RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodgar Tenga ameingilia kati msuguano unaoendelea kati ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara na mdhamini mkuu wa ligi hiyo, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom kuhusiana na kuwapo kwa kipengele cha upekee katika mkataba wa udhamini wa ligi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya TFF jijini Dar es Salaam jana, rais huyo alizionya klabu zinazokiuka makubaliano yaliyomo kwenye mkataba huo na kwamba klabu zitakazoendelea kufanya hivyo zitachukuliwa hatua.
“Tunashukuru kupata mkataba ambao ni mara mbili ya ilivyokuwa awali. Mkataba huu lazima ulindwe na uheshimiwe. Yeyote atayekiuka, atachukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu,” alisema Tenga.
Tenga aliyasema hayo wakati mazungumzo kati ya klabu na mdhamini yakiendelea pia jijini Dar es Salaam jana.
Klabu zinalamikia kuwapo kwa vipengele kadhaa katika mkataba huo, vikiwamo vya posho za wachezaji, usafiri na kipengele cha upekee ambacho kinazuia timu kuvaa jezi au kubandika nembo za wapinzani wa kampuni hiyo kibiashara (makampuni ya huduma za simu).
Tenga alisema kuwa kuwapo kwa kipengele cha upekee lazima kiheshimiwe si wakati wa mechi tu, bali hata wakati wa mazoezi ya timu zote 14 zinazoshiriki ligi hiyo kwa kuwa kampuni hiyo ina haki ya matangazo hadi kwenye viwanja vya mazoezi vya timu hizo.
“Klabu zote zinazoshiri Ligi Kuu lazima zielewe hilo. Hata kwenye viwanja vyao vya mazoezi hawaruhusiwi kuvaa jezi au kubandika mabango ya wapinzani wa Vodacom, maana tulikubaliana hivyo na kampuni hiyo kabla ya kusaini mkataba huu,” alisema.
“African Lyon hawakuelewa vizuri vipengele vilivyomo kwenye mkataba huo ndiyo maana tulizungumza nao baada ya kutokea kwa tukio la timu yao kuingia na jezi zenye nembo ya Zantel wakati wa mechi ya Ligi Kuu.
Alidai kuwa mdhamini mkuu wa Ligi ya England ni benki ya Barclays, lakini Liverpool wanavaa jezi zenye nembo ya wadhamini wao ambao ni benki ya Standard Chartered kwa vile benki hizo mbili si wapinzani kibiashara maana kila moja ina aina yake ya wateja.
Alisema kuwa shirikisho hilo liliamua kuondoa kipengele cha upekee katika udhamini kama ilivyokuwa kwenye mkataba wa miaka mitano wa kampuni hiyo uliomalizika mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini kipengele hicho kimebaki kwenye bidhaa miongoni mwa wadhamini.
Aidha, Tenga alisema kuwa baadhi ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo zinadaiwa kiasi kikubwa cha pesa na shirikisho hilo na kwamba pesa zote zitakazotolewa na wadhamini zitaingizwa kwenye akaunti maalum itakayokuwa chini ya Kamati ya Ligi ya TFF kabla ya kusambazwa kwa klabu husika.
“Klabu zimechelewa kupata fedha kutoka kwa mdhamini mkuu kwa sababu mkataba ulichelewa kusainiwa. Ni kweli kwamba baadhi ya klabu zinadai pesa ya msimu uliopita, lakini klabu nyingi hasa zile kubwa tunazidai kiasi kikubwa sana cha pesa. Safari hii tumefungua akaunti maalum ambapo pesa za wadhamini zitawekwa kabla ya kupelekwa kwa wahusika. Wale wanaodai watalipwa na wale tunaowadai tutakata pesa yetu kwanza kabla ya kuwapatia fungu lao,” alisema.
Alizitaja klabu zinazodaiwa na shirikisho hilo kuwa ni pamoja na Simba, Yanga na Tanzania Prisons na kwamba madeni hayo yalitokana na TFF kuzilipia faini katika nyakati tofauti kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lakini alikataa kutaja kiasi hicho wanachozidai klabu.
Klabu zimekuwa katika mgongano na wadhamini kwa kudai kwamba kiasi wanachotoa cha Sh. bilioni 1.7 kwa mwaka ni kidogo mno kulinganisha na gharama za uendeshaji na kwamba, ili kipengele cha upekee kiendelee kuwapo, ni lazima waongeze fedha hizo na baadhi wamekaririwa wakitaka walau udhamini huo uwe wa Sh. bilioni 4 kwa mwaka.
Wakati ligi kuu ya Bara yenye timu 14 na kuhusisha mechi zaidi ya 180 kwa msimu ikidhaminiwa kwa Sh. bilioni 1.7, timu ya taifa pekee (Taifa Stars) hudhaminiwa na Kampuni ya Bia (TBL) kwa dau la zaidi ya Sh. bilioni 3.5 kwa msimu, bila kujali kwamba mechi zake huwa hazizidi 20 kwa mwaka.
TWIGA STARS
Katika hatua nyingine, Tenga pia aliomba wadhamini wajitokeze kuzisaidia timu za taifa za vijana na timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars) kwa kuwa zina hali mbaya kifedha.
“Tunatumia fedha nyingi sana kuiendesha timu ya Twiga Stars. Kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, tumetumia Sh. milioni 222 kuihudumi timu hiyo wakati wa kambi na mechi ndani na nje ya nchi,” alisema Tenga.
Tenga, ambaye pia ni Rais wa Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), aliushukuru uongozi wa kituo cha televisheni cha Super Sport cha Afrika Kusini kwa kuamua kuonesha baadhi ya mechi za Ligi Kuu msimu huu.