STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, October 15, 2013

Neymar aiongoza Brazil kuizima Zambia

Prediksi Skor Brasil vs Zambia 15 Oktober 2013
MABINGWA wa zamani wa Afrika, Zambia leo imekiona cha moto baada ya kutandikwa mabao 2-0 na wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia za mwakani Brazil katika pambano la kirafiki la kimataifa lililochezwa Beijing China.
Mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa mtokea benchi Oscar katika dakika ya 59 akimalizia pasi murua ya Paulinho na Dede kuongeza jingine dakika ya 66 kwa pasi ya nyota mpya wa Barcelona, Neymar yaliizamisha Zambia ambayo imeondokewa na kocha wake  Herve Renard aliyeteuliwa kuinoa timu ya darajha la kwanza ya nyumbani Ufaransa.
Zambia ilicheza ikiwa na kocha wake mpya, Mfaransa mwingine Patrice Beaumelle.

Katika mechi nyingine; Korea ya kaskazini imeitungua Mali mabao 3-1, huku Japan ikilala 1-0 kwa Belarus, Ufilipino ikiitafuna Pakistan mabao 3-1.


Misri yatunguliwa bao la sita, Ghana yanusa fainali za Kombe la Dunia

Asamoah Gyan and  Wael Gomaa

MAFARAO wa Misri imeendelea kufa mjini Kumasi baada ya muda mchache uliopita wakitunguliwa bao la sita na Ghana katika pambano lao la awali la hatua ya mwisho ya mchujo wa Fainali za Kombe la Dunia kwa Bara la Afrika.
Pamoja na kufanya mabadiliko ya kuwaingiza akina Tshabalala, Misri wamepotea kabisa kwa wewnyeji ambao wanacheza watakvyo wakiwa na uhakika kwa asilimia kubwa kutinga fainali hizo za WC za 2014 zitakazofanyika Brazili.
Bao hilo la sita limetupiwa kimiani na Christian Atsu dakika ya 89 na kuonyesha dhahiri Ghana imeshaingiza mguu mmoja katika fainali hizo licha ya kwamba pambano lao la marudiano baina yao litafanyika Nov. 19.
Game ishaisha na Misri kuwa na kibarua cha kushinda nyumbani kwao mechi ya marudiano kwa mabao 5-0?! Tusubiri tuone!

Siri yafichuka viungo bandia vya binadamu vilivyonaswa Kenya

HATIMAYE mmiliki wa kasha la mizigo lililonaswa katika Bandari ya Mombasa likiwa na sanamu za vibwengo vya kutisha, amejulikana.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, kampuni ya 'Market Masters' wanaomiliki maduka ya Village Market jijini Nairobi wamekiri kuagiza shehena hiyo kwa sherehe zao za kila mwaka. 
Wakati huo huo, mwanasiasa Omingo Magara amekanusha kuagiza shehena hiyo na akaitaka halmashauri ya ushuru nchini KRA kumuomba msamaha mara moja.
Aidha katika habari nyingine zilizonaswa zinasema kuwa huenda pia sanamu hizo nyingine zingekuja nchini Tanzania.

 Xdeejayz

Jahazi la Misri lazidi kuzama, Gyan atupia bao jingine

Asamoah Gyan and  Wael Gomaa
Gyan akichuana na Wael Gomma

JAHAZI ya mafarao wa Misri linazidi kuzama baada ya muda mfupi uliopita Asamoah Gyan kutupia bao jingine la nne kwa Ghana wakati mchezo ukiingia dakika ya 60 hivi sasa.
Gyan katupia bao hilo la pili kwake katika mchezo huo unaochezwa mjini Kumasi katika dakika ya 54.
Hivi punde tena Ghana imepata bao la tano kupitia Sulley Muntari katika dakika ya 73kwa mkwaju wa penati, kuonyesha imepania kuidhiri Misri ambayo imekuwa ikiinyanyasa kila inapokutana nayo ambapo katika mechi 18 za awali za kukutana kwa timu hizo Ghana imeshinda mara nne na kufungwa 9 huku michezo mitano ikiisha kwa sare.

RAIS JAKAYA KIKWETE AKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WENYE WABUNGE LEO


Rais akiwa na viongozi wa vyama vya upinzani  leo ambaye alikutana nao

Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Tundu Lisu  nyuma yake mwenyekiti wa NCCR James Mbatia

Rais akiwa viongozi ikulu leo

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MKUTANO kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni umemalizika Ikulu, Dar Es Salaam, muda mfupi uliopita leo, Jumanne, Oktoba 15, 2013 kwa pande hizo mbili kukubaliana kama ifuatavyo:

Moja , kwamba  vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe mapendekezo yao haraka Serikalini ili itafute namna ya kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya Sheria hiyo.

Pili, kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato huo kwa maslahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa. Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.

Viongozi wa vyama vyama vya siasa waliokutana na Mheshimiwa Rais Kikwete ni Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF; Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA na Mheshimiwa James Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Mheshimiwa Philip Mangula, Mheshimiwa Isaack Cheyo ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa Chama cha UDP Mheshimiwa John Cheyo na Mheshimiwa Nancy Mrikaria ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa TLP Mheshimiwa Augustine Mrema. Waheshimiwa John Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.

Wengine ambao wameambatana na wenyeviti wao ni Mheshimiwa H. Mnyaa na Bwana Julius Mtatiro wa CUF, Waheshimiwa Tundu Lissu na John Mnyika wa CHADEMA na Bwana Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

15 Oktoba, 2013

Mhandisi Bashir Mrindoko azidi 'kuula'



                             TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mhandisi (Eng.) Bashir J. Mrindoko kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kwa kumpandisha cheo kutoka nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Aidha, Rais Kikwete amemhamisha Mhandisi Mbogo Paulo Futakamba, Naibu KatibuMkuu, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwenda Wizara ya Maji kujaza nafasi iliyoachwa na Mhandisi  Bashir Mrindoko.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam leo, Jumanne, Oktoba 15, 2013, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa vile vile Rais Kikwete amemteua Mhandisi Raphael Leyan Daluti kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuchukua nafasi ya Mhandisi Futakamba.

Kabla ya uteuzi  wake, Mhandisi Daluti alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Umwagiliaji na Huduma za Ufundi katika Wizara hiyo ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Balozi Sefue amesema katika taarifa yake kuwa uteuzi na uhamisho huo umeanza Oktoba 13, mwaka huu, 2013.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

15 Oktoba, 2013

Ghana yaikoboa Misri 3-1 ni mapumziko kwa sasa

StarAfrica
Ghana-Black Stars

MABINGWA wa zamani wa Afrika Ghana, ikiwa nyumbani mpaka sasa wakati wa mapumziko inaoongoza kwa mabao 3-1 dhidi na Mafarao wa Misri katika pambano la awali la hatua ya mwisho ya mtoano kuwania Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.
Mkali Asamoah Gyan alianza kuwashtua mabingwa wa kihistoria wa Afrika, Misri kwa bao la dakika nne kabla ya beki wa Misri Wael Gomma kujifunga bao katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na Michael Essien na kuipa Ghana uongozi wa mabao 2-0 kwenye dakika ya 22.
Hata hivyo mkongwe Mohammed Aboutrika aliipunguza machungu kwa kufunga bao la Misri kwa mkwaju wa penati dakika ya 41 kabla ya Abdulmajed Waris kufunga bao la tatu dakika moja kabla ya mapumziko.
Tutaendelea kuwaletea matokeo juu ya mpambano huo,. licha ya kufahamu wapo wengine wanaoufuatilia 'live' kupitia kwenye runinga.

Ashanti United kuendeleza maajabu kesho Chamazi?

* Inaikaribisha Prisons, TFF takabidhi kitanda cha Upasuaji

Kikosi cha Ashanti United
Na Boniface Wambura

LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Oktoba 16 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Ashanti United na Tanzania Prisons itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Nayo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea kesho (Oktoba 16 mwaka huu) kwa mechi moja ya kundi A ambapo Polisi Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa Tessema kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekabidhi kitanda cha upasuaji kwa Hospitali ya Rufani ya Manispaa ya Temeke, ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa jamii.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo (Oktoba 15 mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF ambapo Hospitali ya Temeke iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya hospitali hiyo James Syaga, Mganga Mkuu Dk. Amaani Malima na Matroni wa hospitali hiyo Deodata Msoma. Akikabidhi kitanda hicho chenye thamani ya sh. milioni 6.8, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema amefurahi kuwa ahadi ya kukabidhi msaada huo wa Hospitali ya Temeke umetimia licha ya kuchukua muda mrefu kutokana na ukweli kuwa fedha za kununulia kitanda hicho zinatokana na mchezo wa Ngao ya Jamii wa mwaka jana kati ya Simba na Azam FC. Alisema uamuzi wa kuiteua Hospitali ya Temeke ulitokana na ukweli kuwa pamoja na kwamba ofisi za TFF ziko wilayani Ilala, shughuli nyingi kubwa za Shirikisho linafanyika kwenye Manispaa ya Temeke na hivyo hospitali hiyo hufanya kazi kubwa ya kuhudumia watu mbalimbali wanaopata matatizo wakati wa michezo ya mpira wa miguu. Naye Mganga Mkuu wa Hospitali, Dk. Malima aliishukuru TFF kwa kutimiza ahadi yao na kwamba msaada huo umekuja wakati muafaka kwa kuwa wana vyumba vitatu vya upasuaji, lakini ni viwili tu vilivyo na vitanda kwa hiyo kitanda hicho kitakamilisha chumba hicho kianze kufanya kazi. Alisema Hospitali yake sio tu inahudumia wagonjwa kutoka wilayani Temeke, bali kutoka hata Mkoa wa Mtwara na sehemu nyingine zinazozunguka wilaya hiyo. Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali, James Syaga, ambaye alisema anawakilisha watu wanaohudumiwa na Hospitali ya Temeke, alishukuru kwa msaada huo na kuiomba TFF kuendelea kuangalia uwezekano wa kusaidia hospitali hiyo.

Kamati ya Rufaa ya Maadili yakata mzizi wa fitina

* Yamtupa rupango mgombea miaka 20
* Shafii Dauda, Kidau wapeta
* Mchakato wa  kampeni sasa ruksa
Shafii Dauda aliyepeta, japo amelimwa saini ya Sh Mil. 1

Na Boniface Wambura
KAMATI ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imewaadhibu walalamikiwa watano kati ya saba baada ya kufanya mapitio (revision) kwa uamuzi wa Kamati ya Maadili kutokana na maombi ya Sekretarieti, huku Richard Julius Rukambura akifungiwa miaka 20 kujihusisha na mpira wa miguu.
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha maombi ya mapitio kwa Kamati ya Rufani ya Maadili ili kupata mwongozo kwa vile kulikuwapo mkanganyiko kwenye uamuzi wa Kamati ya Maadili, hivyo kuiwia vigumu kwake kuutekeleza.
Uamuzi huo wa mapitio umesomwa leo jioni (Oktoba 15 mwaka huu) mbele ya waandishi wa habari na wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Victoria Makani.
Rukambura amefungiwa miaka 20 baada ya kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama za kawaida kinyume na Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF na kifungu cha 73(3)(b) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013. Adhabu yake itamalizika Oktoba 15, 2033.
Kabla ya kutoa adhabu hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Rukambura ni mwanafamilia wa TFF kwa vile aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Pamba ya Mwanza, na fomu zake za kuomba uongozi TFF ziliidhinishwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga. Vilevile ni ‘Leadership Aspirant’ kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.
Pia imesema kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kusajili Katiba ya TFF inayokataza masuala ya mpira wa miguu kwenda katika mahakama za kawaida, na kutaja vyombo vya haki vitakavyoshughulikia masuala hayo (judicial organs), Kamati ya Maadili ilikosea kutomtia hatiani mlalamikiwa kwa kuegemea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Shaffih Dauda, Kamati imebaini kuwa mwanafamilia wa TFF kwani ni Mwenyekiti wa Bombom FC, fomu yake ya kuomba uongozi ilipitishwa na klabu ya Simba na pia ameshakuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA), hivyo yeye ni ‘Leadership Aspirant’ kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.
Hivyo Dauda amepatikana na kosa la kimaadili kwa kutotekeleza maagizo rasmi ya TFF ya kutosambaza barua iliyotoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Kamati ya Rufani ya Maadili imempa onyo kali na faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo akishindwa kufanya hivyo atafungiwa mwaka mmoja. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 6(1)(a),(c) na (h) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
Akilipa faini ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea nafasi ya uongozi aliyoomba.
Nazarius Kilungeja amepatikana na kosa la kimaadili kwa mujibu wa kifungu cha 73(8)(a) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwani akijua kuwa ana adhabu ya kinidhamu ya kufungia miaka mitano na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) iliyoanza 2009 alichukua fomu kuomba uongozi TFF.
Hivyo, amefungiwa miaka mitatu, adhabu ambayo itakwenda sambamba na ile ya RUREFA ambapo kifungo chake sasa kitamalizika Oktoba 15, 2016.
Sekretarieti ya TFF imepewa onyo kali kwa kupokea fomu yake ya kugombea na malipo wakati akiwa amefungiwa. Onyo hilo pia limetolewa kwa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Rukwa kwa kuidhinisha fomu yake ya kugombea.
Naye Wilfred Kidao Mzigama ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF amepatikana na kosa la kimaadili kwa kuwa na nyaraka la Kamati ya Utendaji bila kibali na kukiuka taratibu za kuwasilisha malalamiko kwa mujibu wa Ibara ya 12(2) na Ibara ya 50(1) na (5) ya Katiba ya TFF.
Amepigwa faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo akishindwa atafungiwa mwaka mmoja. Akitekeleza adhabu hiyo ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea uongozi kwa nafasi aliyoomba.
Vilevile Kamati hiyo imetoa onyo kali kwa Sekretarieti ya TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa kushindwa kudhibiti nyaraka muhimu za vyombo vyao.
Pia Kamati ya Rufani ya Maadili imempata na kosa la kimaadili Kamwanga Tambwe kwa mujibu wa kifungu cha 73(8) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wakati ana adhabu ya kinidhamu inayomalizika 2014.
Hivyo, amepewa adhabu ya kufungiwa miaka mitatu ambayo itakwenda sambamba na ile ya kinidhamu na kumalizika Oktoba 15, 2016. Pia Sekretarieti ya TFF, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Ruvuma wamepewa onyo kali kwa kupokea na kuidhinisha fomu zake za kugombea uongozi wakati akitumikia adhabu ya kufungiwa.
Kamati ya Rufani ya Maadili imewakuta kutokuwa na hatia ya makosa ya maadili kama ilivyobaini Kamati ya Maadili walalamikiwa Riziki Juma Majala na Omar Isack Abdulkadir, hivyo wana haki ya kugombea uongozi kwa kufuata Katiba na Kanuni za TFF.
Kwa mujibu wa kifungu cha 74(4) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Maadili hauna fursa ya rufani wala marekebisho kutoka chombo kingine chochote isipokuwa FIFA na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Golden Bush yaifyatua Pugu Veterani 1-0

Golden Bush Veterani

ILE timu ya Veterans isiyofungika hapa Dar es Salaam na mikoa ya jirani ilitoa kipigo cha goli dhidi ya wanzetu Pugu Veterans. Goli liliwekwa wavuni Said Swedi baada ya kuna safi kabisa iliyopigwa na Shomari Pengo. Goli hili lilipatikana kipindi cha kwanza mara baada mashambulizi ya haraka haraka yakiongozwa na beki za kupanda na kushuka zikiongozwa na Shadrack Nsajigwa, Faraj huku kiungo kikikamatwa barabara na Ticotico akishirikiana na Said Sued 'Panucci'. Kama si uhodari wa kipa wa Pugu basi Golden Bush tungeibuka na goli zaidi ya 5. Hata hivyo matokeo tumeyafurahia kwasababu tumepata ushindi ambao ulikuwa na walazima.
Kesho Golden Bush tutakuwa Stakishari kwa mualiko wa Stakishari Veterans kucheza mechi ya kirafiki na kusherekea sikukuu pamoja na wenzetu. Baada ya sikukuu timu yetu itaelekea Zanzibar kwa mechi za kirafiki ili kufanya maadalizi ya mwisho kabisa ya gemu yetu ya kufunga mwaka dhidi ya Wahenga. Game hii uwa inakusanya wakazi wote wa Sinza na sehemu mbalimbali za jirani hivyo tunalazimika kufanya maandalizi ya nguvu sana.
Tuko kwenye mchakato wa kuomba udhamini wa game hiyo ya kufunga mwaka, tunashukuru mungu big Companies ambazo zitambua ushawishi mkubwa wa game hii zimeshaonyesha nia ya kutaka kutudhamini na kufunya matanagazo kwa kutumia wachezaji wengi maarufu wanaounda vikosi hivi viwili yaani Wahenga na Golden bush Veterans.

Asanteni
Onesmo Waziri 'Ticotico' Mchezaji Mwandamizi Golden Bush FC.

Ghana, Misri leo hapatoshi zinakutana kwa mara ya 19

Ghana Black Stars
MABINGWA wa zamani wa Afrika na waliowahi kuwa wawakilishi wa bara la Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia, Ghana na Misri leo zinatarajiwa kupepetana katika pambano la awali la hatua ya mwisho wa mchujo wa kuwania fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazili mwakani.
Timu hiuzo zinaumana leo kukamilisha mechi tano za mkondo wa kwanza za mchujo wa mwisho kusaka timu tano za Bara la Afrika zitakaliwakilisha katika fainali hizo za dunia.
Mechi nne za awali zilichezwa mwishoni mwa wiki na kushuhudiwa matokeo ya kusisimua, Ivopry Coast ikiitambia Senegal mabao 3-1, Algeria ikizabuliwa mabao 3-2 na Burkina Faso ugenini, huku Nigeria ikiilaza Ethiopia iliyokuwa nyumbani kwao kwa mabao 2-1 na Cameroon ikivimbiwa na Tunisia na kutoka suluhu ya 0-0.
Pambano la Misri na Ghana zinakumbusha fainali za kombe la Afrika za mwaka 2010 ambapo Ghana walilala bao 1-0 kwa Mafarao. Timu hizo zinakutana leo ikiwa ni mara ya 19 katika michezo ya kimataifa ikijumuisha mechi za mshindano na ile ya kirafiki.
Katika mechi 18 za awali baina ya timu hizo Ghana imekuwa wanyonge ikibamizwa mechi 9 na kushinda michezo minne tu na kuambulia sare katika mechi tano.
Hata hivyo mechi hiyo inazikutanisha Ghana wakionekana wazuri zaidi, licha ya Misri nao kutishwa ikiundwa na wachezaji nyota vijana na kufanya iwe vigumu kutabirika atakayemtesa mwenzake kabla ya kurudiana tena mwezi ujao na kuamua hatma ya timu moja wapo katika uwakilishi wa fainali hizo za dunia.