STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 1, 2014

Libya ndiyo mabingwa wapya wa CHAN-2014

 
LIBYA imeendeleza maajabu ya kushinda michezo yake kwa mikwaju ya penati baada ya usiku huu kunyakua taji la michuano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2014 kwa kuilaza Ghana katika pambano la fainali lililochezwa uwanja wa Cape Town, mjini Cape Town nchini Afrika Kusini.
Timu hizo zilishindwa kutambia katika muda wa kawaida wa dakika 90 na hata zilipoongezwa dakika 30 bado zilishindwa kupenyaza mipira wavuni na kumaliza dakika 120 bila ya kufungana.
Katika hatua hiyo kama ilivyokuwa katika mechi yake ya robo fainali dhidi ya Gabon kisha kwenye nusu fainali dhidi ya Zimbabwe ndivyo ilivyokuwa katika fainali ya leo kwa Libya kuibuka na ushindi wa mikwaju hiyo na kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza wakiwarithi 'ndugu' zao wa Tunisia.
Libya imeshinda taji hilo kwa ushindi wa penati 4-3, ambapo Ghana walipoteza penati mbili za mwanzo kabla ya kujirekebisha na kulazimisha penati kufikia sita na kupoteza ya mwisho iliyowapa waarabu hao taji.
Penati za mabingwa hao zilitumbukizwa kimiani na Faisal Saleh Al Badri, Muataz Mahde Fadel, Ahmed Al Maghasi na Ahmed El Trbi, huku za Mohamed Elgadi na Abdulsalam Omar zikiota mbaya.
Ghana wenyewe walipata penati zao kupitia kwa Attobrah, Saka, Owusu, huku Akuffu, Ainooson na ile ya mwisho ya Tijani zikienda upogo na kuwafanya Black Stars kulikosa kombe hilo kwa mara ya pili katika fainali mbili ilizocheza katika michuano hiyo, mara ya kwanza ikizidiwa kete na DR Congo kule Ivory Coast.

Barcelona yafa nyumbani, Valencia yaifanyizia

FC Barcelona Tickets
VINARA wa Ligi Kuu ya Hispania, Barcelona imeshindwa kutamba nyumbani kwake baada ya kunyukwa mabao 3-2 na Valencia licha ya Lionel Messi kuifungia timu yake bao kwa mkwaju wa penati.
Wenyeji walitangulia kupata bao la mapema kupitia kwa Alex Sanchez aliyefunga dakika ya 7 kabla ya wageni kulikomboa dakika moja kabla ya mapumziko baada ya Dani Parejo kufunga.
Kipindi cha pili kilikuwa cha mchakamchaka zaidi kwa timu zote kutafuta mabao zaidi na walikuwa ni Valencia walipopata bao la pili dakika ya 48 lililofungwa na Pablo Piatti, hata hivyo penati ya Lionel Messi katika dakika ya 54.
Paco Alcacer aliifungia Valencia bao la tatu dakika tano baada ya Messi kufunga penati hiyo na kufanya hadi mwisho wa pambano hilo ambalo lilishuhudia Jordi Alba wa Barcelona akitolewa nje ya uwanja  baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kufuatiwa na nyekundu dakika ya 78.
Pamoja na kipigo hicho cha nyumbani Barcelona bado imebaki kileleni ikiwa na pointi 54 sawa na Atletico Madrid na kufuatiwa na Real Madrid yenye pointi 53.

Nigeria washindi wa tatu CHAN 2014

 Nigeria players at CHAN
BAO pekee lililofungwa na Chinonso Obiozor dakika za jioni zimeiwezesha Nigeria kunyakua ushindi wa tatu katika michuano ya fainali za CHAN 2014 dhidi ya Zimbabwe iliocheza pungufu kwa muda mrefu baada ya mchezaji wao mmoja Mumbara kulimwa kadi nyekundu dakika ya 17 tu ya mchezo huo.
Nigeria ambayo ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kunyakua taji hilo lililokosa mwenyewe safari hii baada ya waliokuwa watetezi Tunisia kushindwa kutinga fainali za Afrika Kusini, ilionyeshana kazi barabara na wapinzani wao ambao licha ya kucheza pungufu lakini ilionyesha uhai mkubwa.
Obiozor alifunga baoa hilo akimalizia kazi nzuri ya Ejike Uzoenyi na kukifita machozi kikosi hicho cha Stephen Keshi kwa kupata nafasi hiyo licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo.
Saa moja baadaye inatarajiwa kupigwa pambano la fainali za michuano hiyo ambayo itatoa bingwa mpya wa CHAN wakati Ghana itakapopepetana na Libya kwenye uwanja huo huo wa Cape Town.
Timu hizo zilifika hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa mikwaju ya penati dhidi ya timu zilizocheza mchezo wa kuwania nafasi ya tatu yaani Zimbabwe na Nigeria.

