STRIKA
USILIKOSE
Wednesday, January 18, 2012
Madame V awakumbuka wajane, yatima
MSANII mahiri wa muziki wa Zouk, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Geita, Vicky Kamata amejitosa kwenye huduma za kijamii akiunda asasi yake binafsi inayoshughulikia kuwasaidia wajane, yatima na wasiojiweza.
Akizungumza na MICHARAZO, Kamata maarufu kama 'Madam V' alisema asasi hiyo inafahamika kwa jina la Victoria Foundation ambayo tayari imeshaanza kuendesha shughuli zake tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Kamata aliyetamba na nyimbo kama 'Wanawake na Maendeleo' na 'Mapenzi na Shule', alisema ameianzisha asasi hiyo kutokana na kuguswa na matatizo ya baadhi ya watu hususan yatima na wajane waliopo ndani ya wilaya ya Geita unaotarajiwa kuwa mkoa.
Alisema kama mwanaharakati kijana anaona ni wajibu wake kujitolea kwa hali na mali kusaidia jamii hiyo ili nao angalau wajione ni wenye kuthaminiwa na kuongeza kuwa kila mtu ambaye ana uwezo wa kuwapiga tafu wenye matatizo wasisubiri kusukumwa.
"Hii ni njia ya kurudisha fadhila kwa jamii kutokana na kukubalika kwa kazi zangu kisanii na kuchaguliwa kwangu kuwa kama Mbunge, hivyo na wengine wenye uwezo wa kuwasaidia wenye matatizo wasisubiri kusukumwa kwani ni jukumu letu," alisema.
Kamata alisema kwa sasa anajiandaa kugawa baiskeli 50 na misaada mingine kwa watu wa tarafa nyingine za Geita baada ya awali kufanya hivyo tarafa ya Bugando, ambapo aligawa baiskeli 30 na kugawa vyakula na magodoro kwa vituo vya kulelea yatima vya Lelea na Feed & Tent International.
Fella asita kutoa albamu ‘Kusonona’
ALBAMU mpya ya miondoko ya 'Rusha Roho' ya Meneja wa kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella iitwayo 'Kusonona Kusonona' haijasambazwa hadi sasa kutokana na kile ambachom mwenyewe amedai kuwa ni kuangalia kwa umakini kama ni muafaka kuitoa sasa ama la.
Akizungumza na MICHARAZO, Fella, alisema albamu hiyo yenye nyimbo sita iliyokuwa isambazwe mwishoni mwa mwaka jana, mpaka sasa haijatoka kwa sabahu hiyo ya kupima 'upepo'.
Fella alisema wakati akijiandaa kuitoa kazi hiyo mtaani, kulikuwa na kazi nyingine lukuki na hivyo kukubali kwamba atulie kwanza ili kuangalia mwenendo wa albamu zilizotangulia na kwamba huenda akaitoa mwisho wa mwezi huu.
"Ile albamu yangu ya 'Kusonona Kusonona' ya miondoko ya taarab, bado sijaiachia hadi sasa kutokana na hali ilivyokuwa sokoni, lakini kwa sasa nipo mbioni kufanya hivyo" alisema Fella.
Aliongeza, licha ya kwamba albamu bado haijaingia sokoni, lakini baadhi ya nyimbo zake zimekuwa zikifanya vema kwenye vituo vya redio na runinga baada ya kusambaza kwa nia ya kuitambulisha albamu hiyo kikiwemo 'Midomo Imewashuka'.
Ndani ya albamu hiyo, Fella amewashirikisha nyota kadhaa wa taarab wakiwemo Khadija Kopa wa TOT, Isha Ramadhani wa Mashauzi Classic na Maua Tego wa kundi la Coast Modern.
Fella alizitaja nyimbo zilizopo ndani ya albamu hiyo kuwa ni 'Simuachi', 'Midomo Imewashuka', 'Mchakamchaka', 'Sijapopoa Dodo', 'Kimodern Modern' na 'Kusonona Kusonona' iliyobeba jina la albamu.
Steve Nyerere kupakua ‘Respect Nyerere’
WAKATI filamu yake ya 'Mr President' ikiendelea kutamba, mkali wa kuigiza sauti za watu, Steven Mengele 'Steve Nyerere', sasa yuko mbioni kufyatua filamu iitwayo 'Respect Nyerere'.
