|
Mtibwa Sugar wana nafasi kubwa ya kukalia kiti cha uongozi wa Ligi Kuu msimu huu leo |
|
Mgambo JKT watakubali kufanywa ngazi kwa Mtibwa Sugar leo Manungu? |
|
Kikosi cha JKT Ruvu kinachotarajiwa kuvaana na Yanga leo Taifa, watakuwa mdebwedo tena kama msimu uliopita? |
|
Yanga watakaokuwa wakijaribu bahati yao kwa JKT Ruvu leo Taifa, watacheka au kununa kama watani zao Simba? |
BAADA ya jana timu ya Azam kushindwa kuwakimbia kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kulazimishwa sare ya kutofunga ana Prisons-Mbeya, Mtibwa Sugar leo ina nafasi ya kukalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo kama itapata ushindi kwa Mgambo JKT mjini Morogoro.
Mtibwa inaikaribisha Mgambo kwenye uwanja wake wa Manungu, Turiani kati ya mechi mbili zinazopigwa leo kukamilisha raundi ya tatu ya ligi hiyo, pambano jingine likiwa ni kati ya Yanga dhidi ya JKT Ruvu.
Mchezo wa Yanga na JKT Ruvu utapigwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo kila timu itahitaji kupata ushindi ili kujiweka nafasi nzuri katika msimamo kabla ya mechi zao zijazo Oktoba 18 na 19 mwaka huu.
Yanga iliyoifumua Prisons-Mbeya kwa mabao 2-1 katika mechi ya mwisho ipo katika nafasi ya 10 kwa sasa ikiporomoshwa na watani zao Simba ambao jana walilazimishwa sare nyingine ya tatu japo wanalingana pointi tatu kila mmoja, ila uwiano wa mabao unawatenganisha Simba wakiwa juu.
Mtibwa ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zake mbili na kuwa timu pekee mpaka sasa iliyoshinda mfululizo baada ya Azam jana kulazimishwa sare na Prisons.
Kama itashinda Mtibwa itaweka rekodi ya kushinda kwa asilimia 100 mechi zake na kukwea kileleni kwa kukusanya pointi 9, japo huenda wakata miwa hao wasipate mteremko kwa Mgambo JKt ambayo inauguza kipigo cha bao 1-0 ilichopewa na Stand United mjini Tanga katika mechi yao iliyopita.
Mtibwa inayonolewa na kocha mzawa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Mexime inajivunia kuwa na wachezaji vijana wenye vipaji vya soka pamoja na kuongezewa nguvu wa makongwe kama Shaaban Nditi, Mussa Mgosi na Vincent Barnabas.
Kwa Yanga itakayokuwa jijini Dar itakuwa na kazi kubwa mbele ya maafande wa JKT Ruvu wanaonolewa na beki wao wa zamani, Fred Felix Minziro kuweza kuendeleza wimbi lao la ushindi.
Baada ya kunyukwa na Mtibwa katika mechi ya kwanza mjini Morogoro, Yanga ilizinduka kwa kuilaza Prisons na leo ingependa kushinda ili kuchupa hadi kwenye Tatu Bora kwani itafikisha pointi sita na kuivuka hata Mbeya City waliopo nafasi ya tatu kwa sasa na pointi zao tano.
Cha kufurahisha Genlson Santana 'Jaja' na Coutinho, pamoja na wakali wote wa Jangwani wapo fiti na kumpa afueni kocha Marcio Maximo kupanga kikosi anachokitaka kusaka ushindi wao wa pili msimu huu.
Hata hivyo vijana wa Minziro ambao wametoka kupokea kipigo toka kwa Kagera Sugar katika mechi iliyopita hawatataka kufanywa ngazi ya kuipandisha Yanga kwenye Tatu Bora kwani wapo nafasi ya pili toka mkiani wakiwa na pointi moja tu.
Kadhalika bado wanakumbuka katika mechi za msimu uliopita walibugizwa jumla ya mabao 9-2 baada ya mechi ya kwanza kufungwa 4-1 na alipokuja kuipokea timu, Minziro alishindiliwa mabao 5-1.
Ngoja tuone mechi hizo mbili za leo zitatoa matokeo gani ambayo yanaweza kupangua msimamo wa sasa ulivyo kama unavyoonekana hapo chini;
MSIMAMO LIGI KUU TANZANIA BARA 2014-2015
P W D L F A GD Pts
01. Azam 03 02 01 00 05 01 +4 07
02. Mtibwa Sugar 02 02 00 00 05 01 +4 06
03. Mbeya City 03 01 02 00 01 00 +1 05
04. Prisons 03 01 01 01 03 02 +1 04
05.Kagera Sugar 03 01 01 01 03 02 +1 04
06.Coastal Union 03 01 01 01 04 04 00 04
07.Stand Utd 03 01 01 01 03 05 -2 04
08. Ndanda Fc 03 01 00 02 06 06 00 03
09.Simba 03 00 03 00 04 04 00 03
10.Yanga 02 01 00 01 02 02 00 03
11. Mgambo JKT 02 01 00 01 01 01 00 03
12. Polisi Moro 03 00 02 01 03 05 -2 02
13.JKT Ruvu 02 00 01 01 00 02 -2 01
14. Ruvu Shooting 03 00 01 02 00 04 -4 01