STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, December 2, 2011

Zanzibar mguu ndani mguu nje Kombe la Chalenji 2011



HATMA ya timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes kuendelea na michuano ya Kombe la Chalenji, inasubiri majaliwa ya sheria ya kumpata best losser, kufuatia goli la Amissi Cedric lililo wapa ushindi Burundi wa goli 1-0 pala walipowakabili Uganda jana.
Zanzibar ilipata ushindi wake wa kwanza kwenye michuano hiyo inayoendelea jijini jana katika pambano lililochezwa mapema kwenye uwanja wa Taifa kwa kuilazaq Somalia mabao 3-0 na kufikisha pointi nne.
Mabao ya mshambuliaji wao hatari Suleiman Kassim 'Selembe', Ally Badru na nahodha Aggrey Morris yaliisaidia Zanzibar kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kutegemeana na matokeo ya makundi mengine yanayochezwa leo na kesho.
Kama mambo yatajipa Zanzibar waliopo nafasi ya tatu katika kundi lao la B nyuma ya Burundi wanaoongoza kwa pointi 7 na Uganda wenye pointi sita itafuzu hatua ya robo fainali.
Kwani kama sio ushindi wa bao 1-0 iliyopata Burundi mbele ya Uganda, Zanzibar isingekuwa na wakati mgumu wa kusubiri kapu la hisani kusonga mbele.
Zanzibar itabidi wangoje hekima za CECAFA kama watapata nafasi katika best loser ingawa kwa kuangalia matokeo ya makundi mengine yalivyo moja ya nafasi ya mshindwa bora kwa 'mashujaa' hao wa Zanzibar ni kubwa, ingawa soka halipo hivyo.
Ndugu zao Tanzania kesho nao watakuwa vitani kupigana kutinga robo fainali, kwa kuumana na Zimbabwe wanaolingana nao pointi tatu, huku Rwanda amabyo itacheza leo dhidi ya Djibout ikiwa imeshajihakikishia nafasi mojawapo ya kucheza hatua hiyo ya mtoani itakayoanza Jumatatu.

TMK kuumwa Kichwa Dar mpaka Mwanza



BAADA ya kimya cha miaka mitatu, kundi la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family, limefyatua wimbo na video mpya iitwayo 'Kichwa Kinauma' itakayotambulishwa katika maonyesho maalum jijini Dar na Mwanza.
Kibao hicho kipya kilichorekodiwa 'audio' yake katika studio za MJ Records na video kutolewa na kampuni ya Visual Lab, inatarajiwa kusambazwa kwenye vituo vya redio na runinga wiki hii na kufuatiwa na maonyesho katika majiji hayo.
Meneja wa kundi hilo, Said Fella 'Mkubwa Fella' aliliambia MICHARAZO kuwa, kazi hiyo mpya itatambulishwa kwa wakazi wa Dar katika onyesho litakalofanyika Jumapili ya Desemba 4 kwenye ukumbi wa Maisha Club na kisha kuvaamia Mwanza Desemba 9.
Fella alisema wakiwa jijini Mwanza, kudni lao litakitambulisha kibao hicho na nyimbo nyingine binafsi za wasanii wa TMK Wanaume Family, kwenye ukumbi wa Villa Park.
"Mkubwa tumefyatua kibao kipya na video yake iitwayo Kichwa Kinauma ikiwa ni baada ya ukimya wa miaka mitatu tangu tutoe kazi ya mwisho na tutaitambulisha rasmi kwa mashabiki wetu katika miji ya Dar na Mwanza," alisema.
Fella aliongeza katika maonyesho hayo mawili ya jijini Dar na Mwanza, pia wataonyesha 'trela' la filamu ya kundi hilo ili kuwapa kionjo tu mashabiki wao kabla ya filamu hiyo kuingizwa sokoni katikati ya mwezi ujao.
"Unajua tumefyatua filamu inayohusiana na kundi letu, hivyo katika maonyesho hayo mawili ya utambulisho wa 'Kichwa Kinauma', pia tutaonyesha trela la filamu hiyo ambayo tutaitoa hadharani katikati ya Desemba," alisema Fella.
Kundi hilo la TMK Wanaume Family, linaundwa na wasanii kadhaa nyota wakiwemo Mhe Temba, Said Chegge, Dogo Aslay anayetamba na wimbo wa 'Nakusemea' na wengineo.

Sikinde yajiandaa kukamilisha albmu mpya

BENDI kongwe ya Mlimani Park 'Sikinde' ipo katika maandalizi ya mwisho ya kufyatua albamu yao mpya itakayozinduliwa mwishoni mwa mwezi ujao.
Katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo, alisema kuwa tayari wameshafyatua vibao kadhaa kwa ajili ya albamu hiyo itakayokuwa na nyimbo sita na watamalizia nyimbo zilizosalia kabla ya katikati ya Desemba.
Milambo, alisema katika harakati za kuitambulisha albamu hiyo wamefyatua video ya kibao chao cha 'Jinamizi la Talaka' ambao unatesa kwenye vituo kadhaa vya redio nchini.
"Sikinde tupo katika maandalizi ya kukamilisha kurekodi albamu yetu mpya itakayokuwa na nyimbo sita, ambayo tutaitoa hadharani mwishoni mwa Desemba," alisema.
Katibu huyo alivitaja baadhi ya vibao vitakavyokuwa katika albamu hiyo itakayochukua nafasi ya 'Supu Imetiwa Nazi' kuwa ni; 'Jinamizi la Talaka', 'Bundi', 'Mihangaiko ya Kazi' na 'Asali na Shubiri'.
Sikinde, kwa muda wa miaka miwili sasa haijatoa albamu yoyote tangu ilipotamba na Supu Imetiwa Nazi ambayo ilifyatuliwa wakati ikiwa chini ya Shirika na Maendeleo Dar es Salaam, DDC iliyowatema rasmi mapema mwaka uliopita.

Poulsen bado hajaniamini-Jabu




BEKI mahiri wa Simba anayezichezea pia timu za taifa, Juma Jabu, amekiri kwamba kocha wa sasa wa timu ya taifa (Taifa Stars), Jan Poulsen hajamuamini ndiyo maana amekuwa haitwi mara kwa mara katika kikosi hicho.
Hata hivyo, alisema kutoaminiwa huko kunatokana na kuwepo majeruhi kwa muda mrefu tangu Mdenmark huyo alipoitwaa timu hiyo toka kwa Mbrazil, Marcio Maximo.
Jabu maarufu kama 'JJ', alisema amekuwa akipata nafasi ndogo ndani ya kikosi cha Stars kwa vile Poulsen hajaridhika naye, tofauti na ilivyo kwa Maximo ambapo panga pangua hakukosekana kikosini.
"Sio siri sijapata nafasi kubwa ndani ya kikosi cha Stars tangu iwe chini ya Poulsen, hii inatokana na kocha kutoniamini pengine kwa vile nilikuwa majeruhi na hivyo kutoonekana dimbani, ila naamini michuano ya Chalenji itanirejesha Stars," alisema.
Alisema kuitwa kwake katika kikosi cha Kilimanjaro Stars ambayo leo inamaliza mechi zake za makundi dhidi ya Zimbambwe, ni fursa nzuri ya kumshawishi Poulsen ampe nafasi ya kudumu katika Stars inayokabiliwa na mechi za kuwania kufuzu CAN 2013 na WC 2014.
Katika hatua nyingine beki huyo alisema mipango yake ya kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini inaendelea vema, ingawa hakupenda kuweka bayana kwa madai suala lake linasimamiwa na wakala wake.
"Mipango yangu ya kwenda Afrika Kusini ipo pazuri, ila mwenye nafasi ya kuliongelea kwa undani ni wakala wangu," alisema Jabu.

Mkenya Kariuki kutua nchini Kesho kupiogana na Nassib Ramadhan



MPINZANI wa Bingwa wa Dunia anayetambuliwa na World Boxing Forum, Nassib Ramadhan 'Manny Pacquiao', Mkenya Anthony Kariuki, anatarajia kutua nchini kesho kwa pambano lao litakalofanyika Desemba 9 jijini Dar es Salaam.
Kariuki na Nassib watapigana katika pambano lisilo la ubingwa la raundi 10 uzani wa Fly kwenye ukumbi wa DDC Keko, ambapo watasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Akizungumza na MICHARAZO, mratibu wa pambano hilo, Pius Agathon, alisema Kariuki atatua nchini leo mchana akiambatana na kocha wake tayari kwa pambano lake ambalo litaenda sambamba na maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru.Agathon, alisema kambi ya Mkenya huyo itakuwa eneo la Keko, wakati mpinzani wake ipo eneo la Mabibo chini ya kocha wake, Christopher Mzazi.
"Mkenya atakayepigana na Nassib Ramadhan atatua nchini Jumamosi (kesho)na moja kwa moja ataingia kambini eneo la Keko, tayari kuvaana na mpinzani wake aliyejichimbia Mabibo," alisema Agathon.
Agathon aliongeza kuwa maandalizi kwa ujumla ya pambano hilo litakalohudhuriwa pia na nyota wa zamani wa mchezo huo walioliletea sifa Tanzania katika miaka 50 ya Uhuru yamekamilika na inasubiriwa siku ya kufanyika kwa mchezo huo.
Alisema siku hiyo kutakuwa na michezo mitano ya utangulizi kabla ya Nassib Ramadhan kupeperusha bendera ya Tanzania mbele ya Mkenya.

BREAKING NEWS: Mr Ebbo hatunaye



Taarifa zilizotufikia muda huu zinasema kwamba aliyekuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Abel Loshilaa Motika 'Mr Ebbo' amefariki alfajiri ya leo na anatarajiwa kuzikwa huko kwao Arusha siku ya Jumapili.
Mr Ebbo aliyetamba na staili yake ya kuimba 'kiswahili cha kimasai', arakumbukwa kwa nyimbo matata kama Mi Mmasai Bana, Maneno Mbofu Mbofu, 'Pombe' na nyinginezo.
Kwa taarifa za awali zinasema alikuwa akiugua kitambo, ingawa haikuwahi kuripotiwa mapema hadi leo tulipopenyezewa taarifa hizi.
Mungu Aiweke Roho ya Mr Ebbo Mahali Pema. Amin