STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 14, 2014

Twiga Stars yalala 2-1 Zambia

Na Boniface Wambura, Lusaka
TWIGA Stars imepoteza mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) baada ya leo kufungwa mabao 2-1 na Zambia (Shepolopolo) kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.
Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Salma Mukansanga timu hizo zilikuwa suluhu.
Wenyeji ndiyo walianza kupata bao lililofungwa na Hellen Mubanga dakika ya 75. Mfungaji huyo aliyeingia kipindi cha pili nchini alimalizia wavuni mpira uliotemwa na kipa Fatuma Omari.
Dakika nne baadaye Zambia ambao walikuwa wakishangiliwa kwa nguvu na washabiki wao baada ya kufunga la kwanza, walipata bao la pili ambalo nahodha wa Twiga Stars, Sophia Mwasikili alijifunga mwenyewe.
Mwasikili alikuwa akijaribu kutoa nje mpira uliopigwa na nahodha wa Shepolopolo, Mupopo Kabange ambapo ulipishana na kipa Fatuma Omari kabla ya kujaa wavuni.
Bao la Twiga Stars lilifungwa na Donisia Daniel dakika ya 90. Beki huyo wa kushoto ambaye pia ni mchezaji wa Tanzanite alipanda mbele kuongeza mashambulizi ambapo akiwa nje ya eneo la hatari alipiga shuti lililomshinda kipa Hazel Nali.
Akizungumza baada ya mechi, Kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage alisema amebaini upungufu katika kikosi chake ambao ataufanyia kazi kabla ya mechi ya marudiano ili timu yake iweze kusonga mbele.
“Kwa matokeo haya bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano nyumbani na kusonga mbele,” alisema Kaijage.
Twiga Stars iliwakilishwa na Fatuma Omari, Fatuma Bashiru, Donisia Daniel, Fatuma Issa, Evelyn Sekikubo, Sophia Mwasikili, Vumilia Maarifa, Mwapewa Mtumwa/Amina Ali, Asha Rashid, Etoe Mlenzi/Zena Khamis na Shelida Boniface.
Timu hiyo inarejea nyumbani kesho kwa ndege ya Fastjet ambapo itatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7 kamili mchana.

Juan Mata afunguka kuhusu Mashetani Wekundu


368919_heroa
Mchezaji ghali zaidi kuwahi kununuliwa na klabu ya Manchester  United, Juan Mata amesisitiza kwamba ana furaha kucheza kwenye sehemu wowote uwanjani atakayopangwa na mwalimu wake na amebakia mtu mwenye furaha tangu alipojiunga na klabu hiyo mwezi uliopita.

Mhispania huyo ambaye amecheza mechi zote nne tangu alipojiunga na timu, na ameiwezesha timu yake kufunga mabao matatu na kuhakikisha inapata pointi 5, huku akichezeshwa kwenye namba tofauti na kocha David Moyes.
Moyes ameshamchezesha Mata kwenye winga zote mbili, amecheza nyuma ya mshambuliaji, lakini kiungo huyo mwenye miaka 25 hana chaguo lolote la sehemu ya kuchezeshwa anachojali ni kuisadia timu yake kushinda.
“Maisha yangu yote ya soka nimekuwa nikicheza upande wa kushoto, kulia na nyuma ya mshambuliaji,” Mata aliwaambia waandishi wa habari.
“Sijali wapi nachezeshwa na kocha wangu. Nina furaha nipo kwenye klabu kubwa sana na nina matumaini tutamaliza msimu vizuri.
“David de Gea amenisaidia kupazoea hapa, pia Chicharito, [Antonio] Valencia, na Rafael, wote wanaongea kihispania na wamenisaidia.”