Filamu hiyo itakayotolewa na kampuni yake ya 'Nyerere the Power', itahusiana na mambo mbalimbali ya kisiasa pamoja na hotuba za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Muigizaji huyo ambaye ni mmoja wa viongozi waandamizi wa Bongo Movie, alisema safari ya kwenda Butiama alipozaliwa Mwalimu Nyerere imeiva kwa ajili ya kufyatua kazi hiyo ambayo alidai kwamba itakuwa kali pengine kuliko ya 'Mr President'.
"Nipo katika maandalizi ya kufyatua kazi mpya ambayo itahusisha masuala ya siasa na baadhi ya hotuba za kusisimua za Mwalimu Nyerere, mmoja wa viongozi wa mfano duniani," alisema Steve Nyerere.
Muigizaji, huyo alisema kila kinachoendelea katika upakuaji wa kazi hiyo atawafahamisha mashabiki wake.
Banana, JB, Riyama waja na DNA
MWANAMUZIKI nyota nchini, Banana Zorro anatarajia kuibukia kwenye filamu kupitia kazi mpya iitwayo DNA aliyoigiza na nyota wa fani hiyo kama Riyama Ally, Jacob Stephen 'JB' na Sabrina Rupia maarufu kwa jina la 'Cathy'.
Kazi hiyo mpya inayohusiana na masuala ya kijamii na namna hila zinavyoweza kufanywa katika upimaji wa vinasaba na kuleta mtafaruku, inatarajiwa kuingia sokoni wakati wowote kuanzia sasa.
Kwa mujibu wa taarifa za wasambazaji, ni kwamba kama anavyotamba katika muziki, Banana ambaye ni mtoto wa gwiji wa muziki wa dansi nchini, Zahir Ally Zorro ameonyesha umahiri mkubwa pia katika filamu.
"Ndani ya DNA, Banana Zorro kathibitisha kuwa habahatishi. Ameshawahi kucheza filamu kadhaa nyuma ikiwemo ya 'Handsome', na humu pia amefanya vizuri sana," imeelezwa katika taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, filamu mpya ya 'I Hate My Birthday' ya Vincent Kigosi 'Ray' inatarajiwa kuanza kusambazwa keshokutwa ambapo ndani yake wameshiriki nyota kadhaa kama Irene Paul na Aunty Ezekiel.
Mdogo wa Nsajigwa 'atua' Bandari Kenya
BEKI wa kutumainiwa wa timu ya 94 KJ inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara ya 94 KJ, ambaye ni mdogo wa nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, Simon Joel Nsajigwa, ametua klabu ya Bandari Fc ya Kenya kwa ajili ya kufanyiwa majaribio.
Mchezaji huyo aliyefanana sura na umbo kama kaka yake, alienda kufanyiwa majaribio katika timu hiyo iliyoshuka daraja msimu huu toka Ligi Kuu ya Kenya, wiki mbili zilizopita baada ya mawakala wa timu kuvutiwa na soka lake.
Kocha wa timu ya 94 KJ, Mwinyimadi Tambaza, alisema walimruhusu mchezaji huyo kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa na amekuwa akiwasiliana naye kila mara kujua kinachoendelea.
Tambaza alisema walipowasiliana naye juzi alimfahamisha kuwa majaribio yake yanaendelea vema na atarejea nchini wiki ijayo ili kusubiri kitakachofuata juu ya hatma yake ya kuichezea timu hiyo iliyodakiwa na kipa Ivo Mapunda kabla ya kuitema iliposhuka daraja na kwenda kujiunga na Gor Mahia.
"Ni kweli beki wetu ambaye ni mdogo wa Shadrack Nsajigwa, yupo Kenya akifanyiwa majaribio katika timu ya Bandari na anatazamiwa kurejea nchini wiki ijayo kuungana na wachezaji wenzake kwa ajili ya duru la pili la Ligi Daraja la Kwanza wakati akisubiri tararibu nyingine za kuichezea timu hiyo ya Kenya," alisema Tambaza.
Tambaza, alisema ana imani kubwa kwa Nsajigwa mdogo kusajiliwa Bandari kutokana na kuwa na uwezo mkubwa kwa nafasi yake ya ulinzi wa pembeni kama ilivyo kwa kaka yake ambaye ni maarufu nchini kama 'Fuso'.
