STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 28, 2012

Jeshi Stars yaivua Magereza ubingwa wa Wavu


MABINGWA mara tatu mfululizo wa michuano ya wavu ya wanawake, Magereza, wamevuliwa ubingwa huo na maafande wenzao wa Jeshi Stars baada ya kubwagwa kwa seti 3-1 katika mechi ya fainali iliyopigwa kwenye viwanja vya Bwalo la Umwema mjini Morogoro.
Kwa upande wa wanaume, timu ya Magereza ilitetea vyema taji lao baada ya kuwachapa Jeshi Stars kwa seti 3-0 katika mechi nyingine ya fainali iliyochezwa jana.
Nahodha wa Jeshi Stars (Wanawake), Zainab Thabit alisema timu yake imetwaa ubingwa huo kutokana na ujasiri wa kupambana hadi mwisho waliouonyesha dhidi ya mabingwa hao wa muda mrefu huku Ester Noel wa Magereza akiahidi kwamba mwakani watajifua zaidi kuhakikisha wanarejesha taji walilopoteza.
Mgeni rasmi katika fainali hizo, Katibu Mkuu Msaidizi wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Mohamed Kiganja, alisema mwamko wa baadhi ya michezo kama wavu umeendelea kuwa ni mdogo kwa kukosa ufadhili na ndio sababu mikoa mingi imeshindwa kuleta timu.
Aidha, Kiganja alilaumu baadhi ya viongozi kuua michezo kwa kugombea nyadhifa kwenye vyama vya michezo kwa matarajio fulani ambayo wakiyakosa huvitelekeza.
Alishauri zifanyike juhudi za kuibua vipaji vipya kwa kuweka nguvu kwenye ngazi ya shule badala ya kuendelea kutumia wachezaji walioibuliwa zamani kwenye michuano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Msingi (UMISHUMTA), ambao wameendelea kuliwakilisha taifa.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania, Muarami Msumi, alitaka serikali kupitia kitengo chake cha uwekezaji kuhakikisha wawekezaji wanapewa masharti ya kujenga viwanja vya michezo kama sehemu ya uwekezaji, sambamba na kuendelea kujenga na kuimarisha viwanja vya michezo kuanzia ngazi za shule za awali.
Timu 11 zikiwamo tatu za wanawake zilishiriki michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment