STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 25, 2014

Ajali tena! Watu watano wafa Kilimanjaro, wanne taaban


PIcha hii haihusiki na habari hii, ila ni kati ya ajali ambazo zimekuwa zikichukua roiho za watanzania wenzetu kila uchao
AJALI za barabarani zimeendelea kuteketeza roho za watanzania baada ya watu watano kufariki katika ajali iliyohusisha magari mawili katika eneo la Boma Ng'ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, watu hao walifariki jana jioni katika njia ya mzunguko ya uwanja wa ndege wa kimataifa ya KIA ikihusisha magari mawili yaliyogongana ubavuni ambapo watu wengine wanne walijeruhiwa.
Inadaiwa mwendo kasi ya magari hayo ndiyo yaliyosababisha vifo vya watu hao watano wakiwamo wanaume watatu na wanawake wawili ambao miili yao iliharibika.
Abiria wanne walionusurika kufa wapo katika hali mbaya na wamelazwa katika hospitali ya mkoa ya Maweni kwa ajili ya matibabu.

Man Utd kuvuna nini Ugiriki katika UEFA Champion League?!


ATHENS, Ugiriki
KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champion League) kinatarajiwa kuendelea tena leo na kesho kwa mechi nne za kumalizia mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora kuwania kucheza Robo Fainali ya michuano hiyo.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester United ambayo imefufuka kwenye ligi ya nyumbani leo itakuwa ugenini nchini Ugiriki kuvaana na Olympiakos Piraeus wiuki moja baada ya timu za Manchester City na Arsenal kupoteza mechi zao za nyumbani dhidi ya Barcelona na Bayern Munich.
Mechi nyingine ya leo itazikutanisha timu za Zenit St Petersburg dhidi ya wana fainali wa mwaka jana,  Dortmund ya Ujerumani.
Katika mechi ya Manchester United dhidi ya Olympiakos Piraeus, wagiriki hao hawajawahi kufanya vyema mbele ya Mashetani Wekundu, japo wenyewe wamenukuliwa wakiapa kwamba piga ua leo ni lazima waigaragaze vijana wa David Moyes.
Mashetani Wekundu waliopata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Crysral Palace kwenye mechi yao ya ligi mwishoni mwa wiki, itahitaji kufanya vyema leo ugenini ili kufufua matumaini ya timu za England kuvuka katika hatua hiyo.
Hata hivyo itakuwa na kazi ngumu kuhakikisha wanaifunga  vinara hao wa Ligi Kuu ya Ugiriki ambao wamefika hatua hiyo ya mtoano kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka minne.
Wagiriki hao wataweka historia kama wataifunga United baada ya kupoteza mara nne katika michuano ya hivi karibuni ilipokutana nayo.
Hata hivyo, kwa sasa Olympiakos Piraeus ipo katika kiwango kizuri baada ya kucheza mechi 26 za ligi bila kupoteza huku ikiongoza kileleni mwa Ligi Kuu ya Ugiriki maarufu kama Super League.
Wakati United Jumamosi ikishinda 2-0 dhidi ya Crystal Palace, Olympiakos iliichapa OFI Crete mabao 4-0 huku Mserbia Marko Scepovic aliyesajiliwa hivi karibuni akifunga mara tatu ‘hat-trick’ yake ya kwanza katika maisha yake kisoka.
"Ningependa kuona hali kama hii, na hamu ya wachezaji wangu dhidi ya United kama walivyoonyesha dhidi ya OFI," kocha Michel alisema wakati timu yake ikipata ushindi wa 24 katika mechi 26 za ligi ilizocheza.
"Kila mechi tunakabiliana nayo kwa umakini sana na tunaamini tutapata matokeo mazuri sana Jumanne (leo)," alisema mshambuliaji huyo wa zamani na wa Real Madrid na Hispania ambaye kwa sasa ana miaka 50.
"Tumegeuza ukurasa mpya na akili zetu sasa tunazielekeza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya United, ninaweza kuona hamu ndani ya macho na katika sura ya wachezaji wangu; wako tayari kwa hilo," aliahidi katika ukurasa wake wa Facebook juzi.
Michel atawakosa baadhi ya wachezaji wake wakongwe baada ya mshambuliaji wa zamani wa Argentina Javier Saviola kuwa majeruhi wa mguu. Kukosekana kwa Saviola inamaana Mnigeria Michael Olaitan mwenye miaka 21 kwa sasa, ambaye amefunga mabao nane katika mechi 15 alizocheza, atapata nafasi ya kuanza sambamba na kiungo mshambuliaji wa Argentina Alejandro Dominguez atakayecheza nyuma yake.
United imesafiri kwenga Ugiriki hiyo ikiwa nafasi pekee kwao msimu huu ya kutwaa kombe lakini hata hivyo matarajio hayo ni madogo sana kwa ubora wao kwa sasa.
Katika mechi hiyo, United itakuwa ikimtegemea zaidi Wayne Rooney (pichani) aliyepewa mkataba mnono wa paundi 300,000 kwa wiki huku akifunga bao safi mwishoni mwa wiki.
Pia, kocha David Moyes atakuwa na uwanja mpana zaidi wa kumjumuisha Marouane Fellaini katika kikosi chake cha kwanza baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Juu ya pambano la Zenit dhidi ya Dotmund, mashabiki wa timu ya Ujerumani watapewa ofa ya chai na vitafunwa kwa Zenit St Petersburg leo, lakini ukarimu huo hautakuwapo dimbani kwani miamba hiyo ya Urusi imepania kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza.
Kocha wa Zenit, Luciano Spalletti anafurahia kiwango cha timu yake kwa sasa; "Tumecheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa muda mrefu sasa, na tumepigana vema msimu huu. Tumekuwa na wachezaji wengi bora jambo linalomaanisha tunaweza kucheza kwa kiwango hiki."
Aliongeza: "Tulitoka sare nyumbani na Porto tulipopaswa kushinda, na ilikuwa hali kama hiyo dhidi ya Austria Vienna, tulipocheza tukiwa 10 uwanjani zaidi ya sasa moja.
"Tulipaswa kunyakua pointi nyingi zaidi, lakini kwa ujumla tunaweza kuwa na furaha kwa kiwango chetu."
Dortmund ilisonga mbele baada ya kuwa kinara wa kundi lao lilokuwa likizijumuisha Napoli, Arsenal na Olympique Marseille kwa kufikisha pointi 12 sawa na vijana wa Arsene Wenger na wa Rafa Benitez lakini wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ndiyo yaliyoibeba miamba hiyo ya Ujerumani ambayo msimu huu haitisha kwenye ligi ya nyumbani.
Baada ya kutwaa ubingwa wa Bundesliga 2011 na 2012 na kumaliza ya pili msimu uliopita, imekuwa ikipanda na kushuka msimu huu na kwa sasa inashika nafasi ya tatu.
Jumamosi ilipata kipigo kikubwa zaidi ugenini msimu huu baada ya kuchapwa 3-0 na Hamburg SV lakini kocha Juergen Klopp anaamini watafanya vizuri leo.
"Tumewahi kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufanya vibaya kwenye ligi ya nyumbani," alisema.
"Ni mashindano tofauti kabisa," aliongeza kiungo Nuri Sahin. "Tutajiandaa vema huko St Petersburg na tunahitaji kupata matokeo mazuri na kurudi nayo Dortmund."