TFF ya Jamal Malinzi yarejesha Kombe la Taifa kivingine

Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliyetangaza mikakati ya kuikwamua Tanzania soka la kimataifa
MASHINDANO maalumu ya mikoa ya kuunda kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Februari 22 hadi Machi 5 mwaka huu, huku ikiigharimu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) takribani Sh. Milioni 360.
Michuano hiyo maalumu itashirikisha mikoa wanachama ya TFF na itakuwa ikichezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini kwa timu mbili za kanda moja kuchuana na inatarajiwa kutoa wachezaji bora 60 wataoweka kambi ya siku 30 Tukuyu, Rungwe mkoani Mbeya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF Jamal Malinzi amesema michuano hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuuunda upya kikosi bora cha Stars, ili kiweze kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika mwakani nchini Morocco.
Malinzi alisema jumla ya timu 32 za Tanzania nzima zitashiriki michuano hiyo, kila mechi moja watakuwepo wasaka vipaji watano ‘Scouts’ kwa ajili ya kumulika wachezaji bora, pia mechi zote zitakuwa zikirekodiwa.
Baada ya zoezi la kuibua vipaji kwenye michuano hiyo, wasaka vipaji wote watajifungia (retreat) kwa muda wiki moja mjini Lushoto, Tanga kupitia rekodi zote za mechi na kuchagua wachezaji 60 bora, ambao watapelekwa Tukuyu, Mbeya kwa ajili ya mazoezi makali na wataalamu mbalimbali.
Wachezaji hao 60 watachujwa baada ya mwezi mmoja na kubaki 30, ambao watachanganywa na wachezaji wa sasa wa Taifa Stars na baadaye kupatikana kikosi bora kwa ajili ya mapambano ya kuwania kufuzu kwa AFCON.
Malinzi alisema wachezaji wa sasa wa Stars nao watakwenda kwenye kambi hiyo mkoani Mbeya mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mwezi Aprili.
“Tunaamini mfumo huo utasaidia kupata vijana wapya wa kuboresha kikosi cha Stars, hatutachagua majina wala kuangalia umri kwa kuwa hiki ni kipindi cha mpito na ni muda mchache umebakia kuelekea kwenye michuano hiyo,” alisema Malinzi.
Machi 5 mwaka huu Stars itashuka dimbani kuumana na Namibia katika mechi ya kirafiki inayotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Rais wa TFF, Jamal Malinzi akikabidhi sehemu ya vifaa vya michezo kwa ajili ya michuano maalum ya kusaka kikosi cha Stars leo (Picha kwa hisani ya Lenzi ya Michezo)

Wakati huo huo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanza rasmi mikakati ya kuiwezesha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufuzu kwa Fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani baada ya kupanga mpango wa timu hiyo kuweka kambi nchini Uholanzi.
Kambi hiyo itakuwa ni maalumu kwa timu hiyo kuweza kujiandaa na hatua ya kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Morocco na kushirikisha jumla ya mataifa 16 yatakayofuzu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema endapo Stars itafanikiwa kupita katika hatua ya awali ya mchujo ikiwa itapangwa kwenye hatua hiyo, wamepanga kuweka kambi nchini Uholanzi ya timu hiyo, ili kujiandaa na hatua ya pili ya makundi.
Malinzi alisema wameamua kufanya hivyo ili kurudia historia ya mwaka 1980 ya Stars kufuzu kwa mara ya mwisho michuano ya AFCON, iliyofanyika nchini Nigeria, ambapo Stars iliweka kambi Uholanzi mwaka 1979 na kufanikiwa kufuzu kwa fainali hizo.
“Tumepokea barua ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) inayotueleza kuwa mechi zetu za mchujo zitaanza kati ya mwezi Mei hadi Agosti kutokana na kiwango chetu kuwa chini ya nchi 21 bora za bara hili, hivyo muda si mrefu tunafikiria kurekebisha benchi lote la ufundi kwa pamoja na kuanza mikakati ya timu hiyo.
“Huenda timu yetu ikaanzia hatua ya mchujo kama CAF walivyotuandikia, ikifanikiwa kufuzu katika hatua ya makundi ttumepanga kuweka kambi nje ya nchi katika nchi ya Uholanzi, na huko timu itapata mafunzo ya kisasa ili kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi,” alisema Malinzi.
Katika hatua nyingine alisema kwa sasa wameshazungumza na Balozi wa Uholanzi hapa nchini kwa ajili ya mipango yao hiyo, pia wamewataarifu wadhamini wakuu wa Stars, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chao cha Kilimanjaro Premier Lager ili kuandaa bajeti ya ziara hiyo. 

MECHI YA TWIGA STARS, ZAMBIA ‘LIVE’ ZNBC

Na Boniface Wambura, Lusaka
KIKOSI cha Twiga Stars kinashuka Uwanja wa Nkoloma, Lusaka nchini Zambia leo kuwavaa wenyeji Zambia (Shepolopolo) katika mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) itakayooneshwa moja moja ‘live’ na televisheni ya Shirika la Taifa la Utangazaji la Zambia (ZNBC).

Mechi hiyo itaanza saa 9 kamili mchana kwa saa za Zambia ambapo Tanzania itakuwa saa 10 kamili jioni huku Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage akiwa tayari ametangaza ‘silaha’ zake kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza.

Watakaoanza kupeperusha bendera ya Tanzania katika mechi hiyo ambayo kiingilio ni bure kwa majukwaa yote isipokuwa lile kuu ni; Fatuma Omari 1, Fatuma Bashiru 17, Donisia Daniel 2, Fatuma Issa 5, Evelyn Sekikubo 15, Sophia Mwasikili 16, Vumilia Maarifa 10, Mwapewa Mtumwa 9, Asha Rashid 14, Etoe Mlenzi 13 na Shelida Boniface 7.