Mashetani Wekundu bado kimeo, walazwa 2-1

Manchester United's Juan Mata
Pamoja na Mata kuonyesha kiwango, Man Utd wamelala muda mfupi uliopita 2-1
Kevin Mirallas
Kevin Miralla akiifungia Everton bao la ushindi dhidi ya Aston Villa

Hull City's Shane Long
Shane Long akiifungia Hull City bao la kuongoza dhidi ya Spurs

UGONJWA unaoisumbua Manchester United msimu huu katika Ligi Kuu ya England bado haujapata tiba, bali ulikuwa umepoa baada ya jioni hii kukandikwa ugenini mabao 2-1 na Stoke City, huku Everton kushinda nyumbani magoli 2-1 dhidi ya Aston Villa.
Mashetani Wekundu hao ambao walizinduka mapema wiki hii kwa kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya Cardiff City, ilishindwa kuendeleza makamuzi yake kwa kulala katika mchezo na kuzidi kuwakosesha raha mashabiki wa klabu hiyo.
Vijana hao wa David Moyes, walienda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0 baada ya wenyeji kupata bao la dakika ya 38 kupitia kwa Charlie Adam kabla ya kulisawazisha dakika chache baada ya kuanza kipindi cha pili kupitia kwa Robin van Persie.
Hata hivyo Charlie Adam aliipigilia msumari mwingine katika 'jeneza' na Man United katika dakika ya 52.
Katika mechi nyingine, Everton ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Aston Villa, huku Southampton ikiwa ugenini ilipata ushindi wa magoli 3-0 dhidi y Fulham.
Tottenham Hotspur walishindwa kutamba ugenini baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Hull City na  Cardiff City kutamba nyumbani kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Norwich City.

Simba yaua Taifa, Ashanti yanyukwa Chamazi

Amis Tambwe aliyepiga 'hat trick' yake ya pili VPL
Kikosi cha Simba
AMISI Tambwe amedhihirisha nia yake ya kunyakua kiatu cha dhahabu baada ya jioni hii kufunha 'hat trick' yake ya pili msimu huu wakati Simba ikipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Oljoro JKT.
Mabao hayo yamemfanya mshambuliaji huyo kutoka Burundi kufikisha jumla ya mabao 13 na kuwakimbia Elias Maguli wa Ruvu Shooting na Kipre Tchetche wa Azam wenye mabao tisa kila mmoja wanaomfukuzia katika magoli.
Simba ilitawala pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa kwani ilianza kuandika bao la kwanza dakika ya 12 tu kupitia Jonas Mkude kabla ya Tambwe kuanza vitu vyake kwa kufunga mabao mawili yaliyofanya Mnyama aende mapumziko wakiongoza 3-0.
Tambwe laifunga bao la kwanza kwake na la pili kwa Simba dakika ya 24 kabla ya kuongeza jingine dakika ya 29 na kuja kupiga 'hat trick' yake ya pili baada ya ile ya kwanza alipoifumua Mgambo kwa magoli yake manne mwaka jana.
Bao hilo la tatu kwake na la nne kwa Simba lilifungwa katika dakika ya 52 akiunganisha krosi ya winga Haruna Chanongo kablka ya kutolewa baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Abdulhalim Humud 'Gaucho'.
Kwa ushindi huo Simba imefikisha pointi 30 na kuendelea kusalia nafasi ya nne nyuma ya Mbeya City ambayo kesho itaikabili Yanga wenye pointi 32 katika pambano jingine linalosubiriwa kwa hamu.
Oljoro inayonolewa na kocha wa zamani wa Coastal Union, Hemed Morocco ilikosa mabao mengi ya wazi katika pambano hilo na hasa kwa mashambuliaji wake Shija Mkina aliyewahi kung'ara na Simba.
Tofauti na mechi yao ya Mgambo, leo Amisi Tambwe alipewa mpira wake na mwamuzi Nathan Lyimo mara baada ya mchezo huo kuisha kwa kupiga hat trick ambayo inakuwa ya tatu, nyingine ilipigwa na Abdalla Juma wa Mtibwa Sugar.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa uwanja wa Chamazi, Ashanti United ilijikuta ikikandikwa mabao 2-0 na Mgambo JKT iliyokuwa chini ya kocha wake mpya Siame aliyempokea Mohammed Kampira.
Kwa ushindi huo Mgambo imefikisha pointi 9, lakini bado imeng'ang'ania mkiani kwa kuzidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Prisons ambayo ina michezo miwili mkononi baada ya pambano lao la kesho dhidi ya Coastal Union kuahirishwa kutokana na tatizo la uwanja wa Sokoine-Mbeya.

Sunderland yaifumua Newcastle kwao 3-0

Fabio Borini scores form the penalty
Sunderland wakijipatia bao lao la kwanza kwa mkwaju wa penati
MABAO matatu yaliyofungwa na Fabio Borini kwa mkwaju wa penati na mengine mawili ya kila kipindi yameiwezesha Sunderland kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya mahasimu wao Newcastle United.
Newcastle waliokuwa nyumbani walikumbana na kipigo hicho baada ya Borini kufungwa bao la mkwaju wa penati dakika 19 kabla ya Adam Johnson kuongeza la pili dakika nne baadaye na kuifanya Sunderland kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao hayo.
Kipindi cha pili pamoja na wenyeji kujaribu kutaka kurejesha mabao hayo, hali ilikuwa ngumu kwao kwa kufungwa bao jingine la tatu kupitia kwa Jacky Colback katika dakika ya 80.
Ushindi huo umezidi kuipaisha Sunderland iliyokuwa ikiburuza mkia hadi mwishoni mwa mwaka jana ikikwea hadi nafasi ya 12 toka ya 17 iliyokuwa ikiishikilia baada ya katikati ya wiki kupata ushindi wa 1-0.
Katika mechi nyingine ya mapema iliyochezwa sambamba na ile ya St James Park, West Ham United ikiwa uwanja wa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Swansea City, licha ya kumpoteza mshambuliaji wake nyota Andy Carroll dakika ya 59.
Mabao yote ya wenyeji yalitupiwa kambani na Kevin Nolan katika dakika ya 26 na 45.
Kwa sasa kipute cha ligi hiyo ya England inaendelea kwenye viwanja vingine ambapo MICHARAZO itaendelea kuwajuza.

Uongozi Yanga watoa ufafanuzi kuhusu Seif Magari


HIVI karibuni kumekuwa na madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu, taarifa za hujuma ndani ya timu yetu ya mpira, uongozi na baadhi ya wanachama.
Ni haki na ni kwa nia njema tu ya wanachama kuhoji mwenendo wa timu yao pale wanapoona-hairidhishi, Ni wajibu wa wanachama kuchanganua mawazo mema na mabaya. 
 
Ushindi au mwenendo mzuri wa timu unatokana na viwango vizuri, nidhamu na ushirikiano wa wahusika wote, Wachezaji, Walimu, Viongozi, Wanachama na wapenzi kwa ujumla.
 
Uongozi ulikutana na wachezaji, walimu, baadhi ya wanachama na wapenzi na kuyazungumzia na kukubaliana kuhusu mapungufu yaliyojitokeza kwa wahusika wote na kuchukua hatua ya kubadilisha technical bench yote na kutoa adhabu na onyo kali kwa baadhi ya wachezaji walionyesha utovu wa nidhamu kwa kipindi kilichopita.
 
Inasikitisha kuona kuwa baadhi ya wadau kwa kutumia vyombo vya habari wanachochea na kutengeneza uhasama ambao kwa kweli haupo ama kwa faida zao binafsi, au kwa kutumiwa na watu wa nje kutuvuruga na kuondoa amani klabuni.
 
Habari zilizoandikwa na moja ya gazeti maarufu za kusema Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa Ndugu Seif Ahmed kuwa si mwanachama halali wa YANGA, eti anahujumu timu na yupo kwa maslahi yake binafsi ni za uzushi na hazina ukweli wowote.
 
Habari hizi zimelenga kuwakatisha tamaa na kuwavunja moyo viongozi wetu ambao wapo mstari wa mbele katika kujenga YANGA. Watu hawa ni hatari sana na hawaitakii merna YANGA na wanafanya hujuma hizi kwa malengo ya kuwapandikiza viongozi vibaraka wa kuidhoofisha timu yetu na kutimiza malengo yao binafsi.
 
Uongozi ungependa kutoa tahadhari kwa wanachama kuwa hizo ni mbinu chafu ambazo zimelenga kutudhoofisha na kutusambaratisha.
 
Wachochezi hawa kwa nyakati tofauti wamekuwa pia wakutuma ujumbe wa simu wenye vitisho na matusi kwa kiongozi huyu na baadhi ya viongozi wenzake.
 
Tunatoa onyo kwa wale wote wanaotuma ujumbe wa simu wenye uchochezi na matusi, kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao mara watakapofanya hivyo tena.
 
Tunawaomba wadau wote wanamichezo na hasa wahariri wa michezo kudhibiti matumizi mabaya ya watu au vyombo vya habari yanayochangia sana kuzorotesha michezo nchini.
 
Uongozi unawaomba Wana Yanga kutulia na kutoa ushirikiano katika kupambana na njama hizi ambazo zinawe a kutudhoofisha tusipokuwa waangalifu ili tushindwe kufikia malengo yetu.
 