Mwisho
Coastal Union yakuna kichwa kwa Simba
UONGOZI wa klabu ya soka ya Coastal Union ya Tanga, umedai pambano lao la awali la duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba litakalofanyika wiki ijayo linawapasua vichwa wakitafakari mbinu za kuweza kuwapa ushindi wa mchezo huo.
Coastal iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, itakwaruzana na Simba katika pambano la marudiano litakalofanyika Jumatano ijayo kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Afisa Habari wa timu hiyo, Eddo Kumwembe, alisema kuwa kuanza duru la pili kwa kuumana na Simba ni mtihani mgumu ambao unawafanya wajipange vema ili kufanya vema kabla ya kufunga safari kuwafuata Mtibwa Sugar kwenye dimba lao la nyumbani.
Kumwembe, alisema uongozi wao upo makini na pambano hilo kwa vile wanataka washinde ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuondoka nafasi za mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo.
"Kuanza na timu kubwa kama Simba ni mtihani unaortuchanganya akili kwa sasa, tukijipanga kwa umakini mkubwa kuona tunaibuka na ushindi kabla ya kwenda kuvaana na Mtibwa huko Manungu," alisema Kumwembe.
Alisema lengo la uongozi wao ni kuona Coastal Union, inatoka maeneo ya mkiani na kuwa miongoni mwa timu za nafasi za juu, hasa baada ya kuongeza nyota kadhaa katika kikosi chao wakati wa usajili wa dirisha dogo.
"Tunataka Coastal ifanye vema kwenye duru hili, ndio maana hata kocha wetu aliamua kufuta mechi yetu dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kusudi arekebishe mambo kutokana na kuwa nyuma ya mipango yake," alisema Kumwembe.
Kumwembe aliongeza, kwa kikosi walichonacho sasa ni wazi timu yao itarejesha makali yake ya zamani yaliyoipa ubingwa wa nchi.
Nyota waliongezwa katika kikosi cha Coastal ni Mkenya Edwin Mukenya, Ally Shiboli, Wanigeria Felix Amechi na Samuel Temi na wakali wengine waliokuwa katika usajili w awali wakiwemo washambuliaji Ben Mwalala na Aziz Gilla.

Mkubwa na Wanae: Kituo cha kuendeleza vipaji
WAKATI kituo cha kuendeleza vipaji vya sanaa kwa vijana cha 'Mkubwa na Wanawe'
kinachomilikiwa na Meneja wa TMK Wanaume Family, Said Fella kilipoanzishwa mwaka jana kilikuwa na msanii mmoja tu, Abdallah Kihambwe 'Dula Yeyo'.
Hata hivyo kikielekea kutimiza muda wa mwaka mmoja mnamo Februari 13, mwaka huu, kituo hicho kina jumla ya wasanii 37, wasichana 10 na waliosalia ni wavulana ambao wote wanaimba na kudansi.
Fella, maarufu kama 'Mkubwa Fella' ambaye ndiye Mkurugenzi wa kituo hicho alisema
alipata wazo la kuanzisha kituo hicho kilichosajiliwa kama kampuni, kutokana na kuvutiwa na mafanikio inayopata kituo kingine cha kuendeleza vipaji cha THT.
Alisema, pia alikianzishwa kwa nia ya kusaidia vijana wadogo kujiepusha kuingia kwenye makundi maovu yatakayoweza kuwapotosha na kufunza stadi za maisha kwa faida yao ya baadae mbali na kuvitumia vipaji vyao vya sanaa kama ajira rasmi.
Fella, alisema tangu kuanzishwa kwa kituo hicho ambayo anashirikiana kukiendesha na
wakurugenzi wenzake, Hamis Tale 'Babu Tale' na Mheshimiwa Temba, kimeweza kuwatoa wasanii karibu saba ambao wameanza kutamba kwenye fani ya muziki nchini.
"Tunashukuru tangu kuanzishwa kwa kituo hiki, tumefanikiwa kuwatoa wasanii kadhaa ambao wameanza kupata mafanikio katika muziki, licha ya kwamba tunakabiliwa na matatizo makubwa katika kituo chtu kwa vile hakina wafadhili wala wadhamini," alisema.
