Kikosi cha Azam kitakachopambana na JKT Ruvu leo usiku |
TATIZO la majeruhi limeendelea kuikumba timu ngumu ya JKT Ruvu baada ya nyota wake Credo Mwaipopo, Damas Makwaya na George Minja kuondolewa katika kikosi kitakachoshuka dimbani leo kuivaa Azam katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Bara itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku na kuonyeshwa ‘live’ kupitia kituo cha televbisheni cha Super Sport.
Azam inasaka pointi tatu zaidi leo kuwapiku vinara Simba na kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi kuu ya Bara.
Akizungumza na NIPASHE jana, kocha wa JKT Ruvu, Charles Kilinda, alisema kuwa Makwaya ataikosa mechi ya leo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli, Minja jeraha la goti na mwaipopo atakuwa nje akiuguza maumivu ya jeraha paja.
Kilinda amesema kuwa anasikitika kuwakosa wachezaji hao, lakini hana hofu kwa vile ana wachezaji wengine wazuri wa kuziba nafasi zao, wakiwamo Ramadhan Kauogo na Dumba Ramadhan.
"Pamoja na kuwakosa majeruhi hao, bado kikosi changu kina ari kubwa ya kuibuka na ushindi," alisema Kilinda.
Hata hivyo, Kilinda alilalamikia ratiba ya ligi kwa kusema kwamba imewabana mno kwani wamejikuta wakicheza mechi tatu mfululizo dhidi ya timu tatu zilizokamata nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita, ambazo ni Simba, Azam na Yanga.
Katika mechi mbili zilizopita kabla ya leo, JKT Ruvu walicheza dhidi ya Simba na kuchapwa 2-0 na kasha wakafungwa tena 4-1 katika mechi iliyopita dhidi ya Yanga.
Endapo Azam itashinda, itakwea kileleni kwenye msimamo wa ligi kwani itafikisha pointi 10, moja zaidi ya vinara wa sasa, Simba.
Coastal Union ya jijini Tanga iliyoshinda nyumbani 3-2 katika mechi yao ya juzi dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani ilikwea hadi katika nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi nane.
Ligi hiyo inayoshirikisha timu 14, itaendelea pia kesho wakati Simba itakapocheza dhidi ya Prisons ya Mbeya kwenye uwanja huo huo wa Taifa kuanzia saa 11:00 jioni huku Yanga na African Lyon wakivaana keshokutwa Jumapili, pia kwenye Uwanja wa Taifa.
Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam utachezewa mechi kati ya Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar itakayochezwa Oktoba 1 kuanza saa 10.30 jioni na mechi ya mwisho ya 'Super Weekend' itachezwa Oktoba 3 kwenye Uwanja wa Taifa na kuwakutanisha mahasimu wa jadi, Yanga na Simba kuanzia saa 1:00 usiku.
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Nchini (TFF) limesikitishwa na taarifa za kifo cha Katibu Mkuu mstaafu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Erasto Zambi kilichotokea Septemba 26 jijini Dar es Salaam kutokana na maradhi.
Zambi ambaye anatarajiwa kuzikwa keshokutwa Jumapili, kabla ya kuwa kiongozi TOC, kwa muda mrefu alikuwa mwalimu wa michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo wanamichezo wengi hasa waliokuwa wanafunzi katika chuo hicho wamepita mikononi mwake.
Kikosi cha JKT Ruvu kikiwa mazoezini |
CHANZO:NIPASHE
No comments:
Post a Comment