YANGA DAIMA MBELE NYUMA MWIKO
 
Yusuf Manji
Mwenyekiti wa Yanga
 
Credit:Young Africans Official's Club

MAJINA YA ASKARI WALIOKUFA AJALINI DODOMA HAYA HAPA

Na. Sylvester Onesmo, Jeshi la Polisi Dodoma.
ASKARI polisi watano mkoani dodoma wamefariki dunia papohapo katika ajali ya gari iliyotokea 31/01/2014 majira ya saa 5 usiku katika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro eneo la Mtumba Center, Kata ya Mtumba Tarafa ya Kikombo Manispaa ya Dodoma, ambapo gari namba  ya usajili T.770 ABT Toyota Corolla lililokuwa likiendeshwa na Askari mwenye namba H. 3783 PC DEOGRATIUS wa Wilaya ya Kongwa.
Gari hilo lilikuwa likitokea Dodoma mjini likielekea Wilayani Kongwa liligongana uso kwa uso na gari namba T.997AVW Scania Bus mali ya Kampuni ya Mohamed Trans lililokuwa likiendeshwa na JUMA s/o MOHAMED, miaka 38, Mkazi wa Mwanza, likitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma na kusababisha vifo kwa askari watano papohapo. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME amewataja Askari hao waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni:-
1.  D.9084 D/CPL. ADOLF S/O MESHACK SILLA mwenye miaka 51, Mgogo.
2.  F.6459 D/C. EVARIST s/o MOSES BUKOMBE mwenye miaka 34, Muha.
3. H.3783 PC. DEOGRATIUS s/o PATRICK MAHINYILA mwenyw miaka 29, Mgogo.
4. WP.10337 PC. JACKLINE d/o AUGUSTINE TESHA mwenye miaka 22, Mchaga.
5.  WP.10382 PC. JEMA d/o JIMMY LUVINGA mwenye miaka 20, Mhehe. 
Wote ni askari Polisi Wilaya ya Kongwa na hakuna abiria aliyeumia katika basi. 
Kamanda MISIME amesema chanzo cha ajali hiyo kulingana na uchunguzi wa awali ni mwendo kasi kutokana na uharibifu uliotokea kwa gari dogo walilokuwa wamepanda askari na jinsi lilivyoburuzwa na basi kwa umbali wa mita 56 kisha kwenda kusimama umbali wa mita 97, kwa hali hiyo umbali kutoka eneo walipogongana hadi basi liliipoenda kusimama ni mita 152. 
Dereva wa Bus alitoroka mara baada ya ajali hiyo kutokea, juhudi za kumtafuta zinaendelea. 
Miili ya marehemu imehifadhiwa chumba cha maiti Hospitali ya mkoa Dodoma.
Aidha Kamanda MISIME ametoa wito kwa madereva kila mara wawe na udereva wa tahadhari na na kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Nani kuwa bingwa wa CHAN 2014

http://www.cafonline.com/userfiles/image/amr%20el%20sadek/trophy1234.jpg
BINGWA mpya wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2014 anatarajiwa kufahamika leo wakati Libya itakapopepetana na Ghana katika mchezo wa fainali utakaochezwa usiku, ukitanguliwa na pambano la kusaka mshindi wa tatu kati ya Nigeria dhidi ya Zimbabwe.
Ghana na Libya zinakutana katika pambano hilo la fainali baada ya kufuzu kwa mikwaju ya penati dhidi ya wapinzani wao hao, Ghana ikiishinda Nigeria mikwaju 4-1 na Libya ikiiacha solemba Zimbabwe kwa penati 5-4.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu za nchi hizo kukutana katika mchezo wa fainali tangu mwaka 1982 na wengi wamekuwa wakitabiria Ghana kunyakua taji hilo ambalo lilikuwa likishikiliwa na Tunisia iliyotwaa mara ya mwisho mwaka juzi.
Hata hivyo timu hizo zilishakutana katika michuano hiyo ya CHAN zikiwa kundi moja na matokeo yalikuwa sare ya 1-1 na hivyo kuwa vigumu kutabiri timu gani itakayoibuka na ushindi.
Kocha wa Ghana, James Kwasi Appiah, amenukuliwa akisema amewaandaa vijana wake kupata ushindi na kutwaa taji hilo baada ya kushindwa kufanya hivyo mwaka wa kwanza wa michuano hiyo walipofungwa na DR Congo.
Hata hivyo alisema hofu yake ni hali ya hewa iliyokuwa Cape Town akiamini inaweza kuwaathiri kwa vile mechi zao zote walizicheza katika mji wa Bloemfontain.
Ghana ni kati ya timu tatu ambazo zimeshiriki fainali za michuano hiyo mfululizo tangu ilipoanzishwa mwaka 2008, ikiwa sambamba na DR Congo waliotwaa ubingwa wa kwanza mwaka 2009 na Zimbabwe.
Libya inayonolewa na kocha kutoa Hispania inataka kuweka rekodi ya kunyakua taji hilo baada ya kushinda mechi zake mbili za Robo fainali na Nusu Fainali kwa mikwaju ya penati ikiipania kuizima Ghana katika muda wa kawaida.
Licha ya mbio za kuwania ubingwa pia leo kutakuwa na hitimisho ya kujua nani ni mfungaji bora wa michuano hiyo ambapo Mnigeria, Ejike Uzoenyi mwenye mabao manne sawa na Bernard Parker wa Afrika Kusini ana nafasi ya kutwaa kiatu cha dhahabu kwa vile mwenzake timu yake imeshatolewa.
Hata hivyo Mnigeria huyo anakabiliwa na upinzani toka kwa Mlibya, Abdulsalam Faraj Omar mwenye mabao matatu ambapo kama akifunga katika fainali dhidi ya Ghana anaweza kuwapiku wenzake.
Abdulsalama hayupo pekee yake katika orodha ya wenye mabao matatu kwani wamo pia Mnigeria Rabiu Ali na Mganda Yunus Sentamu ambaye tayari timu yake ilishafungashwa virago hatua ya makundi.

Zenji yachafuka! Wafaransa wawili wauwawa na kutupwa kisimani

Kisima kilichopo eneo la Matamwe Mkoa wa Kaskazini Unguja ambamo raia wawili wa Ufaransa wanasadikiwa kuuawa na kisha kufukiwa kwa zege.
Kisima kilichopo eneo la Matamwe Mkoa wa Kaskazini Unguja ambamo raia wawili wa Ufaransa wanasadikiwa kuuawa na kisha kufukiwa kwa zege.

RAIA wawili wa Ufaransa wameuawa na kutumbukizwa katika kisima cha maji kilichomo ndani ya uwanja wa nyumba yao na watu wasiojulikana katika eneo la Shehia ya Matemwe Kaskazini, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo zinaeleza kuwa watu hao mtu na mkewe waliuawa hivi karibuni.
DCI Ilembo aliliambia gazeti hili jana kuwa tayari vikosi vya Zimamoto na Uokozi (KZU) na Polisi vimeanza kufukua kisima hicho na kwamba katika hatua ya awali wamefanikiwa kukuta mfupa wa mguu wa kushoto wa mmoja wa watu hao.
Aliwataja wazungu hao kutoka Ufaransa kuwa ni Francois Cherer Robert Daniel na Brigette Mary ambao walikuwa wakiishi kama mtu na mkewe wakiwa na mbwa wao anayeitwa Allan ambaye pia amekutwa amekufa ndani ya nyumba hiyo.
Alisema uchunguzi wa awali umeonesha kuwa Wafaransa hao waliingia nchini kihalali mwaka 2013, na kununua nyumba kwenye ufukwe wa mwambao wa Bahari ya Hindi eneo la Matemwe na kuanza kuishi eneo hilo.
DCI Ilembo alisema polisi tayari wanawashikilia watu watatu wakazi wa Shangani katika Mjimkongwe wa Zanzibar na mmoja anayeishi katika eneo la Kilimani katika wilaya ya Mjini Unguja.
“Kuna askari wanaendelea na kazi ya kuzamia ndani ya kisima kilichomo ndani ya uzio wa nyumba hiyo, kazi bado ni kubwa na siyo ya siku moja,” alisema DCI Ilembo.
Gazeti hili limefanikiwa kufika katika eneo la nyumba hiyo na kukuta askari Polisi wanne wakilinda nyumba hiyo huku harufu kali ikitoka katika shimo la kisima. Hata hivyo, mlinzi wa nyumba hiyo ametoweka katika mazingira ya kutatanisha na simu yake kila ikipigwa imezimwa.
Mlinzi mpya aitwaye Omar Juma ambaye amekutwa akilinda nyumba hiyo baada ya kuajiriwa na mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa amesema alikabidhiwa kazi ya ulinzi kuanzia Januari mwaka huu na hakumkuta mtu yeyote akiishi hapo.
“Kazi yangu ni kazi za ulinzi, nimeletwa hapa na mwajiri, sijui lolote, mwajiri wangu ndiye anayejua kama kulikuwa na watu kabla au la, sina la kusema na sijui nianzie wapi,” alisema Omar.
Sheha wa Matemwe Kusini
Sheha wa Shehia ya Matemwe Kusini, Denge Khamis Silima aliyelizungumzia suala hilo kwa niaba ya Sheha wa Matemwe Kaskazini, aliliambia gazeti hili kuwa taarifa za kutoweka kwa wazungu hao zilianza kuenea kuanzia Desemba 27 mwaka jana.

Denge alisema alianza kupata taarifa za awali kutoka kwa mjumbe mmoja wa Shehia aitwaye Mkadam Tabu Vuia kwamba mlango wa nyumba ya wazungu hao ulikuwa wazi kwa muda mrefu na harufu kali ikitoka na inzi wakubwa wametanda katika eneo hilo.
“Nimeshiriki katika kazi ya kuchimbua kisima, askari wametoa mfupa wa mguu na unyayo unaoaminika kuwa ni wa mtu, ingawa tuliikuta nyumba ikiwa haikuvunjwa milango,” alisema.
Alisema waliingia ndani ya nyumba hiyo kupitia dirishani wakakuta mbwa wa wazungu hao, Allan naye amekufa na kwamba kwa sasa wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa polisi.
Sheha huyo wa Shehia ya Matemwe Kusini alisema mazingira waliyoyakuta ndani ya nyumba hiyo yameonyesha kuwa haikuhamwa kwa muda mrefu na kama kwamba wanatarajia kurejea wakati wowote.
Alisema baada ya kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya, askari polisi walifika katika eneo hilo na kazi ya kuchimba kisima ilianza baada ya kubaini harufu kali ilikuwa inatoka kisimani.
Hata hivyo, kazi ya kuchimba kisima ilikuwa ngumu baada ya kukutana na zege lililojazwa na walipoendelea kuliondoa zege hilo walipata mguu mmoja wa binadamu.
Denge alisema zoezi la uchimbaji wa kisima hicho lilikwama juzi kutokana na ugumu wa zege na hivyo kazi hiyo kuahirishwa na kuendelea jana baada ya kupatikana mashine ya kuchimbua vitu vigumu na vifaa ya kuongeza hewa ya oksijeni.
“Bado hatujafanikiwa kubomoa zege na kuingia kina kirefu kujua kama ipo mifupa zaidi au la, tunawasubiri polisi na askari wa zimamoto waje na vifaa,” alisema Denge.
Agosti 7, mwaka jana raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) walimwagiwa tindikali mjini Zanzibar. Tukio hilo lilitokea saa 1:15 usiku Mtaa wa Shangani eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar, karibu na ofisi za Serikali ikiwamo Wizara ya Sheria na Wizara ya Katiba na Maendeleo ya Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto.
Wasichana hao walifika Zanzibar kwa mwaliko wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Arts in Tanzani.
CHANZO; Mwananchi

WALIOINGIA NA KUTOKA USAJILI WA ENGLAND

USIKU wa jana ndiyo ilikuwa mwisho wa usajili wa dirisha dogo barani Ulaya ambapo klabu zilizokuwa zikipigana vikumbo vilihitimisha harakati zao. Hapa chini ni usajili wa klabu za Ligi Kuu ya England baada ya pazia hilo kufungwa rasmi saa 6 usiku wa jana.
 
ARSENAL:

 Imesajili mchezaji mmoja tu, Kim Kallstrom kwa mkopo kutoka Spartak Moscow, wakati walioondoka ni Chuba Akpom (Brentford, mkopo), Anthony Jeffrey (Wycombe, mkopo), Benik Afobe (Sheffield Wednesday, mkopo), Nico Yennaris (Brentford) Emmanuel Frimpong (Barnsley), Daniel Boateng (Hibernian, mkopo), Park Chu-Young (Watford, mkopo).

ASTON VILLA: 
Waliosajiliwa ni Grant Holt (Wigan, mkopo) na Ryan Bertrand (Chelsea, mkopo), wakati walioondoka ni Stephen Ireland (Stoke), Michael Drennen (Carlisle, mkopo) na Jordan Graham (Bradford, mkopo).

CARDIFF: 

Zaha and Fabio
Waliosajiliwa ni Magnus Wolff Eikrem (Heerenveen, Pauni Milioni 2), Mats Moller Daehli (Molde), Jo Inge Berget (Molde), Kenwyne Jones (Stoke, kubadilishana), Fabio da Silva (Manchester United), Wilfried Zaha (Manchester United, mkopo). Walioondoka ni Rudy Gestede (Blackburn), Filip Kiss (Ross County, mkopo), Nicky Maynard (Wigan, mkopo), John Brayford (Sheffield Utd, mkopo), Peter Odemwingie (Stoke, kubadilishana), Simon Moore (Bristol City, mkopo), Craig Conway (Blackburn Rovers, mkopo) na Andreas Cornelius (FC Copenhagen).

CHELSEA: 
 Waliosajiliwa ni Bertrand Traore (Association Jeunes Espoirs De Bobo-Dioulasso), Nemanja Matic (Benfica, Pauni Milioni 21), Mohamed Salah (Basel Pauni Milioni 11) na Kurt Zouma (Saint Etienne, Pauni Milioni 12.5), wakati walioondoka ni Bertrand Traore (Vitesse Arnhem, mkopo), Kevin de Bruyne (Wolfsburg, Pauni Milioni 17), Ryan Bertrand (Aston Villa, mkopo) Josh McEachran (Wigan, mkopo), Juan Mata (Manchester United, Pauni Milioni 37.1) Michael Essien (AC Milan), Sam Walker (Colchester, mkopo), Nathaniel Chalobah (MIddlesbrough, mkopo), Kenneth Omeruo (Middlesbrough, mkopo), Patrick Bamford (Derby, mkopo) na Gael Kakuta (Lazio, mkopo).

CRYSTAL PALACE: 
Waliosajiliwa ni Jason Puncheon (Southampton), Scott Dann (Blackburn), Wayne Hennessey (Wolves, Pauni Milioni 3), Tom Ince (Blackpool, mkopo) na Joe Ledley (Celtic), wakati walioondoka ni Jason Banton (Plymouth, huru), Jimmy Kebe (Leeds, mkopo), Kwesi Appiah (Notts County, mkopo), Matt Parsons (Plymouth), Jack Hunt (Barnsley, mkopo) na Jose Campana (Nuremburg, mkopo).

EVERTON:
 Waliosajiliwa ni Aiden McGeady (Spartak Moscow), Lacina Traore (Monaco, mkopo) na Jindrich Stanek (Sparta Prague) wakati walioondoka ni Nikica Jelavic (Hull), Matthew Kennedy (Tranmere, mkopo), Shane Duffy (Yeovil, mkopo), Hallam Hope (Northampton, mkopo), Chris Long (MK Dons, mkopo), Matthew Pennington (Tranmere, mkopo) na Johnny Heitinga (Fulham, huru).

FULHAM: 
 
Waliosajiliwa ni Clint Dempsey (Seattle Sounders, mkopo), William Kvist (mkopo, Stuttgart), Lewis Holtby (Tottenham, mkopo), Konstantinos Mitroglou (Olympiacos, Pauni Milioni 12.4) na Johnny Heitinga (Everton, huru), wakati walioondoka ni Bryan Ruiz (PSV, mkopo), Stephen Arthurworrey (Tranmere, mkopo), Marcus Bettinelli (Accrington, mkopo), Jack Grimmer (Port Vale, mkopo), Aaron Hughes (QPR, undisclosed), Dimitar Berbatov (Monaco, mkopo).

HULL: 
Waliosajiliwa ni Nikica Jelavic (Everton), Elliott Kebbie (Atletico Madrid, mkopo), Shane Long (West Brom, Pauni Milioni 6), wakati walioondoka ni Tom Cairney (Blackburn, Pauni 500,000), Conor Townsend (Carlisle, mkopo), Eldin Jakupovic (Leyton Orient, mkopo), Cameron Stewart (Leeds, mkopo), Nick Proschwitz (Barnsley, mkopo), Gedo (Al Ahly) na Aaron Mclean (Bradford).

LIVERPOOL:
 Hakuna aliyesajiliwa, wakati walioondoka ni Adam Morgan (Yeovil, huru), Tiago Ilori (Granada, mkopo), Craig Roddan (Accrington Stanley, mkopo), Ryan McLaughlin (Barnsley, mkopo) na Michael Ngoo (Walsall, mkopo).

MANCHESTER CITY: 
Hakuna aliyesajiliwa wakati walioondoka ni John Guidetti (Stoke, mkopo), Albert Rusnak (Birmingham mkopo), Emyr Huws (Birmingham, mkopo) na Abdisalam Ibrahim (ametemwa).
 
Juan Mata kulia akisaini Mkataba wa Manchester United pembeni ya kocha David Moyes kushoto. Huu ndio usajili uliogharimu fedha nyingi zaidi dirisha hili dogo.

MANCHESTER UNITED; 
Aliyesajiliwa ni Juan Mata pekee kutoka Chelsea kwa Pauni Milioni 37.1), wakati walioondoka ni Jack Barmby (Hartlepool, mkopo), Anderson (Fiorentina), Fabio da Silva (Manchester United), Wilfried Zaha (Cardiff, mkopo), Fabio da Silva (Cardiff), Tom Lawrence (Yeovil Town, mkopo), Tyler Blackett (Birmingham City, mkopo), Sam Byrne (Carlisle United, mkopo), Charni Ekangamene (Carlisle United, mkopo), Tom Thorpe (Birmingham City, mkopo), Federico Macheda (Birmingham City, mkopo), Will Keane (QPR, mkopo) na San Johnstone (Doncaster Rovers, mkopo).

NEWCASTLE;
 Aliyesajiliwa ni Luuk de Jong (Borussia Monchengladbach, mkopo) pekee, wakati walioondoka ni Yohan Cabaye (Paris-Saint Germain, Pauni Milioni 23), Jonas Gutierrez (Norwich, mkopo), Curtis Good (Dundee United, mkopo).

NORWICH;
 Imemsajili Jonas Gutierrez pekee kwa mkopo kutoka Newcastle, wakati walioondoka ni Daniel Ayala (Middlesbrough, Pauni 350,000) na Jamar Loza (Leyton Orient, mkopo).

SOUTHAMPTON;
 Hakuna aliyesajiliwa wakati walioondoka ni Lee Barnard (Southend, mkopo), Danny Fox (Nottingham Forest, mkopo), Billy Sharp (Doncaster, mkopo), Dani Osvaldo (Juventus, mkopo), Jason Puncheon (Crystal Palace).

STOKE; 
Waliosajiliwa ni John Guidetti (Man City, mkopo), Stephen Ireland (Aston Villa), Juan Agudelo (New England Revolution), wakati walioondoka ni Brek Shea (Barnsley, mkopo), Jamie Ness (Leyton Orient, mkopo) na Juan Agudelo (FC Utrecht, mkopo).

SUNDERLAND; 
Waliosajiliwa ni Marcos Alonso (Fiorentina, mkopo), Santiago Vergini (Estudiantes, mkopo), Oscar Ustari (Almeria), Ignacio Scocco (Internacional, Pauni Milioni 3), Liam Bridcutt (Brighton, Pauni Milioni 2.5), wakati walioondoka ni Mikael Mandron (Fleetwood, mkopo), Ji Dong-won (Augsburg), Billy Knot (Port Vale, mkopo), Cabral (Genoa, mkopo), Modibo Diakite (Fiorentina, mkopo), David Moberg Karlsson (Kilmarnock, mkopo), David Vaughan (Nottingham Forest, mkopo) na Duncan Watmore (Hibernian, mkopo).

SWANSEA;
New arrival: Swansea City have signed Bolton striker David Ngog until the end of the season for an undisclosed fee
 Waliosajiliwa ni David Ngog (Bolton), Raheem Hanley (Blackburn), Jay Fulton (Falkirk) na Marvin Emnes (Middlesbrough, mkopo), wakati walioondoka ni Alan Tate (Aberdeen, mkopo), Daniel Alfei (Portsmouth, mkopo), Rory Donnelly (Coventry City, mkopo)

TOTTENHAM; 
Hakuna aliyesajiliwa wakati walioondoka ni Jermain Defoe (Toronto, Pauni Milioni 6), Simon Dawkins (Derby), Shaquile Coulthirst (Leyton Orient, mkopo), Jon Obika (Brighton, mkopo), Ryan Fredericks (Millwall, mkopo), Adam Smith (Bournemouth), Lewis Holtby (Fulham, mkopo).

