STRIKA
USILIKOSE
Sunday, March 2, 2014
Simba yazinduka, Tambwe hashikiki kwa mabao
WAKATI Simba ikizinduka kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuicharaza Ruvu Shooting 'Wazee wa Wiki' kwa mabao 3-2, Mshambuliaji kutoka Burundi, Amissi Tambwe 'Amissi Magoli' akiendelea kujihakikishia kiatu cha dhahabu katika ligi hiyo kwa msimu huu.
Tambwe aliyefunga mabao mawili katika mchezo huo wa leo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa, amefikisha mabao 19 na kufikia rekodi iliyowahi kuwekwa na John Bocco 'Adebayor' misimu miwili iliyopita.
Mrundi huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 23 na kuongeza la pili dakika 33 na kuifanya Simba kwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko yaliyoonekana kuinufaisha zaidi Ruvu walioongeza kazi ya mashambulizi na kujipatia bao la kwanza lililofungwa na Said Dilunga kabla ya Haruna Chanongo kuifungia Simba bao la tatu.
Bao la pili la Ruvu lilifungwa kwa mkwaju wa penati na Lambele Jarime baada ya mmoja wa wachezaji wa Simba kunawa mpira katika harakati za kuokoa mpira langoni mwake.
Kwa ushindi huo Simba imefikisha pointi 35 na kuendelea kusalia nafasi ya nne nyuma ya Mbeya City yenye pointi 36 ambayo jana ililazimishwa suluhu na Oljoro JKT.
Kwa upande wa mbio za kuwania kiatu cha dhahabu, Amissi Tambwe amezdi kuwaacha mbali wapinzani wake baada ya kufikisha jumla ya mabao 19, huku anayemfuata Kipre Tchetche akiwa na mabao 10.
Mwanzoni mwa msimu huu Tambwe alinukuliwa na MICHARAZO akisema amepania kufunga jumla ya mabao 20 msimu huu ili kunyakua kiatu cha dhahabu kitu kinachoonekana kuwa kweli kwani mechi zikiwa bado kama sita kabla ya ligi kufikia tamati ameshafikisha idadi hiyo bao moja zaidi ya lengo lake je atyaifikia rekodi ya Abdallah Juma nyota wa zamani wa Mtibwa aliyefunga mabao 25 katika msimu mmoja? Tusubiri tuone.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment