Add caption |
SIMON Msuva amefanikiwa kunyakua tena tuzo ya Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya mabao yake manne aliyofunga kwenye mechi mbili za awali za Yanga kushindwa kufikiwa na mchezaji yeyote.
Mwaka 2014 winga huyo alinyakua pia tuzo hiyo kwa idadi kama hiyo wakati Yanga ikiwa imeaga mashindano hatua ya robo fainali kwa kuchapwa bao 1-0 na JKU.
Kipa Aishi Manula wa Azam ambaye hakuruhusu wavu wake kuguswa hata mara moja kama alivyofanya kwenye michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2015, alitangazwa kuwa Kipa Bora wa michuano ya mwaka huu ya Mapinduzi, huku beki wa Simba, Method Mwanjali akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mashindano na Said Mohammed wa Taifa akitangazwa Mchezaji Bora Chipukizi.
Mwamuzi Mfaume Ali alitwaa tuzo ya Mwamuzi Bora na kila mmoja kati ya walionyakua tuzo hizo alitwaa kitiota cha Sh 1 milioni moja.
Tuzo hizo na zawadi kwa washindi wote wa michuano ya msimu huu wa 11 ya Kombe la Mapinduzi walikabidhiwa zawadi zao na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein aliyekuwa mgeni rasmi.
Azam ndio mabingwa wapya wa michuano hiyo iliyoanza Desemba 30 mwaka jana kwa kuilaza Simba kwa bao 1-0.