WEST BROMWICH ALBION; 
Aliyesajiliwa ni Thievy Bifouma pekee kutoka Espanyol kwa mkopo,wakati walioondoka Lee Camp (Bournemouth), Shane Long (Hull, Pauni Milioni 6), George Thorne (Derby, mkopo).

WEST HAM: 
Waliosajiliwa ni Roger Johnson (Wolves, mkopo), Antonio Nocerino (Milan), Marco Borrielo (Roma, mkopo) Abdul Razak (Anzhi Makhachkala), Pablo Armero (Napoli, mkopo), wakati waliosajiliwa ni Blair Turgott (Rotherham, mkopo), Jordan Spence (MK Dons, mkopo), Paul McCallum (Hearts, mkopo) na Modibo Maiga (QPR, mkopo).

Jennifer Mgendi ajipanga kutoa mpya

 
MUIMBAJI nyota wa muziki wa Injili, Jennifer Mgendi yupo katika maandalizi ya kufyatua filamu mpya, fani anayoifanya kwa sasa sambamba na hiyo ya kumuimbia Mungu.
Akizungumza na MICHARAZO, Jennifer, alisema ameshaandaa miswada mitatu tofauti ya filamu, lakini hajajua ataanza kuirekodi ipi ili kuwapa burudani mashabiki wake.
Jennifer aliyewahi kutamba na filamu kadhaa ikiwamo Joto la Roho, Teke la Mama Chai ya Moto, alisema kazi ya kurekodi filamu hiyo mpya itafanywa hivi karibuni kwa kushirikisha wasanii nyota wa Bongo Movie na yeye akiwamo ndani ya kazi hiyo.
"Nipo katika maandalizi ya kuanza kurekodi filamu mpya, lakini sijajua nitaanza na ipi kwa sababu mikononi ninazo kazi tatu tofauti," alisema Jennifer aliyejipatia umaarufu mkubwa kupitia nyimbo kadhaa za Injili.
Baadhi ya nyimbo zilizompaisha mwanadada huyo ni pamoja na Mchimba Kisima, Nalia, Asante Yesu na nyingine.

Owino, Mkude kuwakabili maafande taifa


WEKUNDU wa Msimbazi, Simba leo inatarajiwa kushuka dimbani kuvaana na maafande wa Oljoro JKT, huku kocha wake, Zdravko Logarusic 'Loga', akisema huenda akamtumia beki wake wa kati, Joseph Owino aliyekuwa amekwaruzana naye kwenye mazoezi ya timu hiyo wiki mbili zilizopita.

Loga alikwaruzana na nyota huyo wa Kenya kwenye mazoezi ya timu hatua iliyopelekea kumuweka benchi kwenye mchezo uliopita dhidi ya Rhino Rangers.

Hata hivyo Kocha huyo alimaliza matatizo na mchezaji huyo na amemjumuisha kwenye kikosi kilichokuwa kikijiandaa na mchezo wa leo dhidi ya JKT Oljoro, utakaochezwa uwanja wa Taifa huku kiungo Jonas Mkude aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi nyekundu akiwa huru naye kushuka dimbani.

Loga alisema kuwa hakuna tatizo ndani ya kikosi chake na kila mchezaji ana nafasi ya kuwemo kwenye kikosi cha leo.

Alisema kuwa Owino anaweza akacheza lakini ataangalia leo asubuhi wachezaji watakuwa kwenye hali gani ambapo Simba inahitaji ushindi ili kuweza kuwafukuzia wapinzani wao waliopo nafasi tatu za juu.

Simba ipo nafasi ya nne na pointi 27, nyuma ya Mbeya City yenye pointi 31 ambayo kesho itapapatena na Yanga yenye pointi 32 katika pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa.

Vinara wa ligi hiyo Azam wenye pointi 33 wikiendi hii hatakuwa na mchezo wowote, ila leo kuna mechi nyingine kali kati ya Ashanti United dhidi ya Mgambo JKT ya Tanga.

Simanzi! Askari watano wafa ajali Dodoma


TAARIFA zilizotufikia asubuhi ya leo zinasema kuwa, askari watano wamefariki papo hapo baada ya basi la Mohamed Trans, kugongana uso kwa uso na gari ndogo aina ya Toyota Corola katika ajali.
Akizungumza na Radio One, Kamanda wa polisi Mkoani Dodoma, David Misime, amesema kuwa ajali hiyo imetokea majira ya saa 9 usiku kuamkia leo katika kijiji cha Namtumba Mkoani Dodoma na abiria waliokuwemo kwenye basi hilo hakuna aliyejeruhiwa.
"Hakuna aliyejeruhiwa kutoka kwenye basi, lakini dereva aliyekuwa anaendesha abiria hao anafahamika kwa jina la Juma Mohamed, amekimbia mpaka sasa haijafahamika yuko wapi, ameongeza kuwa gari ndogo aina ya Toyota Corola imeharibika vibaya na baadhi ya miili ya askari hao imeharibika. " Tumeipeleka miili hiyo hospital kwa ajili ya kuihifahi huku tukisubiri mipango ya mazishi," amesema David.