakuwa wageni wa Ashanti United kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Prisons Mbeya itaikaribisha Mgambo JKT kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2013-2014
P W D L F A GD PTS
01.Azam 18 11 07 00 35 12 23 40
02.Yanga 17 11 05 01 41 12 29 38
03.Mbeya City 20 09 09 02 24 16 08 36
04.Simba 19 08 08 03 35 19 16 32
05.Kagera Sugar 19 06 08 05 16 15 01 26
06.Coastal Union 19 05 10 04 14 09 05 25
07.Mtibwa Sugar 19 06 07 06 23 23 00 25
08.Ruvu Shooting 19 06 07 06 20 26 -06 25
09.JKT Ruvu 19 07 01 11 16 29 -13 22
10.Prisons 18 04 08 05 17 18 -01 20
11.Mgambo 19 05 05 09 12 27 -15 20
12.Oljoro 21 02 10 09 15 30 -15 16
13.Ashanti 19 03 05 11 15 34 -19 14
14.Rhino Rangers 19 02 07 10 12 23 -11 13
Wafungaji:
17- Tambwe Amisi (Simba)
10- Kipre Tchetche (Azam)
09- Elias Maguri (Ruvu Shooting) Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu (Yanga)
08-Juma Luizio (Mtibwa Sugar), Mrisho Ngassa (Yanga)
07- Peter Michael (Prisons)
06- Themi Felix (Kagera Sugar), Mwegani Yeya (Mbeya City)
05- Tumba Sued (Ashanti Utd), Jerry Santo (Coastal Union)
04- Jerry Tegete (Yanga), Jonas Mkude, Betram Mombeki (Simba), Bakar Kondo, Salum Machaku (JKT Ruvu), Jerome Lambele (Ruvu Shooting), Abdallah Juma (Mtibwa Sugar)
No comments:
Post a Comment