Wachezaji wa akiba ni Maimuna Said 18, Fatuma Hassan 12, Zena Khamis 6, Esther Chabruma 8, Amina Ally 4, Therese Yona 11 na Happiness Hezron 3.

Sikinde yapiga mbizi baharini na kuibukia Kigamboni

Baadhi ya wapiga wa Sikinde wakiwajibika

BENDI kongwe ya muziki wa dansi, Mlimani Park 'Wana Sikinde' leo inatarajia kuvuka bahari ya Hindi na kwenda kufanya onyesho maalum la Siku ya Wapendanao 'Valentine Day' eneo la Mji Mwema Kigamboni.
Onyesho hilo litafanyika kufcuatia maombi ya wadau wa muziki wa dansi wa eneo hilo ambao wanataka kuishuhudia bendi hiyo ikifanya vitu vyake huko kwenye siku hiyo ambayo husherehekewa kote duniani Februari 14 ya kila mwaka.
Mratibu wa onyesho hilo, Michael Yona alisema kuwa amesikia maombi ya wakazi wa Kigamboni na sasa anawapelekea bendi hiyo kongwe ambayo ana uhakika itawaburudisha vya kutosha kwenye siku hiyo maarufu duniani.
"Sikinde wana nyimbo zao mpya kama Kiboyo, Nundu ya Ng'ombe, Kukatika kwa Dole Gumba, Jinamizi la Talaka, Tabasamu Tamu, Deni Nitalipa na nyingine nyingi ambazo nina uhakika itakuwa ni nafasi ya pekee kwa wakazi wa Kigamboni kuburudishwa na nyimbo hizo," alisema Yona.
Alisema kuwa nyimbo hizo ndizo zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu mpya baada ya ile ya 'Supu Imetiwa Nazi' ambayo hadi sasa bado iko sokoni wakati wanamuziki wakiendelea kukuna vichwa ili kukamilisha vitu vipya.
Naye katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo alisema Sikinde alisema kuwa kwa muda mrefu haijafanya onyesho Kigamboni na kwamba ana uhakika wakazi wa eneo hilo wana hamu ya kuwaona Sikinde wakiwaburudisha.
"Kwanza kabisa ieleke kwamba Mlimani Park ni bendi ya watu wote wakiwamo wakubwa na vijana wadogo ambao naamini watakuja kuishuhudia kwenye onyesho hili la Siku ya Wapendanao," alisema Milambo.
Bendi hiyo ilirudia jina lake la zamani la Mlimani Parbk kutoka DDC Mlimani Parik baada ya kuachwa na Shirika la DDC na sasa inajitegemea.

Hassan Vocha kuwa Surprise mashabiki leo

 
MUIMBAJI mpya wa kundi la taarab lililorejea upya la Dar Modern 'Wana wa Jiji', Hassan Vocha, amewaahidi kuwafanyia 'mshangao' mashabiki wa kundi hilo watakaohudhuria utambulisho wake na wasanii wenzake unaofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Vocha na waimbaji wenzake kadhaa walionyakuliwa na kundi hilo lililowahi kutamba na vibao kama 'Pembe la Ng'ombe', 'Kitu Mapenzi' na 'Malavidavi' watatambulishwa leo 'Valantine Day' eneo la Magomeni.
Akizungumza na MICHARAZO, msanii huyo alisema ameandaa kitu 'spesho' kwa mashabiki wa muziki wa taarab katika onyesho hilo maalum.
"Kuna kitu maalum nimewaandalia mashabiki kwa ajili ya utambulisho huo ikizingatiwa onyesho litafanyika Siku ya Wapendanao', naomba waje ukumbini kujua kitu gani hicho," alisema Vocha.
Vocha aliyejipatia umaarufu mkubwa kupitia wimbo wake wenye jina hilo la 'Vocha' alichoimba na Dogo Aslay wakati akiwa Mkubwa na Wanae, alisema jukumu alililopewa kuvaa 'viatu' vya Hammer Q ni changamoto kwake.
"Najua ni changamoto kwangu, lakini kwa vile mimi ni msanii mwenye kipaji nitawapa burudani mashabiki wenye imani nami," alisema Vocha ambaye katika onyesho hilo ataimba karibu nyimbo zote alizoimba Hammer Q.
Uzinduzi huo wa Dar Modern utafanyika Travertine Hotel na kusindikizwa na makundi ya Kibao Kata na Baikoko ambapo Vocha atatambulisha nyimbo mbili alizorekodi katika albamu za kundi hilo za 'Oh My Sweet' na 'Ngoma Inapasuka'.