Aliwataja wasanii wanaokitangaza kituo hicho kwa sasa ni Aslay Isihaka 'Dogo Aslay'
anayetamba na wimbo wa 'Nakusemea' maarufu kama 'Naenda Kusema kwa Mama', Dula Yeyo, Mugogo anayekimbiza na wimbo wa 'Chongochongo' na Hassani Kumbi anayetamba na kibao cha 'Vocha' kilichopo katika mahadhi ya Mduara.
"Wengine ambao tumeanza kuwarekodia kutokana na kuiva kimuziki ni, H. Namba, Bashlee na Asnat wanaotarajia kuibuka na kibao kiitwacho 'Nipe Kidogo', kwa vifupi ni kwamba matunda yameanza kuonekana katika kuwaibua wasanii wapya," alisema.
Fella alisema licha ya kuwafunza namna ya kuimba na kucheza, wasanii waliopo kituo
hapo wanafundishwa stadi za maisha juu ya mapenzi na athari zake, matumizi ya dawa za kulevya na magonjwa mbalimbali kama Ukimwi na mengine na jinsi ya kuepukana nayo.
"Kwa upande wa muziki mwalimu wanayewanoa vijana hao ni Mhe Temba na Dulla Yeyo, wakati Meneja wa kituo ni Yusuf Chambuso na Prodyuza wa kituo ni Suleiman Daud maarufu kama Sulesh au Mr India," alisema Fella.
Juu ya namna ya kukihudumia kituo, Fella alisema wanatumia fedha zao wenyewe wakati wakisubiri kupata ufadhili, ambapo alisema kwa mwezi mzima hutumia si chini ya Sh. Mil moja kwa ajili ya malazi ya chakula.
"Unajua nyumba hii inayowatunzia wasanii ni ya kukodisha, tunalipa pango kwa mwezi
Sh. 250,000, huku huduma ya chakula kwa siku si chini ya Sh 25,000, hiyo ni mbali na
gharama za usafiri na ada kwa wanafunzi tunawaosemesha wenyewe," alisema.
Alisema licha ya wengi wa wasanii wao kutokea majumbani kwao kuja kujifunza fani zao kituo hapo, wapo wasanii 12 wanaoishi katika nyumba hiyo iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam.
Fella alisema matarajio yao hadi kufikia mwisho wa mwa huu wasanii zaidi ya 20 wawe
wameshatoka kisanii, na kuwasaidia vijana zaidi ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo alisema mafanikio hayo yatafikiwa pale atakapopata wafadhili na kuungwa
mkono na serikali katika jitihada zake za kuendeleza sanaa na kuwasaidia vijana kupata ajira kupitia muziki, sambamba na kuwajenga kimaadili.
Fella alisema kituo kwao kitu cha kwanza wanachozingatia ni nidhamu na kuwanyoosha wale wanaoonekana kwenda kinyume, pia wanathamini kipaji cha mtu bila kujali umri wake na bahati nzuri matunda yao yanaonekana kupitia wasanii walioanza kutamba sasa.
Naye Meneja wa kituo hicho, Yusuf Chambuso, alisema kuna vikwazo kadhaa wamewahi kukutana navyo kama baadhi ya wazazi kushindwa kuwaelewa katika wanachokusudia kwa kudhani watoto wao wanafunzwa uhuni, lakini wanapoeleweshwa huwapa sapoti.
Aliongeza wapo baadhi ya vijana wanaoenda kwao huwa hawana uwezo wowote kimuziki, lakini kupitia walimu wao huwasaidia na kuwaweka juu, akimtolea Aslay aliyedai licha ya kugundua kipaji cha muziki, walimsaidia kumweka sawa ndio maana leo anatisha.
Mwisho
Maneno, Matumla kusindikizwa PTA
MABONDIA wakongwe wa ngumi za kulipwa nchini, Rashid Matumla 'Snake Man' na Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo' wanatarajiwa kusindikizwa na mabondia 10 tofauti katika pambano lao litakalofanyika mwezi ujao kwenye ukumbi wa PTA, jijini.
Oswald na Matumla watapigana katika pambano lisilo la ubingwa la uzani wa Super Middle, litakalofanyika Februari 25 kwa nia ya kumaliza ubishi baina yao.
Wawili hao walipigana Desemba 25 mwaka uliopita, na kutoka droo ya pointi 99-99 ambapo kila mmoja alinukuliwa kutokubaliana na matokeo hato akisema alistahili kutangazwa mshindi katika mchezo huo uliochezwa katika ukumbi wa Heinken Pub.
