Deo Lyatto katika majukumu yake ya Uenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF |
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la soka nchini TFF, jana ilitangaza kuzindua rasmi mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho hilo na kutoa fulsa kwa wadau wa soka kuchukua fomu za kuomba kugombea uongozi ndani ya shirikisho hilo.
Uchaguzi mkuu wa TFF umepangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo Deogratias Lyatto, alisema kuwa fomu kwa ajili ya kuomba kuwania uongozi wa TFF zitaanza kutolewa Jumatatu, Januari 14 ambapo zitatakiwa kurudishwa kabla ya Januarui 18.
Lyatto alisema kuwa mbali na kuanza rasmi mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa TFF, pia kamati yake imezindua rasmi mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa bodi itakayoendesha ligi kuu Tanzania bara (TPL- Board).
Lyatto alisema kuwa katika uchaguzi wa TFF, nafasi zitakazogombewa ni pamoja na Rais wa TFF, Makamu wa Rais pamoja na nafasi 13 za wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo ambazo zimepangwa katika kanda.
Pia alisema kuwa kwa upande wa Bodi ya TPL, nafasi zitakzogombewa ni Mwenyekiti wa Bodi, Makamu Mwenyekiti pamoja na wajumbe wawili wa bodi hiyo kutoka katika klabu za ligi daraja la kwanza.
Lyatto alisema kuwa kwa nafasi ya Mwenyekiti na makamu wake wa bodi ya ligi kuu ni lazima wawe wenye viti wa klabu za ligi kuu zilizoshika nafasi ya kwanza mpaka ya sita msimu uliopita.
"Kwa wajumbe wa bodi ni lazima wawe wenyeviti wa klabu za ligi daraja la kwanza ambao wote hao pamoja na mwenyekiti na makamu wake wa bodi lazima wapigiwe kura na vilabu," alisema Lyatto.
Alisema kuwa moja ya sifa za kugombea uongozi TFF na katika kamati ya ligi ni lazima mgombea awe na elimu isiyopungua kidato cha nne isipokuwa kwa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa TFF ambapo atatakiwa kuwa na kiwango cha elimu kisichopungua Shahada ya Chuo Kikuu na awe na uwezo na haiba ya kuiwakilisha TFF ndani na nje ya nchi.
Pia sifa nyingine ni lazima mgombea awe na uzoefu wa uendeshaji wa mpira wa miguu uliothibitishwa kwa angalau miaka mitano na pia asiwe na hatia yoyote ya kosa la jinai na awe amewahi kua ama mchezaji wa mpira wa miguu, Kocha, mwamuzi au kushiriki katika uendeshaji wa mpira wa miguu katika ngazi ya mkoa.
Lyatto alisema kuwa ada ya uchukuaji fomu kwa upande wa Rais wa TFF ni Sh. 500,000, Makamu Rais ni Sh. 300,000 wakati wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF ni Sh. 200,000.
Kwa upande wa bodi ya ligi kuu Mwenyekiti na Makamu wake watachukua fomu kwa Sh. 200,000 wakati wajumbe wa bodi hiyo watachukua fomu kwa Sh. 100,000.
Lyatto alisema kuwa wadau wa soka wenye sifa wabnaruhusiwa kujitokeza kuchukua fomu kuwania uongozi katika chaguzi hizo.
Aidha, alisisitiza wadau wa soka kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi wa TFF.