Tiko Hassan: Kimwana anayetaka mabadiliko, nidhamu Bongo Movie

Msanii Tiko Hassan katika pozi
"NAAMINI kama wasanii wa kike watajitambua na kutulia kwa kuepuka skendo na mambo ya upuuzi ni rahisi kwao kupata tenda zinazoweza kuwaingizia pato la ziada nje ya fani zao kama ilivyo kwa wanamichezo au wasanii wa kimataifa wanaotamba kwa utajiri duniani."
Ndivyo anavyosema Tiko Hassan 'Tiko' mmoja wa waigizaji nyota wa filamu nchini, akizungumzia namna anavyokerwa na baadhi ya wasanii wenzake wa kike wanavyojisahau na kujikita kwenye mambo ya ovyo kiasi cha kuchafua sifa ya sanaa na kuwafanya wasanii wote kuonekana wa ovyo.
"Kwa kweli hili jambo linakera kwa sababu jamii inatutazama kama watu tusiojiheshimu na hata wakati mwingine tunakosa nafasi ya kutumika kama mabalozi wa kutangaza bidhaa na huduma za taasisi kwa sababu ya mambo tunayofanya, imefika wakati wasanii tukabadilika," anasema.
Tiko anasema ingawa kila mtu ana uhuru wa kufanya atakalo, bado wasanii wanapaswa kuwa mstari wa kwanza kulinda maadili na nidhamu ya sanaa kwa sababu inawasaidia kuwaingizia kipato hata kama siyo cha kuridhisha, lakini bado ni ajira inayopaswa kuheshimiwa.
Mwanadada huyo aliyeanza kujihusisha na sanaa tangu akiwa Shule ya Msingi Mbagala Kizuiani kisha Al Haramain, anasema kuna haja vyombo vinavyosimamia sanaa kuwa wakali dhidi ya watu wachache wanaotaka kuwaharibia kazi.
Shabiki huyo wa Yanga, anasema anaamini vyombo kama Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) na hata Bongo Movie Unity wakiwa wakali wanaweza kufanya 'wavamizi' katika fani ya uigizaji kujiondoa wenyewe na kwenda kufanya upuuzi huo kwingine.