Mratibu wa pambano hilo, Issa Malanga, amesema kabla ya mabondia hao wakongwe kupanda ulingoni kutakuwa na michezo kadhaa ya utangulizi ambayo itahusisha mabondia chipukizi na wale wazoefu.
Malanga, alisema baadhi ya mabondia watakaowasindikiza akina Matumla ni Shomari
Mirundi atakayepigana na Mikidadi Abdallah 'Tyson' na Idd Mkenye dhidi ya Shabaan Mtengela 'Zunga Boy'.
Michezo mingine ya utangulizi itawakutanisha, Abdallah Mohamedi dhidi ya Saleh Mkalekwa na Ramadhani Mashudu ataonyeshana kazi na Hassan Kiwale 'Moro Best'.
Malanga alisema anafanya mipango mapambano hayo yapambwe na burudani ya muziki wa kizazi kipya toka kundi la TMK Wanaume Family, ingawa alisema kwa sasa ni mapema mno kwa vile bado hajafanya mazungumzo na wasanii wa kundi hilo.
Matumla na Maneno tayari walishapigana mara nne, mara mbili Matumla akiibuka na ushindi na moja Maneno kutoka kidedea na la mwisho ndilo lililoisha kwa sare inayolalamikiwa na wote wawili.

Juma Mgunda ala shavu Coastal, wawili watimuliwa
WAKATI nyota wa zamani wa kimataifa nchini, Juma Mgunda akila 'shavu' kwa kuteuliwa kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Coastal Union ya Tanga, wachezaji wawili wa timu hiyo wamefukuzwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Wachezaji waliotimuliwa Coastal kutokana na kushindwa kuripoti kwenye kambi ya timu hiyo inayojiandaa na mechi za duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara ni Daniel Busungu na Soud Abdallah aliyewahi kuichezea pia Simba msimu kadhaa ya nyuma.
Afisa Habari wa Coastal, Eddo Kumwembe, aliiambia MICHARAZO jana kuwa, Soud na Busungu wamechukuliwa hatua hiyo kutokana na kuonyesha dharau kwa uongozi wao ambao umekuwa ukiwabembeleza kujiunga na kambi ya mazoezi.
Kumwembe alisema kwa mfano Busungu licha ya kutumiwa nauli kwa ajili ya kwenda kambini hadi sasa hajaripoti wala kutoa maelezo jambo linaloonyesha hana nia ya kuichezea timu yao na ndio maana wamemtimua.
"Kwa kuwa tuna nia ya kuona timu yetu inafanya vema tumewatimua wachezaji hao kwa utovu wa nidhamu, kwani wameonyesha hawana nia ya kuichezea Coastal kwa vile fedha za nauli tumewatimua na bado wanatudengulia," alisema Kumwembe.
Aliongeza katika kuhakikisha wanafanya vema kwenye duru lijalo la ligi kuu linaloanza Jumamosi, timu yao imempa ulaji, mshambuliaji nyota wa zamani wa timu hiyo na Taifa Stars, Juma Mgunda kuwa Kaimu Kocha Mkuu.
Kumwembe alisema Mgunda, amechukuliwa kushika nafasi ya Jamhuri Kihwelu 'Julio' ambaye yupo Oman kwa mambo yake binafsi na atakapokuja ataendelea na cheo chake huku Mgunda atakuwa msaidizi wake katika benchi lao la ufundi.
"Timu kwa sasa ipo chini ya Juma Mgunda akisaidiana na Ally Jangalu, ingawa bado Julio tunamtambua kama kocha wetu hadi atakaporudi baada ya kumaliza mambo yake huko Arabuni," alisema Kumwembe.
Kumwembe, alisema kikosi chao kwa ujumla kipo vema tayari kwa mikikimikiki ya duru la pili, ambapo wao wataanza kwa kuvaana na Simba Jumatano ijayo, jijini Dar.
Mwisho
Snake Boy Jr ataka mabondia wapimwe VVU
BONDIA machachari nchini wa ngumi za kulipwa, Mohammed Matumla 'Snake Boy Jr', ametaka iwe ni lazima kwa mabondia wapimwe VVU kabla ya kupanda ulingoni kwa nia ya kuepusha maambukizi kwa wapiganaji.
