|
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage |
ZAIDI ya Sh. milioni 10 za klabu ya Simba zimeporwa baada ya
Mhasibu wa klabu hiyo, Erick Sekiete (28) kudai kuvamiwa na majambazi sita
katika mtaa wa Sinza kwa Remmy na kuporwa kiasi hicho cha pesa juzi saa 3:20
usiku.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela alisema kuwa Sh. milioni
7.59 na dola za Marekani 2,000 ambazo Simba walizipata baada ya makato ya
mapato ya mechi yao dhidi ya Tusker FC ya Kenya iliyomalizika kwa wenyeji Simba
kuchapwa 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Simba ilipata mgawo wa Sh. milioni 10.6 na dola za Marekani
2,000 (Sh. milioni tatu) kutokana na mapato ya kiingilio cha mechi yao dhidi ya
Tusker. Baada ya makato, walibakiwa na Sh. milioni 7.59 ambazo Sekiete alikabidhiwa,”
alisema Kamanda Kenyela.
Alisema kuwa baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Sekiete na
mwenzake Stanley Phillipo (23) ambaye alidaiwa kuwa ni mwanafunzi, walipanda
kwenye gari aina ya Toyota Premio yenye namba za usajili T869 BKS lililokuwa
likiendeshwa na Said Pamba na kwamba walipofika eneo hilo, dereva aliwashusha
na kwamba wakaanza kutafuta teksi.
Aliendelea kueleza kuwa muda mfupi baada ya kushushwa,
Sekiete na Philipo waliamua kuvuka upande wa pili wa barabara ya iendayo
Kijitonyama ili wachukue teksi lakini ghafla
walilitekwa na watu sita walioshuka kutoka kwenye pikipiki tatu.
“Mmoja wa watu walioshuka kwenye pikipiki alikuwa na
bastola... alifyatua risasi hewani wakati wenzake wakipora begi lenye fedha
kutoka kwa mhasibu,” alisema Kenyela.
Aliendelea kufafanua kuwa wakati watu hao wakimnyang’anya
begi Sekiete walikuwa wakitamka maneno ya kejeli kwa uongozi wa Simba.
Aliyanukuu maneno hayo kwa kusema; “Mnafungwa halafu
mnazingua, na kwa kuwa viongozi wenu wanakula pesa za klabu, nasi hizi tunaziiba.”
Kamanda Kenyela alisema kuwa baada ya watu hao kupora fedha
hizo, walitokomea kusikojulikana na hadi sasa, Jeshi la Polisi linawashikilia
watu watatu akiwamo Sekiete kuhusiana na tukio hilo.
Watu wengine wanaoshikiliwa na jeshi hilo katika Kituo cha
Polisi Magomeni ni Pamba na Philipo ambao walikuwa pamoja na Sekiete kwenye
gari.
“Sisi (Jeshi la Polisi) tulishaonya watu kusafirisha kiasi
kikubwa cha fedha bila ulinzi, tunawashikilia watu hawa watatu kwa sababu
huenda walipanga kuiba fedha hizo,” aliongeza.
“Mazingira ya kuporwa kwa fedha hizo yanatia shaka huenda
kuna kitu kilikuwa kimepangwa ili fedha hizo ziibwe. Iweje mtu akahifadhi
nyumbani kwake kiasi kikubwa cha fedha kama hicho?” alihoji Kamanda Kenyela.
“Kwa sasa mtu yeyote atakayeripoti kuporwa fedha kiasi
kikubwa kama hiki na alikuwa akisafirisha pasipo na ulinzi, tutaanza naye.
“Tunawashikilia wawa watatu kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na
tukio hilo. Tunaomba ushirikiano kutoka watu wenye taarifa juu ya waliohusika
na tukio hili.”
Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage alinukuliwa jana
akidai amesikitishwa na taarifa za kuporwa kwa fedha za klabu yao.
“Mhasibu wetu anaishi Sinza. Alizichukua zile fedha za klabu
akazihifadhi nyumbani kwake ili leo (jana) azipeleke benki,” alisema Rage.