NANDIPHA
Tiko anayependa kula ugali kwa dagaa na bamia na wakati mwingine wali kwa kuku au kisamvu na maharage na kunywa juisi anasema licha ya kipaji cha kuzaliwa cha sanaa, lakini alijikuta akivutiwa na uigizaji kutokana na uigizaji wa Lesego Motsepe 'Nandipha' wa Isidingo the Need.
"Huyu dada ambaye kwa sasa ni marehemu alinifanya nami kuota kuja kuwa muigizaji kwa sababu nilikuwa navutiwa naye kupitia igizo lao la refu linaloendelea mpaka leo kwenye runinga la 'Isidingo the Need'," anasema.
Anasema baada ya kuonyesha makeke katika sanaa shuleni katikati ya miaka ya 2000 alijitosa jumla kwenye sanaa hiyo kupitia kundi la Shirikisho Msanii Afrika.
"Nakumbuka mwaka 2006 ndipo nilijitosa jumla kupitia Shirikisho Msanii Afrika na igizo langu la kwanza lilikuwa 'Chozi' kabla ya kufuatiwa na 'Darubini' kisha nikahamia kwenye filamu," anasema.
Anasema kazi ya kwanza kuicheza ilikuwa 'The Living Ghost' kisha kufuatiwa na utitiri wa filamu kama 'The Devil's Soul', 'Limbwata', 'Check in the Bible', 'My Son' , 'Melvin', Foolish Age na nyingine.
Mwanadada huyo anayefurahia sanaa kumbadilisha maisha yake kutoka kuwategemea wazazi mpaka kujitegemea mwenyewe na akiendesha biashara inayomuingizia pato la ziada anasema kati ya kazi zote alizocheza, filamu ya 'Limbwata' kwake ndiyo bomba  kwake.
"Limbwata, ndiyo filamu ambayo naamini nimeitendea haki, japo kazi nyingine ikiwamo  ya Melvin pia zinanisisimua," anasema.
Tiko anayeota kuja kuwa msanii wa kimataifa pamoja na kumiliki kampuni yake, mbali na uigizaji pia ni muimbaji na mjasiriamali akijihusisha na biashara ya urembo na nguo za wanawake.
Tiko Hassan
FURAHA
Tiko Hassan aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita jijini Dar es Salaam, anasema hakuna tukio la furaha kwake kama siku alipojifungua mwanae kipenzi aitwaye Aisha mwenye miaka nane, ambaye anadai ni kama rafiki na mfariji wake.
"Kwa kweli hili ndilo tukio la furaha kwangu. Aisha amenifanya nijisikie mwenye furaha na kwenye matukio ya huzuni hakuna linaloniliza kama nilipompoteza baba yangu mwaka 2005," anasema.
Msanii huyo aliyesomea kozi ya Uongozi ya Utalii katika Chuo cha African Tourism College, anasema kwa wasanii wa Bongo anamzimia na kumkubali sana Ahmed Salim maarufu kama 'Gabo' akidai akipewa sapoti kubwa anaweza kuwa 'nembo' ya Tanzania kwani ana kipaji na anajua kuigiza.
"Aah! Gabo hana mpinzani kwa sasa Tanzania, licha ya kuibuka siku za karibuni, lakini akiwezeshwa zaidi anaweza kuitoa kimasomaso Tanzania kwa kipaji alichoinacho na umahiri wake katika kuigiza," anasema Tiko ambaye hajaolewa ila ana mchumba anayetarajia kufunga naye ndoa.
Kuhusu sanaa ya Tanzania, Tiko anasema bado inahitaji mabadilkio makubwa, hasa wasanii wakongwe kujitolea kuwasaidia chipukizi badala ya kuwabania kwa kuamini watafunikwa.
"Pia ni lazima wasanii tupendane na kushirikiana bila kubaguana kwa nia ya kuendeleza mbele sanaa yetu na hasa katika kukabiliana na unyonyaji tunaofanyiwa," anasema.
Tiko anayependa kutumia muda wake wa mapumziko kuangalia movie, kuogelea, kulala na kupika anasema kama siyo sanaa huenda angekuwa 'Mama Ntilie' kwa sababu ya kupenda shughuli za jikoni na hasa kupikapika.
"Wallah, kama siyo kipaji cha sanaa naamini ningekuja kufanya kazi ya Mama Ntilie napenda sana kazi ya kupika," anasema.
Tiko anasema ukiondoa Mungu aliyemjalia kipaji na afya na kila kitu kinachomfanya amshukuru kila saa, pia anawashukuru mno wazazi wake, mchumba wake, wasanii wenzake, ndugu na jamaa wote waliomsaidia kwa namna moja au nyingine kumfikisha hapo alipo.
"Kwa kweli mbali na Mungu ninayemshukuru kila dakika kwani bila ya yeye nisingekuwa Tiko Hassan, pia nawashukuru mno wazazi wangu, mchumba wangu, marafiki na wote wanaoniunga mkono katika shughuli zangu ninazofanya kuanzia za sanaa na zile za ujasiriamali," anasema.