Mtoto huyo wa bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla 'Snake Man' alisema kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa katika upimaji afya kwa mabondia kabla ya kupigana hali inayohatarisha usalama wa afya zao ulingoni.
Matumla, alisema ni lazima mabondia wawe wanapimwa afya zao na hasa VVU( Virusi vya Ukimwi), ili kuwaweka salama mabondia wawapo ulingoni ambapo hutokea wakapeana majeraha mauongoni yanayoweza kusababisha maambukizi kati yao.
"Nadhani ipo haja ya kufanyika kwa lazima upimaji wa VVU kama tunataka kuwaweka salama mabondia wetu, mara nyingi tumekuwa tukipanda ulingoni bila kupimwa afya zaidi ya uzito au kupimwa mapigo ya moyo tu, hili ni jambo la hatari," alisema.
Alisema kupitia baba yake amewahi kusikia kwamba kwa mabondia wa nchi za Ulaya wamekuwa makini katika suala la upimaji afya za mabondia kabla ya kupigana kwa lengo la kuwaweka salama na kuwapusha matatizo tofauti na ilivyo nchini.
Bondia huyo 'asiyepigika' tanu aingie kwenye ngumi za kulipwa mwaka juzi, alisema vyama na mabondia wanapaswa kusimamia jambo hilo kwa umakini mkubwa kwa vile inaweza kuleta athari kubwa baadae bila watu kujua tatizo limeanzia wapi.
Aliongeza, hata taarifa kwamba mabondia fulani wamepimwa na kugundulika wapo fiti ni propaganda tu, ukweli huwa hakuna kinachofanyika, japo alikiri suala la upimaji afya ni jambo binafsi la mtu, ila kwa mabondia kama yeye iwe lazima kwa usalama wao.
Kauli ya bondia huyo chipukizi inakaribiana na ile iliyowahi kutolewa na aliyekuwa Bingwa wa Dunia wa WBF, Karama Nyilawila aliyewahi kuvitaka vyama kusimamia suala la upimaji VVU kwa mabondia kabla ya kupanda ulingoni kupigana.
Mwisho
Moro Utd yaipigia hesabu Yanga
KLABU ya soka ya Moro United imesema ipo kwenye mahesabu makali ili kuhakikisha inaibuka na ushindi katika pambano lao la fungua dimba la duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga watakaumana nao Jumamosi ijayo.
Yanga na Moro United zinatarajiwa kushuka dimba la Taifa, Dar es Salaam kuumana katika mechi ya kufungua pazia la duru la pili, ambapo pia siku hiyo kutakuwa na mechi nyingine tatu katika viwanja tofauti nchini.
Katibu Mkuu wa Moro United, Hamza Abdallah, alisema kuwa akili zao zipo kwenye pambano hilo kwa lengo la kupata ushindi katika mchezo huo wa kufungua dimba ili kuanza vema na pia kujiweka katika mazingira mazuri.
Abdallah, alisema wanatambua kuwa pambano hilo litakuwa gumu kutokana na jinsi timu hizo mbili zinapokutana uwanjani mechi yao huwa na upinzani, lakini kubwa kwao ni kuona wanashinda baada ya pambano lao la awali kuisha kwa sare ya 1-1.
"Tunajipanga kuhakikisha tunapata ushindi katika mechi hiyo ya ufunguzi wa duru la pili, tunaamini kikosi tulichonacho ambacho kimeongezewa nguvu na wachezaji wapya na walimu katika benchi la ufundi, kitaisimamisha Yanga Jumamosi," alisema.
Katibu huyo alisema licha ya kwamba imewapoteza wachezaji nyota watatu, Omega Seme na Salum Telela waliorejea Yanga na Gaudence Mwaikimba kuhamia Azam, bado kikosi chao kitafanya vema baada ya kuwanasa wakali wengine kadhaa.
Baadhi ya wachezaji inayojivunia MoroUtd katika kikosi chao cha sasa ni pamoja na Jamal Mnyate toka Azam, Fred Mbuna aliyetoka Yanga, Salum Kanoni na Meshack Abel wote kutoka Simba waliosajiliwa kwenye dirisha dogo lililofungwa hivi karibuni.
Timu hiyo kwa sasa imejichimbia kambini eneo la Tabata, jijini Dar es Salaam tayari kwa ajili ya pambano hilo dhidi ya Yanga.

Subscribe to:
Posts (Atom)